Tuesday, October 18, 2016

NHC YAIBUKA KIDEDEA .MAOMBI YA MBOWE HOTELS YATUPILIWA MBALI

MAHAKAMA Kuu Tanzania, Divisheni ya Ardhi, imetupilia mbali maombi ya Kampuni ya Mbowe Hotels Limited inayomikiwa na Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe Freeman Mbowe ya kutaka kurudishwa kwenye jengo la Billicanas kwa sababu waliondolewa katika jengo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kufuata taratibu zote za kisheria.
Aidha, Jaji Sivangilwa Mwangesi alisema shirika hilo lilifuata taratibu zote kumwondoa mlalamikaji katika jengo hilo na kwamba inashikilia mali zake kihalali hadi atakapolipa kodi ya Sh.Bilioni 1.3 kama anavyodaiwa.

Akisoma uamuzi huo mapema jana Jaji Mwangesi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama yake iliamua kutupilia mbali maombi hayo yaliyofunguliwa chini ya hati ya dharula bila kulipwa gharama.
Jaji alisema madai ya mlalamikaji kwamba aliondolewa kinyume cha sheria katika jengo hilo na kampuni ya udalali isiyosajiliwa hayana mashiko kisheria mahakama inafutilia mbali kesi hiyo.
“Mahakama hii baada ya kupitia hoja za pande zote mbili imeona kwamba mlalamikiwa wa kwanza NHC alifuata taratibu zote kumtoa mlalamikaji katika jengo hilo … pia imeona kwamba kampuni ya udalali Foster Auctioneers and General Traders ilifanyakazi ya kuondoa mali zake kihali, inatupilia maombi haya bila kulipwa gharama ya kesi hii” alisema Jaji Mwangesi.
Aidha akifafanua zaidi jaji alisema pamoja na madai ya kuwepo kwa mkataba kati ya NHC na Mbowe, mkataba huo haukuwahi kutekelezwa kwa hiyo ni sawa na kwamba haupo.Upande wa mlalamikaji uliongozwa na Mawakili Peter Kibatala akisaidiana na John Mallya.

Upande wa walalamikaji uliongozwa na Mawakili Aloyce Sekule, Aliko Mwamanenge na Mariam Mungura.Wakili Mwamanenge akizungumza na Globu ya Jamii nje ya viunga vya mahakama hiyo, alisema mlalamikaji alisema mahakama imetenda haki na kwamba mlalamikaji alidai kuwa na mkataba kati yake na NHC, lakini mahakama hiyo imeona mkataba huo haukuwahi kutekelezwa.
“Mahakama imeona dalali alifanya kazi yake kwa kufuata taratibu za kisheria na hata hizo mali zinashikiliwa na mteja kihalali hadi atakapolipa deni la Sh. Bilini 1.3 ndipo atarejeshewa mali hizo” alisema wakili Mwamanenge.
Kwa upande wake Wakili Mallya alisema wamewasilisha maombi ya kuomba nakala ya uamuzi ili waombe marejeo Mahakama ya Rufani Tanzania.
Pia, wamepeleka maombi ya kuomba chochote kisifanyike katika jengo hilo na kuhusu mali za Mbowe  mpaka uamuzi utakapotolewa na Mahakama ya Rufani dhidi ya maombi yao ya marejeo.
Alisema Jaji katika uamuzi wake amesema mkataba kati ya NHC na Mbowe haukuwahi kutekelezwa na haupo kisheria kwa hiyo tunasubiri nakala ya uamuzi tuupitie ili tuwasilishe maombi ya marejeo mahakama ya juu” alisema Wakili Mallya.
Maombi hayo yaliyosajiliwa mahakamani hapo kwa namba 722 ya 2016 dhidi ya NHC, yalifunguliwa chini ya hati ya dharula baada ya Mbowe kuondolewa kwenye jengo hilo mapema Septemba Mosi, mwaka huu.
Katika hati ya kiapo Mbowe alidai kwamba yeye na mlalamikaji katika mgogoro huo warejee kwenye usuluhishi kwa mujibu wa mkataba wa ubia huo.
Hata hivyo, upande wa walalamikiwa ulipinga hatua hiyo kutokana na kutokuwepo kwa nyaraka hizo mahakamani hapo juu ya mwenendo wa mchakato huo wa usuluhishi, kwani walitoa ilani ya kumhamisha Mbowe katika jengo hilo kwa kufuata sheria.
Pia ilidaiwa kuwa Mbowe katika jengo hilo ni mpangaji na hata mkataba wa ushirikiano unaodaiwa umefanyika kati yao kwa sasa hauwezi kufanyakazi kwa kuwa ulishakwisha muda wake.Katika madai ya msingi Mbowe alidai kuwa si mpangaji katika jengo hilo, bali ni mmbia ambaye anamiliki asilimia 75 katika uendeshaji wake huku NHC wakimiliki asilimia 25. 
Hoja nyingine alidai kuwa, hata kama angekuwa anadaiwa kodi kama wanavyodai NHC, kuondolewa kwake kulifanywa bila kuzingatia sheria kwani hakukuwa na amri ya mahakama inayowapa walalamikiwa nguvu ya kisheria ya kumwondoa. 
Kwa upande mwingine, Mbowe kupitia hati ya kiapo alisema hadaiwi hata senti tano na NHC kama pango la jengo la Billcanas, na kwamba amekuwa akilipa tozo zote zinazotakiwa kwa mujibu wa mkataba baina yake na shirika hilo.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo aliyoiwasilisha mahakamani, mmiliki huyo wa Kampuni ya Mbowe Hotels Ltd alidai kwa mujibu wa mkataba wa ubia wa pande hizo mbili, anapaswa kuwalipa NHC mapato ya jengo kila mwezi.
Katika hati hiyo, Mbowe alisema hadaiwi fedha yoyote kwani amekuwa akitekeleza matakwa hayo ya kimkataba kama yalivyosainiwa mwaka 1997, huku akiambatanisha ushahidi wa risiti ya fedha ambazo amekuwa akilipa.



No comments: