Saturday, July 30, 2016

RAIS DKT. MAGUFULI AENDELEA NA ZIARA YAKE KATIKA WILAYA ZA IGUNGA NA NZEGA MKOANI TABORA

 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 30 Julai, 2016 ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Tabora akitokea Mkoa wa Singida.

Kabla ya kuingia Mkoani Tabora, Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Mji wa Misigiri katika Wilaya ya Iramba ambapo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara katika Mkoa wa Singida kuhakikisha mkandarasi anayejenga daraja la Sibiti anarejea kazini mara moja kukamilisha ujenzi wa daraja hilo.

Rais Magufuli amesema serikali yake imejipanga kumlipa fedha mkandarasi huyo na hivyo hakuna sababu ya kuendelea kusimamisha ujenzi huo.Mkoani Tabora, Rais Magufuli amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika vijiji vya Nanga na Ziba na amefanya mikutano ya hadhara katika miji ya Igunga na Nzega ambako amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itahakikisha inatekeleza ahadi zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2015.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Igunga, Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu kutoanza kutumika kwa kituo cha mabasi na soko na amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Tabora kuhakikisha kituo cha mabasi cha Igunga na soko la Igunga vinaanza kutumika kuanzia Jumatatu ijayo ya tarehe 01 Agosti, 2016.

Kuhusu kero ya maji, Dkt. Magufuli amesema Tanzania imepata mkopo wa dola za kimarekani Milioni 268.35 kutoka nchini India ambazo zitatumika kutekeleza mradi wa kusambaza maji ya ziwa Viktoria katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega, Sikonge na Uyui pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba kuu kuanzia mwaka huu ambapo watu milioni moja na laki moja (1,100,000) watanufaika.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa pamoja na juhudi hizo Serikali imefanya usanifu na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusambaza maji ya kutoka mto Malagarasi kwa ajili ya Miji ya Urambo, Kaliua na Nguruka pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba kuu ambako watu laki sita (600,000) watanufaika.

Aidha, Rais Magufuli amepiga marufuku wakulima wadogo kutozwa ushuru wa mazao watokapo na mazao mashambani.

"Ninapenda tukusanye kodi, lakini sio kukusanya kodi kutoka kwa watu masikini, mtu ametoka shambani na magunia yake mawili au hata matano halafu nyinyi mnamtoza kodi."Mimi sipendi kuwanyanyasa hawa watu wanyonge, mtu akiwa na mazao lori zima hapo sawa lakini sio kwa mtu mnyonge mwenye gunia moja" Amesema Rais Magufuli.

Kuhusu maombi ya Mkoa wa Tabora kutaka kuanzishwa Mkoa mwingine kutokana na ukubwa wa baadhi ya Wilaya Rais Magufuli amesema haioni umuhimu wa kuanzisha Mikoa mipya hapa nchini kwa sasa, na badala yake fedha zitaelekezwa katika huduma kwa wananchi kama vile maji, barabara, miundombinu na huduma za afya.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Nzega
30 Julai, 2016 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na mamia ya wakazi wa Igunga mkoani Tabora katika ziara yake ya kikazi katika Mkoa huo wa Tabora.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wakazi wa Igunga mkoani Tabora mara baada ya kuwahutubia Wilayani hapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wakazi wa Igunga mkoani Tabora mara baada ya kuwahutubia Wilayani hapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wakazi wa Igunga mkoani Tabora mara baada ya kuwahutubia Wilayani hapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nanga Wilaya ya Igunga Ndugu Masesa Kishiwa Makala kutoka Chadema wakati akiwa safarini kuelekea Nzega Mkoani Tabora.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwasalimia wakazi wa Ziba Wilayani Igunga mkoani Tabora hawaonekani pichani wakati akielekea Nzega Mkoani Tabora.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na wabunge wa Mkoa wa Singida wakati akiwahutubia wakazi wa Misigiri Mkoani Singida wakati akiwa njiani kuelekea Mkoani Tabora.
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwasalimia wakazi wa Misigiri Mkoani Singida. PICHA NA IKULU
 
 

No comments: