Wednesday, September 20, 2017

WAKULIMA WILAYANI HAI WASIFU MRADI WA N2AFRICA KWA MBEGU BORA ZA MAZAO YA MAHARAGE

Na Mathias Canal, Kilimanjaro

Wakulima wadogo katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wameipongeza Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mazao ya kilimo ya (IITA) yenye makao makuu yake nchini Nigeria kwa teknolojia walizoanzisha za kutafiti wadudu waharibifu na aina mpya ya mbegu za maharagwe aina ya Jesca, Lyamungo 90 na Uyole njano wanazozitoa kwa wakulima.

Wakulima hao wamesema kuwa mbegu hizo zimepelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya mbogamboga jamii ya mikunde huku katika Wilaya hiyo uzalishaji wa maharagwe ukiwa ndio ukombozi kwa wakulima kufuatia mafunzo na mbinu bora za kisasa wanazopatiwa na wataalamu wa (IITA) kupitia mradi wa N2AFRICA.

Wakizungumza kwa niaba ya wakulima wengine 30 katika Wilaya ya Hai Wanufaika wa mradi wa N2AFRICA Hashim Abdallah mkazi wa kitongoji cha Landi na Lucy David mkazi wa Kitongoji cha Madukani Kata ya weruweru wanasema kabla ya mradi huo walikuwa wanapanda kilo 60 za mbegu katika heka moja na mavuno ya gunia 3 mpaka 5 ambapo hivi sasa matarajio ya mavuno yao yataongezeka maradufu kwani wanatumia kilo 30 za mbegu kwenye heka moja na kuvuna gunia 10 mpaka 15.

Wakulima hao wameomba mafunzo ya kutengeneza mbegu bora za kilimo cha mbogamboga na mafunzo ya jinsi ya kuhifadhi mbegu hizo ili waweze kuendeleza uzalishaji wao wenyewe badala ya kuomba tena mbegu kutoka katika mradi huo wa N2AFRICA.

Pia wameiomba Taasisi ya (IITA) kupitia mradi wake wa N2AFRICA unaojihusisha na usambazaji wa teknolojia ya mazao jamii ya mikunde kuwasaidia kutafuta masoko ili kuboresha zaidi ufanisi wa mauzo yao mara baada ya mavuno.

Wakulima hao walisema kuwa Wakulima wadogo nchini Tanzania huzalisha asimia 70 ya chakula ingawa karibu nusu yao hawazalishi chakula cha kutosha kwa ajili ya mauzo.

Aidha, walisema Wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa teknolojia ya kilimo cha kisasa, kukosa uwezo wa kujipatia pembejeo bora na kukosa huduma za kiufundi za ughani zinazoweza kuwasidia kukuza kilimo pamoja na ukosefu wa mafunzo jambo ambalo kwa sasa wameanza kunufaika nalo kupitia mradi wa N2AFRICA.

Kwa upande wake Afisa Kilimo (Mazao) Halmashauri ya Wilaya ya Hai Bi Matrida R. Massawe alisema kuwa upatikanaji mbegu bora za maharagwe zilizotolewa na mradi wa N2AFRICA zimekuwa na tija kubwa kwa wakulima kwani mavuno yameongezeka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na msimu wa mavuno uliopita.

Alisema kuwa Mradi huo umetatua changamoto ya uduni wa kilimo kwa wakulima kwani walikuwa wakilima pasina kufuata mbinu bora za kilimo hivyo upatikanaji huo wa mbegu bora na mbinu za uongezaji rutuba kwenye udongo umekuwa mkombozi kwa wakulima kwani wanazalisha na kuuza mazao yao kwa faida kubwa.

Massawe aliwahimiza wakulima kuendelea kujifunza kanuni bora za kilimo na kuzingatia ushauri wa kitaalamu unaotolewa na mradi wa N2AFRICA katika uzalishaji wa mazao kwani kilimo kisichozingatia utaalamu na kanuni bora za kilimo hakiwezi kuwa na tija katika jamii.

Hata hivyo Mwaka 2017 katika msimu wa kilimo mafunzo yameendelea kutolewa na Mradi wa N2AFRICA kwa wakulima wa maharagwe ambapo wakulima 30 wamepata mafunzo ya mbegu daraja la kuazimiwa.

Aliwasihi wakulima kutumia fursa hiyo kupitia mradi wa N2AFRICA ili kuweza kuboresha kilimo cha maharagwe ambapo pia amewapongeza wadau hao wa kilimo wa N2AFRICA na kuwaomba kuendeleza kilimo hicho katika maeneo yote ya Wilaya ya Hai ili kunufaisha wakulima wengi zaidi.

Mradi wa N2AFRICA unaendeshwa na na Taasisi ya Kimataifa ya kilimo cha Kitropiki katika ukanda wa joto makao makuu yake ni nchini Nigeria chini ya ufadhili wa Bill na Melinda Gates na kuongozwa na Chuo Kikuu cha Wagenigen cha Uholanzi.


Lucy David akielezea jinsi alivyonufaika Mbegu za maharagwe zilizotolewa na Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mazao ya kilimo ya (IITA) kupitia mradi wa N2AFRICA



Mkulima wa zao la maharagwe aliyenufaika na mbegu zilizotolewa na Mradi wa N2AFRICA Katika Kijiji cha Kikavu Chini, Kata ya Weruweru Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Hashim Abdallah akiwa shambani kuendelea na shughuli zake za kusafisha majani katika shamba lake kabla ya mavuno.




Wataalamu Kutoka Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mazao ya kilimo ya (IITA) wakikagua shamba la Mkulima wa zao la maharagwe aliyenufaika na mbegu zilizotolewa na Mradi wa N2AFRICA Katika Kijiji cha Kikavu Chini, Kata ya Weruweru Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Hashim Abdallah.



Muonekano wa mazao ya maharagwe yakiwa shambani kabla ya mavuno




Wataalamu Kutoka Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mazao ya kilimo ya (IITA) walipotembelea ofisi ya Afisa Kilimo, Umwagiliaji na ushiriki wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Ndg David Lekei





Afisa kilimo (Mazao) wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Bi Matilda Massawe akielezea jinsi wakulima walivyonufaika na mradi wa N2AFRICA katika Wilaya ya Hiyo.



Muonekano wa shamba la maharagwe lililolimwa kwa kufuata mbinu bora na za kisasa za kilimo



Muonekano wa shamba la maharagwe lililolimwa bila kufuata mbinu bora za kilimo



Hashim Abdallah akielezea jinsi alivyonufaika Mbegu za maharagwe zilizotolewa na Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mazao ya kilimo ya (IITA) kupitia mradi wa N2AFRICA

Wataalamu Kutoka Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mazao ya kilimo ya (IITA) wakikagua shamba la Mkulima wa zao la maharagwe aliyenufaika na mbegu zilizotolewa na Mradi wa N2AFRICA Katika Kijiji cha Kikavu Chini, Kata ya Weruweru Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Hashim Abdallah.
Mkulima wa zao la maharagwe aliyenufaika na mbegu zilizotolewa na Mradi wa N2AFRICA Katika Kijiji cha Kikavu Chini, Kata ya Weruweru Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Mwantumu Abdillah akiwa shambani kuendelea na shughuli zake za kusafisha majani katika shamba kabla ya mavuno.
Mkulima wa zao la maharagwe Lucy David Katika Kitongoji cha Madukani, Kata ya Weruweru Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro akielezea mafanikio aliyoyapata kutokana na Mradi wa N2AFRICA, Wengine ni Wataalamu Kutoka Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mazao ya kilimo ya (IITA) walipomtembelea shambani kwake.

No comments: