Tuesday, January 16, 2018

TIMU YA USIMAMIZI WA HUDUMA YA AFYA WILAYA YA LINDI YAAGIZWA KUSIMAMIA UKARABATI WA VITUO VYA AFYA

  Baadhi ya Wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) pamoja na wataalam kutoka Mkoa wa Lindi wakikagua Ujenzi wa jengo la maabara lililojengwa katika  kituo cha afya cha Nyangamara Mkoani Lindi.
Mwonekano wa Nyumba ya Mtumishi iliyojengwa katika kituo cha afya cha Nyangamara kilichopo katika Kata ya Nyamara, wilaya ya Lindi Mkoa wa Lindi.

Angela Msimbira- OR-TAMISEMI LINDI.

Mganga Mkuu wa Mkoa  wa Lindi Bw. Ganchwele Makenge ameiagiza timu ya usimamizi wa huduma ya afya Wilaya ya Lindi kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia  ukarabati wa vituo vya afya ili vijengwe kwa ubora unaotakiwa kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.

Ameyasema hayo kwenye kikao cha pamoja kati ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kushiriana na wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Lindi mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha afya  cha  Nyangamara kilichopo kata ya Nyangamara, Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi.

Bw. Makenge amesema Kamati ya Usimamizi wa Huduma ya Afya inalojukumu kubwa la kusimamia shughuli zote za afya katika Mkoa wa Lindi hivyo hawana budi kuhakikisha Miradi inayotekelezwa na Serikali inasimamiwa kikamilifu ikiwepo Ya ukarabati wa vituo vya afya nchini.

Amesema kuwa Kamati hiyo inahitajika kusimamia wahudumu wa afya katika kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata kanuni taratibu na sheria za utumishi wa umma kwa kuwahudumia wananchi ipasavyo na kuondoa malalamiko yaliyopo  katika sekta ya afya.

Ameiagiza kamati hiyo kusimamia utendaji bora katika vituo vya afya vya Mkoa wa Lindi kwa kuwahimiza wafanyakazi kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa na kutoa huduma stahiki kwa jamii ili kuondoa kero mbalimbali ambazo wananchi wamekuwa wakizituhumu katika sekta ya afya nchini.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Lindi Bw. Bikilo Zuberi amesema kuwa mpaka sasa tayari serikali imeshatoa shilingi milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mtumishi, Ujenzi wa Maabara, Chumba cha Upasuaji, wodi ya wazazi na chumba cha kuifadhia maiti jambo ambalo litapunguza kero kwa wananchi na kuongeza huduma za afya nchini.

Ameishukuru serikali kwa kuweza kuboresha huduma za afya katika Mkoa wa Lindi kwa kutoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha afya cha Nyangamara kwa kuwa awali kituo kilikuwa na changamato ya kutokuwa na majengo ya kutosha ya kutolea huduma kwa wananchi ikiwemo ukosefu wa jengo la maabara, wodi ya wazazi, chumba cha upasuaji, maabara na chumba cha kuhifadhia maiti.

Kwa upande wake,Diwani wa Kata ya Nyangamara Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi Mhe. Ramadhani Malingumu ameipongeza Serikali ya awamu ya Tano kwa kushirikisha wananchi kwenye ujenzi wa vituo vya afya nchini jambo ambalo litasaidia katika kutunza na kusimamia vituo vya afya vilivyojengwa.

Aidha amesema wananchi wa kata hiyo wameshirikishwa katika ujenzi wa kituo hicho kwa asilimia mia jambo ambalo linaimarisha ushirikiano kati ya wananchi na serikali katika kuleta maendeleo katika jamii.

No comments: