Tuesday, October 11, 2016

UFUNGUZI WA MKUTANO WA BUNGE LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI, UNGUJA

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akifuatana na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Daniel F.Kigeda(kulia) na Spika wa Baraza l;a Wawakilishi Zanzibar Mhe,Zubeir Ali Maulid (kushoto) baada ya Kuufungua Mkutano wa Pili wa kikao cha tano cha Bunge la tatu la Afrika Mashariki uliofanyika leo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi "B"Unguja.
-------------------------------------

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amelisisitiza Bunge la Jumuiya ya Afika Mashariki (EALA) kuweka mikakati imara katika kukuza sekta ya utalii kwa nchi za Jumuiya hiyo kwani idadi ya watalii wanaoingia kwenye eneo hilo hailingani na vivutio viliopo. 
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani Mjini Zanzibar, wakati akizindua Mkutano wa Pili wa Kikao cha Tano cha Bunge la Tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) unaofanyika Zanzibar. 
Amesema kuwa pamoja na kwamba eneo hilo la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ina vivutio vingi vya utalii, idadi ya watalii wasiozidi milioni 5 wanaoingia katika eneo hilo kutoka nchi za nje ni ndogo ikilinganishwa na watalii Bilioni moja wanaosafiri kwa mwaka duniani kote.

Dk. Shein ameongeza kuwa kiasi hicho cha watalii hakilingani na umaarufu pamoja na vivutio vilivyopo katika eneo hilo la Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na kueleza matumaini yake kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka iwapo juhudi za makusudi zitachukuliwa. 
“Jumla ya watalii waliotembelea Zanzibar mwaka 2014 walikuwa 311,801 ambapo lengo letu ni kufikia watalii 500,000 mwaka 2020”,alisema Dk. Shein. 
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza Miswada inayotarajiwa kujadiliwa katika kikao cha Bunge hilo ikiwa ni pamoja kuweka Sheria kali zitakazopiga marufuku biashara haramu ya kusafirisha binaadamu ambayo ni uhalifu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu.

Akizungumzia kuhusu Mswada wa kudhibiti matumizi ya vifaa vinavyotengenezewa plastiki ikiwemo mifuko, Dk. Shein alisema kuwa Mswada huo umekuja wakati muwafaka na kwamba Zanzibar tokea mwaka 2011 imeshaaza kutekeleza kwa vitendo Sheria ya kupiga marufuku uagiziaji na uzalishaji wa mifuko ya plastiki. 
Alisema kuwa uwamuzi wa kupiga marufuku bidhaa hizo Zanzibar ulichukuliwa baada ya kuona kwamba mifuko hiyo inaharibu mazingira, yakiwemo mazingira ya bahari pamoja na kuathiri sekta muhimu ya utalii. 
Kwa upande wa Mswaada wa Usawa wa Kijinsia na maendeleo, Dk. Shein alisema kuwa anamatumaini kuwa Mswada huo utatoa njia ya kuinua usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo. 
Dk. Shein alitoa pongezi kwa uwamuzi wa Bunge hilo kwa kuamua kuifanya Zanzibar kuwa Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na kueleza kuwa uamuzi huo ni sahihi kutokana na ukweli kwamba Kiswahili sanifu kinazungumzwa Zanzibar na kuahidi kutoa kila ushirikiano uanostahiki kufanikisha shughuli za Kamisheni hiyo. 
Ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake imechukua juhudi za makusudi za kukiimarisha Kiswahili kufikia kiwango cha Kimataifa na tayari imeingizwa kwenye mitaala ya vyuo vikuu kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) hadi kufikia kiwango cha Shahada ya Uzamifu. 
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuishukuru nchi za Jumuiya hiyo kwa namna ilivyojali na kushiriki kikamilifu kuwasaidia wananchi wa Tanzania walioathirika kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 huko Kagera na kueleza kuwa hatua hiyo inathibitisha kuwa mashirikiano baina ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo hayaishii kwenye mikataba laniki imeenda mbali zaidi kwa kujali ubinaadamu. 
Akizungumzia suala zima la changamoto ya ajira ambayo inaikabili nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Shein alisema kuwa nchi hizo hazina budi kuondoka zilipo ambapo mchango wa Pato la Taifa katika nchi hizo linakisiwa kuwa ni asilimia 8.9 ambayo ni kidogo kufikia lengo la asilimia 25 ambayo nchi hizo zimejiwekea kufikia ifikapo mwaka 2032.

Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina hiostoria ya kuwa ni kitovu kikubwa cha biashara ambapo ilitumika na wafanyabiashara pamoja na wavumbuzi waliokuwa wakisafiri katika ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo Serikali ya M apinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba inaamini kwamba inaweza kurejesha hali yake hiyo ya zamani ambapo hivi sasa imeamua kuimarisha miundombinu ya bandari, viwanja vya ndege na barabara ili iweze kufikia azima yake hiyo. 
Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein aliwataka Wajumbe wa Bunge hilo kuwa tayari kushirikiana na Serikali katika kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha biashara katika ukanda huo wa Afrika ya Mashariki na Kati. 
Dk. Shein ameongeza kuwa maendeleo ya viwanda pekee ndio yatakayowezesha kuondoa changamoto ya ajira katika eneo hillo. 
Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar  Zubeir Ali Maulid akitoa hutuba yake alipongeza kwa kufanyika mkutano huo na kueleza kuwa kufanyika mkutano huo si tu utaimarisha mashirikiano baina ya Mabunge hayo mawili lakini pia, utatoa fursa zaidi ya pande mbili hizo kujifunza namna ya kuendesha shughili za Bunge kutoka kila upande. 
Mapema Katibu Mkuu wa Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki Daniel Fred Kidega alisisitiza suala la amani na utulivu katika eneo la nchi zinazounda Jumuiya hiyo ili wananchi wake waweze kuendelea na shughuli zao bila ya kuhofia kupoteza maisha yao.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuisifu Zanzibar na kueleza kuwa kuna uwezekano mkubwa kuifanya Zanzibar kuwa eneo muhimu la biashara katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na kueleza kuwa inaweza kuwa ni Dubai ya Afrika.

No comments: