Tuesday, July 19, 2016

TAFF yaipongeza Serikali kwa juhudi za kupambana na Uharamia wa kazi za sanaa nchini

 Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF),Simon Mwakifamba,akizungumza na waandishi wa habari,Dar es Salaam,leo kuhusu kuipongeza serikali kupitia wizara husika katika kuanzisha oparesheni ya kuwakamata walanguzi wa kazi za wasanii nchini. Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Wasambazaji wa Filamu nchini,Moses Mwanyilu.
 Mwenyekiti wa Chama cha Wasambazaji wa Filamu nchini,Moses Mwanyilu,akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo wa kwanza kulia ni Rais wa Shirikisho la Filamu Nchini Bw. Simon Mwakifamba.
 Waandishi wa habari wakimsikiliza mwenyekiti wa chama cha wasambaji wa filamu nchini,Moses Mwanyilu (hayupo pichani) wakati akizungumza nao kuhusu wizi wa ulanguzi wa kazi za wasanii nchini.
 Katibu wa Chama cha Wasambaji wa Filamu Tanzania,Suleiman Ling'ande wa katikati,akizungumza katika mkutano huo wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Wasambaza filamu Bw. Moses Mwanyilu.
 Muigizaji wa Filamu za Bongo Movie nchini,Kulwa Kikumba Al maarufu Dude wa pili kushoto ,akitoa ufafanuzi katika mkutano huo juu ya athari za uharamia wa kazi za wasanii mbele ya waandishi wa habari.
 Muanzilishi wa Mtandao wa Filamu Central,Myovela Mfwaisa,akiuliza swali katika mkutano huo.

Habari/Picha Na Ally Daud-Maelezo
CHAMA cha Wasambazaji wa  Filamu Tanzania  na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) vimepongeza hatua iliyochukuliwa na Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo kupitia waziri wake,Nape Nnauye katika kuhakikisha wanatokomeza waharamia na uuzaji wa kazi za wasanii bila kufuata utaratibu za kisheria zilizowekwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa chama cha wasambazaji wa filamu nchini,Moses Mwanyilu,alisema kuwa hatua ya serikali imekuja katika muda muafaka kufuatia kilio cha muda mrefu kutokana na baadhi ya wafanyabiashara na wasambaji wa filamu na muziki kutoka nje ya nchi wamekuwa wakiingiza na kuuza bidhaa hizo bila ya kufuata utaratibu ikiwemo kulipa kodi.

Amesema kuwa wafanyabiashara hao pia wamekuwa wakidurufu filamu za ndani ya nchi na kuziingiza sokoni bila ya wasanii kunifaika na kazi zao ikiwemo kazi hizo kutolipiwa kodi hivyo kupelekea kuziuza kwa bei ya chini ukilinganisha na filamu hapa nchini jambo ambalo linasababisha soko la filamu za ndani kudidimia.

Aidha Mwanyilu ameongeza kuwa  baada ya kilio cha muda mrefu hatimaye wameona jitihada za serikali kupitia kwa wizara inayohusika na masuala ya sanaa kuanza kuchukua hatua za makusudi kufanya oparesheni ya nguvu ya kukamata walanguzi wa kazi za wasanii nchini katika maeneo ya kariakoo.

Kwa niaba ya chama cha wasambazaji wa filamu na shirikisho la filamu Tanzania na vyama vyote vya shirikisho wanapenda kutoa shukrani za dhati kwa wizara ya habari kupitia waziri wake,Nape Nnauye kwa kushirikiana na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA),Bodi ya filamu,Cosota na Baraza la Sanaa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kazi za wasanii nchini zinauzwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na unaotambulika.

Naye Katibu Mkuu wa chama cha Wasambaji wa Filamu Tanzania,Suleiman Ling’ande alisema kuwa tatizo la uharamia katika kazi za wasanii nchini ni changamoto ya muda mrefu kufuatia kuwepo na sheria ambayo imeshindwa kukidhi na kusimamia utaratibu unaofaa hasa katika kuhakikisha kazi za wasanii zinawanufaisha wasanii pamoja na kuliongezea kipato taifa pamoja na kulipa kodi.

Pia Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF),Simon Mwakifamba,amesema kuwa anaunga mkono zoezi linaloendelea kwa wadau wa kazi za wasanii cnhini wakishirikian na serikali katika kuhakikisha wanatokomeza uharamia wa kazi za wasanii wote nchini ili walau kuwapa motisha ya maisha mazuri waigizaji hao ili waendelee kutengeneza kazi nzuri za kuelimisha jamii.

No comments: