Thursday, August 11, 2016

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU KUAGIZA NJE MAKAA YA MAWE, JASI

Baadhi ya wazalishaji, wanunuzi na wafanyabiashara wa madini ya jasi na makaa ya mawe wakijisajili kabla ya kuanza kwa mkutano ulioongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani hivi karibuni katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati) akizungumza na wazalishaji, wanunuzi na wafanyabiashara wa madini ya jasi na makaa ya mawe hivi karibuni katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani akizungumza mbele ya waandishi wa habari, katika mkutano uliowakutanisha wazalishaji, wanunuzi na wafanyabiashara wa madini ya jasi na makaa ya mawe (hawapo pichani) hivi karibuni katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe.

Na Veronica Simba

Serikali imepiga marufuku wawekezaji nchini kuagiza makaa ya mawe na madini ya jasi kutoka nje kwa ajili ya matumizi ya viwanda badala yake imewataka wanunue madini hayo kutoka kwa wazalishaji wa ndani.

Akizungumza hivi karibuni mbele ya waandishi wa habari katika mkutano uliowajumuisha wazalishaji, wanunuzi na wafanyabiashara wa madini ya jasi na makaa ya mawe; Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani alisema hakuna sababu ya madini hayo kuagizwa kutoka nje ya nchi kwani ipo hazina ya kutosha nchini.

Katika Mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam, Dkt Kalemani alibainisha kuwa kwa upande wa makaa ya mawe, hazina iliyopo nchini kwa sasa ni zaidi ya tani milioni 5. “Madini hayo hayajachimbwa na tunataka wachimbaji wadogo na wakubwa waje wayachimbe.”

Akifafanua zaidi kuhusu hazina ya makaa ya mawe iliyopo nchini, Dkt Kalemani alieleza kuwa, hadi sasa, viwanda vinavyozalisha madini hayo vimezalisha takribani tani 50,000 kwa ujumla wake wakati mahitaji ni tani 37,000 tu.

“Kwa hivyo hatuwezi kuelewa kwamba mahitaji ni makubwa kuliko uzalishaji, si kweli hata kidogo. Makaa ya mawe yapo ya kutosha, haturuhusu kuagiza kutoka nje na huo ndiyo msimamo wa Serikali,” alisisitiza.

Halkadhalika, kwa upande wa madini ya jasi, Naibu Waziri Kalemani alieleza kuwa hazina iliyopo nchini kwa sasa ni zaidi ya tani 300,000 na kwamba Viwanda vya ndani bado vinahitaji madini hayo ili kutosheleza mahitaji yao.

“Zipo kampuni za kizalendo zinazozalisha jasi na makaa ya mawe. Niwapongeze Magamba sana, mnazalisha vizuri na mwongeze uzalishaji. Lakini watanzania wengine waige, wazalishe ili wenye viwanda vyote waweze kununua hapa nchini.”

Dkt Kalemani pia aliwataka Maafisa Madini wa Kanda zote nchini hususan maeneo kulipo na Viwanda, wasimamie utekelezaji wa maagizo hayo ya Serikali.

Aidha, agizo jingine alilotoa Dkt Kalemani ni kwa wazalishaji na wanunuzi wa makaa ya mawe kuingia mikataba rasmi, ambapo aliagiza mikataba husika ieleze bayana bei ya kununua na bei hiyo itenganishwe na gharama ya usafirishaji.

“Hatutaki kuambiwa kwamba bei kutoka Afrika Kusini ni rahisi kuliko bei ya kutoka pale Mchuchuma kwenda Mtwara.”

Kuhusu suala la thamani ya makaa ya mawe pamoja na jasi, Dkt Kalemani aliwaagiza Shirika la Umma linalojishughulisha na tafiti mbalimbali pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam kuhusu Viwanda (Tanzania Industrial Research and Development Organization – TIRDO) kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), kufanya kazi ya kutathmini ubora wa madini husika ili kuondoa malalamiko yaliyopo kwamba madini hayo yanayozalishwa hapa nchini yana thamani ya chini yakilinganishwa na yanayozalishwa na nchi nyingine ikiwemo Afrika ya Kusini.

Kuhusu suala la kuwepo bei elekezi za madini hayo, kama walivyoomba wadau kwenye mkutano husika, Naibu Waziri alisema kuwa, Serikali itatathmini umuhimu wake wakati biashara ikiendelea.

Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani aliwaagiza Maafisa Madini wa Kanda zote, kuandaa orodha ya maeneo yenye leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini ya jasi ambayo hayafanyiwi kazi na kuwasilisha orodha hiyo wizarani ili zifutwe na kuwapatia watanzania wenye uwezo wawekeze.

“Nimepata taarifa kuwa kuna jumla ya leseni 1230 za madini ya jasi lakini zinazozalisha ni 472 tu hivyo, nimewapa siku 30 Maafisa Madini kuanzia leo, mtayarishe orodha mlete tufute leseni ambazo hazisimamiwi vizuri,” alisisitiza.

Dkt Kalemani aliwataka wazalishaji pamoja na wanunuzi wote wa makaa ya mawe pamoja na jasi, kuingia mikataba ya kuuziana ifikapo tarehe 20 mwezi huu.

Pia, alielekeza kuwa, kuanzia sasa mahitaji ya madini husika (oda) yawe yanatolewa ndani ya siku 20. “Lisiwe jambo la kushtukiza kwamba mnahitaji leo tani 30 mnatoa oda zizalishwe siku hiyohiyo. Hilo haliwezekani.”

Naibu Waziri pia alisisitiza kwamba ni marufuku kununua madini ya jasi na makaa ya mawe kwa madalali (middlemen) na kuagiza madini hayo yanunuliwe kutoka wazalishaji, kwani husababisha kupanda kwa bei pasipo sababu za msingi.

Aidha, katika mkutano huo, Naibu Waziri Kalemani alimteua rasmi Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu changamoto zinazojitokeza katika masuala husika.

Alieleza kuwa Kamati hiyo itakuwa na wajumbe wengine 12 kutoka kwenye taasisi za wazalishaji na wanunuzi na kutoka ofisi za madini za kanda, ambapo wadau wote watatakiwa kuripoti katika Kamati hiyo endapo watakuwa na tatizo lolote. Alisema kuwa majina ya wajumbe wa Kamati yatatolewa ndani ya siku Tano (5).

Mkutano huo umefanyika kufuatia maazimio yaliyofikiwa katika mkutano uliofanyika mapema mwezi huu (Agosti 3), uliowakutanisha wadau husika chini ya uenyekiti wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

No comments: