Monday, December 5, 2016

RAIS DKT. MAGUFULI AKUTANA NA MKURUGENZI WA MAUZO WA KAMPUNI YA NDEGE YA BOEING, MWAKILISHI MKAZI WA BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA (AfDB) PAMOJA NA BALOZI WA CUBA HAPA NCHINI, IKULU JIJINI DAR ES SALAAM


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 05 Desemba, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika wa Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Boeing yenye makao yake nchini Marekani Bw. Jim Deboo ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kununua ndege kubwa kutoka kampuni hiyo.

Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James.

Baada ya Mazungumzo hayo Rais Magufuli amesema Serikali yake ya Awamu ya Tano imedhamiria kununua ndege nyingine nne zikiwemo ndege kubwa 3 ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja hapa nchini moja kwa moja kutoka nchi zao.

"Sisi hapa tunazungumza kuwa watalii hawajafika hata milioni 2 kwa mwaka, lakini nchi kama Morocco inapata watalii zaidi ya milioni 12 kwa mwaka, hii yote ni kwa sababu hatuna mashirika ya ndege ya kwetu, watalii wakitaka kuja hapa ni lazima waje kwa kuungaunga, wafikie nchi nyingine halafu ndipo wapate moyo wa kuja huku, licha ya kwamba sisi Tanzania ni miongoni mwa nchi 5 duniani zenye maeneo mazuri yenye utalii

"Kwa hiyo niwaombe tu Watanzania wapende mali zao, kwa sababu wakati mwingine nikiangalia mitandao na magazeti ni ajabu huwezi kuamini kama hao ni Watanzania, unakuta wanasifia tu ndege za watu wengine na wanazibeza za kwao" amesisitiza Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ametaja aina ya ndege mpya ambazo Serikali itazinunua kuwa ni ndege 1 aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kufika nchini Mwezi Juni 2017, ndege 2 aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018 na ndege moja aina ya Boeing 787 Dash 8 Dream Liner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 na inayotarajiwa kuwasili nchini Juni, 2018. Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika.

Dkt. Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi za Serikali zenye lengo la kuinua utalii na kuimarisha uchumi wa nchi.

"Tumeleta ndege aina ya Bombardier hapa, zimepunguza gharama za safari mfano kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, sasa wanalipa kati ya 160,000/ hadi 200,000/- wakati nauli ilishafika Shilingi laki 8 na kitu, lakini watu wengine utakuta wanazungumzazungumza wee maneno ya hovyo kwa kutumiwa, tumeshaamua na tutafanya hivyo" amesisitiza Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagana na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika hapa nchini (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero ambaye amepandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Ukanda wa Kusini mwa Afrika katika ofisi zake zilizopo Afrika Kusini.

Rais Magufuli amemshukuru Dkt. Tonia Kandiero kwa juhudi kubwa alizozifanya akiwa Mwakilishi Mkazi wa AfDB hapa nchini ambapo miradi mikubwa na muhimu katika maendeleo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa.

Akizungumza baada ya kuagana na Rais Magufuli Dkt. Tonia Kandiero amemshukuru Rais Magufuli na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano alioupata katika kipindi cha miaka 6 aliyokuwa hapa nchini na amesema anaondoka akiwa ameiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa ya kimahusiano na AfDB ambapo miradi yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni imetekelezwa hususani katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo anayemaliza muda wake baada ya kuiwakilisha nchi ya Cuba kwa miaka minne.

Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo kwa uhusiano na ushirikiano mzuri aliouendeleza kati ya Tanzania na Cuba uliojengwa na waasisi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mhe. Fidel Castro wa Cuba.

Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo amemshukuru Rais Magufuli na Serikali kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Cuba na amesema anaondoka akiwa anaamini kuwa uhusiano kati ya nchi hizi utaendelea kuwanufaisha wananchi ikiwemo miradi mikubwa ya maendeleo na huduma za kijamii.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

05 Desemba, 2016


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo aliyefika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo pamoja na ujumbe wake.
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitazama kitabu cha  picha ya ndege aina ya Boeing 787-8 Dream liner wakati alipokuwa akisikiliza maelezo yake kutoka kwa Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo. Ndege hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 262 na itakuwa na uwezo wa kuruka kutoka nchini Marekani hadi Tanzania bila kutua mahali popote.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Mkurugenzi wa mauzo wa Kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Doto James na anayefuatia ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza kuhusiana na ununuzi wa ndege hiyo mpya aina ya Boeing 787-8 Dream liner mara baada ya kumaliza mazungumzo na Mkurugenzi wa mauzo wa Kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Cuba anayemaliza muda wake nchini George Luis Lopez Tormo aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam.
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Balozi wa Cuba anayemaliza muda wake hapa nchini George Luis Lopez Tormo aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Cuba anayemaliza muda wake hapa nchini George Luis Lopez Tormo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero aliyefika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo. Dkt. Tonia ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Ukanda wa Kusini Mwa Afrika katika Ofisi zake zilizopo Afrika ya Kusini
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na  Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo na kuagana na Mhe. Rais Dkt. Magufuli. Dkt. Tonia ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Ukanda wa Kusini Mwa Afrika katika Ofisi zake zilizopo Afrika ya Kusini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo.Dkt. Tonia Kandiero ameteuliwakuwa  Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Ukanda wa Kusini Mwa Afrika katika Ofisi zake zilizopo Afrika ya Kusini PICHA NA IKULU 

No comments: