Thursday, September 21, 2017

TACAIDS: UKIMWI BADO NI CHANGAMOTO

Kaimu Mkrugenzi Mkuu wa TACAIDS Bw.Jumanne Issango akieleza jambo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati wa mkutano kuhusu changamoto na mafanikio katika kupambana na virusi vya ukimwi nchini kulia ni Kaimu Mkurugenzi Muitiko wa kitaifa wa TACAIDS Bi.Audrey Njelekela mkutano uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za TACAIDS leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na Paschal Dotto-MAELEZO) 

Na Fatma Salum – MAELEZO
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imeendelea kuiasa jamii kuhusu kubadili tabia ili kuepuka maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwani ugonjwa huo bado ni janga kwenye nchi yetu.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo Bw.Jumanne Issango alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio na changamoto za tume tangu ilipoanza kutekeleza majukumu yake.
“UKIMWI bado ni changamoto katika maendeleo ya Taifa letu na umeendelea kuathiri kila sekta, kila imani, matajiri na masikini nchini kote hivyo ni wajibu wa kila mmoja kujitathmini mwenendo wake na kuacha tabia hatarishi ambazo zinachangia kuongeza maambukizi ikiwemo uasherati, ngono zembe, ulevi na kadhalika,” alisema Issango.
Alieleza kuwa kwa miaka ya karibuni hali ya maambukizi ya UKIMWI imeendelea kupungua ingawa kuna tofauti kwenye mikoa, wilaya na makundi ya kijamii.Issango alibainisha kuwa kiwango cha maambukizi Tanzania Bara ni asilimia 5.3 na takwimu hizo ni kutokana na Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI mwaka 2012.
Kwa mujibu wa utafiti huo wanawake walioambukizwa ni asilimia 6.2 na wanaume ni asilimia 3.8 ambapo idadi ya Watanzania wanaokadiriwa kuishi na VVU ni zaidi ya milioni 1.5.“Mikoa inayoongoza kuwa na maambukizi makubwa ni Njombe asilimia 14.8, Mbeya asilimia 9 na mikoa yenye maambukizi ya chini zaidi ni Manyara asilimia 1.5, Tanga asilimia 2.4 na Dodoma asilimia 2.9,” alifafanua Issango.
Aidha alisema kuwa licha ya maambukizi mapya kupungua kwenye jamii bado kiwango cha maambukizi kwenye makundi maalum kimeendelea kuongezeka.Akitaja makundi hayo Issango alisema kuwa ni pamoja na madereva wa magari ya masafa marefu, wachimba madini, wavuvi, wafungwa na wale wanaofanya biashara ya ngono.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Muitikio wa Kitaifa kutoka Tume hiyo Bi. Audrey Njelekela alisema Serikali kupitia TACAIDS inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kukabiliana na janga hilo ikiwemo kuandaa na kutekeleza mikakati madhubuti itakayosaidia kupunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa.
“Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI 2013/14 – 2017/18 unalenga ifikapo 2018 kiwango cha maambukizi kishuke kufikia asilimia 0.16 ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo utafiti unaonesha maambukizi ni asilimia 0.32,” alisema Njelekela.
Alitaja hatua nyingine zinazochukuliwa na tume hiyo ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma hasa kwa vijana, wanawake wajawazito na makundi maalum ikiwemo kujenga Vituo vya Maarifa vinavyotoa huduma za VVU/UKIMWI kwa madereva wa magari ya masafa marefu. 
Aliongeza kuwa juhudu za Serikali kutoa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) zimesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo ambapo kwa sasa wanaotumia dawa hizo ni zaidi ya watu laki 8.
Pia Serikali imeanzisha Mfuko wa Udhamini wa Shughuli za Kudhibiti UKIMWI kwa ajili ya kusaidia kununua dawa, kutoa elimu ya UKIMWI, kupima, kufanya tafiti na kutoa elimu ya uzazi kwa vijana.
TACAIDS ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 22 ya mwaka 2001 kwa lengo la kutoa uongozi wa kimkakati, uratibu na kuimarisha juhudi za wadau wote wanaojishughulisha na kudhibiti UKIMWI nchini.

No comments: