Tuesday, October 17, 2017

NAIBU WAZIRI MGALU AITAKA TANESCO KUWAJIBIKA IPASAVYO KWA WATEJA


Na Veronica Simba - Dodoma

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linawajibika ipasavyo kwa wateja wake ili kukuza imani yao kwa shirika hilo.

Akizungumza na viongozi mbalimbali wa shirika hilo wa Mkoa wa Dodoma, leo Oktoba 17, 2017, Naibu Waziri amebainisha kuwa mojawapo ya njia muhimu ya uwajibikaji kwa jamii ni kupitia utoaji taarifa kwa wateja kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu.

“Mathalani, kunapokuwa na katizo la umeme, wateja walioko eneo husika wanapaswa kutaarifiwa kabla ya katizo hilo ili wajipange,” alisisitiza.

Ameeleza njia nyingine ya shirika hilo kuwajibika kwa jamii, kuwa ni kushughulikia matatizo mbalimbali ya wateja wao kwa wakati na kuachana na utaratibu wa kufanya kazi kwa mazoea.

Kwa upande wake, akiwasilisha taarifa ya kazi ya ofisi yake kwa Naibu Waziri, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Zakayo Temu, ametaja baadhi ya mafanikio ambayo Ofisi hiyo imepata kuwa ni pamoja na kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 100 pamoja na kubadilisha mita ndogo zote, zilizokuwa zikitumika zamani na kufunga LUKU.

Naibu Waziri Mgalu, ametembelea Ofisi za TANESCO Dodoma kwa lengo la kuzungumza na wafanyakazi na kujitambulisha kwao.


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma (hawapo pichani), alipowatembelea kwa lengo la kujitambulisha kwao na kueleza vipaumbele vyake vya kazi.


Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, Zakayo Temu (kushoto), akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi yake kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia), wakati Naibu Waziri alipotembelea Ofisi hiyo na kuzungumza na viongozi.


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (aliyesimama) akizungumza na viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, alipotembelea Ofisi hizo leo Oktoba 17, 2017.


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akisaini Kitabu cha Wageni katika Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dodoma, alipotembelea Ofisi hizo na kuzungumza na viongozi wake (hawapo pichani). Kushoto ni Meneja wa Shirika hilo Mkoa wa Dodoma, Zakayo Temu.



Baadhi ya viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, wakimpokea Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye nguo nyeusi) alipowasili katika Ofisi hizo kuzungumza na viongozi wake.








No comments: