Sunday, September 24, 2017

SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO YA KODI SHULE BINAFSI

Benny Mwaipaja, WFM, Pwani

SERIKALI imeahidi kuyafanyiakazi malalamiko ya wamiliki wa shule za binafsi nchini kuhusu kodi mbalimbali wanazotozwa kwa kuwa Serikali inathamini mchango mkubwa wa taasisi binafsi za elimu katika mapambano dhidi ya adui ujinga.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati wa sherehe za mahafali ya kumi ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Baobab, iliyoko Mapinga, Wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Dokta Kijaji amesema kuwa tayari Serikali imeondoa baadhi ya kodi kwa shule hizo ikiwemo kodi ya mabango, Usalama mahali pa kazi-OSHA, Ada ya zimamoto, na kwamba kikosi kazi kilichoundwa na Serikali kupitia upya kodi zingine zinazoonekana kuwa kikwazo katika utoaji wa elimu, kinaendelea na kazi na matokeo yake yataonekana hivi karibuni.

“Niko kwenye kikosikazi kinachoshughulikia changamoto za kodi kwenye shule za watu binafsi ninaamini suluhisho litapatikana kutokana na Serikali kuthamini mchango wenu mkubwa katika kuwapatia vijana wetu elimu” alisema Dkt. Kijaji

Alieleza kuwa katika Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2017/2018, suala hilo litazingatiwa na kuwataka wamiliki wa shule binafsi nchini kuwa watulivu wakati jambo hilo linafanyiwakazi tena kwa umakini mkubwa.

Awali Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Baobab, Bw. Halfan Swai, pamoja na kuiomba Serikali ifute kodi mbalimbali wanazotozwa kwa kuwa hawafanyibiashara bali wanaisaidia Serikali kutoa huduma kwa jamii, ameomba pia isaidie  kuangalia viwango vya riba vinavyotozwa na taasisi za fedha nchini kwa kuwa zinawawekeka katika mazingira magumu wanapohitaji mikopo ya kuendeleza shule zao.

Wanafunzi 149, (wavulana 14 na wasichana 135)  wa Shule hiyo wanaotarajiwa kuhitimu masomo yao ya kidato cha nne hivi karibuni, wameahidi kufanya vizuri katika mitihani yao kwa kuwa wameandaliwa vizuri na walimu waliobobea katika ufundishaji pamoja na mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia shuleni hapo.

Dokta Ashatu Kijaji, mbali na kuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, yeye na familia yake wameshuhudia mtoto wao Samira, akiagwa wakati wa mahafali hayo yaliyohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wazazi, ndugu na jamaa wa wanafunzi hao.
Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (Katikati), wakiimba Wimbo wa Taifa wakati wa Mahafali ya 10 ya Kidato cha Nne ya Shule mchanganyiko ya Sekondari Baobab, iliyoko eneo la Mapinga, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ambapo wanafunzi 149 wanatarajiwa kuhitimu masomo yao majuma machache yajayo.
Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Baobab Bw. Halfan Swai, akiiomba Serikali iangalie changamoto ya riba ya mikopo inayotolewa an taasisi za fedha pamoja na kuondoa kodi mbalimbali zinazotozwa shule binafsi kwakuwa taasisi hizo zinaisaidia Serikali kutoa huduma kwa wananchi wake, wakati wa Mahafali ya 10 ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Baobab, wakionyesha ishara ya umoja, upendo na mshikamano wakati wakiimba wimbo wa kuwaaga wanafunzi wenzao wakati wa Mahafali ya 10 ya Kidato cha Nne ya shule yao.
Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 10 ya Shule ya Sekondari Baobab, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akihutubia Jumuiya ya Shule ya Sekondari Baobab, wakati wa mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaotarajiwa kufanya mitihani yao siku chache zijazo.
Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 10 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Baobab, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akimkabidhi zawadi mmoja wa wanafunzi mwenye ulemavu aliyefanya vizuri katika baadhi ya masomo wakati wa sherehe ya kuwaaga, iliyofanyika shuleni hapo.
Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 10 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Baobab, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), (Katikati), akikabidhi keki kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Baobab, iliyoko Mapinga, Bagamoyo, mkoani Pwani, ikiwa ni alama ya kusherehekea siku yao ya kuagwa shuleni hapo.
Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 10 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Baobab, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akiwa katika Picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaotarajiwa kuhitimu masomo yao hivi karibuni, wakati wa sherehe ya kuwaaga shuleni hapo.
Familia ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akiwa na mumewe Dkt. Kachwamba, wakimpongeza binti yao Samira anayetarajiwa kuhitimu masomo yake ya Kidato cha Nne katika Shule ya Seondari Baobab, iliyoko Mapinga, Bagamoyo mkoani Pwani ambapo Naibu Waziri alikuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali hayo ya 10 ya Kidato cha Nne. Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango.

No comments: