Sunday, August 6, 2017

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAFANYA MABADILIKO KWA BAADHI YA WATENDAJI WAKE

KATIKA kuongeza ufanisi kwenye utendaji, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amefanya mabadiliko ya baadhi ya watendaji kwenye wizara na idara zilizo chini ya wizara hiyo.

Mabadiliko hayo madogo yamegusa Chuo Cha Taifa cha Utalii, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) na Idara ya Utalii kwenye makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Akitangaza mabadiliko hayo mwishoni mwa wiki mjini Dodoma, Waziri Maghembe alimtaja Deogratius Mdamu kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Zahoro Kimwaga TAWA kukaimu nafasi ya Mkuu wa Shughuli za Utaliiwa Picha.

Profesa Maghembe alisema pia amemteua Phillip Chitaunga, kuwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Maendeleo ya Utalii kwenye makao makuu ya wizara, ili kujaza nafasi iliyoachwa na Uzeeli Kiangi aliyestaafu utumishi kwa mujibu wa sheria.

"Kwenye Chuo chetu cha Taifa Utalii, ninamteua Dk. Shogo Mlozi kuwa Kaimu Mkuu wa Chuo ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Utalii na Ukarimu kwenye Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)," alisema.

Pamoja na hao, Waziri huyo alimtaja Stephen Madenge kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chuo cha Taifa cha Utalii ambaye anabadilishana nafasi na Martina Hagwet, anayekwenda kushika wadhifa wa Kaimu Meneja wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Kampasi ya Temeke.

Aidha, Waziri Maghembe alisema kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori, amemteua Dk. James Wakibara kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu nafasi iliyoachwa wazi na Martin Loibooki anayerejeshwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), kupangiwa kazi nyingine.

Uteuzi zaidi kwenye mamlaka hiyo, umefanywa kwa Imani Nkuwi, kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Biashara na Utalii kuchukua nafasi ya Mzamilu Kaita, anayerejeshwa Wizarani kupangiwa kazi nyingine.

"Wa mwisho kwenye mabadiliko haya ni Mabula Misungwi, tunayemteua kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Himasheria yaani Protection ili kuchukua nafasi ya Faustine Masalu atakayepangiwa kazi nyingine hapo baadaye," alisema.

Mabadiliko hayo alisema ni ya kawaida na kwamba utekelezaji wake unaanza mara moja ambapo Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi aliyathibitisha kwa barua rasmi iliyoandikwa Agosti 3, mwaka huu.

No comments: