Thursday, September 21, 2017

WAKAZI WA ARUSHA WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO KWA MKANDARASI

 Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya Cheil Engineering Bw. Shin Soo akimueleza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati) maendeleo ya ujenzi wa barabara ya mchepuo (Arusha bypass), inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 42.4. Kushoto ni Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha Mhandisi Johnny Kalupale.
 Mafundi wa Kampuni ya M/S Hanil-Jiangsu J/V wakiendelea na ujenzi wa moja kati ya madaraja makubwa saba yanayojengwa katika barabara ya mchepuo (Arusha bypass), inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 42.4.
 Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Arusha Mhandisi Johnny Kalupale (kulia) akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) hatua mbalimbali za maendeleo ya ujenzi wa barabara ya mchepuo (Arusha bypass), wakati Waziri huyo alipoikagua, mkoani Arusha.
 Moja kati ya madaraja saba yanayojengwa katika barabara ya mchepuo (Arusha bypass), inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 42.4, jijini Arusha.
 Tingatinga likiendelea na kazi ya ujenzi wa awali ya madaraja katika barabara ya mchepuo (Arusha bypass), inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 42.4, jijini Arusha.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya Cheil Engineering Bw. Shin Soo (katikati)alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya mchepuo (Arusha bypass), inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 42.4 jijini Arusha.Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ametoa wito kwa wakazi wa Arusha kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Hanil-Jiangsu J/V ili kuweza kukamilisha kwa wakati ujenzi wa barabara ya mchepuo (Arusha bypass), inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 42.4.

Akikagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo mkoani humo, Profesa Mbarawa amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza msongamano wa magari katikati ya jiji hilo na hivyo kuvutia watalii na kukuza uchumi wa mkoa.

"Kukamilika kwa barabara hii ya Arusha bypass kutapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano kwani magari makubwa ya mizigo yatatumia mchepuo huu na kurahisisha huduma za usafirishaji jijini Arusha", amesema Waziri Mbarawa.Ameongeza kuwa Wizara yake itasimamia kwa ukaribu ujenzi wa barabara hiyo ili ikamilike kwa wakati uliopangwa na viwango vinavyostahili vilivyokubalika.

Aidha, Prof. Mbarawa ameupongeza Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani humo kwa usimamizi mzuri wa barabara ya Sakina-Tengeru KM 14.1 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na kusisitiza kuitunza barabara hiyo ili idumu kwa muda uliopangwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Barabara wa Wizara hiyo (Sekta ya Ujenzi), Eng. Ven Ndyamukama, amesema Wizara kwa kushirikiana na TANROADS itaendelea kuhakikisha barabara na madaraja yote nchini yanajengwa kwa viwango vilivyopo kwenye usanifu wa kina (Detail design), na thamani ya fedha inapatikana.

Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha Mhandisi Johnny Kalupale, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuendelea kumsimamia mkandarasi huyo ili akamilishe mradi kwa wakati kama walivyokamilisha ujenzi wa barabara ya Sakina-Tengeru KM 14.1 na kwa ubora unaostahili.

Mhandisi Kalupale, ameeleza changamoto zinazoikabili barabara hiyo kuwa ni wingi wa  udongo wa tifutifu na  mfinyanzi na hivyo kulazimu Usanifu wa kina wa barabara hiyo kurudiwa upya.

Ujenzi wa Barabara ya Arusha bypass unatarajiwa kutumia zaidi ya shilingi Bilioni 67 ikiwa ni ushirikiano wa fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania na ujenzi wake utahusisha madaraja makubwa 7, maboksi kalvari 55 na madaraja ya bomba 55.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments: