Monday, December 5, 2016

Wanawake wasisubiri nafasi za upendeleo wa uongozi – ANNA ABDALLAH

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Aliyekuwa Mbunge wa Viti maalum (CCM), Mhe. Anna Abdallah amewataka wanawake nchini kuacha kusubiri nafasi za upendeleo wa nafasi za uongozi katika vyombo mbalimbali vya maamuzi nchini.

Mhe. Anna Abdallah ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa mahojiano maalum juu ya maendeleo na nafasi ya wanawake katika nafasi za uongozi ndani ya miaka 55 tangu nchi yetu ipate Uhuru wake mwaka 1961.
Amesema kuwa, katika miaka ya nyuma nafasi nyingi za maamuzi katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi zilikua zikiongozwa na wanaume pekee hali iliyosababisha wanawake kuwa nyuma kimaendeleo hivyo kupelekea Mashirika mbalimbali ya kupigania haki sawa kwa wote kuanza harakati za kuwafanya wanawake wajitambue na kufahamu umuhimu wao.
“hivi sasa wanawake wameelimika na wana kila sababu ya kuwa viongozi katika ngazi mbalimbali za serikali na Taasisi zisizo za Kiserikali ndani na nje ya nchi kwa sababu wana uwezo wa kutoa mawazo chanya yenye kuleta maendeleo, pia ni jambo la kufurahisha kuona jamii imekubali mabadiliko haya kwa kuwaruhusu wanawake wapaze sauti zao katika utatuaji wa changamoto mbalimbali zinazoikabili Serikali na wananchi kwa ujumla,” alisema Mhe. Mama Anna.  
Ameongeza kuwa wanawake waliopata nafasi ya kushika nyazfa mbalimbali wako mstari wa mbele katika jitahada za kutatua matatizo yanayoikabili jamii kama vile mila na desturi potofu zikiwemo za ukeketaji, unyanyasaji wa wanawake na watoto, mimba na ndoa za utotoni pamoja na uzazi salama.
Aidha, Mbunge huyo Mstaafu amelipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupiga hatua kubwa kiutendaji kwani sasa hivi kuna demokrasia huru ndani ya Bunge ambapo nafasi za kuchangia zimekuwa zikitolewa kwa usawa.
Amefafanua kuwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Afrika ya Kusini (SADC) ilipitisha azimio la Maendeleo ya Wanawake ambapo waliamua Mabunge yote ya Nchi Wanachama kutenga Asilimia 10 kwa ajili ya Wabunge Wanawake hivyo Serikali ya Tanzania iliona ni jambo zuri kuwashirikisha wanawake kwa kuwateua kuwa Wabunge wa Viti maalumu ili nao waweze kujumuika na kutoa mawazo yao katika kuendeleza nchi.
”Pamoja na kuongezeka kwa idadi ya Wabunge wanawake wa Viti Maalumu lakini ni vizuri wanawake wakaonyesha uwezo wao katika kupigania kupata nafasi hizo na sio kupendelewa kwani  ushindi wanaoupata wakati wa kugombea Ubunge majimboni ni ishara tosha kuwa wanaweza kuwa viongozi wenye kutoa maamuzi sahihi,” aliongeza mama Anna.
Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015, idadi ya Wabunge wanawake Viti Maalumu ilikuwa 113, Wabunge wa Majimbo 25 na wa kuteuliwa 2  ambapo kwa mwaka  2016 hadi 2020 Wabunge wanawake wa Majimbo ni  21 na Viti Maalum 127 wakati walioteuliwa na Mhe. Rais 3 na waliotoka Baraza la wawakilishi Zanzibar 2.

No comments: