Tuesday, July 19, 2016

Serikali na British Council Tanzania zashirikiana kuwapiga msasa Mashirikisho ya Sanaa kuhusu Fursa ya Sanaa ya Afrika Mashariki.


Kaimu Mkurugenzi British Council Tanzania, Bi. Nesia Mahenge (kulia) akiwaelekeza baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania pamoja na Wadau wa masuala ya Sanaa kuhusu Fursa ya Sanaa inayodhaminiwa na Taasisi hiyo, 19 Julai, 2016 jjijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Leha Kihimbi (kulia) akiwasisitizia baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania pamoja na Wadau wa masuala ya Sanaa kuhusu umuhimu wa Fursa ya Sanaa inayodhaminiwa na Taasisi hiyo, 19 Julai, 2016 jjijini Dar es Salaam.PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.
Kaimu Mkurugenzi British Council Tanzania, Bi. Nesia Mahenge (wa pili kushoto waliokaa mbele) akiwaelekeza baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania pamoja na Wadau wa masuala ya Sanaa kuhusu Fursa ya Sanaa inayodhaminiwa na Taasisi hiyo, 19 Julai, 2016 jjijini Dar es Salaam.
 
 

Serikali na British Council Tanzania yawapiga msasa Mashirikisho ya Sanaa namna ya kuandika Mapendekezo ya Mradi wa Fursa ya Sanaa ya Afrika Mashariki.

SERIKALI kwa kushirikiana na British Council Tanzania imekutana na baadhi ya Viongozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirikisho mbalimbali ya Sanaa nchini na kuwapatia elimu juu ya namna ya kuandika Mapendekezo (Proposals) za Mradi wa kuwania fursa ya sanaa inayodhaminiwa na British Council Tanzania.

Elimu hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa British Council Tanzania, Bi. Nesia Mahenge pamoja na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sanaa, Bi. Leah Kihimbi lengo likiwa kuwahamasisha wasanii kote nchini kuchangamkia fursa hiyo inayodhaminiwa na Taasisi hiyo yenye Makao yake Makuu nchini Uingereza.

Awali akieleza kuhusu fursa hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa British Council Tanzania, Bi. Nesia Mahenge amesema kwamba fursa ya sanaa kwa Wasanii zinahusisha sehemu tatu ikiwemo fursa ijulikanao kama nAnA (new Arts new Audiences) ambayo ndiyo imefunguliwa kwa sasa na baadaye fursa nyingine mbili za Creative Hustle pamoja na Mobility East Africa zitafuata.

Ameeleza kuwa kuhusu vigezo vya kujiunga na fursa hiyo ni pamoja Wasanii kuwa na umri kuanzia miaka 18-35, kuwa na Ushirikiano (Partnership) katika ya nchi tano zinazohusisha fursa hiyo, kuwa na Kampuni binafsi au ya Shirikisho, fursa inahusisha fedha ya uandikaji wa Pendekezo (Proposal) zitakazotolewa ni kuanzia paundi 2,000 hadi paundi 20,000 pamoja na kuwa na akaunti namba katika benki fulani.

Amefafanua kuwa, fedha zitakazotolewa na British Council Tanzania sio za mkopo bali ni kwa ajili ya wasanii wote ambao watafanikiwa kuwania fursa hiyo ambapo kwa sasa amesema kwamba wanaanza na fursa ya nAnA, hivyo amewahimiza wasanii nchini kupitia mmoja mmoja pamoja na Mashirikisho yao kuanza kuandika mapendekezo ya kuomba fursa hiyo kwa kujaza fomu ambayo inapatikana katika tovuti ya www.britishcouncil.or.tz

“Fedha hizi sio za mkopo, mtu akifanikiwa kuzipata haimaanishi kuwa anapaswa kuzirejesha, isipokuwa British Council wao watakuwa wanafuatilia ni kwa namna gani fedha hizo umeweza kufanikisha wazo lako na lina faida gani katika jamii ama wengine wamenufaika vipi na wazo lako”, alisema Bi. Mehenge.

Ameongeza kuwa, Wasanii pamoja na Mashirikisho hayanabudi kusaidiana katika kufanikisha suala hilo kwa kuelekezana juu ya namna ya kuwapata watu wenye ujuzi wa jinsi ya kuandika Mapendekezo (Proposals) na kuziandika kwa wingi ili Wasanii wa Tanzania wapate nafasi ya kushinda fursa hiyo kwani kuna nchi nyingine nazo zinahusika na fursa hiyo ambazo ni za Afrika Mashariki.

Kuhusu mwisho wa kuwasilisha maombi hayo, amesema kwamba, tarehe ya mwisho ni 31 Julai mwaka huu,lakini wasanii hawanabudi kuwa na hofu kwani bado wana nafasi kubwa ya kuandika na kuweza kushinda hiyo fursa, kwani kinachomata ni wazo zuri msanii alilokuwa nalo na sio tu uandishi mzuri.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Leah Kihimbi amewasisitizia Wasanii kote nchini kuchangamkia fursa hiyo bila kuwa na woga kwani ni fursa ya pekee ya kuwanufaisha na kazi zao na kuiletea sifa Taifa.

“Msiogope kuandika kuomba hii fursa, kwani kuna wenzenu pia wanaitafuta, jitahidini kushirikiana ili mwisho wa siku Tanzania iwe na miongoni mwa wasanii watakaowania fursa hii, na kwa kufanya hivyo mtakuwa mmelejengea heshima Taifa letu”, alisema Kihimbi.

Fursa ya Sanaa kwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla ni fursa inayodhaminiwa na British Council Tanzania ambapo wasanii wanatakiwa kuiomba kwa kuandika mapendekezo kuhusu mawazo yao juu ya mambo wanayotarajia kuyafanya kupitia sanaa na namna gani itanufaisha jamii huku ikihusisha nchi tano za Afrika Mashariki zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Ethiopia.

No comments: