Tuesday, September 26, 2017

NAIBU WAZIRI WAMBURA AHITIMISHA MASHINDANO YA FLATEI JIMBO CUP MBULU

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Mbulu

Halmashauri zote nchini zimetakiwa kutenga maeneo ya michezo wakati wa kupanga mipango miji kwa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yao.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura alipokuwa akifunga fainali ya mashindano ya Jimbo Cup inayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Mhe. Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay iliyochezwa katika eneo la kata ya Dongobesh Wilaya ya Mbulu Mkoani wa Manyara.

“Natoa wito kwa Halmashauri zote ikiwemo halmashauri yenu ya wilaya ya Mbulu wakati wa kupanga matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya mipango miji mkumbuke kutenga maeneo ya michezo, Baraza la Michezo la Taifa litatoa mafunzo ya michezo na utaalam” alisema Naibu Waziri Wambura.

Akikabidhi zawadi za washindi katika mashindano hayo ambao ni timu ya Qatajiring kutoka kijiji cha tumati ambao ni mshindi wa kwanza na timu ya Zahanati kutoka kijiji cha Diomati mshindi wa pili, Naibu Waziri Wambura amewahimiza wachezaji na wananchi kuthamini michezo kwa kuwa ni ajira, inaleta umoja na mshikamano miongoni mwa jamii.

Dakika 90 za fainali hizo ziliisha kwa timu zote kufungana bao 2-2 na hatimaye timu ya Qatajiring iliibuka kidedea kwa ifunga timu ya Zahanati kwa penati 4-1.Akionesha umuhimu na umahiri wa wilaya ya Mbulu katika michezo, Naibu Waziri Wambura amesema wilaya hiyo imekuwa kitovu cha wanamichezo bora hasa mchezo wa riadha ambao wameiletea sifa Tanzania ndani na nje ya nchi.

Wanamichezo hao ni pamoja na John Stephen Akhwari nguli mchezo wa riadha aliyeweka historia ya kimataifa aliyewahi kusema “Nchi yangu haikunituma kuanza mashindano, ilinituma kumaliza mashindano”Filbert Bai na wanaridha wengine.

Aidha, Naibu Waziri Wambura amewashauri waandaaji wa mashindano hayo washirikishe pia mchezo wa netiboli ili kuwaendeleza watoto wa kike katika mchezo huo.Kwa upande wake mdhamini wa mashindano hayo Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay amesema kuwa alivutiwa kuanzisha mashindano hayo ili vijana wajihusishe na michezo na kuboresha na kuendeleza afya zao na kuachana na masuala yanayoweza kupoteza maisha yao na nguvu kazi ya taifa

Mashindano hayo yalishirikisha timu 24 kutoka Mbulu Vijijini tangu kuanzishwa kwa mwezi Julai mwaka huu na kufikia kilele Septemba 25 ambapo fainali ilichezwa katika viwanja vya Dongobesh na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali na mashabiki lukuki kutoka maeneo yote ya halmashauri hiyo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura akiongea na Wananchi wakati wa kuhitimisha fainali za Flatei Jimbo Cup wilayani Mbulu.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura (kulia) akimkabidhi nahodha wa timu ya Qatajiring zawadi mbalimbali mara baada ya kuibuka kidedea baada ya kuifunga timu ya Zahanati wakati wa fainali za Flatei Jimbo Cup wilayani Mbulu. Katikati ni mdhamini wa mashindano hayo Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay.
Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay akiongea na Wananchi wakati wa kuhitimisha fainali za Flatei Jimbo Cup wilayani Mbulu.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura (aliyevaa miwani) akikagua timu za Qatajiring na timu ya Zahanati wakati wa fainali za Flatei Jimbo Cup wilayani Mbulu. Katikati ni mdhamini wa mashindano hayo Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay.
Baadhi ya mashabiki wakifuatilia fainali ya Flatei Jimbo Cup wilayani Mbulu kati ya timu za Qatajiring na timu Zahanati iliyochezwa katika kiwanja cha Dongobesh.Picha na Eleuteri Mangi,WHUSM, Mbulu

No comments: