Sunday, October 16, 2016

WANANCHI WAJICHUKULIA SHERIA MKONONI WAUA MTU MMOJA ALIYEDAIWA KUWA NI PANYA ROAD MBAGALA JIJINI DAR ES SALAAM


Na Dotto Mwaibale

WANANCHI wa Mbagala sabasaba wamemuua kwa kumshambulia kwa mawe na kisha kumchoma moto kijana mmoja anayedaiwa kuwa ni mharifu wa kundi la panya road ambaye alikuwa na wenzake zaidi ya 15 ambapo wawili kati yao walipoteza fahamu kutokana na shambulio hilo.

Tukio hilo la kushambuliwa kwa panya road hao lilitokea majira ya saa 11 jioni katika eneo la Mbagala Sabasaba baada ya vijana hao kukurupushwa walipokuwa wakikimbia walipokuwa wakifanya uhalifu maeneo ya sabasaba Magengeni na Mbagala Zakhem.

Polisi waliofika eneo la tukio walilazimika kutumia risasi za moto kuwatawanya wananchi ili waweze kuuchukua mwili wa kijana huyo ambaye hakufahamika jina lake.

Akizungumza na mtandao wa www.habari za jamii.com mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Khalfan alisema usalama wa wananchi upo mashakani kufuatia kundi hilo la panya road.

"Hawa panya road walikuwa zaidi ya 15 wakitokea Mbagala Zakhem ambako walikuwa wakikimbizwa na wananchi baada ya kufanya uhalifu na walipofika hapa Sabasaba walizingirwa na wananchi ambapo watatu kati yao walianza kushambuliwa na mmoja kupoteza maisha baada ya kuchomwa moto " alisema.

Alisema vijana wawili kati yao walijeruhiwa vibaya na kupoteza fahamu lakini wenzao wengine walifanikiwa kukimbia kuelekea maeneo ya Yombo Dovya huku wakiahidi kurudi kulipiza kisasa kufuatiwa kuuawa kwa mwenzao.

Mkazi mwingine wa Mbagala kwa Mangaya aliyejitambulisha kwa jina la Seif Mwarami alisema vijana hao wataendelea kuuawa na wananchi kwa kuwa kila wanapokwenda kutoa taarifa polisi hawachukuliwi hatua yoyote badala yake uachiwa na kurudi mitaani kuendeleza uhalifu wao" alisema Mwarami.

Aliongeza kuwa kutokana na kuwa na umri mdogo wanashindwa kupelekwa kwenye mahakamani kutokana na kulindwa na sheria ya utoto jambo linalowatia hasira wananchi na kuamua kujichulia hatua mkononi na kuanza kuwaua.

Alisema vijana hao wamekuwa wakitokea maeneo ya Kitunda, Moshi Baa na Yombo kwenda kufanya uhalifu maeneo ya Mbagala.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi (ACP), Gilles Muroto alipopigiwa simu jana jioni ili kuzungumzia tukio hilo alisema alikuwa kwenye mkutano hivyo apigiwe baadae.

Hata hivyo jeshi la polisi mara kadhaa limekuwa likataa kuwepo kwa kundi hilo la panya road likieleza kuwa wao wanawahesabu kama walivyo wahalifu wengine wa matukio ya ujambazi na mengine.
 ' Samahani kwa kutumia picha hii nia ya kuitumia ni kujaribu kuonesha changamoto ilivyo kwa vijana hawa wanaopoteza maisha kwa kujihusisha na kundi hilo la panya road'

Wananchi wakiangalia mwili wa kijana anayedaiwa kuwa ni wa kundi la kihalifu la panya road aliyeuawa baada ya kufanya uhalifu maeneo ya Mbagala Zakhem Dar es Salaam leo jioni. Katika tukio hilo vijana wengine wawili walipoteza fahamu kutokana na kipigo cha wananchi.

 Wananchi wakiangalia mwili wa kijana huyo (haupo pichani).
Wananchi wakiangalia mwili wa kijana anayedaiwa kuwa ni wa kundi la kihalifu la panya road aliyeuawa baada ya kufanya uhalifu maeneo ya Mbagala Zakhem Dar es Salaam leo. Katika tukio hilo vijana wengine wawili walipoteza fahamu kutokana na kipigo cha wananchi.

No comments: