Thursday, October 13, 2016

Vijana jitokezeni kupima ukimwi kujenga taifa lililo na afya bora – Mkwinda

Mratibu kutoka Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA) Bw. Joseph Muhoja (kulia) akizungumza na vijana wenye umri chini ya miaka 18 kuhusu namna kijana anavyopaswa kujitambua na maambukizi ya virusi vya ukimwi leo katika viwanja vya Sabasaba kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Simiyu.
Baadhi ya vijana wenye umri chini ya miaka 18 wakifuatilia mada iliyokua ikitolewa na Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi leo katika viwanja vya Sabasaba kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Simiyu.
Mjumbe kutoka Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Bibi. Happiness Malamala (kulia) akitoa elimu ya namna ya kutumia kinga kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa vijana waliotembelea banda la NACOPHA leo katika viwanja vya Sabasaba kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Simiyu.
Mwezeshaji kutoka Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Bw. Hamidu Mkwinda (kulia) akitoa elimu ya kujitambua na namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi wakati wa ziara ya wajumbe kutoka NACOPHA walipotembelea katika kituo cha mabasi cha Somanga leo katika Mkoa wa Simiyu kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Vijana wakifanya mashindano ya kula biskuti na kunywa soda wakati wa ziara ya wajumbe kutoka Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA) walipotembelea kituo cha mabasi cha Somanga kutoa elimu ya nanma ya kujitambua na kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi leo Mkoani Simiyu kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.

…………………………………………………

Na: Genofeva Matemu – WHUSM

Vijana nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao ili waweze kujitambua na kupata mbinu mbadala zitakazowazesha kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi ili kujenga taifa lililo na afya bora.

Hayo yamesemwa na Mwezeshaji kutoka Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA) Bw. Hamidu Mkwinda alipokua akizungumza na vijana waliojitokeza kupata elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi wakati wa wiki ya vijana kitaifa na kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru leo katika Viwanja vya Sabasaba Mkoani Simiyu.

“Vijana wanatakiwa kujitambua na kujua haki zao ili wasije wakaangukia katika wimbi la ulaghai na anasa ambazo zitawapelekea kutokufikia malengo yao na wakati mwingine kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi bila kutarajia” amesema Bw. Mkwinda.

Aidha Bibi. Happiness Malamala kutoka NACOPHA amewataka vijana kutokukata tamaa pale wanapojitambua kuwa wamepata maambukizi ya virusi vya ukimwi kwani kuwa na virusi vya ukimwi sio mwisho wa maisha bali watambue kwamba virusi vya ukimwi ni kama magonjwa mengine yasiyotibika kama vile kisukari, kansa na presha.

Naye Mratibu kutoka Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA) Bw. Joseph Muhoja amesema kuwa NACOPHA inashiriki katika Wiki ya Vijana kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kuhakikisha vijana wanajua haki zao za msingi hususani vijana wa kike waliopata jukumu la kuwa wazazi katika umri mdogo wajue aina ya ukatili wa kijinsia na jinsi ya kukabiliana nao.

Bw. Muhoja amesema kuwa NACOPHA imejipanga kutoa amasa kwa vijana kuhusu ushauri nasaha na kupima ili wajue hali yao ya kiafya na jinsi ya kujikinga na kuwakinga wengine, lakini pia kupitia maonesho haya vijana wanapata elimu ya afya ya uzazi na makuzi ili vijana waweze kujikinga na mimba zisizotarajiwa au kupata watoto katika wakati usio sahihi.

NACOPHA kupitia ufadhili wa watu wa Marekani (USAID) inatekeleza mradi wa SAUTI YETU, mradi unaojihusisha na masuala ya ufuatiliaji, utendaji wa serikali na masuala ya utawala bora, na pia kuwajengea uwezo wananchi waishio na VVU na UKIMWI ili sauti zao zisikike, waweze kushirikishwa katika mambo ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kutambua haki za msingi, kisheria na kuchangia mawazo katika utekelezaji wa sera na sheria mbalimbali.

No comments: