Tuesday, July 12, 2016

HOJA YA HAJA: ‘Mishemishe’ Adui wa Awamu ya Tano

Na Eng.Gilay Shamika
Moja kati ya mambo muhimu katika muundo wa nchi ,shirika,kampuni au taasisi ni pamoja na kuwa na kipengele cha dira (vision) na mwongozo,mbinu,njia ( mission) za kutimiza dira au malengo.Dira (vision) inaonesha kwa muhtasari nini kusudio,lengo,mwelekeo au nia.Aidha  mwongozo,mbinu,njia (mission) za kutimiza dira huonesha ni kwa namna gani kusudio,mwelekeo au nia hiyo itafikiwa na ama shirika,kampuni au taasisi na pengine mtu binafsi anapojiwekea malengo yake.Maneno hayo mawili ndiyo hubeba taswira nzima ya shughuli zote. 
Dira (vision) ambayo ni mtazamo au mwelekeo wa jumla ni jambo la kudumu wakati mbinu (mission) za kutimiza lengo ni jambo linalobadilika kutokana na wakati,elimu,teknolojia na uwezo wa kifedha.
Kila nchi ina nembo yake ya kitaifa ambayo huwa katika nyaraka za Serikali.Nembo ya taifa ndiyo hutoa tafsiri nzima ya ‘vision’ na ‘mission’ ya taifa husika.Ni kwa umuhimu huo ndiyo haswa sababu mahsusi ya nembo hiyo kuwekwa juu ya nyaraka za kiserikali kuonesha kuwa yote yatendwayo kiserikali yanapaswa kuakisi nembo hiyo….. Vision na Mission za taifa. Wangapi wanaelewa nembo ya taifa na tafsiri yake katika kutekeleza ‘vision na mission’ za taifa?Kunahaja ya viongozi,watawala na wananchi kuelewa kwa kina jambo hili.Uelewa wa maneno hayo mawili ni muhimu sana katika kuendesha shughuli zetu za kila siku kama taifa.Maneno hayo ndiyo msingi wa ujenzi wa taifa,taasisi,wakala,kampuni n.k.
Kama ilivyo katika ujenzi wa nyumba, ramani ya nyumba ndiyo inayotoa tafsiri ya sura nzima ya nyumba.Fundi asipoelewa kutafsiri ramani, nyumba husika haitajengeka kama ilivyopaswa na wakati mwingine inaweza kuhitajika ivunjwe ili apewe fundi mwingine ajenge kwa mujibu wa ramani. 
Katika kutimiza majukumu ya taifa hali ni kama hiyo,vision na mission ndiyo ramani inayoelekeza sura ya taifa tulitakalo kiuchumi,kisiasa na kiutamaduni.Tusipo jua umuhimu wa kutenda kwa mujibu wa vision na mission ya taifa, kuna uwezekano mkubwa wa kubadili viongozi na njia za kiutendaji kila mara na hivyo kukosa mwelekeo kwa namna fulani.Aidha hali ya kutokuwa na vision na mission, inatoa fursa kwa kiongozi katika idara au sekta yoyote kuanzisha vision na mission yake ya jinsi gani atatekeleza majukumu yake, yaweze kuwa mazuri au mabaya na kuligharimu taifa ama kumlazimu rais kufanya teuzi kila mara kukidhi mahitaji ya nchi.
Uelewa wa maneno haya mawili ni muhimu sana kwa afya ya taifa maana ndiyo hujenga taasisi imara katika kusimamia uendeshaji wa kila siku na hakuna jinsi ya fursa ya mtu kuendesha mambo anavyopenda.Hivyo kwa pamoja hatuna budi kutilia umuhimu jambo hili ili sote tuenende kwa mujibu wa dira ya taifa inayoeleweka kwa kila mtu.

Umuhimu wa maneno hayo mawili huonekana katika kila Nyanja ya maisha.Mfano; Kwa upande wa chama cha siasa ‘vision’ ni kupata fursa ya kutawala na ‘mission’ huwa ni sera za chama ambazo ndizo huonesha ni kwa nanma gani chama kitafikia lengo hilo na kudumisha lengo hilo.Kwa upande wa dini ‘vision” ni kufika kwa muumba (kuokoka,kuongoka,kutakasika n.k) na ‘mission’ ni utaratibu mzima wa dini husika kama amri za Mungu,nguzo za imani na utaratibu mzima wa kutimiza ibada.
Wananchi nao katika shughuli zao za kila siku wanajua umuhimu wa maneno hayo na ikapelekea kuyatohoa kama ‘mission town’ na ‘mission mission’ – mishemishe!!! Wakiwa na maana ile ile ya mbinu au harakati za kutimiza malengo yao ya kujipatia mkate wa kila siku.Tofauti na nchi zilizoendelea,nchi za kiafrika mara nyingi mbinu (mission) za kufikia malengo huwa hazipo kisayansi zaidi bali mara nyingi huwa ni matakwa ya mtu,mbinu za kishirikina,mbinu zilizo kinyume na sheria,mbinu zisizo za kiutu, ubinafsi,n.k
Je kwa sasa wananchi tunaelewa kama taifa ‘mission’ zipi tunazotumia?, je ni BRN,je ni MKUKUTA,je ni MKURABITA,je ni UWEKEZAJI, je ni TASAF, la hasha hii ni mikakati tu.Wananchi na taifa kwa ujumla wake waeleweshwe kwa dhati.
Ukifika kariakoo,manzese na kwingineko utaona mbinu (mission mission- mishemishe) rasmi na zisizo rasmi wanazotumia vijana kujipatia mkate wa kila siku.Hali hii ya mbinu (mission- mishemishe) za kufikia malengo zisizo rasmi imekuwa ndiyo maisha ya jamii nzima ya kitanzania na kupelekea kuonekana yeyote anaefuata njia rasmi anapoteza muda (analeta za kuleta,mnoko,ana tubania) na wale wasiofuata njia rasmi kuonekana wanaenda na wakati ( mtu poa/mshikaji/jembe letu kiaina). 
Mtazamo huu umeota mizizi na kuwa ndiyo hulka ya Watanzania waliowengi kuanzia ngazi ya familia mpaka ngazi ya Kitaifa.Tuungane na rais na viongozi wengine wenye hulka tofauti na hii ili kama taifa tulejee kwenye misingi sahihi na endelevu.
Mtazamo huu kwa sasa unaanza kubadilika hasa katika kiwango cha kitaifa.Watanzania wameanza kuona umuhimu wa kukemea ‘mishemishe’ zisizo rasmi hasa kwa ngazi ya kitaifa na kutaka hatua kuchukuliwa dhidi ya wahusika.Kwa maisha ya kila siku mitaani kwetu,hali hii ya mishemishe zisizo rasmi bado inakubalika kwa kiasi kikubwa.Katika mikusanyiko utasikia watu wakishauriana jinsi ya kuiba,kudhurumu,kudanganya,kufanya ushirikina na n.k.Ipo haja kubwa pia kwa sisi wenyewe mitaani kwetu kubadilika na kuwajibishana ili taifa liwe na vision na mission rasmi tangu ngazi ya kaya hadi taifa badala ya dira tuliyonayo ya mishemishe zisizo rasmi.
Ukiongea na wageni wanasema watanzania wanauelewa wa hali ya juu sana ila tatizo ni  uadilifu – mishemishe zisizo rasmi.!!! Wanaendelea kusema kuwa ‘hakuna makubaliano unayoweza fanya na mtanzania na yakabakia kama mlivyo kubaliana.Kwa mtanzania nilazima makubaliano ya aina moja yaanzishe makubaliano mengine.Mlivyokubaliananae jana, leo anabadilika au anakuja na nyongeza,mapungufu au anabisha yote mliyoafikiana siku ya awali’. Mnyumbuliko huu wa makubaliano hupoteza lengo zima la jambo husika.
Tatizo hili limepelekea kuwa vigumu sana waajili kupata wafanyakazi waaminifu.Unapoanza biashara tatizo la kwanza unalokabiliana nalo nikupata wafanyakazi waaminifu ambao dhana ya mishemishe zisizo rasmi haijawaingia akilini.Je wanapatikana kwa dhati kabisa?
Kama nilivyosema hapo juu,ubaya wa mbinu zisizo za kisayansi ni kutoweza kujua kwa uhakika kama lengo au malengo uliyofikia niendelevu au ya muda mfupi.Hakuna uhakika pia wakupata mrejesho stahiki katika kupima malengo yako na hivyo kufanya usiweze kupangilia ukipatacho maana mbinu zitumikazo ni pata-potea.
Tofauti ya kiwango cha elimu,teknolojia na utamaduni wa taifa moja hadi lingine,ndivyo huashiria mbinu,muongozo (mission) upi utumike katika kufikia lengo(vision) la nchi kimaendeleo.Mataifa yote yaliyoendelea yalianza kuandaa ‘vision’ na ‘mission’ za nchi zao.’Vision’ zao zimeendelea kudumu daima ila ‘mission’ ndiyo zimekuwa zikibadilika kutokana na kiwango cha elimu na tekinolojia katika mataifa husika.
Kimsingi vision ya taifa lolote ni kuleta maendeleo ya taifa kwa ujumla.Mbinu za kufikia malengo hayo (mission – mishemishe) ndiyo hutofautiana.Kwa mataifa yaliyoendelea,mbinu hizo hubuniwa na wataalam katika kila nyanja na baada ya hapo taasisi,wakala,mamlaka na dola nzima huzitumia bila kuingiliwa na hisia za kisiasa.Waasisi wa taifa letu hawakuwa nyuma kulijua hilo,yakuwa mbinu za kufikia malengo ya taifa lazima kwanza yaendane na kiwango cha elimu,teknolojia na uwezo wa kifedha.Aidha tawala zilizofuatia nazo zimejitahidi kutambua jambo hili.
 Itakumbukwa karume alitumia kamba,mambo,koleo na sululu kujenga makazi yaliyopo pale Zanzibar.Watu walibeza awali na kuhoji kwanini asilete wataalam kutoka nje.Mpaka leo makazi yale ndiyo yanayotoa fursa kubwa ya makazi kwa wazanzibari.Dira ilikuwa ni kuwapatia wananchi makazi.Alitumia elimu,teknolojia  na uwezo wa kiuchumi wa wakati huo kufikia dira ya kuwa na makazi kwa wananchi wake.
Vilevile mwalimu kipindi cha vijiji vya ujamaa aliwaasa wananchi kujituma kuanzisha vijiji kwa kutumia teknolojia ya ujenzi baina yao ya nyumba za tofali za kuchoma,wahunzi kuchonga zana za kilimo mpaka pale taifa litakapo kuwa na uwezo wa wataalam na fedha za kuagizia matrekta ambayo kimsingi baadae yaliagizwa.
Je leo hii bado tunaelewa umuhimu wa kutenda kulingana na kipato na kiwango cha elimu cha wananchi wetu? Tumejionea mara zote wataalam walio letwa kufanyakazi nchini wanavyoshindwa kufikia ufanisi waliokuwa nao huko nje.Sababu kuu ikiwa ni mfumo wa mishemishe zisizo rasmi ambazo wenzetu hao hawa kuzizoea bali wanakumbana nazo hapa kwetu.
Taifa kwa sasa lipo katika kipindi cha mpito kuelekea nchi ya ahadi kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni japo sina uhakika na jambo la kiutamaduni…..maana umagharibi umetamalaki hatuna utamaduni wetu tena hususan kwa vijana wetu wa kizazi cha ‘ku-chat’.
Tafiti nyingi za kiuchumi na maendeleo ya jamii zinaelezea Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazo fikia maendeleo ya juu iwapo tu mishemishe zisizo rasmi zitasitishwa na hivyo wataalam na taasisi husika kufanyakazi kwa uwazi na kwa ufanisi. Nukuu kutoka makala mojawapo ya Gilay Shamika inasema ‘Ili tuendelee tunahitaji taasisi imara zenye wataalam wanaojiamini na wasio na weledi unaotiliwa shaka pamoja na vyama vya siasa sikivu pale linapokuja suala la kitaaluma.’ Haya yatatimia tu kama vision na mission zitakuwa za dhati na zenyekueleweka kwa jamii nzima.
Mawaziri wanaosifika kwa sasa kiutendaji,wanachokifanya sasa ni kuzuia mishemishe zisizo rasmi ambazo zimeota mizizi na kuonekana ndiyo mfumo wa maisha ya kitanzania.Ni muda muafaka kwa taifa kwa ujumla wake kuacha kuendekeza mishemishe zisizo rasmi na kujikita katika mishemishe zilizo rasmi na za kisayansi ili tusonge kama taifa.
Tuwaunge mkono wote akiwemo mheshimiwa rais kulifikisha taifa katika nchi ya ahadi ambayo Mwalimu na Karume walikuwa wamepania kutufikisha.Mtakubaliana nami kuwa kwa sasa nchi ipo katika kipindi muhimu sana kuliko kipindi chochote kile katika uhai wake.Ni kipindi cha kuvuka kutoka nchi isiyotumia utajiri wake kiufanisi na kuingia miongoni mwa nchi zinazotumia utajiri wake kwa manufaa ya kitaifa.
Tukikosea sasa hakuna jinsi nyingine tena tunaweza kudurusu na kurekebisha makosa yetu.Dunia ipo katika kipindi cha ‘information age’.Mataifa makini yanatumia fursa ya kuwa na taarifa ya maliasili na teknolojia ya nchi nyingine na kujipanga nao wafanye nini kuendana na kasi ya teknolojia na kupata maliasili husika kutoka mataifa hayo.Tanzania kila tulichonacho kinafahamika na kinahitajika kwa waliowengi.Ni jukumu letu kuacha mishemishe zisizo rasmi na kutumia fursa ya maliasili tulizonazo kufaidika. Tumuunge mkono Waziri wa Nishati na Madini katika jitihada zake na pia tusisite kumshauri kwa nia njema pale ambapo tunaona mapungufu.
Fahari ya Tanzania kwa sasa ni maliasili tulizo nazo,tukisha zichezea hatuna cha maana kingine. Kingine kipi hasa ambacho mtanzania anaweza jivunia na akaonekana wa maana duniani.Amani na utulivu si jambo la kujivunia bali ndiyo mfumo hasa wa maisha ya watu waliostaarabika unavyopaswa kuwa.Ustaarabu huu unatimia pale viongozi wanapotenda kwa manufaa ya taifa na wananchi kuliona hilo likitendeka na wao kuwa na mamlaka ya kushauri,kuhoji na kuchagua kwa uwazi.Hii ndiyo dhana ya Serikali ni wananchi.
Katika nchi nyingi za kiafrika,dhana ya serikali ni wananchi huwa na mashiko siku moja tu……siku ya kupiga kura na baada ya hapo mambo hugeuka na kuwa serikali ni viongozi waliochaguliwa.Maana ndiyo mwisho wa wananchi kuwawajibisha viongozi na serikali kwa ujumla.Jambo hili kwa muda mrefu limezoeleka na kuonekana kiongozi anaweza kufanya lolote na wananchi wasiwe na lakufanya kumwajibisha.
Nchi zilizoendelea zimekuwa zikiongozwa na mfumo wa ‘utatu’ – 1.viongozi, 2.wananchi wa kawaida na 3. mashirika yasio ya kiserikali.Hapa kwetu jambo hili bado linasuasua hasa kwa upande wa asasi zisizo za kiserikali na wananchi wa kawaida.Viongozi bado wanaamini kuwa wao pekee ndiyo wenye mamlaka na uwezo wa kuongoza bila kukosolewa.Hawaamini kuwa wanatakiwa kushirikiana na wananchi wa kawaida na asasi zisizo za kiserikali katika kila hatua ya utekelezaji wa jambo lolote isipokuwa masuala ya usalama wa taifa.
Viongozi wajenge tabia ya kuwajibika kwa wananchi na waone wananchi wanahaki ya kuhoji utendaji wao pamoja na kupata taarifa.
Kwa awamu hii ya tano, hali hii imebadilika kwa kiasi kikubwa sana.Hakuna kauli za ‘unanijua mimi ni nani’? Hizi zilikuwa ni tambo za viongozi dhidi ya wananchi.Kwasasa viongozi wananyenyekea wananchi na kwakweli wanatoa huduma kwa ufasaha.Hongera Rais kwa hili.
Wananchi wa kawaida nao watambue ni wajibu wao kushirikiana na viongozi bila kujali itikadi za vyama katika kutekeleza malengo ya jamii husika.Aidha ni jukumu la wananchi kudai maelezo ya utekelezaji badala ya kuwaachia viongozi na mwisho wa siku kulalamika tu.
Asasi zisizo za kiserikali lengo kuu la kuanzishwa ni kuweza kutoa fursa kwa wataalamu ambao hawakupata nafasi serikalini watumie taaluma yao kwa kusaidiana na wataalamu waliopo serikalini. Hivyo basi inatarajiwa kwa mfano asasi ya mambo ya sheria, ifatilie mambo ya kisheria yanayopitishwa na Serikali na kushauri pale wanapoona mapungufu na kuwashauri wananchi njia ya kufuata katika kukidhi matakwa hayo ya kisheria.
Makundi haya matatu yakitimiza wajibu wake na kila kundi kuona ni haki ya kundi lingine kuwajibisha,kushauri au kukosoa lingine, taifa litasonga mbele bila misuguano isiyo na tija na kufikia malengo ya pamoja.Hivyo umuhimu wa utatu huu katika uhai wa taifa haunabudi kutiliwa mkazo.
Taifa limekuwa,majukumu yamekuwa,fikra zimekuwa hivyo viongozi,wananchi na asasi zisizo za kiserikali nao wakubaliane na mfumo wa utatu ili taifa lisonge salama na kuondokana na mfumo wa mishemishe zisizo rasmi.Wananchi tuwe tayari pale serikali inapohitaji ushirikiano wetu na kukiri mazuri yaliyofanywa na serikali.Pia serikali itoe ushirikiano pale wananchi wanapo hoji na kutaka ufafanuzi wa jambo fulani.
Maneno kama wamechochewa ,wanatafuta umaarufu wakati wananchi wanauliza jambo la msingi hayajengi taifa letu. 
Rais wa awamu ya tano, Dkt. John Pombe Makufuli, ni muumini wa mishemishe zilizo rasmi. Anaamini katika kutenda kwa haki na kuweka mbele maslahi ya Taifa. Kwasababu tumezoea mishemishe zisizo rasmi kwa muda mrefu, itamchukua muda mrefu kurekebisha taifa kurudi katika mishemishe rasmi. Pia tulio wengi itatuchukua muda kuamini na kukubaliana na mtazamo mpya wa kufuata taratibu katika kupata kipato kwa njia halali.
Binaadamu ni kiumbe asie penda mabadiliko ya ghafla, shime tushikamane na Rais katika kutenda kwa mujibu wa haki na hivyo taifa liende katika misingi ya haki na hatimae Maendeleo endelevu.
Tushikamane na Serikali ya awamu ya tano kama taifa kwa pamoja tuanze sasa kufanya kazi ya ujenzi wa taifa kwa mfumo wa utatu na kila upande umwamini mwenzie mpaka hapo jamii nzima itakapo ona njia pekee ya kuendelea ni kufanya mambo rasmi kwa njia rasmi badala ya mishemishe zisizo rasmi. UTII KWA SERIKALI HUKUZA USHIRIKIANO WA UTATU NA KUHARAKISHA MARIDHIANO NA HATIMAE MAENDELEO YA TAIFA.
Mungu ibariki Serikali ya awamu ya tano,Mungu ibariki Tanzania tuitakayo, Mungu ibariki afrika.  

No comments: