Wednesday, March 29, 2017

Profesa Muhongo: Wananchi lipieni umeme ofisi za Tanesco pekee

Na Veronica Simba – Singida
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wananchi wote, hususan wanaounganishiwa huduma ya umeme vijijini, kufanya malipo husika katika Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) peke yake na siyo kwa mtu mwingine yeyote.
Aliyasema hayo hivi karibuni kijijini Mkwese, Wilaya ya Manyoni wakati akizindua Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika Mkoa wa Singida.
Profesa Muhongo alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakitapeliwa na watu mbalimbali kwa kuombwa rushwa ili waunganishiwe umeme au kulipishwa gharama zaidi ya zile zinazostahili, na baada ya kufuatilia, imebainika kuwa wanaofanya utapeli ni watu wasiohusika kabisa na uunganishaji umeme.

Ili kuepuka utapeli huo, Waziri Muhongo amewataka wananchi kufahamu taratibu zinazopaswa kufuatwa wakati wa kuunganishiwa umeme ikiwa ni pamoja na kujua kiasi wanachopaswa kulipia na ni nani wa kumlipa.
Aidha, aliitaka Tanesco kuhakikisha inaendelea na zoezi la kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zote wanazotoa ili wananchi wawe na uelewa wa kutosha na hivyo kuepuka kutapeliwa.
Alisema kuwa, baadhi ya wananchi wanadhani kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ndiyo wenye jukumu la kuchukua malipo kutoka kwa wananchi wanaounganishiwa umeme vijijini.
“Anayepokea malipo yote ya umeme ni Tanesco. Siyo REA wala Wizara. Wananchi mjue hilo. Mwingine yeyote akidai malipo ya umeme, kataeni,” alisisitiza.
Waziri Muhongo aliwataka Wakuu wa Wilaya mbalimbali kuhakikisha wanamkamata na kumweka ndani mtu yeyote anayepita katika maeneo yao na kudai malipo ya umeme kutoka kwa wananchi wakati siyo Ofisa wa Tanesco.
“Mambo ya malipo yote yanafanywa Tanesco. Wala huyu Mkandarasi hakusanyi fedha. Kama ataomba fedha za kuunganishia watu umeme au za nguzo, huo ni wizi na utapeli. Lazima mumshtaki.”
Akielezea kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Profesa Muhongo alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inaundoa umaskini wa wananchi kwa kuwapatia huduma muhimu ikiwemo umeme.
“Injini mojawapo nzuri na muhimu ya kuondoa umaskini wetu ni kuhakikisha tunakuwa na umeme wa uhakika, unaotabirika na wa bei nafuu.”
Alisema, Serikali inatambua kuwa wananchi walio wengi wanaishi vijijini ndiyo maana Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo inaishia mwezi wa sita mwaka huu, fedha zake nyingi zilipelekwa kwenye miradi hususan ya umeme vijijini.
Profesa Muhongo alisema kuwa, ili kuwapunguzia wananchi gharama ya kufuata huduma ya kuunganishiwa umeme kwenye Ofisi za Tanesco ambazo ziko mbali, Serikali imeagiza maafisa wa shirika hilo kutangaza tarehe watakapofika kugawa fomu za kujiandikisha pamoja na vituo vitakavyotumika kufanyia malipo.
Alitoa rai kwa Serikali za Vijiji kutoa ushirikiano kwa Tanesco, ikiwezekana kuwapatia chumba au Ofisi ya kutolea huduma kwa siku watakazopanga kutoa huduma katika vijiji husika.
Waziri Muhongo alieleza kuwa, kwa Mkoa wa Singida, Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu utatekelezwa kwa vipindi viwili tofauti ambapo sehemu ya kwanza itahusisha upelekaji umeme katika vijiji 185 kwa gharama ya shilingi bilioni 47.36. Aliongeza kuwa utekelezaji wa sehemu hiyo ya kwanza umeanza mwezi Februari mwka huu na unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 2019.
Alimtaja Mkandarasi Nakuroi Investment Co. Ltd ambaye alimtambulisha pia kwa wananchi na kumkabidhi kwa viongozi wa Serikali na Wabunge wa Singida, kuwa ni mmoja wa makandarasi watakaoshiriki katika utekelezaji wa Mradi husika katika Mkoa huo.
Aidha, Profesa Muhongo alieleza kuwa, sehemu ya pili ya mradi huo mkoani Singida, itaanza kutekelezwa baada ya sehemu ya kwanza kukamilika mwaka 2019 ambapo vijiji 82 vitapatiwa umeme na hivyo kufikisha umeme katika vijiji vyote vya Mkoa wa Singida ifikapo Mwaka 2021.
Uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa Mkoa wa Singida ulihudhuriwa na wananchi, viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na baadhi ya wafadhili wa Mradi husika ambao ni Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Katarina Rangnitly na Balozi wa Norway nchini, Hamme Hanie Kaarstad.

WADAIWA SUGU NA TANESCO WAONJA JOTO YA JIWE MKOAN KIGOMA

Na Rhoda Ezekiel Kigoma.

SHIRIKA la umeme Tanzania TANESCO Mkoani Kigoma imesitisha huduma za umeme kwa Mamlaka ya Maji safi na Mazingira KUWASA, kufuatia deni la umeme la shilingi bilioni 1.3 ambalo halijalipwa tangu mwaka 2013 hadi sasa hali inayopelekea kukosekana kwa Maji Manispaa ya Kigoma na kupelekea dumu moja la maji kuuzwa shilingi 1000.

Akizungumza na Globu ya Jamii,Kaimu Mkurugenzi wa KUWASA, Muhandisi Mbike Jones alisema Mamlaka ya Maji ilikatiwa umeme wiki iliyopita kufuatia deni lililokuwa linadaiwa tangu mwaka 2013 na limeshindwa kulipwa kutokana na Mamlaka hiyo kutegemea fedha hizo kulipwa na Wizara ya maji.

Jones alisema KUWASA ilijitahidi kufanya mazungumzo na TANESCO waweze kurudisha umeme na kudai kuwa ni maelekezo kutoka Makao makuu, mpaka sasa Wizara imejitahidi kufanya mzungumzo na Wizara ya fedha na kudai kuwa watalitatua tatizo hilo baada ya mazungumzo na Shirika la umeme waweze kulipa kidogo kidogo.

Alisema Mpaka sasa KUWASA inadai taasisi za serikali milioni 380 na Wananchi milioni 330, hali inayopelekea kukwamisha zoezi la ulipwaji wa deni hilo kushindwa kulipwa, na aliwaomba Wananchi na Taasisi zinazo daiwa kulipia madeni hayo ili maji yaweze kurudishwa na kuepukana na kero hiyo.

" niwaombe wananchi wawe wavumilivu na waendelee kuchemsha maji wanayo yachota kwenye vyanzo vya maji, ili kuepukana na magonjwa ya milipuko na wawe wavumilivu jitihada zinaemdelea za kuhakikisha tatizo hilo linakwisha na kuendelea kupata maji kama mwanzoni", alisema Jones.

Nao Baadhi ya Wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji , Athumani Rashidi na Destina Paulo walisema kumekuwa na tatizo la maji hali inayopelekea Dumu moja la maji kuuzwa shilingi 1000 hali niyopelekea Wananchi wenye kipato kidogo kushindwa kumudu gharama hizo na kushindwa kununua.

Paulo alisema kwasasa wanalazimika kwenda kuchota maji kwenye mito na Visima vilivyoko mbali na mji kilomita nane kutokea Mjini hali hiyo inawapelekea kushindwa kukabiliana na kero hiyo, na waliiomba serikali na mamlaka inayo husika kuliahughurikia suala hilo ilikuepukana na kero hiyo.


Baadhi ya wakazi kutoka maeneo mbalimbali wakichota maji kwenye vyanzo vya maji vinavyopatikana mjini humo.

WAZIRI MWAKYEMBE APOKELEWA OFISINI KWAKE DODOMA


 Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof Elisante ole Gabriel akiteta jambo na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Harrison Mwakyembe na wakati waziri huyo alipowasili Ofisini kwake Mjini Dodoma.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akisalimiana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Anastazia Wambura wakati alipowasili Ofisini kwake Mjini Dodoma.
  Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe akisalimiana na baadhi ya wakurugenzi na wakuu wa Taaisi zilizo chini ya Wizara yake wakati alipowasili Ofisini kwake Mjini Dodoma.
  Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe akitia saini katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ofisini kwake Mjini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura akitia saini katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ofisini za Wizara Mjini Dodoma.
 Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof Elisante Ole Gabriel (aliyesimama) akifafanua jambo kwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe (katikati) kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Anastazia Wambura.
 Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura(kushoto) akimkaribisha Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe (katikati) kuzungumza na waandishi wa habari Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof Elisante Ole Gabriel.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu mikakati yake katika kuiongoza Wizara.
 Baadhi ya wakurugenzi wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe(hayupo pichani) wakati alipokuwa akizungumza nao alipowasilikatika Ofisi za Wizara Mjini Dodoma.

Picha zote na Raymond Mushumbusi WHUSM Dodoma.

MKUU WA WILAYA YA CHEMBA AZINDUA ZOEZI LA UTHAMINI

Mkuu wa Wilaya ya Chemba Ndugu Simon Ezekiel Odunga akizungumza na wananchi wa kata ya Farkwa wakati wa uzinduzi wa zoezi la uthamini mali ili kupisha ujenzi wa bwawa la Farkwa.
Mkuu wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma akiongozana na baadhi wa Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Wataalamu wa Halmashauri, Wataalamu kutoka Wizara ya Maji, Uvuvi na umwaguliaji, Wataalamu wa Bonde la Kati na Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wamezindua zoezi la uthamini wa mali za wananchi wa vijiji viwili vya Mombose na Bubutole watakaohama kupisha mradi mkubwa wa Ujenzi wa bwawa la Farkwa mkoani hapa.

Mradi wa bwawa la Farkwa ni mradi mkubwa ambao huenda ukawa ni mkubwa katika Ujenzi wa mabwawa makubwa kuliko yote barani Afrika. Mradi huu uliasisiwa na baba wa Taifa tangu mwaka 1970 utazinufaisha Wilaya za Bahi, Chemba, Chamwino na Dodoma Manispaa na utegemea kutumia pesa za Tanzania zaidi ya Tilioni 2.

Kufuatia umuhimu wa mradi huu na uwijio wa makao makuu ya nchi mkoani Dodoma, serikali imezamilia ifikapo mei mwaka huu zoezi la Uthamini wa mali za wananchi wanaohama kupisha mradi huu mkubwa katika Vijijini vya Mombose na Bubutole vilivyopo Wilayani Chemba pamoja na vijiji vinavyopitiwa na njia Kuu ya bomba linalopeleka Maji eneo la Kilimani mjini Dodoma liwe limekamilika tayari kwa kuwalipa wananchi ili Ujenzi wa bwawa uanze.

Ujenzi wa mradi huu unategemea kuchukua miaka mitatu 2017-2021 mpaka kukamilika kwake. Hivyo wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Wataalamu wa uthamini kwa kuwa wameusubiri mradi huu kwa zaidi ya miaka 47 na leo serikali imepata fedha ya kuutekeleza.

Mhe Mkuu wa Wilaya ya Chemba Ndugu Simon Odunga wamewataka wananchi hao kujiepusha na watu wasiopenda maendeleo yao na nchi yetu kwa ujumla wa anaopita pita huko na kujifanya watetezi wa haki za wananchi. Swali hao watetezi walikuwa wapi tangu 1970 waje leo ambapo mradi unaanza kutekelezwa.? 

Aidha, amesisitiza wananchi ambao ni wamiliki halali wa maeneo husika ndio wajitokeze kwenye uthamini huo ili kuepusha udanganyifu na migogoro isiyo ya lazima wakati wa malipo yatakopoanza. Kwani kuna baadhi ya wananchi zi waaminifu na atakayefanya hivyo akibaini sheria kali dhidi yake zitachukua mkondo.

Kwa upande wa Wataalamu Mkuu huyo wa Wilaya amewataka kutumia akili, uweledi na taaluma zao katika kuhakikisha kila mwananchi wa maeneo hayo anapata haki yake stahiki kwa mujibu wa sheria za uthamini.

Katika Mkutano huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Mhe Rajabu Muheshimwa ameongea kwa kupongeza juhudi za Serikali kwa kuamua kuanza mradi huu na zaidi kusihi wananchi kutoa ushirikiano kwa Wataalamu, hali kadhalika Mhe Diwani wa Kata ya Farkwa Ndugu, Suleiman Gawa amesisitiza kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu pia Wataalamu wahakikishe wanaorodhesha mali zote za wananchi zinazotambulika kisheria ili kuepusha migongano hapo baadae.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya amewataka Viongozi wa Vijiji na vitongoji kusimamia zoezi hili kikamilifu kwani wao ndio wanaowafahamu wananchi wao pia watoto ambao wanamiliki mali lakini hawatambuliwi kisheria kutokana na umri wao.

REA YAMWONDOA MKANDARASI MZEMBE
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye kipaza sauti) akiwatambulisha wafanyakazi wa Kampuni ya Nakuroi Investment Co. Ltd (waliochuchumaa), ambao watatekeleza Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mkoani Singida.
Sehemu ya umati wa wananchi waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Singida. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni katika Kijiji cha Mkwese, wilayani Manyoni.
Moja ya vikundi vya ngoma kutoka Manyoni, kikitumbuiza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Singida. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni katika Kijiji cha Mkwese, wilayani Manyoni.


Na Veronica Simba – Dodoma

Wakala wa Nishati Vijijini (REA), umesitisha mkataba wa Mkandarasi Spencorn Services, aliyekuwa akitekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya pili kwa Mkoa wa Singida.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga aliyasema hayo hivi karibuni katika hafla ya uzinduzi wa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini awamu ya Tatu katika Mkoa wa Singida, uliofanyika kijijini Mkwese, wilayani Manyoni.

Mhandisi Nyamo-Hanga alimweleza Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Mradi huo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwa, ufanisi wa kazi wa Mkandarasi husika haukuwa mzuri hivyo kusababisha baadhi ya vijiji ambavyo vilipangwa kupelekewa umeme katika REA II, kutofikiwa na huduma hiyo.

“Tumechukua hatua za kinidhamu. Tumemsimamisha kazi na tutaleta wakandarasi wapya ambao wataendelea na kazi ya kusambaza umeme pale alipoishia.”

Aidha, Mkurugenzi Nyamo-Hanga alitoa shukrani kwa Serikali kwa ushirikiano na msaada ambao imekuwa ikitoa, ulioiwezesha REA kuendelea na zoezi la kuwafikishia umeme wananchi wa vijijini kwa mafanikio makubwa.

Alisema kuwa, gharama ya utekelezaji wa REA III Mkoa wa Singida ni shilingi bilioni 47.36 ambapo jumla ya vijiji vitakavyonufaika ni 267. Aliongeza kuwa, Mkandarasi atakayetekeleza Mradi huo ni Nakuroi Investment Co. Ltd.

“Tutaanza na kuunganisha umeme katika vijiji 185 na baadaye tutamalizia vijiji 82 vitakavyokuwa vimebaki, na kuwezesha vijiji vyote vya Mkoa wa Iringa kuwa na umeme kwa asilimia 100.”

Idadi ya vijiji vilivyo na umeme hadi sasa kwa Mkoa wa Singida ni 196, sawa na asilimia 42.

Mhandisi Nyamo-Hanga, amewataka wananchi watakaounganishiwa umeme katika Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Tatu, kama ilivyokuwa kwa Mradi wa Awamu ya Pili; kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao mapema ili wakati mkandarasi atakapofika katika maeneo yao, wawe tayari kulipia na kuunganishiwa umeme.

Vilevile, ameomba Serikali za Kata na Vijiji kubainisha maeneo maalum ya viwanda ambayo katika mradi huu, yatafikishiwa miundombinu ya umeme mkubwa ili kuwezesha wajasiriamali vijijini kupatiwa umeme utakaowezesha kuanzishwa kwa viwanda vidogo vidogo na vikubwa vijijini kwa gharama nafuu.

Uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaendelea katika Mikoa mbalimbali nchini. Mpaka sasa, uzinduzi umekwishafanyika katika Mikoa ya Tanga, Pwani, Dodoma, Iringa, Mbeya, Songwe, Mara na Singida. Kwa Mkoa wa Shinyanga, uzinduzi utafanyika tarehe 1 Aprili, mwaka huu.

WAZIRI MAKAMBA ATOA MAAGIZO KWA MAMLAKA YA NGORONGORO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mara baada ya kutembelea eneo hilo kujionea changamoto za kimazingira. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akiongea na Baraza la wafugaji (hawapo pichani) katika Wilaya ya Ngorongoro. Wafugaji hao walimweleza Waziri kilio cha muda mrefu cha mradi wa Josho Wilayani hapo, Waziri Makamba ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Ngorongoro na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kuleta ufumbuzi mapema. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mara baada ya kutembelea eneo hilo kujionea changamoto za kimazingira.

……………..

Na Lulu Mussa,Ngorongoro


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais mwenye dhamana ya usimamizi wa Mazingira nchini Mhe. January Makamba amesema kuwa ni lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kudhibiti mimea inayohatarisha uoto wa asili katika Mamlaka ya Ngorongoro.

Katika kutatua changamoto hii, Waziri Makamba ameagiza kuundwa kwa jopo la wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na Tecknolojia, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Hifadhi za Taifa za Tanzania, Wizara ya Kilimo na Mifugo na Mamlaka ya Ngorongoro ndani ya miezi sita kufanyika kwa utafiti wa kina wa kisayansi wa kubaini mbinu mpya ya kupambana na mimea hiyo vamizi inayotawala mimea inayotumiwa na wanyama.

Akizungumza katika kikao kilichojumisha Wahifadhi wa Mamlaka ya Ngorongoro na Wajumbe wa Baraza la wafugaji, Waziri Makamba amesikitishwa na kitendo cha Uongozi wa Mamlaka ya Ngorongoro kushindwa kuandaa mpango kabambe wa usimamizi wa hifadhi baada ya ule wa awali kuisha muda wake. 
 
Waziri Makamba ameuagiza uongozi wa Ngorongoro kuandaa mpango huo mapema na kuwa shirikishi. ” Mpango mtakoandaa hakikisheni kuwa unakuwa shirikishi kwa jamii inayozunguka na wadau na Taasisi muhimu likiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Waziri Makamba pia ameagiza kufanyika kwa ukaguzi wa kimkakati wa Mazingira utakaojumuisha Wilaya nzima ya Ngorongoro na kuitaka Mamlaka ya Ngorongoro kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kutekeleza wajibu huo mapema. Ukaguzi huo wa kimkakati wa kimazingira kwa Wilaya hiyo unatazamiwa kutoa mtazamo wa hali ya mazingira kwa miaka hamsini ijayo.

Aidha, Waziri Makamba ameagiza kufanyika kwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira ama Ukaguzi wa Mazingira katika Hotel zote zilizopo eneo la hilo na kulitaka Baraza la Taifa la Hofadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupita siku ya Alhamisi tarehe 30/03/2016 kuwaandikia adhabu na kuwatoza faini wahusika wote ambao hawana vyeti hivyo. “Haiwezekani toka mwaka 2004 Sheria ipo na mpaka leo watu wanaendea na mchakato, hii haikubaliki!” Alisisitiza Makamba.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba ametoa miezi sita kwa wamiliki wa Hotel zilizopo katika Mamlaka ya Ngorongoro kuwekeza katika mfumo mpya wa kuvuta maji kutoka Mto Lukusale na kusitisha mfumo wa sasa wa kutoa maji kwenye creator. Pia Makamba ameutaka ungozi wa Mamlaka ya Ngorongoro ndani ya miezi sita kuandaa ramani itakayoonyesha mito na vijito vyote vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo.

Waziri Makamba ametoa maagizo hayo leo juu ya namna bora ya kutumia rasilimali ya “creater” kwa ajili ya utalii na Uhifadhi wa Mazingira, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa zuio la mifugo ndani ya crater. Ziara maalumu na mahsusi ya kukagua utekelezaji na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira inayofanywa na Waziri Makamba hii leo imefika Wilayani Ngorongoro.

RC Simiyu amaliza mgogoro wa wanakijiji na wawekezaji

Mkuu wa Mkoa wa Simiiyu, Anthony Mtaka akifungua kikao cha usuluhishi baina ya mwekezaji wa Mwiba Holdings na wadau wa maendeleo mkoani Simiyu kilichofanyika mwishoni mwa wiki.
 
 
 MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amefanikiwa kumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya mwekezaji katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) Makao iliyopo wilayani Meatu, na baadhi ya vijiji vinavyounda jumuiya hiyo. 

Mwekezaji huyo Mwiba Holdings, amekuwa na mgogoro wa mipaka, mkataba wa kumiliki ardhi na uanzishaji wa ranchi na baadhi ya vijiji hivyo kiasi cha kusababisha kuwa na mahusiano mabaya na wananchi ambao wamekuwa wakisusia misaada mbalimbali inayotolewa na mwekezaji huyo. 
 
Hata hivyo, chanzo halisi cha mgogoro huo kimegundulika kuwa ni viongozi wa baadhi ya vijiji ambao wamekuwa wakipigania maslahi yao binafsi huku wakisambaza taarifa za upotoshaji juu ya mwekezaji huyo na kujenga chuki kwa wananchi. 
 
Vijiji vinavyounda WMA ya Makao ni pamoja na Makao, Iramba ndogo, Sapa, Mwangudo, Jinamo, Lukale, Mbushi, Mwabagimu na Sunga. Baadhi ya viongozi hao wa vijiji pia wamekuwa wakisambaza taarifa potofu kwa wananchi kwamba Mkuu huyo wa mkoa na mkuu wa wilaya ya Meatu wamehongwa na mwekezaji ili kuwakandamiza wananchi, jambo lililothibitika kuwa si la kweli.
 
 Kutokana na mgogoro huo kuzidi kuota mizizi huku uongozi wa CCM Mkoa wa Simiyu nao ukichukua upande, Mtaka alilazimika kuitisha kikao cha usuluhishi kilichoshirikisha wadau wote wakiwamo Kamati ya Siasa ya CCM mkoa na wilaya, viongozi na watendaji wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya, viongozi wa vijiji tisa vinavyounda WMA Makao, mwekezaji na wadau wengine akiwamo Mbunge wa Meatu na Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu. 
 
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa, Mtaka aliwakemea viongozi wanaoeneza taarifa potofu wilayani humo na kusababisha shughuli za maendeleo kukwama huku akiahidi kuwachukulia hatua zinazostahili viongozi wa namna hiyo. “Katika masuala ya maendeleo ya wananchi sina mzaha. Nipo tayari kuwa kiongozi unpopular (asiyependwa) ili mradi shughuli za maendeleo za wananchi zinaenda mbele. 
 
“Mgogoro na Mwiba umekuwa kama mkuki mnaojichoma wenyewe kila siku kwa sababu wenyewe ndiyo mlioingia mikataba na mwekezaji wakati sisi hatukuwapo na wala hatuna maslahi yoyote binafsi hivyo acheni maneno maneno, kaeni chini mzungumze tusonge mbele,” alisisitiza Mkuu huyo wa mkoa. “Mmefikisha malalamiko, tena kwa maandishi hadi kwa Waziri Mkuu lakini uhalisia ni kuwa mengi mliyopeleka hayana ukweli, ni hisia na mengine ni fitna tu. Sasa wekeni kila kitu hadharani hapa, tumalize suala hili leo na tujikite zaidi katika mambo ya maendeleo,” alisema.Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Dk Titus Kamani akizungumza katika kikao cha usuluhishi baina ya wananchi wa Meatu na Mwekezaji wa Mwiba Holdings kilichofanyika mjini Mwanhuzi mwishoni mwa wiaki.Mkuu wa Mkoa wa Simiiyu, Anthony Mtaka akifungua kikao cha usuluhishi baina ya mwekezaji wa Mwiba Holdings na wadau wa maendeleo mkoani Simiyu kilichofanyika mwishoni mwa wiki
 
Kuhusu mgogoro wa mpaka hasa katika kijiji cha Buhongoja ambako alama ya mpaka yenye namba 314 inadaiwa kusogezwa kinyemela kwa umbali wa kilomita 10, Mkuu huyo wa mkoa alizitaka pande zinazohusika kukutana na kutatua tatizo hilo kwa kurejea katika eneo la awali bila ya mikwaruzano yoyote. Aliamuru pia pande zinazohusika katika suala la mkataba wa umiliki wa ardhi,kukaa meza moja na kuacha mambo ya kukimbilia kwa wasuluhishi ambao wamekuwa wakidai fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kwa maendeleo ya vijiji au wilaya ya Meatu.
 
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini aliahidi kupeleka wataalam watatu watakaosaidiana kutatua mgogoro huo wa umiliki wa ardhi watakaosaidiana na wake wa wilaya ili kutatua suala hilo ndani ya wiki mbili. Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Makao, Anthony Phillipo alieleza kuwa kijiji kilazimika kupelaka suala hilo kwenye Tume ya Usuluhishi wa Migogoro Dar es Salaam ambako kijiji walishindwa kulipa gharama za usuluhishi huo walizotozwa na Jaji Mstaafu Thomas Mihayo. 
 
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani alieleza chama hicho tawala kusikitishwa na mgogoro huo unaokwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho. “Ndugu zangu, sisi tunajiandaa kushinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kwa hiyo tunawaomba tusikubali kuingizwa katika migogoro kama hii ambayo haina tija kwa wananchi.
 
 “Tunataka wakati wa uchaguzi utakapofika tushinde pila pressure (msukumo) yoyote na tunachotaka ni mshikamano,maelewano mazuri baina ya wadau wote ili tufanye shughuli za maendeleo kwa faida ya mkoa wetu wa Simiyu na wilaya ya Meatu,” alisisitiza. 
 
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Mpina Luhaga ambaye pia ni mbunge wa Kisesa wilayani Meatu alisema katikA kikao hicho kuwa mwekezaji huyo amekuwa akifuata sheria zote za nchi katika utekelezaji wa majukumu yake na ni wazi kwamba wananchi watashindwa katika madai yote wanayofungua katika Tume ya Usuluhishi wa migogoro. 
 
“Mimi nimefuatilia malalamiko haya ya wananchi serikalini na hasa Wizara ya Maliasili na Utalii na hawa jamaa wamefuata taratibu zote na wanalipa tozo zote wanazostahili kulipa hivyo tunapaswa kuwa waangalifu,” alisema. Mkurugenzi wa Mwiba Holdings, Abdulkadir Mohamed Luta alisema kuwa Kampuni hiyo ipo tayari kukaa meza moja na kusaidia usuluhishi wa mgogoro wowote ili wajikite zaidi katika shughuli za maendeleo ya wananchi.
 
 Aliongeza kwamba kampuni hiyo ilikuwa tayari kugharamia hata suala la mkataba wa umiliki wa ardhi lililofikishwa Tume ya Usuluhishi wa Migogoro ili mradi tu suala hilo liishe na waendelee na mambo ya maendeleo Alisema watazifanyia kazi hoja zote zilizotolewa na wananchi katika kikao hicho na kwamba sera ya kampuni hiyo ni kushirikiana na wananchi na wamekuwa wakitekeleza sera hiyo kwa vitendo. 
 
Mbunge wa Meatu, Salum Khamis maarufu kwa jina la Mbuzi, alisema kuwa hana mgogoro na mwekezaji yoyote lakini hatakaa kimya kutetea maslahi ya  wananchi wake ambao ndio waajiri wake kila atakapoona kuna sababu ya kufanya hivyo. 
 

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Pius Machungwa aliahidi kuipatia kiwanja cha kujenga ofisi Kampuni ya Mwiba Holdings katika makao Makuu ya wilaya hiyo ili iwe karibu na wananchi, na kwamba watashirikiana na kampuni hiyo katika shughuli za maendeleo wilayani humo.

MTANZANIA ALIYEWEKA REKODI YA KUPANDA MLIMA KILIMANJARO KWA MUDA MFUPI AMUANGUKIA WAZIRI MWAKYEMBE


Gaudence Lekule akiwa katika kilele cha Uhuru ,Mlima Kilimanjaro baada ya kukimbia kwa muda wa wa saa 8:36 mpya akiwa Mwafrika na Mtanzania wa kwanza kutumia muda huo kupanda kilele cha mlima Kilimanjaro na kushuka.

Gaudence Lekule akipanda mlima Kilimanjaro huku akikimbia wakati akiweka rekodi baada ya kutumia muda wa saa 8:36 mapema mwaka huu.
Lekule akifurahia mara baada ya kufanikiwa kuweka ekodi ya kutumia muda wa saa 8:36 kupanda Mlima Kilimajaro na kushuka.


Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

MTANZANIA ,Gaudence Lekule (31) anayeshiriki michezo ya kupanda milima kwa kasi (Mountain Run) amemuomba Waziri mpya wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo ,Dkt Harison Mwakyembe kutupia jicho michezo mingine kwani ina nafasi kubwa ya kutangaza na kuletea sifa taifa.

Lekule anayeshikilia rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza Duniani kupanda kwa muda mfupi katika Mlima Kilimanjaro akitumia muda wa jumla wa saa 8:36 alitoa wito pia kwa kampuni,taasisi binafsi na za serikali kujitokeza kudhamini wanamichezo kutokana na eneo hilo upo uwezekano wa kujitangaza zaidi kidunia.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum,Gaudence alisema kwa sasa yupo katika maandalizi ya kuweka rekodi mpya katika milima mirefu na maarufu Duniani kwa kufanya mazoezi ya awali hapa nchini na baadae nje ya nchi.

“ Nashukuru kuitangaza Tanzania kidunia na tayari nimepata mialiko mingi ya kwenda nje kushiriki mashindano ya Mountain Run ,Lengo langu ni kuweka rekodi katika milima mirefu duniani hivyo bado naendelea na mazoezi na nitaendelea kufanya mazoezi hapa kwetu na badaae nje ya Tanzania”alisema Gaudence .

Alisema hadi sasa rekodi ya Dunia inashikiliwa na raia wa nchi ya Ecuador, Karl Egloff aliyetumia muda wa saa 6:53 kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro ,rekodi aliyoweka mwaka 2014 akivunja rekodi ya Kilians Jornet raia wa Hispania aliyetumia muda wa saa 7:20 kupanda na kushuka mlima Kilimanjaro mwaka 2010.

Lekule alisema changamoto iliyopo kwa sasa ni mabadiliko hali ya hewa inayochangia kushindwa kufanya mazoezi na upatikanaji wa mahitaji kama chakula pamoja na mavazi kwa ajili ya mchezo huo unafanyika kuanzia urefu wa mita 3500 hadi 5800.

Akizungumzia kilichomsukuma kushiriki mcezo mchezo huo,Lekule ,mkazi wa kiraracha Marangu wilaya ya Moshi alisema raia wa kigeni wamekuwa wakishiriki katika michezo ya aina hiyo kwa ajili ya kuweka rekodi hivyo akaona ni wakati wa waafrika pia kushiriki katika uwekaji wa rekodi Duniani.

Alisema raia wa Ecuador ,anayeshikilia rekodi ya dunia aliposikia ameweka rekodi akiwa ni mwafrika na Mtanzania wa Kwanza alituma salamu za pongezi huku akimtaka kwenda kwenye milima iliyopo nchi za nje kutafuta rekodi nyinine.

“ Egloff alifurahi sana na kunipa moyo na kunitaka nikatafute rekodi nje ya Afrika kwa sababu nina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri Ulaya na kuipa sifa Tanzania,ni ngumu sana mtu kukimbia kwenye urefu kama uliopo Mlima Kilimanjaro na katika maisha inahitaji moyo sana.”alisema Lekule.


Rekodi za kidunia.

Mara ya kwanza rekodi ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kasi kwa Afrika ilikua inashikiliwa na Saimon Mtui akitumia muda wa saa 9 : 20 mwaka 2006, baadae raia wa Hspania Kilians Jornet alitumia muda wa saa 7:20 mwaka 2010.

Mwaka 2014 ndipo Karl Egloff raia wa Ecuador anayeshikilia rekodi ya Dunia hadi sasa alitumia muda wa saa 6 :53 mwaka 2014 na sasa Mtanzania Gaudence Lekule ameweka rekodi ya kuwa Muafrika na Mtanzania wa Kwanza akitumia muda wa saa 8:36 .

Solly Mahlangu kutoka nchini Afrika kusini athibitisha kushiriki tamasha la Pasaka jijini Dar


MWIMBAJI wa kimataifa wa nyimbo za injili, Pastor Solly Mahalangu kutoka nchini Afrika Kusini, amethibitisha kushiriki Tamasha la Pasaka linaloadhimisha miaka 17 tangu kuasisiwa kwake mwaka 2000 chini ya uratibu wa kampuni ya Msama Promotions.

Solly ambaye amekuwa king’ara vilivyo katika muziki wa injili kama mwimbaji anayejipambanua na wengine kama mchangamshaji zaidi jukwaani, pia ni kiongozi wa kanisa nchini Afrika Kusini , hivyo kuenfesha huduma zote mbili kila moja kwa wakati wake.

Alex Msama, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo litakalozinduliwa April 16, mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea katika mikoa mingine mitano, alisema jana kwamba mwimbaji huyo amethibitisha kushiriki tukio hilo lenye kubeba hadhi na vionjo vya kimataifa.

“Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, nina furaha kubwa kusema kuwa mwimbaji wa kimataifa wa nyimbo za injili kutoka nchini Afrika Kusini, amethibitisha kushiriki tamasha la Pasaka la mwaka huu litakalofanyika katika mikoa sita ikiwemo Dar es Salaam,” alisema.

Alisema ujio wa Mahlangu katika tamasha hilo, kunafanya maandalizi ya Tamasha hilo yazidi kuimarika kutokana na umaarufu wa mwimbaji huyo anayesifika ndani na nje ya Afrika Kusini kwa huduma ya uimbaji wa nyimbo zenye ujumbe wa kuvutia wengi na kuchangamsha jukwaa.

Msama alisema kwa vile si mara ya kwanza kwa Mahlangu kushiriki Tamasha la Pasaka, wadau na wapenzi wa Tasmaha hilo wajitokeze kwa wingi kuja kufaidi Baraka za Mungu kupitia ujumbe wa Neno la Mungu kutoka kwa mwimbaji huyo na wengine kibao akiwemo malkia wa muziki wa injili Afrika Mashariki, Rose Muhando.

Alisema Mahlangu ambaye atakuwa na kundi lake, atashirikiana na waimbaji wengine walitangazwa tayari ambao tayari wapo katika maandalizi ya nguvu kwa lengo la kutoa huduma bora siku hiyo ya uzinduzi wa Tamasha hilo lenye kubeba maudhui ya kueneza ujumbe wa neno la Mungu na sehemu ya mapato kusaidi makundi maalumu.

Msama alisema Tamasha la mwaka huu litabeba uzinduzi wa albamu mbili; moja ya Muhando inayoitwa Jitenge na Ruth pamoja na albamu mpya ya Kwaya ya Kinondoni Revival ya jijini Dar es Salaam, iitwayo ‘Ngome Imeanguka.’

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu maandalizi ya tamasha hilo litakalofanyika Aprili 16 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. 
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu maandalizi ya tamasha hilo litakalofanyika Aprili 16 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. 
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu maandalizi ya tamasha hilo litakalofanyika Aprili 16 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. 

MAGAZETI YA LEO JUMATANO MACHI 29,2017