Friday, April 28, 2017

RC NCHIMBI AZIAGIZA HALMASHAURI ZA SINGIDA KUANZISHA MABWAWA YA UFUGAJI WA SAMAKI.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ameziagiza halmshauri zote za Mkoa wa Singida kuanzisha mabwawa ya ufugaji wa samaki ili kutunza mazingira, kuongeza kipato na kuwa darasa la kufundishia vikundi na wananchi wengine.

Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo mapema asubuhi ya leo katika shamba ya ufugaji wa samaki la Mikumbi lililopo manispaa ya Singida linalomilikiwa na Bwana Charles Kidua wakati wa uzinduzi wa mavuno ya kwanza ya samaki aina ya kambare katika mabwawa matatu kati ya sita yaliyopo katika shamba hilo.

Amesema halmashauri zionyeshe mfano kwa kuiga mbinu ya ufugaji wa samaki katika kutunza mazingira kwakuwa itaongeza kipato cha halmashauri pia halmashauri iangalie namna ya kufundisha ufugaji wa samaki vikundi vya vijana kuliko kuwapa mikopo ya pesa ambayo huishia kutumika vibaya.

Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa uwepo wa mabwawa hayo ya ufugaji wa samaki unaonyesha kuwa Mkoa wa Singida sio kame na wala sio mkoa masikini na uko tayari kuandaa chakula kulisha mikoa ya jirani hasa makao makuu ya nchi ambayo ni Dodoma.

“Tumejipanga na tuko vizuri kuhakikisha Dodoma inapata chakula kizuri na cha uhakika, Singida sio kame wala masikini, samaki hawafugwi kwenye ukame, Singida sio kame hata kidogo” amesisitiza Dkt. Nchimbi.

Ameongeza kuwa watendaji wote wanapaswa kuziishi taaluma zao kama ambavyo mmiliki wa mabwawa hayo ambaye ni afisa maliasili ambaye ameweza kuanzisha bwawa la samaki na hivyo kuwataka watendaji wengine mfano maafisa kilimo, mifugo kuwa mifano kwa jamii kwa kuonyesha manufaa ya taaluma hizo.

Naye mmiliki wa mabwawa hayo Bw. Charles Kidua amesema amekuwa na wazo la kuanzisha mabwawa ya ufugaji wa samaki kwa muda mrefu lakini amefanikiwa kuanzisha mradi huo mwaka 2016 kwa gharama ya shilingi milioni 12.

Kidua amesema kuanzishwa kwa mabwawa hayo kumewafaidisha baadhi ya wananchi amabo tayari wamejifunza kutka kwake na kuchukua vifaranga vya samaki kwake.

“Ukiwa na eneo zuri lenye maji uanzishaji wa ufugaji wa samaki kwa bwawa moja unaweza kukugharimu shilingi laki tatu tu, jirani yangu hapa yeye ameanzisha bwawa lake na kuchukua vifaranga hapa kwangu, kuna wananchi wengine pia wameanzisha mabwawa yao kupitia elimu wanayojifunza kutoka hapa” amesema Kidua.

Ameongeza kuwa changamoto aliyokumbana nayo katika kuanzisha mradi huo ni pamoja na ukosefu wa vifaranga wa samaki katika mikoa jirani na hivyo kumlazimu kuvifuata Mwanza hali ambayo inaongeza gharama.

Baadhi ya maofisa wa serikali na wananchi walioshuhudia uvunaji wa samaki hao wamekiri kuhamasika na wao kuanzisha ufugaji wa samaki. Mavuno ya samaki aina ya kambare katika shamba hilo yatafuatiwa na uvunaji wa samaki wengine aina ya sato ambao pia wapo katika mabwawa ya shamba hilohilo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (wa pili kulia) akishiriki kuvua samaki aina ya kambare kwenye bwawa lililopo kwenye shamba la samaki la Mikumbi mjini hapa ikiwa ni sehemu ya uzinduzi uvuvi kwenye shamba hilo.Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (wa kwanza kulia) akitoa maelekezo kwa mmiliki wa shamba la ufugaji samaki la Mikumbi Bw. Charles  Kidua (wa pili kulia) wakati akikagua shamba hilo lenye mabwawa sita yaliyofungwa samaki aina ya sato na kambare.
Mmiliki wa shamba la samaki Mikumbi mjini Singida na afisa maliasili Mkoa wa Singida Charles Kidua (aliyenyoosha mkono) akimweleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (wa kwanza kulia) muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa uvuvi kwenye shamba hilo asubuhi ya leo.
Baadhi ya samaki aina ya kambare waliovuliwa mapema leo kwenye uzinduzi wa uvuvi shamba la samaki la Mikumbi lililopo mjini hapa

No comments: