Wednesday, November 30, 2016

PLAN INTERNATIONAL YAZINDUA MRADI WA KUWAWEZESHA VIJANA NA WATOTO KUPITIA MICHEZO

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Shirika la Plan International limezindua Mradi wa Kuwawezesha Vijana na Watoto kwa Njia ya Michezo ili kuwajengea uwezo wa kuwa mawakala hai wa mabadiliko chanya katika jamii zinazowazunguka.

Mradi huo umezinduliwa leo Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya hiyo, Wanchoko Chinchibera ambaye ametoa wito kwa watendaji wa Serikali, wazazi pamoja na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha mradi huo unatekelezeka.

Chinchibera amesema mradi huo umekuja wakati muafaka kwani watoto na vijana wanakabiliwa na changamoto ya ulinzi, usawa wa kijinsia pamoja na ushirikishwaji mdogo katika michezo hivyo kupitia mradi huo watapata maendeleo mazuri ya kielimu na kimakuzi pamoja na fursa ya kutatua changamoto zao. 

“Kupitia michezo tunajenga afya, akili, malezi na makuzi ya mtoto lakini pia michezo ni sehemu ambayo watoto wanaweza kupaza sauti zao na kujadili kuhusu haki zao za msingi kwa njia ya nyimbo na mashairi hivyo tunaamini kuwa tukianza kuwashirikisha watoto katika suala zima la michezo tutatengeneza kizazi chenye maendeleo,”alisema Chinchibera.

Ameongeza kuwa kupitia michezo, vipaji vingi vitaibuliwa ambavyo vitasaidia katika kutengeneza ajira mbalimbali zitakazowawezesha vijana kujikomboa kiuchumi na kuchangia katika pato la taifa hivyo amewahakikishia wananchi kuwa mradi huo utazaa matunda mazuri.

Kwa upande wake Meneja Miradi wa Shirika hilo, Grace Semwaiko amesema mradi huo ni sehemu ya mpango mkakati wa tatu wa shirika hilo ambao kwa ujumla unalenga kufikia jumla ya watoto 3,075 na vijana 3,109 katika kuwahakikishia ulinzi na usawa wa kijinsia.

“Ni matumaini yetu kuwa mradi huu utatekelezwa vizuri na hatimaye kufikia malengo tuliyojipangia yakiwemo ya kukua kwa uelewa kwa jamii na wadau wote kuhusu usawa wa kijinsia, kuhakikisha vijana na watoto waliowezeshwa wanaleta mabadiliko katika jamii pamoja na kuimarika kwa ulinzi wa watoto katika ngazi ya jamii hadi taifa,” alisema Bi Grace.

Alifafanua kuwa mradi huo unawalenga wanafunzi wa Shule za Msingi kuanzia darasa la 4 hadi la 7, wanafunzi wa Shule 6 za Sekondari, walimu, wazazi, viongozi wa jamii na watendaji wa Vijiji, Kata pamoja na Watoto na Vijana ambao hawasomi.

Mradi huo utaratibiwa na shirika la Plan International pamoja na shirika la Right to Play na utatekelezwa katika Kata mbili za Kiluvya na Malumbo zilizopo wilayani humo ambapo jumla ya vijiji 10 vitanufaika. 

Aidha Bi.Grace aliongeza kuwa Mradi huo unatarajiwa kuwa wa miaka miwili na utagharimu jumla ya shilingi 641,468,700 ambapo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2018.

Shirika la Plan International la nchini Ujerumani ni miongoni mwa mashirika ya Kimataifa yasiyo ya kiserikali ambayo yameonyesha juhudi kubwa za kuibua miradi mbali mbali katika jamii na kuifadhili katika sekta za Afya,Maendeleo ya jamii,Wanawake,Watoto na Michezo.
 Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani, Wanchoko Chinchibera akiongea na wanafunzi pamoja na wadau mbalimbali wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kuwawezesha Vijana na Watoto kwa Njia ya Michezo uliozinduliwa leo wilayani humo.Mradi huo unaratibiwa na Shirika la Plan International.
 Meneja Miradi wa Shirika la Plan International, Grace Semwaiko akielezea kuhusu malengo ya mradi wa Kuwawezesha Vijana na Watoto kwa Njia ya Michezo uliozinduliwa leo wilayani Kisarawe.Mradi huo unaratibiwa na Shirika la Plan International.


Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani, Wanchoko Chinchibera akikagua timu ya mpira ya watoto wakati wa mradi wa Kuwawezesha Vijana na Watoto kwa Njia ya Michezo uliozinduliwa leo wilayani humo.Mradi huo unaratibiwa na Shirika la Plan International.

No comments: