Wednesday, September 21, 2016

PROFESA MUHONGO AWAKUTANISHA WABUNGE WA MARA NA KUWAKABIDHI VITABU VYA SHULE

Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa tatu kutoka kulia) akizungumza jambo wakati wa makabidhiano ya vitabu vya shule za Sekondari na Msingi. Wengine katika picha ni baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Mara kutoka vyama mbalimbali ambao walifika kwa ajili ya kukabidhiwa vitabu.
Shehena ya vitabu ambavyo vilikabidhiwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa Wabunge wote wa Mkoa wa Mara.
Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akimkabidhi vitabu Mbunge wa jimbo la Tarime, Ester Matiko (Chadema) katikati. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Naano ambaye alishuhudia makabidhiano hayo.
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) kulia akitoa shukrani kwa Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kushoto) mara baada ya kukabidhiwa vitabu vya shule za Msingi na Sekondari kwa ajili ya shule za jimbo lake. Wengine katika picha ni wabunge wa Mkoa huo.
Mbunge wa jimbo la Bunda Vijijini, Boniface Mwita (CCM) katikati akipokea vitabu vilivyokabidhiwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto). Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Vicent Naano.
Mbunge wa jimbo la Serengeti na Katibu wa Umoja wa Wabunge wa Mkoa wa Mara, Marwa Ryoba (Chadema) akizungumza wakati wa makabidhiano ya vitabu. Wa pili kulia ni Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye alikabidhi vitabu hivyo kwa wabunge wa Mkoa huo.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekabidhi vitabu vya sayansi na hesabu 25,000 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500 kwa Wabunge wote wa Mkoa wa Mara kwa ajili ya shule za msingi na sekondari mkoani humo.

Makabidhiano hayo yamefanyika jana katika uwanja wa Mukendo uliopo Musoma Mjini Mkoani Mara na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Vicent Nnano na wananchi mbalimbali waliofika katika uwanja huo ili kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Profesa Muhongo alisema lengo la kukabidhi vitabu hivyo kwa wabunge hao ni kuhakikisha elimu hususan katika masomo ya sayansi inaboreka ili kuwa na wanayasansi wengi zaidi.

Alisema vitabu hivyo ni kwa majimbo yote ya Mkoa wa Mara bila kujali itikadi za kivyama. "Ndugu zangu vitabu hivi ni kwa ajili ya kuboresha elimu kwa watoto wa Mkoa huu, ninakabidhi kwa wabunge wote bila kubaguana. Itikadi za kivyama hazina nafasi katika suala la maendeleo," alisema Profesa Muhongo.

Aliongeza kuwa anatarajia kupokea shehena nyingine ya vitabu ambayo atakabidhi kama zawadi ya Krismasi kwa shule zenye maktaba za Musoma Vijijini.

"Lengo langu ni kuhakikisha Mkoa wetu wa Mara unarudisha hadhi yake ya ufaulu mashuleni hasa katika masomo ya sayansi kama ilivyokuwa huko zamani," alisema.

Aliongeza kwamba ajenda kuu ya wabunge wote wa Mkoa wa Mara ni maendeleo kwa wananchi na kuahidi kuwa ataendelea kutoa misaada mbalimbali katika majimbo yote ya mkoa huo.

"Huu ni mwanzo na sio mwisho; ninaahidi kuendelea kushirikiana na wabunge wote wa Mkoani hapa katika kuhakikisha kunakuwa na maendeleo endelevu," alisema Profesa Muhongo.

Alisema Wabunge wa Mkoa wa Mara wameamua kuweka kando tofauti zao za kisiasa na badala yake kushirikiana ili kuleta maendeleo kwa wananchi waliowachagua.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Katibu wa Umoja wa Wabunge wa Mkoa wa Mara ambaye ni Mbunge wa jimbo la Serengeti (Chadema), Marwa Ryoba alimpongeza Profesa Muhongo kwa upendo na uzalendo alionao kwa wananchi wa Mara na kuahidi kuendelea kumuunga mkono kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa huo.

"Profesa Muhongo ni Mwenyekiti wa Umoja wetu, tunafarijika na tunayo bahati sana kuwa na Mwenyekiti wa aina hii maana yeye si mtu wa maneno zaidi hua ni vitendo," alisema Ryoba.

Ryoba aliahidi kuhakikisha vitabu vinatumika kama ilivyokusudiwa na aliwasihi wananchi wa Mara kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Profesa Muhongo za kuwaletea maendeleo.

Wabunge wengine waliokuwepo kwenye makabidhiano hayo ni Ester Matiko (Tarime Mjini, Chadema), John Heche (Tarime Vijijini, Chadema), Boniphace Mwita (Bunda Vijijini, CCM), Kangi Lugora (Mwibara, CCM) na ambao hawakufika walituma wawakilishi.

Wabunge hao kwa pamoja walimshukuru Profesa Muhongo na walimpongeza kwa uzalendo wake na kueleza kuwa ni mfano wa kuigwa.

1 comment:

Anonymous said...

GOOD! WAVITUMIE KWA USAHIHI NDO VIONGOZI TUNAOWATAKA.APELEKE NA MKOA MWINGINE BASI!