Tuesday, June 7, 2016

JK ATAKA VIJANA WAAMINIWE NA KUWEZESHA

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (awamu ya nne) Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete jana jumanne alitoa mhadhara wa 13 wa Kumbukumbu ya Rafael M. Salas ulioandaliwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu ( UNFPA), mhadhara huo ulikuwa ni sehemu ya vikao vya mwaka vya Bodi na Mifuko ya Umoja wa Mataifa vinavyoendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Pamoja naye Meza Kuu ni Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dr. Babatunde Osotimehin, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Elliason, Rais wa Bodi, na Balozi Carmelita R. Salas, mjane wa Bw. Rafael M. Salas
Sehemu ya washiriki wa mhadhara wa 13 kumbukumbu ya Rafael M. Salas, uliofanyika siku ya Jumanne ambapo mzungumzaji mkuu alikuwa ni Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Kikwete. Tanzania ni Mjumbe wa UNFPA.

baadhi wa Maafisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Dr. Babatunde Osotimehin akielezea jambo kwa Mhe Rais mstaafu Jakaya Kikwete, wengine ni Balozi Carmelita Salas, Mjane wa Rafael M. Salas aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa UNFPA
Mhe Jakaya Kikwete akiteta jambo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa muda mfupi kabla ya kuanza kwa mhadhara wa 13 wa kumbukumbu ya Rafael Salas uliofanyika katika ukumbi wa ECOSOC katika Umoja wa Mataifa.

Na Mwandishi Maalum, New York

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amesema,     ingawa   idadi kubwa ya vijana wasiokuwa na  uhakika wa maisha yao wala kazi zenye tija na staha wapo katika nchi zinazoendelea, dunia katika ujumla wake inapashwa  kuonyesha  utashi wa kisiasa na udhubutu   wa kuwekeza    kupitia vijana.

Amesema,  mazingira   ya mamilioni ya vijana  kukaa bila shughuli ya aina yote kunatoa mwanya kwa vijana hao   kurubuniwa   na kutumiwa na watu wasiokuwa  na nia  njema na hivyo kutishia  hali ya Amani,  usalama na ustawi wa mwanadamu na hatimaye kushindwa kufikia au kupata faida za kidemografia na maendeleo endelevu.

Mhe. Kikwete ameyasema   hayo jana ( jumanne) hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, wakati alipotoa mhadhara   wa  13 wa kumbukumbu ya Rafael M. Salas. Mhadhara huu  ambao  mada yake  ilikuwa ni “ kuwekeza kwa vijana ili kupata faida ya kidemografia na maendeleo endelevu” uliandaliwa na  Shirika  la    Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu( UNFPA) ikiwa ni sehemu ya   mikutano ya mwaka ya  Bodi  za Mashirika na Mifuko  iliyopo chini ya Umoja wa Mataifa.

 Miongoni wa  viongozi  waliohudhuria na  kushiriki mhadhara  ni  pamoja na  Naibu  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Bw. Jan Eliasson, na  Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA  Dr. Babatunde Osotimehin ,  Bi. Carmelita R. Salas ambaye ni Mjane wa  Bw.  Rafael Salas aliyekuwa  Mkurugenzi  Mtendaji wa  kwanza wa  UNFPA, Mabalozi na wataalamu mbalimbali.

“Tafiti na taarifa mbalimbali zikiwamo za Umoja wa Mataifa, zinaonyesha wazi  ongezeko la  idadi kubwa ya vijana  wanaokadiriwa kufikia 1.8 bilioni  idadi ambayo ni hazina na raslimali kubwa, lakini  pamoja na uwingi wao, wengi bado wanaishi katika hali ya umaskini uliokidhiri,  na ukosefu wa fursa mbalimbali ambazo zingewazesha  kuishi  maisha yenye staha”. akasema Kikwete.

Na kuongeza kuwa, kati ya vijana hao 1.8 bilioni, 74 milioni hawana  ajira  akiwaelezea kama vijana wanaosubiri treni  kando ya reli, treni ambayo haiji.  Mazingira haya  yanadhihirisha upotevu wa  raslimali kubwa ambayo imewekezwa kwa vijana hao na  ambao wamepoteza matumaini.

Akafafanua zaidi kwa kutoa takwimu mbalimbali zinazoonyesha tofauti  ya  faidia za kidemografia  kati ya mabara ya Ulaya, Asia, Amerika ya Latini na Afrika ikiwa ni pamoja na utofauti wa matumizi ya raslimali watu kwa nchi zile ambazo zimethubutu kuwekeza kwa vijana.

Rais Mstaafu Kikwete katika  mhadhara wake huo  na ambao ulipokelewa vema sana na wajumbe waliohudhuria, pia ametoa  vielelezo vya kitakwimu vinavyoainisha  namna  gan  bara la  Afrika  lilivyo nyuma  karibu katika ikielemewa  kila eneo kuanzia  upatikanaji na   utoaji wa huduma za uzazi salama,  idadi ya wakunga wenye elimu ya kutosha, upatikanaji wa huduma za afya,  elimu,  maendeleo ya kijamii na yenye tija na stahiki na  kiwango  cha matumizi ya njia za kisasa  za uzazi wa mpango.

“Vijana  wakiwezeshwa, wakiaminiwa,  wakipewa fursa na wakithubutishwa wanauwezo mkubwa sana wa kuleta mabadiliko. Tunatakiwa  kuwaamini, tunatakiwa kuwashirikisha na kusizisikia sauti zao” amesema.
Na kuongeza kuwa , mipango  na sera zinazoandaliwa kwaajili yao vijana  ni vema  zikawa  shirikishi na kuzingatia  mawazo, maoni na matakwa ya vijana.

“ Haya  na mengi mengi yakitekelezwa kwa kuzingatia mazingira  ya kila nchi na vipaumbele vyake,  tunaweza kugema nguvu kazi hii kubwa kujiletea maendeleo endelevu pasipo kumwacha yeyote nyuma” akasisitiza  Rais Mstaafu.
Katika  hotuba  yake hiyo iliyosheni takwimu na utafifi wa kisayasi, siyo tu  kwamba imeainisha hali halisi ya  mazingira waliyomo vijana bali pia imechochea  majadiliano na takafuri  ya kina.

Baadhi ya mambo  ambayo ameyatilia mkazo ni pamoja na  umuhimu wa  jamiii kuzingatia uzazi salama na wa mpango na kuwa na idadi ndogo  ya  watoto na ambayo wazazi wataweza kuimudu na elimu  itakayokidhi mahitaji ya  soko la ajira  lishe bora na  uchumi imara na endelevu.

Akimkaribisha Rais Mstaafu kuzungumza,  Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Elliason pamoja na  mambo mengine  alimwelezea  Mhe. Kikwete  kuwa ni kiongozi  mpenda amani na  aliyemstari wa mbele katika kusimamia  afya ya mama na mtoto.

No comments: