Friday, October 14, 2016

WADAU WAANZA KUPITIA MWONGOZO WA KUKABILIANA NA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA KATIKA MASOKO JIJINI DAR ES SALAAM

 Mwezeshaji wa Kisheria katika Soko la Ilala Mchikichini, Charles Beatus (kulia), akiwaongoza wenzake kupitia mwongozo wa kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia masokoni jijini Dar es Salaam leo. Mwongozo huo umeandaliwa na Shiriki la Equality for Growth (EfG). Kutoka kushoto ni msaidi wa kisheria kutoka Soko la Tabata Muslim,  Saada Juma na Said Mnijuka kutoka Soko la Ilala Mchikichini.
 Mwanasheria wa Manispaa ya Ilala, Bonaventule  Mwambaja (kulia), akitoa mada kwa wawezeshaji wa kisheria masokoni na wadau wengine.
 Majadiliano yakiendelea.
 Majadiliano yakiendelea.
wadau wakiwa kwenye mkutano huo.Dotto Mwaibale

Na Dotto Mwaibale

WASAIDIZI wa kisheria katika masoko ya Manispaa za Ilala na Temeke na wadau  mbalimbali wameanza kupitia mwongozo wa kupambana na ukatili wa kijinsia masokoni ulioandaliwa na shirika lisilo la Serikali la Equality for Growth (EfG) utakaosaidia kuwabana watu wanaofanya vitendo hivyo katika masoko mbalimbali.

Mwongozo huo unatajwa kuwa moja ya sababu kubwa zitakazosaidia kupunguza vitendo vya ukatili katika masoko ambavyo vinaonekana kukithiri, huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake.

Akizungumza wakati wa warsha ya kiufundi ya kupitia mwongozo huo Dar es Salaam leo, Ofisa Mradi wa Mpe Riziki si Matusi unaoendeshwa na shirika hilo, Suzan Sita alisema, mwongozo huo umeandaliwa kukabiliana na vitendo vya ukatili ambavyo vilikuwa havizingatiwi kwa ukaribu.

Alisema shirika hilo lilifanya utafiti ambao ulionesha kuwa japo kuna asilimia kubwa ya wanawake wanaokumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hwaripoti popote huku wale wanaoripoti utatuzi wa miggoro yao hauridhishi.

“Hata wakati wa utayarishaji wa mwongozo huu, ilidhihirika kwamba kuna sekta zinazotoa huduma mbalimbali hazishirikishwi kikamilifu… Mapendekezo yaliyotolewa na wadau wengi ni kuboresha utaratibu uliopo,” alisema Sita.

Alisema shirika hilo limeshirikiana na Ofisi ya Manispaa ya Ilala, Idara ya Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Diwani Ilala pamoja na taasisi zingine kuandaa mwongozo huo.

Alifafanua kuwa mwongozo huo unaainisha majukumu ya kamati zitakazohusika, pamoja na wadau wake kama polisi na Idara ya Ustawi wa Jamii katika kusikiliza na kutoa uamuzi, pia kuhamasisha na kutoa utetezi masokoni.

Alisema ili kukomesha ukatili wa kijinsia ni lazima kuwepo na sheria za kupambana na vitendo hivyo katika masoko. Mradi huo kwa sasa unatekelezwa katika masoko ya Temeke na Ilala jijini la Dar es Salaam.

Mkutano uliwashirikisha viongozi wa masoko, maofisa wa polisi kutoka dawati la jinsia, viongzi wa manispaa, Idara ya Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Diwani Ilala, wasaidi wa haki za kisheria na kamati za maendeleo ya kata.

Akizungumzia kuhusu mwongozo huo, mjumbe wa bodi ya kamati ya mitumba ya soko la Mchikichini, Said Mnijuka alisema, utasaidia kupunguza kero za wateja na baadhi ya wafanyabiashara kutokana na baadhi ya mambo yamekuwa yakifanyika kiholela.

Alisema awali vitendo vya ukatili wa kijinsia vilikuwa ni kwa asilimia 100 lakini tangu kuanza kwa mradi huo vimepungua hadi kufikia asilimia chini ya 70.

No comments: