Thursday, July 21, 2016

TUMEANZA UTEKELEZAJI WA ELIMU JUMUISHI-TANZANIA

Na  Mwandishi Maalum
Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania  imeanza kwa namna moja ama nyingine  utekelezaji wa  lengo namba Nne  ya Maendeleo  Endelevu kuhusu  Elimu la Maendeleo Endelevu (SDG4) kwa  kutoa  elimu   bure kuanzia shule  ya msingi hadi sekondari ikiwa ni  pamoja  na kuifanya  jumuishi kwa makundi  yote ya jamii wakiwamo  walemavu wa aina mbalimbali.

Hayo yameelezwa na   Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  katika Umoja wa Matifa, Balozi Tuvako Manongi  wakati  wa majadiliano  kuhusu    utekelezaji wa  lengo   namba Nne ambalo ni  kati ya Malengo 17  ya Maendeleo Endelevu,  maarufu kama agenda 2030 yaliyopitishwa  mwezi  septemba mwaka jana  na viongozi wakuu  wa nchi na serikali.

Balozi Manongi alikuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu katika  majadiliano hayo, ambayo yalimhusisha pia Waziri Mkuu wa Norway, Mhe. Erna Solberg na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Bi. Irina Bakova na  yaliandaliwa kwa ushirikiano wa UNESCO na  UNICEF kama sehemu ya Mkutano wa  Kilele wa Kisiasa  wa Baraza   la Uchumi la Umoja wa Mataifa ( ECOSOC) unaoendelea hapa  Umoja wa Mataifa.

 SGD4  pamoja na mambo mengine   inatilia mkazo na kutoa   kipaumbele cha pekee katika utoaji na upatikanaji wa  elimu ambayo ni jumuishi, yenye ubora  na inayowafikia makundi yote ya jamii, hususani watoto, wanawake na walemavu.

Akielezea  namna Tanzania ilivyojipanga katika  utekelezaji wa  SDG4 kwa sasa  na kwa baaday,Balozi Manongi  amesema    Tanzania  imejipaga vema  kisera, kisheria na  kimkakati katika kuhakikisha kwamba  kila mtanzania  bila kujali ni wa kundi gani  anapata fursa ya elimu na si elimu  tu bali elimu yenye ubora wa hali ya  juu na inayokidhi mahitaji  na mazingira ya sasa.

Pamoja na kuainisha  sera na sheria mbalimbali  ambazo serikali inazitekeleza katika eneo hilo la  elimu, Balozi Manongi  anasema,  kuwa na sera nzuri, sheria nzuri na mikakati mizuri hakuwezi kuwa kigezo pekee cha kufanikisha utekelezaji wa  SDG4.

“ Kwa Tanzania  tatizo siyo sera,   sheria au  mipango  na mikakati, tatizo ni  raslimali fedha  ya kutosha ( bajeti) itakayowezsha utekelezaji wa SDG4 na  malengo mengine kwa ukamilifu  unaotakiwa”. Anasema Balozi

 Kutokana na  changamato  hiyo  ya ufinyu wa raslimali fedha,  Mwakilishi  huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa anasisitiza haja na umuhimu wa ushirikiano wa karibu  baina ya  Serikali Kuu,  Sekta Binafsi na  Wadau wa Maendeleo kwa lengo la kuhakikisha kwamba hakuna  yeyote atakaye achwa nyuma.

Akizungumzia  zaidi  utekelezaji wa  SGD4 achia mbali  utoaji wa elimu  bure kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari, na  kuhakikisha elimu inawafikia wote, Balozi Manongi amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba hivi karibuni  Serikali imetangaza kutenga kiasi cha fedha kwaajili ya kuwasomesha watu wenye matatizo ya ualibino.

“pamoja na  changamoto mbalimbali    serikali yangu inajitahidi sana kuyafikia makundi mbalimbali ya jamii,  wawe ni watoto wa kike,  watoto wanaoishi katika mazingira magumu, ama  jamii za wafugaji na wawindaji lakini pia  imekwenda mbali zaidi  katika kuhakikisha kwamba jamii yenye mahitaji maalum   nayo inafikiwa” akasisitiza Balozi Manongi.

Akizungumzia zaidi kuhusu uamuzi wa   Serikali ya  awamu ya Tano wa  kuifanya elimu ya msingi hadi  Sekondari kuwa bure.  Balozi amewaeleza wajumbe wa majadiliano hayo kwamba, maana  ya uamuzi huo ni  kuwa mtoto wa kitanzania  atafaidika na elimu ya bure kwa  miaka kumi na moja. Na  vile vile  Tanzania  inakuwa sehemu ya utekelezaji wa baadhi ya  kipengele  cha SDG4 kinachopendekeza utoaji wa elimu  bure ili iwafikia watu wengi zaidi.

Washiriki wengine  katika majadiliano hayo walikuwa ni  Mwakilishi wa Kudumu ya  Jamhuri ya Korea Balozi Oh Joon ambaye pia ni  Rais wa ECOSOC, Waziri wa Elimu kutoka Bolivia  Bw. Bw. Roberto Iván Aguilar Gómez, Bw. Guy Ryder,  Mkurugenzi Mkuu  wa  Shirika la Kazi Duniani  (ILO)  Mwakilishi wa Kudumu  wa  Ufalme wa Morroco katika Umoja wa Mataifa, Balozi Omar Hilale, Bi. Alice Albright kutoka  Global Partnership for Education (GPE),Bi Silvia Montoya, kutoka Tasisi ya Takwimu ya  UNESCO na Bi. Josephine Bourne kutoka UNCEF.


No comments: