Wednesday, July 20, 2016

UTUMIKISHWAJI WA WATOTO BADO NI TATIZO KUBWA NCHINI.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka 2014 katika uzinduzi wa matokeo hayo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
 Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Dkt. Abdallah Possi akionyesha Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka 2014. Uzinduzi huu umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
 Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani nchini Tanzania, Azfar Khan akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka 2014.
 Baadhi viongozi waliohudhulia katika uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka 2014.
Mwakilishi wa shirika la UNICEF, Cecilia Baldeh akizungumza na wadau mbalimbali katika uzinduzi wa ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka 2014 iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo.

UTUMIKISHWAJI wa Watoto bado ni tatizo kubwa nchini ambapo kati ya watoto watatu wenye umri wa miaka 5 - 17, mtoto mmoja anafanya kazi ambazo ni hatarishi katika maisha yake kiafya, kimwili na kisaikolojia.

Akizungumza katika uzinduzi wa Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka 2014, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Dkt. Abdallah Posi amesema tatizo la utumikishwaji wa watoto bado ni kubwa hapa nchini na hivyo ni wajibu wa jamii kuwekeza katika elimu badala ya kuwaajiri au kuwatumikisha watoto.

“Utumikishwaji wa watoto bado ni tatizo kubwa duniani kote si Tanzania pekee, kwani kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO), asilimia 11 ya watoto wote duniani (watoto milioni 264) wenye umri wa miaka 5 – 17 wanatumikishwa kwenye ajira za aina mbalimbali,” amesema Dkt. Posi.

Dkt. Posi amesema kwa mujibu wa ripoti ya utumikishwaji wa watoto Tanzania wa mwaka 2014/15, watoto wenye umri wa miaka 5 – 17, watoto milioni 4.2 ambao ni sawa na asilimia 28.8 wanatumikishwa katika kazi mbalimbali za kiuchumi. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema utafiti huu umebainisha kuwa, watoto wanafanya kazi zaidi katika sekta za Kilimo, Misitu na Uvuvi ambazo zinaajiri asilimia 92.1 ya watoto wote wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi.

Dkt. Chuwa ameongeza kuwa watoto hutumia zaidi ya nusu ya muda wao (asilimia 58.8) wa siku kujihudumia na usafi binafsi ambapo wasichana wameonekana kutumia asilimia 59.2 na wavulana hutumia asilimia 58.3 kujihudumia.

Aidha, shughuli za kujisomea kwa watoto ni asilimia 15.5 ambapo wavulana wanatumia muda mrefu zaidi kujisomea kwa asilimia 16.4 na wasichana hutumia asilimia 14.6 kujisomea.

No comments: