Wednesday, August 26, 2015

TAASISI YA BILL NA MELINDA GATE YAANGALIA UWEZEKANO WA KUSAIDIA UKUSANYAJI WA TAKWIMU ZA KILIMO NCHINI TANZANIA.


Afisa Mwandamizi anayeshughulikia Sera na maendeleo ya kilimo kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Bill na Melinda Gates Bw. Stanley Wood akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam mara baada ya kufanyika kwa kikao cha mazungumzo na viongozi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) nchini Tanzania kuangalia uwezekano wa taasisi hiyo kusaidia miradi ya ukusanyaji wa Takwimu za kilimo nchini Tanzania.Kushoto kwake ni Mratibu wa miradi wa Taasisi hiyo Bi.Bhramar Dey.
 Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt.Albina Chuwa akizungumza na waandishi wa habari Kuhusu umuhimu wa takwimu za Kilimo nchini Tanzania na mikakati ya Serikali na wadau mbalimbali katika kufanikisha upatikanaji wa Takwimu za kilimo nchini.Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi hiyo Bw.Morrice Oyuke.
 Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Prof.Innocent Ngalinda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati ya chuo anachokiongoza katika kutoa elimu kwa watakwimu wa kilimo nchini Tanzania na mpango wa chuo hicho kuimarisha shughuli za ukusanyaji wa takwimu za  kilimo kwa kutumia wataalam wanaozalishwa.
Mtakwimu mwandamizi kutoka Benki ya Dunia Bi.Elizabeth Talbert( kulia) na Meneja wa Idara ya Viwanda na Ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Joy Sawe wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kati ya viongozi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na wawakilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya Bill na Melinda Gates jijini Dar es salaam.

Picha na Veronica Kazimoto.

Na Mwandishi Wetu - Aron Msigwa 
Taasisi ya Kimataifa ya Bill na Melinda Gate imekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)kuangalia namna ya inavyoweza kusaidia  upatikanaji wa Takwimu Bora za Kilimo nchini Tanzania.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kufanyika kwa  mazungumzo hayo jijini Dar es salaam, Afisa Mwandamizi wa Taasisi hiyo anayeshughulikia Sera na maendeleo ya kilimo Bw. Stanley Wood amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali Barani Afrika na Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika  zilizopewa kipaumbele na kunufaika na taasisi hiyo.

Amesema kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kufanikisha ukusanyaji na usambazaji wa takwimu mbalimbali ambazo zimekuwa na matokeo chanya, taasisi hiyo inaangalia uwezekano wa kusaidia upatikanaji wa takwimu bora za kilimo.

" Juhudi kubwa imefanywa na Tanzania katika kufanikisha mambo mbalimbali, kwa upande wetu tumeona vipaumbele vilivyopo ili tuweze kuona namna  tunavyoweza kutoa mchango wetu kusaidia ukusanyaji wa takwimu Bora za kilimo , kikubwa ni kuendelea  kujenga ushirikiano wa kuwezesha ufanisi wa tafiti mbalimbali" Amesema.

Wood ameeleza kuwa taasisi ya Bill na Melinda Gates imekuwa ikichangia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo Barani Afrika kupitia mashirika ya kimataifa yanayohusika na utoaji wa huduma kwa umma na kuitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi chache za Bara la Afrika  zinazonufaika na miradi  hiyo.

Amesema taasisi ya Bill na Melinda Gate kwa kipindi kirefu imekuwa ikitoa kipaumbele kusaidia miradi ya afya hasa mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi, kusaidia huduma za Afya ya mama na mtoto  pamoja na kuweka mkazo  katika kuimarisha huduma za maji safi na maji Taka Barani Afrika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzania Dkt.Albina Chuwa amesema kuwa Sekta ya Kilimo imeajiri watu wengi na inachangia asilimia 27 kwenye pato la Taifa.

Amesema kutambulika kwa Takwimu za kilimo kuna umuhimu mkubwa katika uchumi wa Tanzania na kazi kubwa inayofanywa na NBS ni kuhakikisha kuwa  inakwenda na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia katika kukusanya takwimu zake.

Dkt.Chuwa ameipongeza Taasisi hiyo ya kimataifa ya Bill na Melinda Gates kutokana na jinsi  inavyosaidia kufanikisha miradi mbalimbali ya maenedeleo Barani Afrika

Amesema Chini ya Mradi wa kuimarisha na kuboresha Takwimu za kilimo ambao uko chini ya shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) Taasisi ya Bill na Melinda Gate imekuwa mstari wa mbele kuzisaidia nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania.

Amefafanua kuwa Chini ya mradi huo Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeandaa mpango mkakati wa miaka 5 wenye lengo la kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na usambazaji wa Takwimu za Kilimo.

Naye Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Prof.Innocent  Ngalinda amesema kuwa Tanzania inaendelea kujenga uwezo wake wa ndani katika kuimarisha shughuli za tafiti kwa kutumia wataalam waliopo nchini.

Amesema Tanzania kupitia chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika ambacho kiko miongoni mwa vyuo vichache barani Afrika vinavyotoa mafunzo kwa watakwimu, kinaendelea kuwajengea uwezo wataalam wa ndani ili waweze kufanya tafiti za kilimo zenye matokeo chanya katika maendeleo ya taifa na sekta ya kilimo.

No comments:

Post a Comment