Friday, July 29, 2016

Advans Bank sasa yawa rasmi Letshego Bank (T) Limited

 Benki ya Advans ya Tanzania imebadili jina kuwa Letshego Bank (T) Limited kufuatia umiliki wa asilimia 75 za hisa za benki hiyo iliyonunuliwa na kampuni ya Letshego Holdings Limited baada ya kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 19.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa muonekano mpya wa benki hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bw. Yohane Kaduma alisema umiliki huu uliyofanyika tangu mwaka 2015, umefanya Letshego kuwa mbia mkuu wa benki hiyo huku asilimia 25 ikiendelewa kumilikiwa na wanahisa waanzilishi ambao ni Advans SA, na Shirika la Maendeleo ya Uholanzi (FMO) ambao kwa mujibu wa Bw. Kaduma, watendelea kutoa ushirikiano kiuongozi na kiutawala.

Bw. Kaduma aliongeza kuwa pamoja na kuzindua muonekano mpya wa benki hiyo, Letshego ya Tanzania pia imezindua safari ya mabadiliko itakayoiwezesha kuwa kinara katika kuvumbua na kutoa huduma za kifedha ambazo ni shirikishi kwa wanajamii wote (financial inclusion).

Alisema uboreshwaji wa huduma zitakazotolewa na benki hiyo inalenga kusaidia katika kutatua matatizo muhimu ya wateja wao ambayo ni pamoja na kuweka amana, kukopa, kufanya malipo na hata huduma za bima.

“Mwonekano huu mpya wa Letshego Bank ni badiliko ambalo linafanyika katika nchi zote 10 barani Afrika ambapo tupo, na unazindua upya safari ya mabadiliko inayochukuliwa na Letshego. Kwa Tanzania, mabadiloko tuliyoyafanya kama benki, yanaendana pia na dira ya Serikali ya kuleta mendeleo ya kiuchumi na huduma za jamii kwa wananchi wake,” alisema Bw. Kaduma.

Aliongeza kuwa benki ya Letshego inashauku ya kujenga utamaduni chanya wa kukopa na ujumuishwaji wa kifedha kwa watanzania.

“Tunafanya kazi ili kusaidia kuhakikisha kwamba huduma zetu za kifedha zinaleta maana na mabadiliko kwa Watanzania. Wateja wetu ndiyo wamewezesha jina na huduma zetu kukua kufikia hatua tuliyo nayo leo. Tunawashukuru na tunawahakikishia kwamba tunafurahia kuendelea kutoa ufumbuzi wa kifedha utakao boresha maisha yao,” aliongeza Bw. Kaduma.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika kuboresha huduma zeo ndani ya mwonekano huu mpya, pia benki hiyo itaendelea kufanikisha lengo lao la kutoa huduma jumuishi za kifedha ambazo zitaleta uboreshaji wa maisha ya wadau weo wote.

“Letshego Bank inaanzisha ufumbuzi wenye lengo la upatikanaji wa mikopo ya kilimo, elimu, afya na nyumba kwa watu wenye kipato cha chini, cha kati na wajasiriamali wadogo. Wateja na wadau wetu wote, wataendelea kupata huduma za kuweka akiba na kufanya malipo. Katika hili, na ili kuhakikisha kwamba huduma zetu zinapatikana maeneo mengi ya Tanzania, Letshego Bank ina mpango wa kutoa huduma za kibenki kupitia vituo zaidi ya 100, kwa kuitumia Faidika kama wakala wake. Tunaamini kwa ushirikiano wa vyombo husika, hili litawezekana, na Watanzania wengi zaidi watafurahia huduma zetu,” alisema Bw. Kaduma.

Bw. Kaduma alifafanua kuwa hapa Tanzania, Letshego imekuwako kwa miaka 10 sasa kupitia kampuni inayojulikana kwa jina la kibiashara la Faidika.Aliongeza kuwa Advans Bank (ambayo sasa ni Letshego Bank) imekuwako Tanzania kuanzia mwaka 2011. “Katika miaka hii sita ya utoaji wa huduma za kifedha ambapo tumekuwako katika mikoa ya Dar es Salaam (matawi 3), Mwanza na Mbeya, tumetoa ufumbuzi wa masuala ya kifedha ambayo ni rahisi, stahiki, na nafuu kwa zaidi ya watanzania 26,000 nchi nzima,. Huduma hii ikitolewa na wafanyakazi zaidi ya 200 kwenye matawi haya,” alifafanua Bw. Kaduma.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa Letshego ni neno la ki-Setswana linalomaanisha ‘support’ – au Harambee kwa Kiswahili, neno hili huashiria uwezo wa taasisi  kuweza kushirikiana na serikali na watumishi wa serikali, pamoja na wajasiriamali wadogo na wa kati (MSEs)  ili kuweza kutoa huduma  rahisi, nafuu na mahsusi zitakazoweza kuboresha hali ya jamii.


“Muonekano wetu mpya ni wa kisasa zaidi na ukiendana na dhana nzima ya ‘Harambee’, inaonyesha msingi imara, na kwamba sote tunaweza kukua pamoja,” alisema Bw. Kaduma.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Letshego ya Tanzania Bw. Yohane Kaduma (wa pili kulia) akionyesha nembo na muonekano mpya ya benki hiyo iliyobadilishwa kutoka kutambulika kama Advans Bank kuwa rasmi Letshego Bank. Wanaoshuhudia ni Dru Jayaratne (wa kwanza kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa FAIDIKA Bw. Mbuso Dlamini (wa pili kushoto) na Meneja Rasilimali watu wa benki ya Letshego Bi. Rehema Ngusar. 
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Letshego ya Tanzania Bw. Yohane Kaduma akiomwonyesha Mkurugenzi Mtendaji wa FAIDIKA Bw. Mbuso nembo na muonekano mpya ya benki hiyo iliyobadilishwa kutoka kutambulika kama Advans Bank kuwa rasmi Letshego Bank.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Letshego ya Tanzania Bw. Yohane Kaduma (wa pili kulia) akipongezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa FAIDIKA Bw. Mbuso Dlamini (wa pili kushoto) mara baada ya kuzindua nembo na muonekano mpya ya benki hiyo iliyobadilishwa kutoka kutambulika kama Advans Bank kuwa rasmi Letshego Bank. Wanaoshuhudia ni Dru Jayaratne (wa kwanza kulia), na Meneja Rasilimali watu wa benki ya Letshego Bi. Rehema Ngusar. 
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Letshego ya Tanzania Bw. Yohane Kaduma (kulia) akifurahia jambo pamoja na baadhi ya wateja wa benki hiyo Bi. Flora Ferdinand (katikati) na Bi. Farida Walele (kushoto), mara baada kuzindua rasmi muonekano na nembo mpya ya benki hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo awali kama Advans Bank. 
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Letshego ya Tanzania Bw. Yohane Kaduma (kulia) akifurahia jambo pamoja na baadhi ya wateja wa benki hiyo Bi. Flora Ferdinand (katikati) na Bi. Farida Walele (kushoto), mara baada kuzindua rasmi muonekano na nembo mpya ya benki hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo awali kama Advans Bank. 
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Letshego ya Tanzania Bw. Yohane Kaduma (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajume wa bodi na watendaji wa kampuni ya FAIDIKA, pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo mara baada kuzindua rasmi muonekano na nembo mpya ya benki hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo awali kama Advans Bank. 
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Letshego ya Tanzania Bw. Yohane Kaduma (aliyevalia suti na tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi wafanyakazi wa benki hiyo mara baada kuzindua rasmi muonekano na nembo mpya ya benki hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo awali kama Advans Bank.

No comments: