Monday, December 19, 2016

PROF. MBARAWA: ATOA TAHADHARI UHARIBIFU WA MIUNDOMBINU

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewatahadharisha watanzania kuepuka vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya barabara husasan katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

Ameyasema hayo wakati akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Dodoma-Babati yenye urefu wa KM 188.1, sehemu ya Mela-bonga ambapo imeripotiwa kuwepo vitendo vya uharibifu wa miundombinu kwa muda mrefu.

'Napenda kutoa wito kwa watanzania kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kuacha vitendo vya kuchoma matairi barabarani, kwani hali hii hupelekea kuharibu barabara kwa kiasi kikubwa ambazo Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuzijenga", amesema Prof.Mbarawa.

Aidha, amekemea vitendo vya baadhi ya madereva kumwaga mafuta barabarani na baadhi ya wananchi kupitisha mifugo kwenye barabara ambapo vyote kwa pamoja vinaharibu miundombinu ya barabara.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali ikiwemo kuwaripoti wale wote wanaohujumu miundombinu ya barabara nchini.

Sambamba na hilo, amewaasa madereva wa vyombo vya moto kuwa makini barabarani kwa kuzingatia sheria za alama za barabara ikiwemo kuendesha vyombo hivyo kwa mwendo unaotakiwa ili kudhibiti ajali za barabarani zinazoweza kuepukika.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Dodoma- Babati yenye urefu wa KM 188.1, Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa barabara hiyo inatarajiwa kukamilika mwakani kwani kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za ujenzi wake.

"Kazi inaenda kwa kasi kubwa, matumaini yangu ni kwamba ifikapo mwishoni mwa mwaka 2017, barabara hii itakamilika kwa viwango bora tulivyokubaliana kwenye mkataba", amesisitiza Profesa Mbarawa.
Amefafanua kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza umbali wa masaa kwa abiria wanaosafiri kupitia njia ya Singida wanaotoka Dodoma na mikoa ya jirani kuelekea Manyara, Moshi na Arusha.

Ameongeza kuwa barabara hiyo itasaidia kuiunganisha Tanzania na Nchi za kutoka Kusini na Kaskazini mwa bara la Afrika, hivyo kufungua fursa za kibiashara kwa wananchi na kuongeza pato la Taifa kupitia sekta ya utalii.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Dodoma, Eng. Leonard Chimagu, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa viwago vinavyostahili na kuahidi kukamilika kwa wakati.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya H.P Gauff, Eng. Kini C. Kuyonza (wa tatu kulia), inayosimamia mradi wa ujenzi wa barabara ya Mela-Bonga yenye urefu wa KM 88.8. wakati alipokagua barabara hiyo, wilayani Babati.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiongea na mmoja wa madereva wa Basi linalofanya safari zake katika mikoa ya Dodoma-Babati, wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Mela-Bonga yenye urefu wa KM 88.8.
 Ujenzi wa barabara ya Mela-Bonga yenye urefu wa KM 88.8 inayojengwa kwa kiwango cha lami ukiendelea. Mradi huo unajengwa na Mkandarasi wa Kampuni ya M/s China Railway Seventh Group na unatajiwa kukamilika mwezi Agosti mwakani.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akishindilia nondo kwenye moja ya ujenzi wa barabara ya Mela-Bonga yenye urefu wa KM 88.8, inayojengwa kwa kiwango cha lami, alipokuwa akikagua mradi huo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akikaza nondo katika ujenzi wa barabara ya Mela-Bonga yenye urefu wa KM 88.8, alipokuwa akikagua barabara hiyo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akishiriki kucheza ngoma za asili ya Kirangi katika kijiji cha Bicha, wilaya ya Kondoa mara baada ya kuongea na wakazi hao katika ziara yake ya ukaguzi wa mradi wa barabara ya Dodoma-Babati.
 Muonekano wa Daraja la Kelema ambalo ni moja ya madaraja makubwa 4 yanayojengwa katika barabara ya Mayamaya-Mela KM 99.35. Daraja hilo lenye urefu wa mita 205, lina uwezo wa kubeba tani 100.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akikagua tabaka la lami katika barabara ya Mayamaya-Meya KM 99.35, alipokagua barabara hiyo.

No comments: