Wednesday, June 8, 2016

WAZIRI WA AFYA AZINDUA BARAZA LA USHAURI LA AFYA YA JAMII NA MAZINGIRA

Na KhadijaKhamis –Maelezo Zanzibar 8/06/2016.

Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo amelizindua rasmi Baraza la Ushauri la Afya ya Jamii na Mazingira lenye wajumbe nane kutoka sekta za Serikali na sekta binafsi .

Akizindua Baraza hilo katika Wizara ya Afya Mnazimmoja, alisema lengo la kuundwa Baraza hilo ni kudhibiti hali ya afya na mazingira ili kuisaidia jamii kujiepusha na maradhi ya mripuko na maradhi ya kuambukiza.

Alisema Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Muhammed Shein alimteuwa Mwenyekiuti wa Baraza hilo mwaka 2013 lakini kutoakana na kutokuwepo wajumbe ambao huteuliwa na Waziri anaehusika na Afya lilishindwa kufanyakazi kwa muda wote.

Aliwataka wajumbe hao kuwa wabunifu katika kutafuta fedha za kusaidia kuendesha kazi bila kutegemea Bajeti ya Wizara kwani fedha wanazopata ni kidogo na haziwezi kuendesha Baraza kwa ufanisi.Ameeleza matumaini yake kwa wajumbe hao, kutokana na umahiri wao wa masuala ya Afya na Mazingira, watafanyakazi kwa mashirikiano na kuleta ufanisi mkubwa kwa jamii ambayo imetuzunguka .

Nae Mwenyekiti wa Baraza hilo Omar Juma Khatib alimshukuru Waziri wa Afya kwa kuona umuhimu wa kuwepo Baraza hilo na kuharakisha kuteuwa wajumbe kuanza kazi rasmi.Ameahidi kuwa atashirikiana na wajumbe kuhakikisha kuwa wanapunguza vifo vinavyotokana na mazingira machafu na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa .

“Wajumbe kazi iliyopo mbele yetu ni muhimu sana kwani inagusa maisha ya watu wetu, hivyo tunapaswa kutoa michango na mapendekezo yetu katika kufanikisha kazi hii, ”alisisitiza Mwenyekiti.Wajumbe wa Baraza hilo wamemshukuru Waziri kutokana na muda mfupi tokea achukue nafasi hiyo kuona kunaumuhimu wa kuundwa rasmi Baraza kwa kufanya uteuzi wa wajumbe.

Wameahidi kuwa watatoa ushirikiano wa karibu kwa Mwenyekiti wao ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Serikali ya kuundwa Baraza la Ushauri wa Afya na Mazingira yanafikiwa .IDARAYA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo akisoma baadhi ya vifungu vya sheria ya Baraza la Ushauri la Afya ya Jamii na Mazingira kabla ya kulizindua Baraza hilo katika hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo akimkabidhi sheria Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Afya ya Jamii na Mazingira Dk. Omar Juma Khatib mara baada ya kulizindua.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Afya ya Jamii na Mazingira Dk. Omar Juma Khatib akizungumza na wajumbe wa Baraza hilo wakati wa uzinduzi, kushoto yake Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Afya ya Jamii na Mazingira Dk. Omar Juma Khatib akizungumza na wajumbe wa Baraza hilo wakati wa uzinduzi, kushoto yake Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo.
Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo akimtakia Kheri Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Afya ya Jamii na Mazingira Dk. Omar Juma Khatib katika utendaji wa kazi zake. Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.
 

No comments: