Tuesday, July 12, 2016

WATAKIWA KUWA TAYARI KUFANYA KAZI VIJIJINI.

 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Enterberth Nyoni  akitoa ufafanuzi kwa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kuhusu uboreshaji wa vyuo kwa kujitegemea  wakati wa kikao kazi cha wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii mjini Dodoma.
 Baadhi ya Wakuu wa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii waliohudhuria Kikao Kazi mjini Dodoma wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa kikao hicho leo mjini Dodoma.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ndani wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Dickson Rusage akitoa ufafanuzi kwa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kuhusu matumizi mazuri ya rasilimali fedha, watu, utunzaji wa mali za Serikali na Utekelezaji wa dhana ya Utawala Bora katika Taasisi za Maendeleo ya Jamii leo mjini Dodoma.
Mkurugenzi wa Utawala na Uendeshaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Eliasifu Mlay akitoa ufafanuzi kuhusu uzingatiaji wa Maadili katika Utumishi wa Umma wakati wa kikao kazi cha Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii leo mjini Dodoma.
Picha na Aron Msigwa - MAELEZO.

Na.Na Msigwa - MAELEZO.
Maafisa Maendeleo ya Jamii wanaohitimu mafunzo  katika vyuo mbalimbali nchini na wale waliko kazini wametakiwa kuwa tayari kufanya kazi vijijini ili kuwawezesha wananchi kuzitumia fursa za maendeleo zilizoko katika maeneo wanayoishi kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Enterberth Nyoni  wakati akitoa ufafanuzi kuhusu Utendaji Kazi wa Maafisa hao  wakati wa kikao kazi cha wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii mjini Dodoma.

Amesema Maafisa Maendeleo popote walipo lazima watambue kuwa wao ni dira na chachu ya mabadiliko ya kuwafanya wananchi kubadilika kwa kufanya kazi kulingana na mabadiliko na rasilimali zilizopo katika maeneo yao.

Amesema kuwa dhana ya Maendeleo ya Jamii ni pana na ikilenga kuwafanya wananchi kutumia rasimali zinazopatikana katika mazingira yao kujiletea maendeleo akibainisha kuwa maafisa Maendeleo wanaozalishwa katika vyuo mbalimbali lazima washiriki kikamilifu katika katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu kwa kuwapatia elimu, ushauri na mbinu mbalimbali za kuondoa umaskini.

Kuhusu ubora wa kiwango cha taaluma ya maendeleo ya Jamii inayotolewa  katika vyuo mbalimbali amesema kuwa ipo haja ya kuendelea kujenga msingi imara vyuoni na kuandaa vigezo vya kuwapima maafisa maendeleo ya Jamii kwa kuangalia ufanisi wa utendaji kazi wao wa kila siku.

Amefafanua kuwa jukumu kubwa la vyuo hivyo pamoja na mambo mengine ni kubadilisha mitazamo ya wanafunzi walioko vyuoni kwa lengo la kuwafanya kuwa chachu ya mabadiliko na kuwa msaada kwa wananchi wanaowatumikia.

Kuhusu mafunzo kwa vitendo Bw.Enterberth amesema kuwa ipo haja kwa wanafunzi walio katika mafunzo  kupangiwa mazoezi kwa vitendo katika   maeneo ya vijijini kwa kuwa ndiko liliko chimbuko la shughuli Maendeleo ya jamii na kutoa wito kwa wahitimu hao kuwa tayari kufanya kazi katika mazingira ya vijijini.

Aidha,amesema kuwa katika kufanya mabadiliko katika taaluma ya maendeleo ya jamii  kitaanzishwa Chama au Bodi ya kitaaluma kusimamia wahitimu wanaomaliza katika vyuo mbalimbali kwa lengo la kupima uelewa, ubora na viwango kabla ya kuruhusiwa kuitumikia jamii.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mafunzo kwa maafisa maendeleo ya Jamii walioko kazini amesema kuwa Serikali inaendelea kulifanyia kazi jambo hilo kwa kuhakikisha kuwa mafunzo rejea kwa maafisa maendeleo ya jamii walioajiliwa yanatolewa ili maafisa hao waweze kwenda na kasi ya maendeleo na mabadiliko yanayotokea katika jamii.

Kwa upande wao baadhi ya Wakuu wa vyuo hivyo wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu namna bora ya kuboresha maslahi ya vyuo hivyo hususan kiwango cha taaluma inayotolewa wameiomba Serikali kwa kushirikiana na wanataaluma husika kuanzisha Bodi itakayosimamia suala la viwango  na uhakiki wa wataalam wanaohitimu.

Aidha, wamebainisha kuwa katika miaka ya hivi karibuni idadi ya wahitimu wa fani ya Maendeleo ya Jamii imeongezeka jambo linalotoa matumaini ya kukua kwa taaluma hiyo na kuiomba Serikali kuendelea kuweka vigezo vya udhibiti ili kulinda viwango vya huduma zinazotolewa.

No comments: