Wednesday, May 24, 2017

Shule ya Lucky Vicent yang’ara Juma la Elimu jijini Arusha


Nteghenjwa Hosseah - Arusha

Shule ya msingi Lucky Vicent yaibuka na mshindi wa Jumla Kitaaluma kwa kushika nafasi ya kwanza Kimkoa katika maadimisho ya Juma la Elimu yaliyoadhimishwa katika viwanja vya Arusha School jijini hapa.
Shule hiyo iliyopata na msiba wa wanafunzi 32, walimu 2 pamoja na dereva  kutokana na ajali ya Coastal hivi karibuni imefanya vizur katika mitihani ya darasa la saba iliyofanyika mwaka 2016 katika ngazi ya Mkoa na Wilaya hivyo kujinyakulia Kombe pamoja na Cheti.
Akipoka zawadi hizo za Ushindi Mwel Mkuu wa Shule hiyo Bw. Innocent Mushi alisema wanafarijika kupata zawadi hizo ingawa bado simanzi na majonzi yametanda shuleni kwa wanafunzi pamoja na uongozi wa shule hiyo.
“Tunamshkuru Mungu kwa Shule yetu kufanya vizuri na  hizi ni jitihada za walimu kufanya kazi kwa bidii  pamoja na wafunzi kuzingatia yale wanayofundishwa na walimu wao hakika zawadi hizi zimetupata faraja katika kipindi hiki kigumu tunachopitia.” Alisema Mwl. Mushi.
Katibu Tawala wa Jiji la Arusha Ndg. David Mwakiposa ambaye ndiye  mgeni rasmi katika maadhimisho hayo  amepongeza shule zote zilizofanya vizuri Kitaaluma kwa mwaka uliopita  ikiwa ni pamoja na Walimu na Wanafunzi na pia alitembelea miradi ya kiubunifu inayoendeleza sanaa za wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kupata ajira hapo baadae.
Mwakiposa alisema “Taifa lolote haliwezi kuendelea pasipo wananchi wake kuelimika hivyo nichukue fursa hii kuweka msisitizo kwa walimu na viongozi mbalimbali katika sekta ya  elimu kufundisha wanafunzi kwa weledi  na kutoa elimu bora ili malengo mbalimbali ya kitaaluma yaweze kufikiwa”
Pia aliongeza kwa kusema kuwa amefurahishwa na kuhamasishwa sana katika maonyesho yaliyofanywa na wanafunzi hasa maonyesho ya mafunzo ya kitaaluma,  kisayansi na ufundi stadi na kusisitiza kuwa endapo watashirikisha jamii taaluma  walizofundishwa  na walimu wao na wakiwezeshwa na wadau wa elimu basi Tanzania yetu itapiga hatua kubwa hasa katika suala zima la uchumi wa viwanda.
Miongoni mwa maonyesho yaliyoweza kuonyeshwa  na wanafunzi wa kawaida na  wenye ulemavu ikiwemo viziwi, matatizo ya akili na wasioona ni pamoja na utaalamu wa kusindika maparachichi na kutengeneza  mafuta  yanayoweza kutumika kama kilainishi katika karakana za vyuma vyenye kutu na dawa  ya ngozi, ujuzi wa kutengeneza dawa ya kung’arishia viatu pamoja na  ushonaji wa nguo na vitambaa vya kupambia majumbani.
Pia wanafunzi walionyesha namna ya  kuzalisha umeme kwa kutumia nyaya, utengenezaji wa mapambo kwa kutumia shanga zinazotokana na makaratasi na watoto wenye ulemavu wa kusikia wanavyoweza kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)katika kujifunza mambo mbali mbali.

Maadhimisho ya Juma la Elimu hufanyika kila mwaka lengo ikiwa ni kutathimini ubora wa Elimu, kuwatambua waliofanya vizuri kitaaluma na kuonyesha kwa vitendo ubunifu wa wanafunzi na sanaa inavyokua katika sekta ya Elimu. 
Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha Ndg. David Mwakiposa akizungumza wakati wa maadhimisho ya Juma la Elimu katika Jiji la Arusha.

 Kaimu Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Bi. Eunice Tondi akisoma taarifa katika maadimisho ya juma la Elimu yaliyoadhimishwa katika viwanja vya Arusha School jijini hapa.

 Wanafunzi wa darasa la nne wakifurahi maadhimisho ya Juma la Elimukatika viwanja vya Arusha School.

No comments: