Saturday, October 29, 2016

WANASHINYANGA WAOMBA KIWANDA CHA KUTENGENEZA MKAA RAFIKI KWA MAZINGIRA KATIKA SIKU YA USAFI KITAIFA

 Baadhi ya wakazi wa Mji wa Shinyanga wakishiriki katika zoezi la usafi wa mazingira leo, Mjini Shinyanga. 
 Katikati Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina, Kushoto Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi Josephine Matiru,  na Bwana Daniel Sagata Pamoja wakijiandaa kuanza zoezi la usafi wa mazingira katika eneo la Binzatana Mjini Shinyanga mapema leo. 
 Naibu Waziri Ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe Luahaga Mpina akishiriki katika zoezi la kupanda miti Mjini Shinyanga leo.
 Viongozi pamoja na baadhi ya wananchi wa mkoa wa Shinyanga katka zoezi la usafi wa mazingira mjini Shinyanga leo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe Luhaga Mpina akiongea na baadhi ya wananchi wa mkoa wa Shinyaga katika eneo la Binzanata baada ya kukamilisha zoezi la usafi wa mazingira na kupanda miti mapema leo. ( Picha zote na Habari na Evelyn Mkokoi wa OMR).


EVELYN MKOKOI-SHINYANGA

Uongozi wa mkoa wa Shinyanga kupitia Mkuu wa Wilaya yake Bi Josephine Matiru umeiomba serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Kujenga kiwanda kitakacho tengeneza mkaa utokanao na mabaki ya miti ambao ni rafiki kwa mazingira ili kunusuru hali ya mkoa huo kuendelea kuwa jangwa kutokana na ukataji miti ovyo kwa matumizi ya makaa manyumbani, matumizi mengine na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkuu wa wilaya hiyo ametoa ombi hilo leo mbele ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina aliposhiriki siku ya usafi kitaifa ya mwisho wa mwezi October ambapo zoezi hilo lilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania December Mwaka jana na kuendelea kutekelezwa kila jumamosi ya mwisho wa mwezi kama siku maalum ya usafi nchini.

Bi Materu aliendelea kusema kuwa, Mkoa wa shinyanga unakumbana na changamoto kubwa ya ukataji miti ovyo ambayo ingeweza kukabiliwa kwa kutumia mabaki ya miti, taka na maranda ya mbao kutengeneza mkaa rafiki kwa mazingira na kusema kuwa mkoa na wilaya ya shinyanga imebarikiwa kuwa na miti ya aina mbali mbali ambazo mazingira yangetunzwa vizuri na kutumia malighafi hiyo ya taka kutengeneza mkaa banifu akitolea mfano kiwanda cha kutengeneza mkaa rafiki wa mazingira cha Zanzibar.

Kwa Upande wake Naibu Waziri Mpina alikiri kupokea maombi ya mkuu wa wilaya huyo na kueleza kuwa serikali itakuwa tayari kujenga kiwanda cha kutengeneza mkaa mjini shinyanga “Na pengine katika Mbio za Mwenge Mwakani tukijaaliwa tunaweza kuzindua kiwanda hicho kama mradi wa mfano.” Alisisitiza Mpina. “Lazima tuwe na viwanda vya mkaa rafiki kwa mazingira sasa na wafanya biashara wa gas za manyumbani sasa ufike wakati nao washushe bei ili asilimia kubwa ya watanzania waweze kutumia nishati hiyo.” Alifafanua Mpina.

Akizungumzia suala ya usafi wa Mazingira ambapo sambaba na hilo Naibu Waziri Mpina Pia alishiriki zoezi la upandaji miti katika eneoa la Binzamata, alisema kuwa watanzania wana kila sababu ya kujijengea utamaduni wa usafi wao pamoja na mazingira kwani hata vitabu vitakatifu vinasisitiza usafi wa mazingira akitolea mfano kitabu cha Biblia takatifu cha kumbu kumbu la Torati 23:11-14 na kusema kuwa “Pahala Pachafu hapana Utukufu wa Mungu na hauwezi kuonekana mahali hapo na haya siyo maneno yangu wala ya Rais Magufuli, ni maneno ya biblia hivyo watendaji katika ngazi zote mzingatie utekelezaji wa sheria yya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake na kuwachulia hatua wale wote watakao kiuka sheria hiyo.”

“Ni jukumu la kila mtu kufAnya usafi na kila wilaya na Halmashauri ijetengenezee mwongozo na sheria ndogo ndogo katika eneo hili la usafi wa mazingira na lazima watu wawajibike.”

Naibu Waziri Mpina Pia alisisitiza zoezi la upandaji miti ili kuweza kukabiliana na athari zitokanazo na Mabadiliko ya tabia nchi na kurudisha uoto wa asili.

Akitolea mfano wa kasi ya serikali ya awamu ya tano katika zoezi la usafi wa mazingira Mpina alisema “ watu walidhani Mhe. Rais alivyozindua siku ya usafi zilikuwa ni nguvu za soda, kasi tuliyonza nayo ndiyo tutakayo maliza nayo, waharibifu wa mazingira lazima sheria iwashughulikie.” Alisisitiza Mpina.

Akizungumzia wananchi wanaoabudu siku ya Jumamosi Mpina alisema Sheria ndogo ndogo za mazingira za Halmashauri na miji ni vizuri zikaona namna ya kuweza kuwapa nafasi na wao ya kuabudu na kushiriki usafi katika siku hiyo.Siku ya kila Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi imetengwa na serikali ikiwa ni maalum kwa ajili ya usafi nchini.

No comments: