Monday, February 27, 2017

SERIKALI YAISHUKURU AfDB KUKUBALI KUFADHILI MIRADI YA UJENZI WA BARABARA NA USAFIRISHAJI WA UMEME ILI KUFUNGUA KANDA YA MAGHARIBI

Dkt. Philip Mpango (Mb) (kushoto) na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero wakifurahia uhusiano mzuri uliopo kati ya benki hiyo na serikali ya Tanzania
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kukubali kuendelea kufadhili miradi ya maendeleo ya kipaumbele hususani ya ujenzi wa barabara na usafirishaji wa umeme ili kufungua fursa za kiuchumi katika kanda ya Magharibi.
Dkt. Mpango ametoa shukrani hizo alipokutana na Wakurugenzi Watendaji 12 wanaowakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuharakisha kazi za upembuzi yakinifu na hatimaye kutoa fedha ili utekelezaji wa miradi ya Maendeleo kuanza mapema iwezekanavyo.
Amesema kuwa Benki hiyo iliahidi kutoa fedha ili kujenga barabara ya Nyakanazi, kupitia Kibondo, Kasulu hadi Manyovu, kwa kiwango cha lami na kwamba mradi huo ukipatiwa fedha na kukamilika kwa wakati kutasaidia kuchochea biashara ya wakazi wa maeneo hayo na Nchi jirani ya Burundi.
Pia mradi wa North – West grid wa kusafirisha Nishati ya Umeme kutoka Shinyanga hadi Mbeya kupitia Kigoma Katavi na Rukwa. Mradi huu utawezesha Mikoa ya ukanda wa Magharibi kupata Nishati ya uhakika ya umeme na kufungua fursa za Maendeleo mbalimbali yakiwemo ya  ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati.
“Katika kikao hicho tumewaeleza Wakurugenzi hao wa AfDB hatua mbalimbali ambazo Serikali inazichukua katika kutatua changamoto ya Miundombinu ya Umeme na Barabara, kupanua fursa za Ajira, na kuharakisha maendeleo ya  ukuaji wa Sekta ya Kilimo ambayo inategemewa na wananchi wengi” Alifafanua Waziri Mpango.
Aidha amewaeleza wageni juu ya jitihada za Serikali ya Mhe. Dkt. John  Pombe Joseph Magufuli za kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, kupambana na rushwa na biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Waziri Mpango ametumia fursa hiyo kuomba AfDB kusaidia kujenga uwezo wa Tanzania kukabiliana na majanga yakiwemo ya matetemeko ya ardhi, ajali kubwa za majini na kwenye migodi. Maeneo mengine ambayo AfDB imeombwa kuisaidia Tanzania ni uvunaji wa rasilimali za bahari (blue economy), kuelekeza mitaji katika Sekta ya kilimo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia nchi.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameipongeza Benki ya AfDB kwa kuwa mdau mkubwa wa Maendeleo ya nchi za Afrika na hasa Tanzania kwa kuwa imekuwa mnufaika mkubwa wa program/ miradi inayofadhiliwa na  Benki hiyo.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wageni hao watakapokuwa wakitembelea miradi mbalimbali inayogharamiwa na AfDBi katika siku takribani tano ambazo watakuwepo nchini.
Kwa upande wa Wakurugenzi Watendaji wa AfDB wanaoziwakilisha nchi zao, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Elizabeth Mmakgoshilekethe, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa mafanikio ya kiuchumi kwa kuwa Tanzania imekuwa na viashiria vingi ambavyo vinaonesha uchumi wa Taifa ni imara ukilinganisha na nchi nyingine katika bara la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.
Aidha wameitaka Tanzania kuendeleza jitihada za kupambana na Umaskini hasa katika maeneo ya vijijini na kuongeza fursa za ajira ili kuharakisha maendeleo. Pia wameipongeza Serikali kwa mikakati waliyonayo kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa  miaka mitano kwa kuwa unaendana na vipaumbele vya Benki hiyo.

Benki hiyo imeitaka pia Tanzania kushiriki na kuchangamkia fursa za miradi ya kikanda hasa katika Nishati ya Umeme, Barabara na Reli na pia kuhakikisha utawala bora. 

No comments: