Friday, February 24, 2017

REA III kuja na umeme mwingi

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa, utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA)utakuja na umeme mwingi kutokana na kujengwa kwa njia za kusafirisha umeme wenye msongo mkubwa.

Profesa Muhongo aliyasema hayo kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa REA Awamu ya Pili , katika Wilaya za Rorya na Butiama mkoa wa Mara ambapo pia alieleza mipango ya Serikali katika utekelezaji wa REA awamu ya Tatu.

Prof. Muhongo aliongeza kuwa, REA III itajikita katika kuyafikia maeneo yaliyorukwa katika awamu ya I na ya pili, kuyafikia maeneo ambayo hayajafikiwa kabisa na nishati hiyo, vilevile awamu hiyo itajikita katika matumizi ya nishati jadidifu hususan katika maeneo yote ya visiwani.

Vilevile, alisema kuwa, lengo la Serikali kupeleka umeme mwingi na wa uhakika katika maeneo ya vijiji ni kuchochea mapinduzi ya viwanda vidogo vidogo na hivyo kuwataka wananchi kuachana na siasa badala yake wajikite katika shughuli za kiuchumi ili kuchochea maendeleo ya kijamii na Taifa kwa ujumla.

" Wananchi tunatakiwa kuachana na siasa badala yake tujikite katika shughuli za kiuchumi. Tuzungumzie uchumi na maendeleo. Umeme ndio kichocheo kikuu cha uchumi na ndiyo maana Serikali inatekeleza mradi wa REA ili kufikia azma hiyo," amesisitiza Prof. Muhongo.

Pia, Prof. Muhongo alisisitiza suala la fidia katika utekelezaji wa REA awamu ya tatu na kueleza kuwa, serikali haitatoa fidia kwa wananchi watakaotoa maeneo yao ili kupitisha nguzo za umeme na kueleza kuwa, wanaotaka fidia wachague kati ya fidia au kupelekewa nishati hiyo. REa Awamu ya Tatu inatarajia kutekelezwa kuanzia mwezi Machi mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mhandisi Hamis Komba alimweleza Profesa Muhongo kuwa, Shirika hilo limeridhia kutoa sehemu ya eneo lake katika mgodi wa Buhemba linalotumiwa na wachimbaji wadogo ili waweze kulitumia kwa shughuli za uchimbaji madini .

Mhandisi Komba amesema kuwa, eneo hilo linaendelea kupimwa ili kujua ukubwa wake na kuongeza kuwa shughuli ya kuligawa kwa vikundi 13 vilivyojiandikisha litafanywa siku ya jumatatu tarehe 27 Februari, 2017, baada ya ukubwa wa eneo husika kujulikana.

Kutokana na kutoa eneo hilo ambalo lilikuwa linamilikiwa na STAMICO, Mhandisi Komba amewataka wachimbaji watakaopewa eneo husika kufanya shughuli za uchimbaji unaozingatia usalama, Sheria na taratibu za uchimbaji madini.

Profesa Muhongo alitembelea Wilaya za Rorya na Butiama katika Kata za Mirwa, Tai na Muriaza tarehe 23 Februari,2017
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akiongea jambo wakati akiwaeleza wananchi na wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari ya Nyamagongo Wilaya ya Rorya kuhusu utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya III. Shule hiyo ni miongoni mwa maeneo ambayo yatafikiwa katika mradi wa REA awamu ya Tatu. Wengine wanaofuatilia ni Meneja wa TANESCO Kanda ya Ziwa Mhandisi Amos Maganga, (katikati) Meneja wa TANESCO Wilaya ya Rorya, Sospeter Kswahili (wa kwanza kulia). Wengine ni Mtaalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini Mhandisi Emmanuel Yesaya na Mkandarasi wa Kampuni ya Angelica International.
Afisa Uhusiano na Huduma za Jamii kwa Wateja kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), James Vesso, akitoa elimu kuhusu Kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wa Kijiji cha Muriaza Kata ya Muriaza Wilaya ya Butiama wakati wa Ziara ya Waziri wa Nishati na Madini kijijini hapo. Kifaa hicho hakihitaji mtandao wa umeme katika nyumba.
Meneja wa TANESCO Kanda ya Ziwa Mhandisi Amos Maganga, akizungumza jambo wakati wa mkutano wa Waziri wa Nishati na Madini wananchi wa Nyamagongo ambapo Waziri na wataalam wa REA na TANESCO wameeleza kuhusu utekelezaji wa REa Awamu ya Pili na ya Tatu. Wengine ni Mameneja wa TANESCO, Wilaya ya Rorya na Mkoa wa Mara, na Wataalam kutoka REA na TANESCO.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Saimon Chacha na viongozi wa Mkoa, wakimkaribisha Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) wilayani humo kwa ajili ya ziara ya kukagua miradi ya REA awamu ya II na kueleza mipango ya Serikali kuhusu utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mhandisi Hamis Komba, akiwaeleza wachimbaji wadogo kuhusu shirika hilo kuridhia kutoa sehemu ya eneo lake la Buhemba kwa ajili ya wachimbaji kufanya shughuli za uchimbaji madini.
Mtendaji Kata wa Mirwa, Neema Philipo,akisoma majina ya vikundi vya wachimbaji wadogo ambavyo vitapewa sehemu ya eneo la STAMICO, Buhemba. Wengine wanaofuatilia ni Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kushoto), Kaimu Mtendaji Mkuu wa STAMICO, Mhandisi Hamis Komba, (wa kwanza kushoto) Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Mashariki, Mhandisi Juma Sementa na Watendaji kutoka STAMICO na wachimbaji wadogo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akitoa rambirambi kwa baadhi ya wazazi ambao mmoja wa wachimbaji wadogo alifariki katika ajali ya kifusi iliyotokea katika mgodi eneo la Buhemba, Mkoani Mara.
Sehemu ya wananchi wa wananfunzi katika eneo la Nyamagongo Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, hayupo pichani.
Naibu Mhariri wa Gazeti la Jamhuri Jackton Manyerere (wa pili kulia) akiongea jambo wakati Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akitoa heshima katika Kaburi la Baba Mzazi wa Manyerere., Jakcton Nyambereka Nyerere aliyefariki dunia tarehe 19/2/2017/. Wa kwanza kulia ni Mhariri wa gazeti la Mtanzania Kulwa Keredia. Kushoto ni baadhi ya waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari. Waziri alifika kuhani msiba wa wahariri hao Manyerere na Keredia wakati wa ziara yake Wilayani Butiama.

No comments: