Monday, July 18, 2016

RAIS DKT. MAGUFULI AZUNGUMZA NA MAAFISA WA JESHI LA POLISI WALIOPANDISHWA VYEO IKULU JIJINI DAR ES SALAAM,AWATAKA KUCHUKUA HATUA DHIDI YA WANAOLETA MATATIZO

  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi Tanzania kuwaondoa watumishi wote wasiokuwa askari polisi na ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa taratibu na ufujaji wa fedha za umma ili kulinda heshima, nidhamu na uadilifu ndani ya jeshi hilo.

Rais Magufuli ametoa maelekezo hayo leo tarehe 18 Julai, 2016 muda mfupi baada ya Naibu Makamishna wa Polisi 25 na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi 35 kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, Ikulu Jijini Dar es salaam.

Pamoja na kutoa agizo la kutaka wasio askari polisi kuondolewa katika utumishi wa jeshi la polisi, Rais Magufuli pia ameagiza jeshi hilo lichukue hatua dhidi ya wote wanaokabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha wakiwemo wanaodaiwa kuiba mabilioni ya shilingi zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi wa sare za askari mwaka jana 2015.

"Mnajua kupeleleza, mna vyombo vyote, ofisi ya IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi) ipo palepale, ofisi ya DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) ipo palepale, Makamishna wote mnazunguka mnakwenda palepale, mwizi mnae palepale, mnashindwa kumshika.

"Kama mnafikiri kuwa na raia katika jeshi la polisi wanawaharibia kazi zenu hamisheni raia wote na wapelekeni utumishi, kwani hakuna mhasibu ambaye ni askari polisi? hakuna mhandisi ambaye ni askari polisi? hakuna afisa tawala ambaye ni askari polisi? Mimi nafikiri kama matatizo ya wizi na wafanyakazi hewa yanaletwa na raia waliomo ndani ya jeshi la polisi na majeshi yetu mengine, IGP kaorodheshe raia wote wanafanya kazi Jeshi la Polisi ili waondolewe na tuwapangie kazi nyingine uraiani" Amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri linayofanya iliyoliwezesha kujenga imani kubwa kwa watanzania na ametaka viongozi wa Jeshi hilo wawaongoze askari walio chini yao vizuri, wawatie moyo na waache vitendo vya kuwakatisha tamaa kwa kuwaadhibu ama kuwatisha pale wanapochukua hatua stahiki dhidi watu wanaovunja sheria.

"Sasa mimi niwaombe nyinyi, wale wadogo mnaowaongoza mkawape mamlaka ya kutimiza wajibu wao, hata kama ameshika gari la IGP liache lishikwe IGP atakwenda kujieleza mwenyewe, hata akishika gari la RPC afanye hivyohivyo, hata akishika gari la Waziri au gari la Rais mwacheni atekeleze wajibu wake, sheria ni msumeno, tunawanyima nguvu hawa wa chini wanapotimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria halafu unamwambia liachie, ukifanya hivyo aliyeshikwa anatoka pale akiwa anatamba kwelikweli na yule askari unamvunja nguvu ya kufanya kazi" Amesisitiza Rais Magufuli. 

Rais Magufuli pia amelitaka jeshi hilo kuungana na vyombo vingine vya serikali katika kutekeleza shughuli zake zikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali bandarini, katika sekta ya utalii na maeneo mengine, kukabiliana na vitendo vya rushwa na kuondoa watumishi hewa.

Tukio hili la Naibu Makamishna wa Polisi na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda na limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Makatibu Wakuu na Viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
18 Julai, 2016


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Maafisa wa Jeshi la polisi aliowapandisha vyeo vya Naibu Kamishna wa Polisi DCP na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ikulu jijini Dar es Salaam. 
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Kedmon Andrew Mnubi akila kiapo cha Ahadi ya uadilifu pamoja na Maafisa wengine wa Jeshi la Polisi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mwamini Marco Rwantale   akila kiapo cha Ahadi ya uadilifu pamoja na Maafisa wengine wa Jeshi la Polisi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ahmada Abdalla Khamis akisaini hati ya kiapo cha Ahadi ya Uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Frasser Rweyemamu Kashai akisaini hati hati ya kiapo cha Ahadi ya Uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ahmada Abdalla Khamis akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwagaia vitafunwa wageni mbalimbali waliofika Ikulu kwa ajili ya kushuhudia Maafisa wa Polisi walipondishwa vyeo wakati wakila kiapo. 



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwagaia vitafunwa baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria tukio hilo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwagaia vitafunwa baadhi ya Maafisa mbalimbali wa Polisi waliokula kiapo cha Maadili Ikulu jijini Dar es Salaam. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mwigulu Nchemba akizungumza jambo na Naibu wake Hamadi Masauni mara baada ya Maafisa wa Jeshi la Polisi waliopandishwa vyeo kula Kiapo ahadi ya uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam.PICHA NA IKULU.
   
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika picha na meza kuu baada ya kushuhudia maafisa waandamizi wa polisi waliopandishwa veyo wakila kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo, wakiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora Mhe Angellah Kairuki, Naibu Waziri wa mambo ya Ndani Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Meja Jenerali Projest Rwegasira, Kamishna wa maadili ya Utumishi wa Umma  Jaji Mstaafu Salome Kaganda na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika picha na meza kuu na  maafisa waandamizi wa polisi waliopandishwa vyeo baada ya kula kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo, 
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika picha na meza kuu na  maafisa waandamizi wa polisi waliopandishwa vyeo baada ya kula kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo, 
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika picha na meza kuu na  maafisa waandamizi wa polisi waliopandishwa vyeo baada ya kula kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo, 

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika picha na meza kuu na  wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama maafisa waandamizi wa polisi  baada ya maofisa waliopandishwa vyeo kula kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo, 

No comments: