Monday, October 10, 2016

UZINDUZI WA AWAMU YA PILI YA MRADI WA KUONGEZA SIFA ZA KUAJIRIKA KUPITIA MAFUNZO YA UFUNDI STADI (EEVT) KWA MIKOA YA MTWARA NA LINDI.

 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya (wa tatu kutoka kushoto) akila keki na viongozi na watendaji mbalimbali wa taasisi za kiserikali na wadau wa maendeleo kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Kuongeza Sifa za Kuajirika Kupitia Mafunzo ya Ufundi Stadi (EEVT)kwa mikoa ya Mtwara na Lindi. Uzinduzi huo ulifanywa na Mheshimiwa Naibu Waziri Mhandisi Manyanya, Jumanne, 27 Septemba, 2016 katika chuo cha VETA Mtwara.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya (wa tatu kutoka kushoto) akikata keki maalum kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Kuongeza Sifa za Kuajirika Kupitia Mafunzo ya Ufundi Stadi (EEVT) kwa mikoa ya Mtwara na Lindi. Uzinduzi huo ulifanywa na Mheshimiwa Naibu Waziri Mhandisi Manyanya, Jumanne, 27 Septemba, 2016 katika chuo cha VETA Mtwara.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya (wa tatu kutoka kushoto) akikata keki maalum kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Kuongeza Sifa za Kuajirika Kupitia Mafunzo ya Ufundi Stadi (EEVT)kwa mikoa ya Mtwara na Lindi. Uzinduzi huo ulifanywa na Mheshimiwa Naibu Waziri Mhandisi Manyanya, Jumanne, 27 Septemba, 2016 katika chuo cha VETA Mtwara.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya, leo Jumanne, 27 Septemba, 2017 amezindua Awamu ya pili ya Mradi wa Kuongeza Sifa za Kuajirika Kupitia Mafunzo ya Ufundi Stadi (EEVT) katika Mikoa ya Mtwara na Lindi. 

Uzinduzi huo umefanyika katika Chuo cha VETA Mtwara.
Katika Mradi huo makampuni ya Mafuta na Gesi chini ya mwamvuli wa mradi wa Kuchakata Gesi Asilia (TLNG) unaojumuisha BG/Shell, ExonMobil, Ophir Energy, Pavilion Energy, na Statoil, yametoa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 1.9, karibu sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 4, ili kuendeleza mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kuajirika, hususani kwa vijana wa mikoa ya Lindi na Mtwara.  

Kiasi hicho cha fedha kitatumika katika kutekeleza Awamu ya pili Mradi wa Kuongeza Sifa za Kuajirika Kupitia Mafunzo ya Ufundi Stadi (EEVT) utakaotekelezwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Shirika la Kimataifa la Huduma za Kujitolea (VSO) na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kupitia mpango wake wa Kuendeleza Ujuzi katika Sekta ya Mafuta na Gesi (SOGA).

Mradi wa EEVT unalenga katika kuboresha uwezo wa kuajirika kwa vijana wa mikoa ya Mtwara na Lindi, kwa kuzingatia kuongezeka kwa mahitaji nguvukazi yenye ujuzi katika sekta ya uziduzi (extractive industry) ikijumuisha uchimbaji madini, gesi na huduma zinazoendana na maeneo hayo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya alizindua rasmi awamu ya pili ya mradi huo katika hafla iliyofanyika kwenye chuo cha VETA Mtwara jana (Jumanne, Septemba 27, 2016).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi, mwakilishi wa TLNG, Bi. 
Kate Sullam alisema kuwa mashirika hayo yameamua kutoa ufadhili wa awamu ya pili ya mradi baada ya kuona mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu ya kwanza ya mradi uliotekelezwa na VSO and VETA kupitia vyuo vya VETA Mtwara na Lindi, mwaka 2012 hadi 2015

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya aliwashukuru TLNG na wadau wote katika juhudi zao za kusaidia kuendeleza ujuzi nchini na kuwaomba makampuni mengine kuingia kwenye mradi huo kwani utawanufaisha pia wao kwa kuwapatia nguvukazi yenye ujuzi, hivyo kuongeza tija katika makampuni yao.

Aliwaasa wakazi wa mikoa ya Mtwara na Lindi kushiriki kwa kujiunga katika mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kunufaika vyema na fursa za ajira zinazozidi kuongezeka katika ukanda wa Kusini mwa Tanzania kutokana na kuongezeka kwa uwekezaji unaochangiwa na kugundulika kwa gesi asilia.

“Mafunzo ya ufundi katika nchi nyingi yamekuwa chachu ya maendeleo endelevu. Nchi nyingi zilizoendelea zinatilia mkazo elimu na mafunzo ya ufundi stadi. Nchi kama Japani haina rasilimali za asili lakini iliwekeza katika rasilimali watu na kuwa nchi ya pili duniani kiuchumi,” alisema.  

Kaimu Mkurugenzi Mkuuwa VETA, Bw. Geoffrey Sabuni alisema kuwa Mradi alisema kuwa Mradi wa EEVT ni miongoni mwa miradi ya kipekee katika kusaidia VETA kufikia Malengo Namba 1 na 2 ya Mpango Mkakati wa Nne wa VETA ambayo yanahusu Kupanua Fursa za Upatikanaji wa Mafunzo ya Ufundi Stadi na Kuongeza Uwezo wa Kuajirika kwa Wahitimu wa Ufundi Stadi.

Akiwasilisha kuhusu Mradi, Mkurugenzi wa Mafunzo wa VETA, Bi. Leah Dotto alisema kuwa awamu ya kwanza ya mradi imewanufaisha wanafunzi 477 wakiwemo wasichana 103 na wavulana 374, idadi ambayo ni zaidi kwa kiasi kikubwa kuliko lengo la awali la mradi ambalo lilikuwa kufikia vijana 280.

Alitaja mafanikio mengine ya kujivunia kutokana na mradi huo kuwa ni pamoja na kuongeza uwezo wa vijana kuajirika kwa urahisi ambapo zaidi ya asili 51 ya wahitimu wa ufundi waliokuwa kwenye mradi huo walipata ajira ndani ya miezi sita baada ya kuhitimu na asilimia 93 waliweza kupata vyeti vya kutambulika kimataifa baada ya kufaulu mitihani ya Taasisi ya City and Guilds ya Uingereza. 

Alisema kuwa awamu ya kwanza ya mradi ilihusisha fani sita ambazo ni Uchomeleaji na Uungaji Vyuma, Useremala, Ufundi Bomba, Umeme, Utayarishaji wa Chakula na Ufundi Magari..

Alisema, awamu ya pili itaongeza fani tatu mpya ambazo ni Ujengaji wa majukwaa (Scaffolding and Rigging), Upakaji rangi viwandani (Industrial painting) na Uendeshaji wa mitambo mizito (Heavy duty Equipment Operation) kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira hususan sekta ya gesi na mafuta.

“zaidi ya wanafunzi 550 wanatarajiwa kunufaika na mradi kwa kupata ujuzi unaotambulika kimataifa; zaidi ya walimu 30 watapata mafunzo mafunzo maalum; zaidi ya wanafunzo 105 watafundishwa juu ya mfumo wa Pasi ya Afya na Usalama kazini na hatimaye kutunukiwa pasi za kimataifa za Afya na Usalama Kazini; na zaidi ya makampuni 30 yanatarajiwa kuingia kwenye mradi kupitia kutoa fursa za mafunzo kiwandani, jambo ambalo ni kitovu cha awamu ya pili ya mradi,” alisema.

No comments: