Tuesday, October 18, 2016

WAZIRI NAPE AKIWASILISHA MUSWADA WA HABARI KUIBADILI TAALUMA


SERIKALI imewasilisha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii Muswada wa Huduma za Habari ikieleza kuwa ni sheria itakayoleta mageuzi makubwa nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa akiwasilisha muswada wa sheria hiyo leo mjini Dodoma ambapo amesema sasa sekta ya habari inakwenda kuwa taaluma kamili.

Waziri Nnauye amesema Sheria hii italeta mifumo ya kisasa ya usimamizi wa sekta ya habari na mifumo ambayo inaweza kugusa au kubadili namna wanahabari walivyozoea kutenda au kufikirika kwa sasa lakini akasema sekta hiyo iwe tayari kwa mabadiliko.

“Niwaombe wanatasnia wenzangu tuwe tayari kwa mabadiliko haya ili taaluma yetu iheshimike na sisi wenyewe tuheshimike zaidi” alisisitiza Mhe. Nnauye.Aidha Mhe. Nnauye ametoa wito kwa wadau wote kuunga mkono muswada huo utakaojadiliwa katika Bunge lijalo la Novemba mwaka huu. 

“Tuko hapa kuboresha na sio kusuguana tukae tuiandae tasnia bora zaidi kwa kupitia na kutoa maoni juu ya Muswaada huu wa Sheria ya Huduma za Habari 2016” alifafanua Mhe. Nnauye.Ameongeza kuwa kwa sasa hadi wakati wa Bunge lijalo Serikali ipo tayari kupokea na kuyafanyia kazi maboresho yatakayolenga kufikia maono ya muswada huu kutoka kwa wadau ili kuipa heshima stahiki sekta ya habari.

Alisema kuwa muswada huo licha ya huu utatatua changamoto za kutotambulika kwa sekta ya habari kama taaluma kamili inayopaswa kuheshimiwa, pia utatatua changamoto ya kukosekana vyombo madhubuti na huru vya usimamizi wa tasnia.

Alisema kutokana na hayo muswada unapendekeza kuundwa kwa Bodi ya Ithibati itakayoainisha sifa za mwanahabari na kuwasajili.Aliitaja taasisi nyingine inayoundwa kuwa ni Baraza Huru la Wanahabari ambalo litakuwa na wajibu wa kuandaa na kusimamia maadili ya wanahabari na watawajibishana wenyewe kwa wenyewe.

Wasomi wanena

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Benson Bana anasema kuwa kuja kwa sheria hiyo ni jambo la busara kwa sababu kwa sasa weledi wa uandishi wa habari uko chini.

“Sheria hii iwe na makali zaidi kwa wanahabari ambao watakiuka utaratibu na maadili. Hakuna nchi ambako wanahabari wanajiendea tu bila uratibu,” alisema,Alisema ni vyema na ni wakati mauafaka kwa sekta ya habari kuwa taaluma kamili na kushauri kuwa wanaoitumikia fani hiyo kwa sasa wawe tayari kwa mabadiliko.

Naye Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt William John Walwa alisema sheria imekuja wakati muafaka na inapaswa kutatua changamoto za fani hiyo.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akiwasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mswada wa Sheria ya Huduma za Habari 2016 leo Mjini Dodoma Oktoba 18,2016.

No comments: