Wednesday, October 5, 2016

IMPACTAFYA YAZINDUA KAMPENI YA KUWAHAMASISHA WATANZANIA KUWA NA TABIA YA KUFANYA MAZOEZI KUEPUKANA NA MATATIZO YA KIAFYA

Mkurugenzi wa IMPACTAFYA, Bhakti Shah akizungumza mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani),katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO mapema leo jijini Dar,kuhusiana na uzinduzi rasmi wa program ya Mazoezi Movement to Fitness kuhamasisha Watanzania kuwa na kaliba ya kufanya mazoezi kuepukana na matatizo yatokanayo na kutofanya mazoezi,Kulia ni mmiliki wa blog ya jamii 8020fashions,Shamim Mwasha ambaye ni  mmoja wa watakaokuwa wahamasishaji wakubwa kuhusiana na programu hiyo na shoto ni  mshauri wa masuala ya afya kwa Jamiii,Dkt Fred  Mashili.
Mmiliki wa blog ya jamii 8020fashions,Shamim Mwasha ambaye ni  mmoja wa watakaokuwa wahamasishaji wakubwa kuhusiana na programu hiyo,akitoa ufafanuzi zaidi kwa Wanahabari namna ya uhamasishaji huo utakavyofanyika,shoto ni Mkurugenzi wa IMPACTAFYA, Bhakti Shah.
Pichani kati Dkt Fred Mashili ambaye ni mshauri wa masuala ya afya kwa Jamiii na mmiliki wa Blog ya Jamii Health akielezea umuhimu wa kufanya mazoezi na namna ya kuijenga na kuilinda afya yako isikumbwe na magonjwa mbalimbali yatokanayo na kutokufanya mazoezi.


KAMPUNI ya IMPACTAFYA imezindua rasmi program ya Mazoezi Movement to Fitness kuhamasisha Watanzania kuwa na kaliba ya kufanya mazoezi kuepukana na matatizo yatokanayo na kutofanya mazoezi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Idara ya  Habari MAELEZO, Mkurugenzi wa IMPACTAFYA, Bhakti Shah amewataka watanzania kuamka na kulichukulia suala la kufanya mazoezi kuwa jambo la kupewa kipaumbele.

Alisema Tanzania iko hatarini kupoteza mamillioni ya watu ambao ni nguvu kazi ya jamii kwa kutofanya mazoezi, “Ugonjwa wa kisukari ambao kwa kawaida huwapata watu wazima unaongezeka kwa haraka ulimwenguni pote na sasa hata vijana wapo hatarini kwa sababu hawafanyi mazoezi, asilimia 20 hivi ya vifo vyote vilivyotokea miongoni mwa watu walio na umri wa miaka 21 hadi 45, vilisababishwa na kukosa kufanya mazoezi.”

Alihoji kama Teknolojia Ni Baraka au Laana? Bhakti alisema “Leo watu wana afya bora na wanaishi muda mrefu zaidi kuliko wale walioishi karne nyingi zilizopita kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia ambayo imekuja na Vifaa vya kisasa vya matibabu, lakini ni teknolojia hiyo hiyo iliyoleta mashine ambazo zimesaidia kupunguza kazi nyingi ngumu na hivyo watu wengi waishi maisha ya kukaa tu bila kufanya mazoezi yakutosha.” alisema

“Katika ripoti iliyochapishwa hivi karibuni yenye kichwa cha habari International Cardiovascular Disease Statistics, Shirika la Moyo la Marekani lilieleza kwamba “mabadiliko ya kiuchumi, watu kuhamia mijini, usitawi wa viwanda, na kuenea kwa biashara za kimataifa, na mitandao ya kijamii, imesababisha kuleta mabadiliko katika mitindo ya maisha ambayo huchangia ugonjwa wa moyo.” Ripoti hiyo inataja “kutofanya mazoezi na kula vyakula visivyofaa” kuwa mambo yanayochangia sana ugonjwa huo.

Alisema Mtindo wa maisha wa leo wa mijini, mfanyakazi anaweza kuketi mbele ya kompyuta karibu siku nzima, aende mahali popote atakapo kwa gari lake, na atazame televisheni na kubrows kwenye mitandao ya kijamii jioni yote, na hivyo kujiingiza katika maradhi ambayo yamehatarisha maisha.

“Watu wengi zaidi wanapendelea kutumia motokaa na pikipiki badala ya baiskeli, asilimia 25 ya safari zote hazizidi kilometa moja hivi, asilimia 75 ya safari nyingi fupi hufanywa kwa gari. Hii ni hatari” alisema.

Alisema, Teknolojia ya kisasa pia imefanya watoto wakae tu bila kufanya mazoezi ya kutosha. Uchunguzi mmoja ulioonyesha kwamba kadiri michezo ya video inavyozidi kuwa yenye kufurahisha na halisi, ndivyo watoto wanavyotumia wakati mwingi zaidi kutazama televisheni na vitumbuizo vingine ambavyo huwafanya watoto hao wakae tu bila kufanya mazoezi ya kutosha.

Akiongela hatari za kukaa tu bila kufanya Mazoezi ya kutosha alisema watu wengi wanapatwa na matatizo ya kimwili, kiakili, na kihisia. Akitolea mfano, hivi karibuni shirika moja la afya nchini Uingereza liliripoti kuwa “Watoto wasiofanya mazoezi wanaweza kukabili hatari ya kutojiheshimu, kuwa na wasiwasi mwingi na mifadhaiko mingi. Ripoti hiyo ilisema kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto hao watavuta sigara na kutumia dawa za kulevya kuliko watoto wanaofanya mazoezi.

Bhaktti alieleza kuwa Watu wengi hupatwa na shinikizo kubwa la damu, kiharusi na ugonjwa wa moyo, aina fulani za kansa, ugonjwa wa mifupa, na uwezekano mkubwa wa kuwa wanene kupita kiasi kwa kula vyakula vyenye kalori nyingi na kutofanya mazoezi.

“Swala la kutofanya mazoezi ni TIME BOOM . Matatizo na madhara yatokanayo na kutofanya mazoezi ni ya Ulimwenguni Pote, ni wakati sasa Tanzania Kuamka. Tunayaita mashirika, makampuni na watu binafsi kuungana nasi katika MOVEMENT TO FITNESS kuliokoa taifa hili.

Alisema tayari zipo Nchi nyingi sasa zinazoendesha kampeni zao za Kitaifa za kufanya mazoezi kama vile Mexico, Brazili, Jamaika, New Zealand, Finland, Shirikisho la Urusi, Morocco, Vietnam, Afrika Kusini, na Slovenia. inafaa kwa Tanzania kuwa na wasiwasi kuhusu hali ilivyo sasa.

“Ingawa hatari za kutofanya mazoezi kabisa zimezungumziwa sana, sisi tunasema si lazima uwe na membership card ya gharama kubwa kuwa na afya bora. Unaweza kutembe na kukumbia na ratiba nzuri ya kufanya mazoezi hayo” alisema.

“Kuendesha kampeni yetu tumewateua machampion wetu “Shamim Mwasha, mmiliki wa blog ya jamii 8020fashions na Monica Joseph, Mon Finance pamoja na wengine akiwemo msanii Manyolee ambaye ametunga na kuimba wimbo wakwanza Tanzania kuhamashisha ufanyaji wa mazoezi.”

“Kupitia Movement to fitness tuna kipengele cha Fun run walk ambayo yakwanza ilifanyika mwezi uliopita wa september, fun run walk nyingine inafuata mwezi huu wa kumi, tarehe 8 siku ya jumaamosi pale Golden tulip oysterbay kuanzia saa 10 hadi saa 1 usiku, ambapo tutatoa mbinu mbalimbali za kuwa fit kiakili na kimwili. Tunawakaribisha kujiunga nasi kwa kujiandikisha kupitia no ya simu 0754 694643 au email move@impactafya.com

“Kila mmoja wetu ana daraka la kutunza afya yake mwenyewe. Jiulize, ‘je nimefanya mazoezi ya kutosha? Ikiwa sivyo, ninaweza kufanya nini ili niongeze mazoezi yangu?’ unaweza kuwasiliana nasi na kujiunga na Movement to Fitness ambayo inasimamia na kufuatilia mwendo wako mzima wa kuishi kama mwanamazoezi.

No comments: