Friday, November 25, 2016

Serikali yawataka maafisa elimu kupanga muda wa kusikiliza kero za walimu na kuzitafutia ufumbuzi kuongeza morali ya walimu kufundisha.




Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Said Jafo akisaini kitabu cha wageni shule ya sekondari Segera, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Wiliam Makufwe na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe.
Picha ya pamoja ya Mhe. Selemani Said Jafo na waalimu wa shule ya sekondari ya Segera.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni akitoa utambulisho mfupi kwenye ukumbi wa Halmashauri.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe akitoa taarifa fupi ya Wilaya kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Handeni.
Naibu waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mh. Selemani Said Jafo akizungumza ma watumishi wa Wilaya ya handeni.
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Viongozi wakisikiliza kwa makini maagizo ya Naibu Waziri ikiwa ni pamoja na kuwa na usimamizi bora wa rasilimali fedha.


Serikali imewataka maafisa elimu kupanga muda wa kusikiliza kero za walimu na kuzitafutia ufumbuzi ili kuongeza morali ya walimu kufundisha. Agizo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe.Seleman Said Jafo alipokuwa akiongea na walimu wa shule ya sekondari Segera iliyopo wilayani Handeni, wakati wa ziara ya kiserikali Wilayani Handeni na Mkoa wa Tanga.

Mhe.Jafo alisema kuwa wapo baadhi ya Maafisa elimu ambao wanajifanya kuwa ni Miungu watu linapokuja suala la kusikiliza na kutatua kero za walimu. Waziri Jafo alisema “Wapo walimu wanaotembea umbali mrefu kufuata huduma makao makuu ya Halmashauri kwa wakubwa wao mara nyingi wameshindwa kutatuliwa kero zao hali inayopelekea usumbufu, Kuanzia leo 24/11/2016 napiga marufuku tabia hiyo”. 
 
Aliongeza msisitizo kuwa Maafisa elimu wapo kwa lengo la kuwasikiliza walimu na kuwasaidia kutatua kero zao ili waweze kujikita katika ufundishaji wa wanafunzi. Alisema kuwa walimu ni watu muhimu sana nchini ila wamekuwa wakikatishwa tamaa na utendaji wa baadhi ya maafisa elimu. Aliongeza kuwa kero kubwa ya walimu ni kutokupanda madaraja kwa wakati na kutopata stahiki zao ikiwa ni pamoja na posho za likizo,uhamisho na madai mengine.

Wakati huohuo, Naibu Waziri aliiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kukamilisha miradi yote ya SEDP-II ambayo haijakamilika kuhakikisha inakamilika kabla au ifikapo tarehe 20/12/2016. Alisema kuwa katika kusimamia miradi hiyo na miradi ya maendeleo kwa ujumla kila mtu lazima atimize wajibu wake na kuhakikisha fedha iliyotengwa na kutolewa inatumika vizuri na thamani yake kuonekana kwa muda mrefu (value for money).

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI aliwataka Maafisa utumishi pia kusimamia vizuri haki za watumishi ili kuwawezesha watumishi wote kufanya kazi kwa moyo na kuwaondolea msongo wa mawazo usio wa lazima. 
 
“Maafisa utumishi wakifanya kazi zao kwa weledi na kutimiza wajibu wao, Halmashauri haitakuwa na malalamiko kutoka kwa watumishi kitu ambacho kitaongeza ufanisi katika utendaji wao”. Vilevile, aliwataka kutambua michango ya watumishi bora na wanaojituma kufanya kazi wanapotimiza wajibu wao kwa juhudi na maalifa kuwepo na utaratibu wa kuwapa pongezi na motisha ( acknowledgement).

Aidha amewaeleza waweka hazina kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kufuat sheria taratibu na kanuni zilizopo za Halmashauri kwani kufanikiwa au kutofanikiwa kwa malengo ya Halmashauri kunachangiwa kwa kiasi kikubwa kwa utendaji kazi wa waweka hazina wa Halmashauri.”Mwekahazina atayeshindwa kutimiza wajibu wake atapisha nafasi hiyo kwa mtu mwingine ambaye ataweza kusimamia kwa ufanisi”alisema.

Pia aliwaagiza wakurugenzi wa Mjini Bw. Kenned Haule na Bw. William Makufwe Mkurugenzi wa Handeni Vijijini kuweka malengo ya utendaji kazi kwa kutumia mfumo wa Opras kwa kila mkuu wa Idara na kitengo na kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu utendaji kazi wa watumishi hao, ili kutambua kwa kiasi gani malengo hayo yamekamilishwa. Wametakiwa kuhakikisha pia wanakuza vipaji vya watumishi kwa kutumia elimu na taaluma walizonazo ipasavyo ili kuendeleza Halmashauri.

Wakurugenzi wametakiwa kuhakikisha pia watumishi wa idara ya maendeleo ya jamii wanatumika ipasavyo katika kuhudumia jamii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha za miradi ya vikundi vya vijana na kinamama zinatolewa na kutumiwa kama ilivyokusudiwa.

Mwisho Naibu Waziri aliwashukuru watumishi na kuwaomba wapendane kwani upendo baina ya watumishi ni chachu ya maendeleo na kwamba kila mtumishi afanye majukumu yake kwa kukuza thamamani ya kazi yake na kutoa ushirikiano kwa viongozi wetu hasa wabunge. Aliwakumbusha watumizi kufanya kazi kama ajira kwani wanapata mishahara, kuacha alama ( legacy) na kufanya kazi kama ibada kwa kuwatumikia wananchi.

Aidha Aliwataka Waheshimiwa Madiwani kufanya maamuzi sahihi pindi linapofika suala la kufanya maamuzi kwa manufaa ya wananchi na sio kunufaisha Viongozi wachache au kikundi cha watu. Hasa upatikanaji wa eneo la kujenga ofisi za Halmashauri zilizo gawanywa ili kuondoa gharama zisizo za lazima za ulipaji fidia wa maeneo.

Mkuu wa wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe aliahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri kwa karibu na ukamilifu wake kwa dhati .

Nae Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, Mhe. Omary Kigoda pamoja na kutoa shukrani kwa ziara ya Naibu Waziri, alichukua fulsa hiyo kumuomba Naibu Waziri kusaidia upatikanaji wa watumishi wa sekta ya afya kutokana na uhaba mkubwa wa watumishi wa kada hiyo hali inayofifisha huduma kwa jamii. Alisema kwamba watumishi waliopo ni 25% ya watumishi wanaohitajika hivyo upungufu ni mkubwa.

Naibu Waziri Jafo alifanya ziara ya siku moja Wilayani Handeni ambapo pamoja na mambo mengine aliongea na watumishi wa wilaya hiyo.

Alda Sadango

Afisa Habari

Halmashauri ya Wilaya ya Handeni

25/11/2016

No comments: