Thursday, June 29, 2017

MAKALA YA MATUMIZI ENDELEVU YA ARDHI YATAEPUSHA JANGWA NA UKAME NCHINI

Jovina Bujulu-MAELEZO.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 193 zilizosaini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na kuenea hali ya jangwa duniani (UNCCD). Mkataba huu unalenga kupambana na tatizo la uharibifu wa ardhi katika maeneo yenye ukame na kufanya juhudi za kuyahifadhi.

Mkataba huu ni muhimu kwa nchi yetu ambayo uchumi wake unategemea ardhi kwa ajili ya kilimo ambacho kinachochea maendeleo na ajira kwa wananchi walio wengi.

Hivi karibuni dunia iliadhimisha siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ambayo ilikiongozwa na kauli mbiu isemayo “Ardhi ni makazi yetu tuitunze kwa manufaa ya baadaye”. Kauli mbiu hii inahamasisha jamii kutunza ardhi kwa kuwa ndiyo makazi yetu.

Akiongea hivi karibuni mjini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba alisema kuwa kauli mbiu hii inahimiza jamii kuongeza juhudi za kutunza ardhi, na kuzingatia maendeleo endelevu ya rasilimali tulizo nazo kwa ajili ya maendeleo ya sasa na kwa vizazi vijavyo.

Madhumuni ya kuadhimisha siku hii ni pamoja na kuongeza uelewa miongoni mwa jamii na kujua athari za jangwa na ukame katika maisha ya kila siku ya binadamu na jinsi ya kuthibiti hali hiyo.

“Malengo hayo yanadhihirisha umuhimu wa utunzaji wa ardhi na udongo kwa matumizi endelevu hasa kwa ajili ya kilimo, mifugo, na huduma nyingine kama utalii wa wanyama pori na uwindaji.” Aliongeza Mhe. Makamba.

Umuhimu wa kutunza ardhi pia unaonekana katika kuhifadhi vyanzo vya maji na miti ili kuwezesha shughuli za uzalishaji mali na uwekezaji katika viwanda ili kuleta ustawi wa jamii.

Hali ya uharibifu wa ardhi na vyanzo vya maji imeongezeka kwa kasi na kuongeza ukame, upungufu wa mazao ya kilimo na kuongeza umaskini miongoni mwa jamii.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 61 ya eneo la nchi yetu liko hatarini kugeuka jangwa. Hali hii ni tishio kubwa kwa maendeleo ya nchi kwani uwepo wa jangwa ni kikwazo kikubwa kinachosababisha kushuka kwa uchumi, hasa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa kwa kiasi kikubwa na hatari ya kuenea kwa jangwa na ukame. Waziri Makamba aliitaja mikoa mbayo iko katika hatari kubwa ya kugeuka jangwa kuwa ni pamoja na Singida, Dodoma, Shinyanga, Geita, Simiyu, Manyara na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Arusha.

Madhara ambayo yameanza kuonekana ni pamoja na kukauka kwa vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali, vifo vya mifugo na wanyama pori, upungufu wa mvua kutokana na kukata miti holela, kupungua kwa maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo.

Aidha, jangwa na ukame vinasababisha tabaka la juu la ardhi kuwa wazi na hivyo kusababisha mmomonyoko wa udongo, hali ambayo inapunguza rutuba na hivyo kupunguza uzalishaji wa mazao kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na kuwepo kwa hatari ya kuwepo kwa jangwa na ukame, Serikali ya Awamu ya Tano inafanya jitihada kubwa za kukabiliana na janga hilo kwa kusimamia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/2017 hadi 2020/2021 ili kusimamia maliasili, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Malengo ya mpango huu ni pamoja na kuhakikisha kuwa mchango wa pato la taifa unaotokana na matumizi endelevu ya misitu, maji, na rasilimali za bahari linafikia asilimia 10, ongezeko la eneo la misitu kwa hekta 130,000, upandaji wa miti 100,000,000 kwa nchi nzima ifikapo 2020.

Hatua za kimkakati za mpango huo ni pamoja na kulinda, kurejesha na kuhamasisha matumizi endelevu ya mifumo ya mazingira ya nchi kavu na misitu ili kukabiliana na jangwa na shughuli zinazosababisha jangwa.

Mikakati mingine pamoja na kutekeleza Mpango Kazi wa Kitaifa wa kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame wa mwaka 2014 hadi 2018 ambao unahusisha programu za upandaji miti, kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi, kulima kilimo kinachofuata njia za kisasa, ufugaji bora na wa kisasa na kuanzisha maeneo ya hifadhi na kulinda yaliyopo.

Kwa upande wa ushiriki wa wananchi katika kukabiliana na hali hii, mkakati huu utatekelezwa kila kijiji, kitongoji, mtaa, kaya, na taasisi, na utamshirikisha kila mwananchi.

Lengo ni kuhakikisha nchi yetu inakuwa ya kijani ikiwa ni pamoja na kurekebisha changamoto zilizojitokeza katika mikakati na kampeni zilizopita, pamoja na motisha na ushiriki wa sekta binafsi. Mkakati huu umeanza kutekelezwa katika baadhi ya maeneo.

Serikali pia imeweka mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwaelekeza shughuli nyingine za uzalishaji mali ili waepuke utegemezi wa maliasili ya misitu ambapo programu ya upandaji miti ya mwaka 2016 hadi 2021 inalenga kupanda miti zaidi ya milioni 280 kila mwaka hasa katika maeneo yaliyo katika hatari zaidi ya kugeuka jangwa.

Mikakati yote hii itafanikiwa endapo kila mwananchi atakuwa sehemu ya kupunguza kuenea kwa tatizo hilo kwa kuzingatia matumizi endelevu ya ardhi.

Matumizi hayo ni pamoja na kupanda na kutunza miti ambako kutasaidia ulinganifu katika shughuli za kilimo, ufugaji, misitu, uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuhakikisha mifumo ya ikolijia inategemeana na haiingiliwi.

Ni wakati sasa muafaka kwa wananchi kuunga mkono wito wa Mhe. Makamba kushiriki kikamilifu katika kutekeleza kauli mbiu ya mwaka 2017 ya siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ili kutunza ardhi kwa vizazi vijavyo.

No comments: