Tuesday, June 30, 2015

Dkt. Magufuli akagua ujenzi wa Daraja la Kigamboni-Kukamilika mwezi wa Tisa mwaka huu

 Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli (wakwanza kulia) akifanya ukaguzi katika mradi wa ujenzi wa Daraja la Kigamboni. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mfuko wa Hifadhii ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhan Dau. Mradi wa Ujenzi wa Daraja hilo umefikia Asilimia 85, na unatarajiwa kukamilika mwezi wa tisa mwaka huu.
 Taswira ya mbele ya Daraja la Kigamboni ambalo linatajajiwa kumamilika mwezi wa Tisa. 
 Kazi za Ujenzi wa Daraja la Kigamboni ukiendelea kwa kasi
 
 Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli akikagua moja ya nguzo za barabara za juu flyovers katika maingilio ya Daraja la Kigamboni. Katika eneo hilo kutajengwa barabara za juu ili kuruhusu magari kupita kwa urahisi wakati wa kuingia na kutoka katika daraja hilo.
 Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli akiwa ameambatana na Watendaji mbalimbali wa Wizara ya Ujenzi pamoja na NSSF wakifanya  ukaguzi wa ghafla katika mradi wa ujenzi wa  daraja la Kigamboni.
 Meneja Mradi wa Ujenzi Daraja la Kigamboni kutoka NSSF, Karim Mataka wakwanza kulia akitoa maelezo ya Ujenzi wa Daraja la Kigamboni.
 Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli (wapili kulia) akikagua eneo la barabara za kuingia katika Daraja la Kigamboni.
 Sehemu ya barabara za Maingilio ya Daraja la Kigamboni zikiwa katika hatua za mwisho kukamilika.
Sehemu ya Katikati ya Daraja la  Kigamboni kama inavyoonekana. Picha zote kwa Hisani ya Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Ujenzi

WASHINDI WA TUZO ZA TANAPA 2014 WAKABIDHIWA TUZO JIJINI MWANZA

Meneja Mawasiliano wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ,Pascal Shelutete akitoa neno la ukaribisho katika hafla ya utoaji tuzo kwa wanahabari waliofanya vizuri katika uandishi wa masuala ya Uhifadhi.Hafla iliyofanyika katika Hotel ya Gorden Crest jijini Mwanza.  
Baadhi ya wageni waalikwa katia hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Hifadhi za Taifa ,Tanzania (TANAPA) Allan Kijazi akizungumza katika hafla hiyo juu ya lengo la kuanzishwa kwa tuzo hizo kwa wanahabari nchini.
Mkuwa wa Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza,Baraka Konisaga akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mwanza wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa Wanahabari waliofanya vizuri katika uandishi wa masuala ya Uhifadhi.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo,Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu akizungumza wakai wa hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi wa Tuzo zitolewazo na TANAPA kwa wanahabari.
Mkuu wa Majaji walioshiriki kupatikana kwa washindi wa tuzo zitolewazo na TANAPA kwa wanahabari,Dkt Ayoub Ryoba akizungumza katika hafla hiyo.
Dkt Ryoba akitambulisha majaji wenzake walioshiriki katika kupata washindi.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo,Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu akitoa ,Ngao,Vyeti pamoja na mfano wa Hundi kwa washindi wa tuzo za TANAPA 2014 zitolewazo kwa wanahabari.
Mkuu wa Majeshi Mstaafu,Meja Jenerali ,Mirisho Sarakikya akizungumza katika hafla hiyo zaii akizungumzia historia ya namna alivyoshiriki zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro zaidi ya mara 38.
Mgeni Rasmi katika Hafla hiyo,Lazaro Nyalandu ,akitunuku tuzo kwa Meja Jenerali,Mirisho Sarakikya pamoja na kitambulisho maalumu ambacho kitamuwezesha kuingia bila malipo katika hifadhi 16 za Taifa.
Meja Jenerali ,Sarakikya akifurahia zawadi hiyo iliyotolewa na TANAPA.
Mwandishi wa Habari wa Channel ten Cassius Mdami akizungumza kwa niaba ya washindi wa tuzo hizo.
Mgeni rasmi ,Lazaro Nyalandu akiwa katika picha ya pamoja na washindi.
Mgeni rasmi ,Lazaro Nyalandu akiwa katika picha ya pamoja na wahariri katika vyombo mbalimbali vya habari.
Mgeni rasmi ,Lazaro Nyalandu akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari walioshiriki katika hafla hiyo.


Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini aliyeko jijini Mwanza.

MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA BENKI YA POSTA TANZANIA (KUFUTA NA KUWEKA MASHARTI YA MPITO), 2015 (THE TANZANIA POSTAL BANK {REPEAL AND TRANSITIONAL PROVISION} ACT, 2015)

 (Yanatolewa chini ya Kanuni ya 86(6) ya kanuni za Bunge,Toleo la mwaka 2013)
Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu,Subhanahu wa Taala kwa kutujalia sote afya njema na kuendelea na kazi ya kulitumikia Taifa.
Pili nishukuru Chama changu cha CUF kwa uamuzi wake wa busara wa kunirejesha mimi kuwa Mgombea wa Jimbo la Mkanyageni na kama ukataji wa majimbo utaathiri Jimbo hilo, naamini chama pia kitafanya uamuzi wa hekima na busara kwa faida ya Chama wala sio matakwa binafsi ya yoyote.
Tatu nichukue nafasi hii kumpongeza Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif kwa ukomavu, uvumilivu na uhodari wake kisiasa na hata kama walimzuia kuingia katika Baraza, yeye alikwishafanya uamuzi mapema zaidi wa kutokwenda katika Baraza hilo maana hakuwa tayari kwenda kinyume na wajumbe wa Baraza kutoka CUF wakiwemo mawaziri. Uamuzi huo alioufanya mapema zaidi kuungana na Wawakilishi wake ndicho kilichomfanya Spika wa Baraza na wajumbe wa CCM kukasirika na kuchukua uamuzi wa chuki na kisasi ambao kwa waliokuwa hawajui wanadhani kuwa yeye alikuwa na shauku ya kwenda Barazani humo.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha CUF cha kususia baraza ni cha demokrasia popote pale Duniani kinachoonesha kutokukubaliana na jambo kwa njia ya kistaarabu. Kwa kuwa uchaguzi huru ni mchakato na unaanzia katika daftari la kuandikisha wapigakura, hivyo basi kitendo chochote cha kuwazuia au kutokuwaandikisha wapiga kura iwe Bara au Zanzibar ni jambo la hatari la kukiuka Demokrasia na kuufanya uchaguzi usiwe huru na wa haki.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaisihi,kuionya na kuitaka Serikali iwaandikishe watu wote wenye sifa katika daftari la wapiga kura kwa Bara au Zanzibar ili kufikisha makisio ya wapigakura milioni 24. Aidha
Haitakuwa uchaguzi huru na haki ikiwa idadi kubwa ya wapiga kura imeachwa kuandikishwa na kukoseshwa haki yao ya kikatiba.
Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa ni kwamba hali ya siasa Zanzibar imeshavurugwa na ilianzia pale vikosi vya ulinzi vilivyopewa silaha kuwapiga wananchi katika zoezi la kujiandikisha. Baya zaidi ni pale askari hao wanapovaa ki-ninja ili wasionekane nyuso zao na kuwachukua baadhi ya wananchi majumbani kwao usiku wa manane na kuwapiga na kuwatesa  kisha kuwatupa mwituni wakiwa taaban.
Mheshimiwa Spika, vitendo hivi vinavyofanywa sasa Zanzibar haifai kuvinyamazia na ni lazima Serikali ya Jamhuri ya Muungano ichukue hatua madhubuti vinginevyo vinakaribisha machafuko yasiyo na ulazima-Mwanzo wa kutoweka kwa amani uanza taratibu na kama hatua zisipochukuliwa majuto yatakuwa ni mjukuu. Amani tayari imeanza kutoweka Zanzibar!!!
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni kwamba UKAWA utatoa mgombea Urais mmoja na kuleta matumaini ya Watanzania na wanaojidanganya kuwa tutafarakana wanaota ndoto za mchana na watasubiri sana jambo hilo la kufarakana halitatokea.

Mheshimiwa Spika, muswada huu unaoletwa na Serikali kwa ajili ya kupitishwa una lengo la kufuta Sheria ya Benki ya Posta Tanzania, Sura 301 na kuweka masharti yatakayoiwezesha benki hiyo kusajiliwa na kuwa Kampuni, na pia kuweka masharti ya mpito kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa Sheria hii inayopendekezwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa maelezo ya Mheshimiwa Waziri aliyoyatoa katika Kamati ya Fedha, Uchumi Viwanda na Biashara ni kwamba Benki ya Posta ilikuwa inafanya kazi bila ya kukidhi matakwa ya sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo ni wazi Taasisi hiyo haikuwa na haina vigezo vya kuitwa Benki, hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani inasema hata kama Serikali itabadili  sheria ili ikidhi kigezo cha kuitwa benki  kwa mujibu wa sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006. Ambacho ni kusajiliwa chini ya sheria ya makampuni Sura, 212, lakini bado kigezo cha mtaji kitaendelea kuwa ni tatizo katika kutimiza matakwa ya  sheria ya Benki na taasisi za fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umiliki wa benki hii tunaweza kusema ni kuwa taasisi hii inamilikiwa na Watanzania kwa asilimia mia moja (100%), kwa maana kwamba Serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 86.4, Tanzania Zanzibar inamiliki asilimia 3.05, Shirika la Posta Tanzania  asilimia 8.23 na Posta na Simu SACCOS asilimia 2.68. Kuhusu Zanzibar Kambi Rasmi ya Upinzani inazotaarifa kwamba inakusudia kuwekeza kiasi cha shilingi 950,000,000/- ili kuongeza hisa zake na kufikia asilimia 10 kutoka asilimia 3.05 za sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tatizo ni mtaji na mtaji unapatikana kwa wananchi kama utaratibu ulitumika kwa Serikali kupunguza hisa zake na kuwamilikisha wananchi, kabla ya kuziweka kwenye Soko la Hisa kwa sababu tahadhari kubwa ichukuliwe ili hisa hizo zikiachwa kwenye soko zisije kuchukuliwa na wageni wachache wenye fedha, na ile dhamira ya kuwa Benki ya watanzania ikatoweka na kuleta migogoro na Serikali kama ilivyofanywa na PSRC kwa makampuni mengine.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa dhati kabisa inatoa pongezi kwa utawala na bodi ya wakurugenzi ya benki ya Posta Tanzania na hasa Mtendaji wake Mkuu kwa kuweza kuiondoa benki kutoka kwenye mtaji hasi wa shilingi milioni 78  mwaka 1992 hadi kuwa na mtaji chanya wa shilingi milioni 32,142 mwaka 2014. Hii ni kazi kubwa ukitilia maana na ushindani wa mabenki uliopo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, katika kifungu cha 2 cha muswada  kinachohusu tafsiri ya maneno “benki” limetolewa tafsiri kuwa ni Benki ya Posta Tanzania. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema tafsiri hiyo ingeongezewa maneno kuwa ni Benki ya Posta Tanzania iliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria ya Benki na Taasisi za Fdha ya mwaka 2006.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza hivyo kwa kuwa toka mwanzo Benki hiyo  ilikuwa inaitwa hivyo lakini haikuwa inakidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya Mwaka 2006.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haipingani na hoja ya  ubadilishwaji wa sheria ya uanzishwaji wa Benki ya Posta bali inasisitiza tena hitaji la mtaji, Serikali isikimbilie kutafuta wawekezaji toka nje ya nchi, madhara yake kimbilio hilo tumeliona kupitia Benki ya Biashara (NBC 1997 Ltd). Tunaamini wapo watanzania wenye fedha nyingi za kuwezesha kutimiza sharti la mtaji kwa mujibu wa sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 6 cha muswada kinahusu kuhamisha wafanyakazi waliokuwa watumishi wa Benki ya posta  na kuwa watumishi katika kampuni mpya. Jambo hili limeleta mgogoro sana na watanzania wengi ambao wana kesi zao mahakama za kazi kwa kiasi kikubwa ni kutokana na kampuni kubadilisha muundo wake. Ni maoni ya Kambi  Rasmi ya Upinzani kwamba Serikali ihakikishe na kusimamia maslahi ya watumishi, pamoja na  muswada huu wa sheria umetambua suala hilo ingekuwa ni vyema muswada ukaweka kifungu cha adhabu pale utawala wa benki utakapokiuka matakwa ya kifungu hiki.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kutoa changamoto kwa watendaji wakuu wa mabenki yetu hasa (NMB, NBC, Dar es Salaam Community Commercial Bank, DTB, Akiba Commercial Bank  na sasa TPB n.k) kwa nini hasa hazijitanui hadi nchi za jirani hata kama sio zaidi ya Bara letu la Afrika?
Mheshimiwa Spika, tulitarajia NMB kwa kuwa inamilikiwa na Waholanzi kwa asilimia kubwa kuwa itafungua tawi lake Uholanzi na katika Mataifa mengine ya Ulaya, lakini imekuwa ni kinyume badala yake wanachota faida ya hapa na kupeleka nje. Tusaidieni kueleza tatizo liko wapi? Kama wenzetu wa Kenya mabenki yao yanajaa Tanzania mabenki yetu kwanini hayana matawi Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia, Zimbabwe, DRC n.k.
Je, ni kweli tumekosa ubunifu na uthubutu kiasi hicho? Kama ni sheria kazi yetu kama wabunge ndio kazi tunayotakiwa kuifanya ili kuleta ustawi katika sekta ambazo sheria zinawazuia.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani,
Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.

………………………
Mohamed Habib J. Mnyaa (Mb)
K.n.y Msemaji Mkuu-Kambi Rasmi ya Upinzani, Wizara ya Fedha
29.06.2015


MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MASOKO YA BIDHAA YA MWAKA 2015 (COMMODITY EXCHANGE ACT,2015)

 (Yanatolewa chini ya Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Bunge, toleo la mwaka 2013)
1.   UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, muswada huu ulio mbele yetu kwa malengo yake kama utasimamiwa vyema ni mzuri kwani utaboresha mifumo ya mauzo ya  mazao ya kilimo na bidhaa zingine kwa kadri mahitaji ya nguvu za soko yatakavyopelekea.  Katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara ya mwaka 2014/15 alieleza dhamira na uhitaji wa kuwepo kwa mfumo huu wa soko la bidhaa. Kwani alieleza uwepo wa kitu kinachoitwa COWABAMA -  
(Collective Warehouse Marketing Systems) na kueleza kuwa huo ni mwendelezo wa kuanzisha Soko la Mazao na Bidhaa (Commodity Exchange Market).

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haina pingamizi na muswada huu wa Sheria ya Commodity Exchange  kwani hili lilikuwa ni hitaji la wadau ambao wanashiriki katika mfumo mzima wa Stakabadhi za mazao Ghalani. Tunaamini kwa kiasi kikubwa wahusika katika mfumo huu wameshirikishwa kwa hatua zote za uandaaji wa muswada huu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako ikiwa imefanya jitihada zozote za kuhakikisha kuwa elimu kwa umma hasa kwa wadau wote wa mfumo wa masoko ya bidhaa inatolewa.  Sheria nyingi zinazoletwa katika Bunge hili zimekua zikilalamikiwa kutowafikia walengwa na hivyo utekelezaji wake siku zote umekua ukileta migogoro isiyoisha na mwishowe kusababisha hasara si tu kwa wazalishaji bali pia kwa watumiaji wa mwisho. Ni mikakati gani imewekwa ili kuhakikisha kuna utoaji elimu endelevu katika masuala ya masoko ya bidhaa?
Mheshimiwa Spika, hali ya miundombnu nchini hasa usafiri wa barabara na reli ambao ndio tegemezi kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa hasa za kilimo ni mbaya na isiyoridhisha. Sote ni mashahidi kuwa , pamoja na Serikali kujisifu kwa kuweka mtandao mkubwa wa barabara lakini barabara hizi hazijajengwa kwa ubora na ziinaleta changamoto kubwa za usafirishaji wa bidhaa hasa kipindi cha mvua. Leo tunapotaka kupitisha muswada huu wa masoko ya bidhaa, ni kwa kiasi gani tumeandaa mikakati ya kuimarisha miundombinu ili wauzaji na wanunuzi wa bidhaa wasipate hasara? ikiwa tutaendelea kuwa na miundombinu mibovu kama ilivyo sasa, ni dhahiri kuwa hata utekelezaji wa Sheria hii utakua mgumu na hivyo kuwa na Sheria bubu isiyoendana na mahitaji ya masoko ya bidhaa na hivyo kudidimiza uchumi badala ya kuinua uchumi .
Mheshimiwa Spika, maendeleo ya teknolojia katika masoko ya bidhaa ni mojawapo ya sababu zitakazoweza kufanikisha ama kufelisha utekelezaji wa Sheria hii. Ni kwa kiasi gani Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na ukuaji wa teknolojia utakaomwezesha mtumiaji wa masoko ya Bidhaa ya Tanzania kuendana na mtumiaji wa masoko ya bidhaa mahali pengine duniani?

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuletwa kwa Sheria hii katika Bunge lako, ni dhahiri kuwa ili sheria hii iweze kutekelezwa kwa kiwango kinachotakikana, kanuni na miongozo yake ni lazima iwepo. Ikiwa Sheria hii italetwa na kanuni zitachelewa kutungwa, basi utekelezaji wake hautakua na maana yoyote na hivyo kuchangia kwa migogoro na migongano ya kisheria

2.   MAPITIO YA MUSWADA

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 5 cha muswada kinachohusu malengo ya mdhibiti yanayohusiana na masoko ya bidhaa. Kambi Rasmi inapenda kupata taarifa ya kina kwani Mdhibiti ambaye ni CMSA yeye hana bidhaa bali bidhaa zinazotakiwa kuingia katika soko ambalo liko chini yake ziko chini ya mamlaka zingine ambazo zimeanzishwa kisheria na zinazo kanuni zake za uendeshaji; mamlaka hizo ni kama vile bodi ya Korosho, Bodi ya Kahawa, Bodi ya nafaka na  Mazao mchanganyiko: Hivyo basi  kwa kuangalia majukumu ya mdhibiti katika sheria hii ni dhahiri kuwa taasisi hizo hazitakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria zilizozianzisha.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi inaungana na wadau ambao wameliona tatizo hizo la kuziweka pembeni mamlaka na wakala za Serikali kama ambavyo baadhi yake  zilivyoainishwa hapo juu, kwani kuna bidhaa ambazo zinatakiwa ziingie katika mfumo mzima  au mnyororo wa uongezwaji wa thamani  kabla ya kuwekwa katika soko la bidhaa. Na hapa Wizara mbalimbali zinahusika, na Waziri aliyetajwa ni Mmoja tu Waziri wa Fedha. Hii inaweza kukwamisha utekelezaji wa mfumo huu ambao tunaamini kuwa ni kwa faida ya wazalishaji wa bidhaa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo kuhusiana na suala hilo la kutokutambuliwa na sheria kwa watendaji wengine wa Serikali ambao ni nguzo pia katika kuhakikisha bidhaa inauzwa, au wako karibu na wazalishaji.
Mheshimiwa Spika, katika kifungu cha 6 kinachohusu majukumu au kazi za mdhibiti, limetumika neno “Institutions” lakini neno hilo halijatolewa tafsiri, hivyo basi ni muhimu neno hilo likatolewa tafsiri  yake ili kuondoa mkanganyiko kwa wadau wa Sheria hii.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 8(3) kinasema kwamba
“A company which is licensed as a commodity exchange shall not appoint any person to the position of Chief Executive Officer or Managing Director, senior management or the Board of Directors, change a substantial shareholder or change the organization structure without obtaining prior confirmation of the Authority”.
Mheshimiwa Spika, ni vyema Kambi Rasmi ya Upinzani ikapata maelezo ya kina kuhusiana na katazo hilo kwani kampuni pindi inaposajiliwa kwa mujibu wa sheria za makampuni sura ya 212, inakuwa na bodi yake na inakuwa na mamlaka kamili, na pia katika utendaji wake wa kazi bodi ndiyo yenye mamlaka ya kuteua nani awe ni mtendaji mkuu wa kampuni husika kwa vigezo walivyoweka wao.

Mheshimiwa Spika, Aidha, kulingana na mazingira ya kampuni ni jukumu la kampuni husika au wanahisa ambao ni wakurugenzi kuingiza mwanahisa au kumtoa kulingana na Articles of Association (makubaliano yao)  zinavyosema. Sasa kitendo cha kuomba ruhusa kwanza kwa Mdhibiti wa Uendeshaji wa Soko la Bidhaa ni kuingilia mambo binafsi ya Kampuni husika. Tukumbuke kuwa Mtendaji Mkuu ni mwajiriwa na si mmiliki pale ambapo  mmiliki akiona mtendaji mkuu hafanyikazi wala kutekeleza majukumu yake kwa maslahi ya wanahisa hivyo ni jukumu la Bodi ya wakurugenzi kuchukua maamuzi.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 3 na 4 cha muswada kinatoa ishara kama kwamba (makampuni yote) wale wote waliopata leseni “licensees” za soko la bidhaa ni mali ya Mamlaka,  tukumbuke kwamba wadau wakuu wengi ni sekta binafsi hivyo kuiambia sekta binafsi isibadilishe mfumo wa utendaji kazi na watendaji wake, ni kuingilia masuala binafsi ya kampuni. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema, Jambo hili halikubaliki kabisa na hivyo basi vifungu hivyo vifutwe kwa lengo la kuleta tija.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 9 (1) (b), (c) katika muswada bado vinaingilia mamlaka binafsi ya Kampuni na pia vinaweka ulinzi ambao utasababisha watendaji kujiona nao ni wamiliki na hivyo kuathiri utendaji kazi wao. Hoja ya Msingi ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani ingependa kuuliza ni kwanini ulinzi huo wa nafasi ya Mtendaji Mkuu hadi kuwekwa katika Sheria? Ni kweli kwamba haina ushindani pale wenye kampuni wanapotaka kufanya mabadiliko ya uongozi? Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kufuta vifungu hivyo vya ulinzi wa nafasi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 67 cha muswada ambacho kinaelekeza kutumia maelezo ya kifungu cha 66(c ) cha sheria ya CAPITAL MARKET kuhusiana na tafsiri ya maneno ya mienendo mbalimbali ambayo hairuhusiwi kwenye biashara ya masoko ya bidhaa. Katika hilo Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kitendo cha kutumia  rejea ya sheria nyingine “cross reference” ya sheria nyingine kwenye sheria hii ni uzembe, kwani sio mara zote mtumiaji wa sheria hii atakuwa katika nafasi ya kuwa na sheria nyingine ambayo inafanyiwa rejea.

Aidha, Mheshimiwa Spika, kifungu hicho hicho kimetumia maneno “manipulation, rigging Bucketing and Cornering” lakini kwa bahati mbaya katika kifungu cha 2 cha muswada kinachohusu tafsiri ya maneno, maneno hayo hayapo. Pia kwa kuwa tunatarajia sheria hii iwe toshelevu katika matumizi yake. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha kwamba kila kifungu katika sheria hii kijitosheleze badala ya kufanya rejea katika kifungu kingine cha sheria nyingine.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 70 cha muswada kinachohusu “liability to pay damages” kuwa mtu yeyote atakayekutwa na hatia katika sehemu nzima ya XIII mbali ya kosa la kijinai kwa kosa husika  pia atalazimika kufidia hasara iliyotokea katika manunuzi. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kwamba kwa kuwa kitendo chochote cha kupanga kinachopelekea hasara kwa bidhaa hasa za kilimo. Maana yake ni kuhatarisha maisha ya mkulima, hivyo basi adhabu kali inatakiwa kutajwa kwenye sheria hii. Kwani adhabu ilivyowekwa katika muswada huu wa sheria haiko wazi ili kuwafanya wenye nia ovu kushtuka.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 82 cha muswada kinachohusu ulinzi “immunity” kuwa mamlaka, afisa au mtumishi yeyote hatahesabika ametenda kosa kwa kutenda au kutokutenda jambo na kupelekea hasara wakati akitimiza wajibu wake kwa nia njema, hadi pale itakapo bainika kuwa alikuwa ana nia mbaya.

Mheshimiwa Spika, kifungu hiki kama ambavyo kwa sheria nyingine zilizopita Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa haikubaliani na kifungu cha aina hii kwani kinahalalisha uzembe. Kwa sekta ya afya,  uzembe wowote unagharimu maisha ya mtu na pia hapa tukiachia sheria kuwa na kifungu hiki, maana yake tunatoa mwanya wa kutokuwajibika na mwishowe ni hasara na inaweza leta athari kubwa  kwa wanunuzi wa bidhaa na mara zote hasara inapelekwa kwa mzalishaji hasa mkulima kwa kuwa yeye ndiye mnyonge katika mfumo wa masoko ya bidhaa za kilimo. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kifungu hiki kifutwe.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema  hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

…………………………………
David Ernest Silinde (Mb)
K.n.y Waziri Kivuli- Wizara ya Fedha
29.06.2015





ACACIA YAKUSANYA SHILINGI MILIONI 800 ZA KUSAIDIA SEKTA YA ELIMU, BAADA YA KUPANDA MLIMA KILIMANJARO

 MKUU wa wilaya ya Tarime Mkoani Mara, Glorious Luoga, (Katikati), akinyanyua juu mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi Milioni 800, baada ya kukabidhiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampouni ya Acacia, Brad Gordon, (kushoto), katika hafla fupi iliyofanyika kwenye lango la kushukia kutyoka kilele cha  Mlima Kilimanjaro, Mweka, Juni 28, 2015,  Fedha hizo ambazo ni kwa ajili yab kusaidia sekta ya eli kwa watoto kutoka familia duni, zimetokana na wafanyakazi wa Acacia na familia zao pamoja na marafiki, kupanda Mlima Kilimanjaro kwa nia ya kuchangisha fedha chini ya mpango wa kampuni hiyo wa "CanEducate".

Kampuni ya Uchimbaji Acacia, inayojishughulisha na uchimbaji na utafutaji madini, , imekusanya zaidi ya shilingi milioni 800 kupitia upandaji wa hisani wa mlima Kilimanjaro ambao unalenga kuchangisha fedha za kusaidia sekta ya elimu nchini chini ya mpango wa “CanEducate”, uliobuniwa na kampuni hiyo miaka mitano iliyopita.
Timu ya wafanyakazi, marafiki na wanafamilia wa Kampuni ya Acacia wapatao 21 wakiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Brad Gordon, wamerudi kutoka safari ya kupanda mlima Kilimanjaro iliyowachukua siku sita.
Kupitia mpango huo wa CanEducate, mpango ambao unatoa ufadhili wa elimu kwa watoto wanaotoka familia duni, zinazoishi maeneo yanayozunguka migodi inayomilikiwa na kampuni hiyo, ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi, Acacia imeanza utaratibu wa kila mwaka wa kualika wafanyakazi, marafiki na wahisani kuchangisha fedha kwa njia hiyo ya upandaji mlima.
Akizungumza na wandishi wa habari kwenye lango la kushukia la Mweka, Afisa Mtendaji Mkuu wa Acacia amesema ni jambo la kujivunia kuona kampuni imefikia lengo la kukusanya kiwango cha dola 200,000, sawa na shilingi za Kitanzania Milioni 800, kupitia zoezi hili, fedha ambazo zitakuwa na matokeo makubwa sana  kwa kugusa maisha ya watoto wengi nchini Tanzania.
“Tayari tumekwisha fikia lengo la kukusanya dola 200,000 huku michango zaidi ikiendelea kumiminika. Tunayaasa makampuni na watu binafsi kuendelea kuchangia kwani zoezi lipo wazi hadi mwisho wa mwezi Julai,” alisema Brad.
Aidha, ameongeza kuwa kwa kila dola moja itakayochangwa na wafadhili, pia Kampuni ya Acacia itaongeza dola moja na hivyo kufanya jumla ya fedha zitakazoelekezwa kusaidia sekta ya elimu kupitia mpango huu kufikia kiasi cha dola 400,000 kwa mwaka huu.
Kwa kuzingatia kuwa inagharimu kiasi cha dola 75 kwa mwaka kupeleka mwanafunzi shuleni nchini Tanzania, fedha zilizokusanywa zina uwezo wa kusaidia wanafunzi zaidi ya 2,000 wasioweza kumudu gharama za masomo hususani kutokea jamii jirani na migodi ya Acacia yaani Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara iliyoko mkoani Shinyanga na Mara.
Mpango wa CanEducate ulianza mwaka 2010 kwa kuwanufaisha wanafunzi takribani 158 katika maeneo ya Bulyanhulu na hadi mwisho wa mwaka 2014 mpango umekuwa hadi kufikia kuwanufaisha wanafunzi zaidi ya 1,800 katika maeneo ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara na wanafunzi hawa wameonyesha ufaulu mzuri katika shule mbalimbali katika mitihani yao ya Taifa.
Mlima Kilimanjaro,, unatambulika kuwa  mlima mrefu zaidi barani Afrika nan i wa tatu duniani ambao kufikia kilele cha Uhuru mita 5,895 ni hatua ya juu barani Afrika. Kampuni ya Acacia ina mtazamo kuwa  Elimu humfanya binadamu kuwa huru sababu ambayo inaufanya mpango wa CanEducate kufaa kukusanya  fedha kupitia kupanda mlima hadi kufikia kilele cha Uhuru Peak.
Waweza kuchangia Elimu kupitia upandaji mlima huu wa hisani, kupitia tovuti ifuatayo;
http://caneducate.ca/kili-climb.html
 Brad, (kushoto), akikabidhi hundi hiyo kwa Mkuu wa wilaya ya Tarime, Glorious Luoga
 Brad, akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo, akiwa
 Brad Gordon, (wakwanza kulia), akiongoza timu ya watu 21, wakiwemo wafanyakazi wa Acacia na familia zao pamoja na marafiki, kushuka Mlima Kilimanjaro wakitokea kileleni, kwenye lango la Mweka
 Furaha baada ya kufanikiwa kufika Kilele cha Mlima Kilimanjaro na kurejea salama
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad  Gordon, (Katikati), Makamu wa Rais wa Acacia anayeshughulikia masuala ya kampuni, Deo Mwanyika, (wakwanza kulia), Meneja Mkuu wa uendelezaji wa kampuni ya Acacia, Asa Mwaipopo, (wapili kulia), Mkuu wa wilaya ya Tarime Glorious Luoga, (watatu kulia),wakiwa katika picha ya pamoja na watu 21 waliofanikiwa kupanda Mlima Kilimanjaro
 Brad, akipongezana na Deo
Deo akitoa shukrani baada ya timu ya watu 21, walioongozwa na Brad, kufanikiwa kupanda na kurejea salama kutoka kilele cha mlima Kilimanjaro

KESI YA MIRATHI YA MALI ZA MWANDISHI WA HABARI MKONGWE NCHINI YAUNGURUMA JIJINI ARUSHA

Mwandishi wa habari mwandamizi marehemu
Betty Luzuka aliyefariki mwezi Agosti mwaka 2013 jijini Arusha.
Mwandishi wetu, 
Arusha
KESI ya kugombea  mirathi ya mwandishi wa habari mkongwe nchini marehemu Betty Luzuka imeibua mapya  mahakamani mara baada ya ushahidi wa njia ya video kumuonyesha mke wa aliyekuwa ofisa mwandamizi wa  jumuiya ya  Afrika Mashariki , Phil Makini Kleruu aitwaye Hilda Kleruu akichukua fedha za marehemu kabla na baada ya marehemu kuaga dunia.
Hilda, ambaye amefunguliwa kesi na kaka wa marehemu, Ssarongo Luzuka, akimtuhumu kujimilikisha mali za marehemu bila kufuata utaratibu wa kifamilia na kimahakama mara baada ya marehemu kuaga dunia Agosti mwaka 2013 katika hospitali ya Shree Hindu ya jijini Arusha baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kesi hiyo ya mirathi inayovuta hisia za watu mbalimbali jijini Arusha  ipo katika mahakama ya mwanzo ya Maromboso  yenye nambari 222 ya mwaka 2013 inaitaka mahakama hiyo ipitie hukumu yake iliyotolewa Septemba 27 mwaka 2013  na hakimu Prince Gideon iliyompa  ushindi kaka wa marehemu.
Hata hivyo,upande wa mdaiwa umepinga hatua hiyo kwa  kutokuridhishwa na hukumu hiyo kutokana na kudai kuwa ana wosia halali alioachiwa na marehemu uliomilikisha mali zake zote  ambazo ni nyumba tatu zilizopo maeneo ya Njiro,Olmatejoo na Pemba road,mamilioni ya fedha zilizopo katika akaunti mbalimbali  pamoja na shamba lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 3 lililopo eneo la Mkonoo mkoani Arusha.
Katika kesi hiyo iliyopo mbele ya hakimu  wa mahakama hiyo,Moka Mashaga upande wa  wadai  wanaitaka mahakama kutupilia mbali  wosia uliowasilishwa na mdaiwa kwa kuwa ni batili,umepikwa  na kwamba sahihi ya marehemu imeghushiwa.
Ushahidi uliotolewa mahakamani hapo wiki iliyopita kwa njia ya video na upande wa mdai katika kesi hiyo aliiambia mahakama kuwa mdaiwa (Hilda) alikuwa akitoa fedha kwa nyakati tofauti katika benki ya  CRDB tawi la Mapato  jijini Arusha kwenye akaunti ya marehemu huku akitambua kuwa siyo msimamizi halali wa mali za marehemu hali ambayo iliwalazimu wao kufika polisi kutoa taarifa na hatimaye akaunti hizo kuzuiwa hadi kesi hiyo itakapomalizika.
Ssarongo aliiambia mahakama hiyo kwamba yeye na dada yake Jully Luzuka ndiyo waliochaguliwa na familia kuwa wasimamizi wa mali za marehemu kupitia kikao cha familia kilichofanyika Septemba 27 mwaka 2013 na kisha baadaye kuthibitishwa na mahakama bila shaka na wakati hayo yakifanyika hakuna mtu yoyote aliyejitokeza kuonyesha ameachiwa wosia na  marehemu.
 Ssarongo aliiambia mahakama hiyo kwamba mdaiwa alichukua jumla ya kiasi cha sh,milioni 8 kupitia akaunti ya marehemu kwa nyakati tofauti ikiwemo siku ambayo marehemu aliaga dunia ambayo ni Agosti 8 mwaka 2013 ambapo kwa mujibu wa taarifa walizopatiwa na benki ya CRDB zinaonyesha siku hiyo alichukua jumla ya kiasi cha sh,milioni moja.
“Tulikuwa tukijiuliza maswali mengi je kuna hela za marehemu zimeanza kutoka?je kadi zake za benki ziko wapi ,tulihoji hizi laki nne mara laki mbili mara milioni moja kupitia simu yake ya mkononi zinatoka wapi? tukasema hii hapana ndipo tukaenda benki na polisi kuwajulisha kuomba waiblock(waizuie)”Ssarongo aliiambia mahakama hiyo

Ssarongo alienda mbali zaidi na kuiambia mahakama hiyo kwamba walishangaa marehemu dada yao baada ya kufariki, Hilda Kleruu pamoja na mumewe Kleruu ghafla walijichagua kuwa wasimamizi wa mazishi ya marehemu dada yao bila kuwashirikisha ndugu ambapo Hilda alishika nafasi ya mweka hazina huku mumewe ambaye aliwahi kuwa mtumishi katika jumuiya ya Afrika Mashariki  akishika nafasi ya mwenyekiti wa kamati ya mazishi.
Hata hivyo,shahidi mwingine katika kesi  hiyo ambaye ni dada wa marehemu, Jully Luzuka, alijikuta akiangua kilio mahakamani hapo wakati akitoa ushahidi ambapo mbali na kuiomba mahakama hiyo iwatendee haki pia alisema kuwa katika kipindi chote alichougua marehemu hakuwahi kujulishwa na mdaiwa  kwamba marehemu ni mgonjwa mahututi pamoja kwamba alikuwa akimuuguza nyumbani kwake.
Shahidi mwingine ambaye ni mdogo wa marehemu,Theresa Charlote, aliiambia mahakama  kwamba anakumbuka wakati wa kuanua matanga katika kikao cha familia hakuna mtu yoyote aliyejitokeza kusema kwamba ameachiwa wosia na marehemu pamoja na tamko la kumtaka mtu yoyote aliyeachiwa wosia huo kujitokeza.
“Nakumbuka wakati wa kuanua matanga kaka Ssarongo aliuliza je kuna mtu yoyote ameachiwa wosia na marehemu lakini hakuna hata mmoja aliyejitokeza kusema ana wosia huo”Charlote aliiambia mahakama hiyo
Mara baada ya mahakama hiyo kusikiliza ushahidi huo hakimu anayesikiliza kesi hiyo aliamua kuihairisha hadi Julai 6 mwaka huu ambapo mashahidi wanne kutoka upande wa wadai watafika mahakama hapo kutoa ushahidi wao kabla ya mahakama hiyo kupanga  tarehe ya hukumu.