Monday, February 27, 2017

RC AAGIZA ZOEZI LA USAJIRI WA WAFUGAJI KWENDA SAMBAMBA NA USAJIRI WA WAKULIMA

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amewaagiza Viongozi wa Serikali Mkoani humo ngazi ya Wilaya hadi kata kuwa na madaftari ya kuwasajiri wakulima ifikapo Machi 31, mwaka huu.

Dkt. Kebwe ametoa agizo hilo Februari 22 mwaka huu wakati anatembelea kiwanda cha kuzalisha Mpunga cha KPL kilichopo katika Wilayani ya Kilombero ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano aliyoifanya Wilayani humo.

Katika maelezo yake Dkt. Kebwe amesema zoezi la usajiri wa wafugaji pamoja na mifugo yao lazima liende sambamba na zoezi la usajiri wa wakulima kwa lengo lilelile la kupata takwimu halisi kwa Mkoa mzima na si kuwa na takwimu za mezani.

“Sambamba na kazi ambayo tuliianza mwaka jana mwezi wa sita ya utambuzi wa mifugo kazi ambayo inaendelea awamu ya pili, madftari ya wafugaji sehemu kubwa yameanza kuwepo wafugaji wanatambuliwa. Kwa hiyo vitu hivi viwili lazima viende sambamba hii inasaidia kutengeneza maoteo katika Halmashauri zetu. Huwezi kufanya maoteo bila kuwa na tax base” alisema Dkt. Kebwe

Mkuu huyo wa Mkoa ameonekana kuridhishwa na juhudi zinazooneshwa na baadhi ya wakulima hususani wa Wilaya ya Kilombero kujihusisha katika kilimo na kusema amejionea mwenyewe watu wamelima mashamba makubwa ingawa mvua zimechelewa kunyesha tofauti na maeneo mengine ambapo wamelima maeneo madogo.

Hata hivyo amesema ametoa maelekezo kwa Mkoa wote kufikia tarehe 31 ya mwezi wa tatu kila Halmashauri iwe na madaftari haya ya wakulima. Hii itatusaidia sana kujua kiasi mtu anacholima na anachotegemea kuvuna hivyo kuwa na takwimu zenye uhakika.

Amesema kuwa na madaftari ya kutunzia takwimu kwa masuala ya kilimo ni maelekezo ya siku nyingi ya Serikali na ni takwa la kisheria na hiyo inasaidia kupata msingi wa mapato katika Halmashauri zetu (tax base) kwani bila kuwa na madaftari hayo takwimu ambazo zitakuwa zinatolewa kwa sehemu kubwa zitakuwa hazina uhalisia.

Lakini Dkt. Kebwe pia alishauri uongozi wa kiwanda cha KPL kuwa pamoja na kujishughulisha na kilimo cha mpunga waongeze jitihada ya kulima zao la mahindi ambalo kwa sasa lina soko la uhakika na kuwataka pia kuuza ziada ya mahindi watakayoyapata kwa Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula – NFRA.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. James Ihunyo amesema, madaftari ya wakulima na wafugaji yatasaidia kupunguza kama sio kuondoa kabisa migogoro baina ya wakulima na wafugaji Kwani Kwa kujua takwimu zao kwa usahihi itasaidia Serikali kufanya maandalizi ya kutenga maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo kwa usahihi pia, kupitia mradi wa Serikali unaohusika na kupima maeneo yote ya Ardhi na kuyarasimisha kwa wananchi (Land Tenure supporting Program).

Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero …….Londo amesema, uwepo wa madaftari ya wakulima kwanza itasaidia kujua idadi ya wakulima wote wa Halmashauri yake, kujua mazao wanayolima na ukubwa wa mashamba yao pamoja na takwimunyingine. Lakini pia kuwa na maoteo sahihi ya mazao yatakayopatikana na tatu kuondoa mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya wafanya biashara wanaojificha nyuma ya wakulima wakati wa kulipa kodi za mazao kwani sekta ya Kilimo ndiyo inabeba Halmashauri hiyo kiuchumi.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Mh. Steven Kebwe akishiriki katika kazi ya kiwekea mifugo alama ikiwa ni utambuzi wa mifugo hiyo.
Ng’ombe ambao tayari wamesha wekewa alama.

No comments: