Monday, June 6, 2016

PROF. MBARAWA AIONYA KAMPUNI ZA SIMU



Meneja wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) mkoa wa Iringa Eng. Ekael Manase akitoa taarifa ya Utendaji kwa Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Watendaji wa kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Mkoani Iringa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akihakiki ujumbe wa Simu uliotumwa kwa mteja kumtahadharisha kuhusu zoezi la kuzima simu feki.Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw,Richard Kasesela na Kushoto Meja wa kampuni ya Simu(TTCL) Mkoa wa Iringa Eng.Ekael Manase.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Meneja wa kampuni ya Simu (TTCL) Mkoa wa Iringa Eng. Ekael Manase kuhakikisha mnara wa simu unaanza kutoa huduma kwa wanakijiji wa Idodi katika Jimbo la Kalenga kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Kidamali wilayani Iringa mara baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Kidamali wilayani Iringa mara baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua chumba cha huduma ya Intanet cha Shirika la Posta Iringa na kusisitiza kudhibiti kompyuta hizo zisitumike kwazama picha zenye uvunjifu wa maadili.



PROF. MBARAWA AIONYA KAMPUNI ZA SIMU

Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa kampuni za simu nchini zilizoingia makubaliano na Serikali kupeleka huduma ya Mawasiliano vijijini kukamilisha kazi hiyo vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani Iringa mara baada ya kukagua mitambo ya kampuni ya simu ya (TTCL) na kubaini kwamba bado kuna baadhi ya vijiji havijafikiwa huduma ya mawasiliano licha ya mkataba wa kutekeleza kazi hiyo kati ya serikali na kampuni hizo kusainiwa miaka miwili iliyopita.

“Tulikubaliana kwenye mkataba na tukawapa fedha kwa ajili ya kupeleka mawasiliano vijijijni hivyo ifikapo mwezi julai kampuni yoyote ya simu itakayokuwa haijatimiza makubaliano hayo tutaipiga faini”. Amesema prof. Mbarawa.

Kuhusu suala la kukatwa kwa mkongo wa taifa wa mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Iringa Prof. Mbarawa amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa mtu au taasisi itakayoharibu miundombinu hiyo.

Aidha, amemuagiza meneja wa TTCL mkoa wa Iringa Eng. Ekael Manase kuhakikisha kuwa minara iliyojengwa katika maeneo ya vijiji Mkoani humo inaanza kutoa huduma ya mawasiliano kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amekagua barabara ya Iringa-Kalenga hadi Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye urefu wa KM 134 ambayo usanifu wake umekamilikka na kusisitiza kuwa itajengwa kwa kiwango cha Lami.

Naye Mbunge wa Isimani ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Willium Lukuvi amesema ujenzi wa barabara hiyo ukikamilika utafufua uchumi wa Mkoa wa Iringa kwa kuwa utavutia wawekezaji na watalii katika Hifadhi ya Ruaha.

Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku nne katika Mkoa wa Iringa ya kukagua maendeleo ya Miundombinu ikiwa ni mkakati wa Serikali kufufua uchumi wa Mkoa huo.

Imetolewa na itengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments: