Wednesday, June 8, 2016

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2016/2017

      UTANGULIZI
1.      Mheshpika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17.  Pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vinavyoelezekina makadirio ya Bajeti. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016 pamoja na Muswada wa Sheria ya kuidhinisha matumizi ya Serikali wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.

2.      Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa baraka na amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa kuniruhusu kusimama hapa mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17. Aidha, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais na mwanamama wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya nchi yetu. Nampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa kwa kuchaguliwa na wananchi wa jimbo la Ruangwa kuwa Mbunge wao na kuteuliwa na Mhe. Rais na kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda pia kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuongoza Bunge letu Tukufu.  Kadhalika, natumia fursa hii kumpongeza Mhe. Mohamed Othman Chande, Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa kuongoza mhimili wa Mahakama kwa weledi mkubwa.

3.      Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niwashukuru sana waheshimiwa wenza wa viongozi wetu wa kitaifa: Mama Janet Magufuli, Bwana Ameir Hafidh Ameir (mume wa Mhe. Makamu wa Rais), Mama Mwanamwema Shein, Mama Mary Majaliwa, Mama Fatuma Ramadhani Mganga (mke wa Mhe. Spika), Bwana James Andilile (mume wa Mhe. Naibu Spika) na Mama Saada El-Maamry Othman (mke wa Mhe. Jaji Mkuu) kwa kuwasaidia na kuwatunza viongozi wetu vizuri.  Asante kwenu wote na Mungu awabariki.

4.      Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine natoa shukrani za pekee kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Mbunge na Waziri wa Fedha na Mipango. Ninatambua kwamba wananchi wa Tanzania wananidai! Tarehe 29 Februari, 1968 Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwasilisha hati ya madai kama ifuatavyo, nanukuu: “Tunadai nini basi kwa wale wenzetu waliojaliwa kupata elimu? Tunadai huduma kwa wananchi na huduma ambayo ukubwa wake utalingana na kiasi cha elimu waliyoipata” mwisho wa kunukuu. Hivyo, napenda kumuahidi tena Mhe. Rais na Watanzania kwamba nitaibeba dhamana hii kwa bidii na uadilifu ili kulipa deni langu kwa nchi yangu. Vilevile, nawapongeza waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kwenu na kuwa sehemu ya Bunge hili.  Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wenzangu na Naibu Mawaziri kwa dhamana kubwa tuliyopewa na Mheshimiwa Rais kuwatumikia Watanzania. Nampongeza pia Dkt. Thomas Kashililah, Katibu wa Bunge na Bw. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa kuratibu vyema shughuli za Bunge na Mahakama kwa mtiririko huo. Napenda pia kumpongeza Prof. Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukagua na kutoa taarifa za matumizi ya fedha za umma kwa wakati.

5.      Mheshimiwa Spika, ninaishukuru sana Kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya uenyekiti wake Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara vijijini na Makamu Mwenyekiti Mhe. Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kwa kuchambua kwa kina bajeti za Mafungu yote na kutoa mapendekezo na ushauri. Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti wa kamati za kisekta kwa ushauri na mapendekezo waliyotoa wakati wakichambua rasimu ya Bajeti hii. Ninamshukuru pia Mhe. George Mcheche Masaju (Mb), Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.

6.      Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge wa Jimbo la Kondoa kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na pia ninamshukuru kwa ushirikiano anaonipatia katika utekelezaji wa majukumu yangu. Aidha, napenda kumshukuru Dkt. Servacius B. Likwelile, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango kwa uratibu na usimamizi mzuri wa maandalizi ya Bajeti hii. Kadhalika, nawashukuru Naibu Makatibu Wakuu; Gavana wa Benki Kuu; Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania; Msajili wa Hazina; Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu; Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; Wakuu wa idara, vitengo na Watumishi wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa waliyoifanya kukamilisha Bajeti hii.

7.      Mheshimiwa Spika, Bajeti hii imezingatia mawazo na mapendekezo ya wadau mbali mbali wakiwemo wenye viwanda, wafanyabiashara na wengine wengi. Nawashukuru wote kwa mawazo na ushauri wao. Kipekee niwashukuru wajumbe wa kamati ya wataalamu na ushauri wa masuala ya kodi (Task Force) na kamati ya kitaifa ya ushauri wa kodi (Think Tank) kwa ushauri wao mzuri walionipa.

8.      Mheshimiwa Spika, kwa kukamilisha shukrani hizi, napenda kutoa shukrani maalum kwanza kwa Prof. Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, mwalimu wangu na mfano bora wa maisha yangu kikazi.  Amenilea kitaaluma na kikazi tangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Benki ya Dunia, na ameendelea kunishauri katika utumishi wangu Serikalini. Ninamshukuru sana kwa uzalendo na unyenyekevu wake na ninamtakia kheri na afya njema yeye na familia yake. Pia ninapenda kutoa shukrani maalum kwa rafiki yangu mpenzi, mke wangu Mbonimpaye kwa kunitunza vizuri, lakini hasa kwa kuniombea msaada wa Mungu siku zote akishirikiana na watoto wetu, wanafamilia wengine na marafiki zetu. Asanteni na Amani iwe kwenu! Aidha nawashukuru viongozi wa dini mbalimbali na watanzania wote ambao waliitikia rai ya Rais wetu Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kumuombea na wanatuombea sana na sisi wasaidizi wake ili tujitoe na kuwatumikia  watanzania, na hasa maskini, kwa bidii na unyenyekevu. Mungu awabariki! Kadhalika, nawashukuru sana wananchi wa kijiji cha Kasumo, wilaya ya Buhigwe nilikozaliwa, pamoja na wananchi wa Kasulu na mkoa wa Kigoma kwa ujumla. Asanteni kwa kunilea na kwa mapenzi yenu mema.

9.   Mheshimiwa Spika, hotuba hii inawasilisha Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”. Serikali inaleta Bajeti hii kwa dhamira ya kweli ya kutekeleza ahadi zake zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ili kukidhi kiu na matarajio ya Watanzania. Malengo makuu ya kiuchumi ya Bajeti hii ni mawili. Kwanza ni kutatua matatizo yanayowakabili wananchi ili kuleta matumaini mapya ya maisha mazuri zaidi kwa wananchi wetu, hasa wa kipato cha chini. Lengo hili litahusisha kufanya mabadiliko makubwa katika utendaji wa Serikali, hususan kurejesha nidhamu ya kazi na uwajibikaji, na kuondokana na ufanyaji kazi kwa mazoea, pia kuimarisha uadilifu na usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali za Taifa. Pili ni kujenga uchumi wa kipato cha kati kiuhalisia kwa kusimamia kwa umakini utulivu wa uchumi na uendelezaji wa viwanda vitakavyoongeza ajira hasa kwa vijana wetu nchini na kuongeza tija kwenye kilimo ili kuongeza kipato katika sekta hii inayotegemewa na wananchi wengi.

10.     Mheshimiwa Spika, wakati Mheshimiwa Rais akifungua Bunge hili tarehe 20 Novemba 2015, alibainisha maeneo yanayolalamikiwa sana na wananchi, na kuelekeza Wizara, Ofisi na Taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua malalamiko hayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Naomba niyarejee kwa kifupi. Kwanza ni rushwa katika maeneo yote ya utoaji huduma kwa wananchi; Pili, ni upotevu wa mapato, ujangili, wizi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha, uzembe na urasimu katika maeneo mbalimbali; eneo la tatu ni huduma zisizoridhisha za upatikanaji wa maji, elimu bora na afya; eneo la nne ni migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, vijiji na hifadhi, wananchi na wawekezaji, wananchi na wamiliki wa mashamba pori na uvunjaji wa sheria za ardhi.

11.     Mheshimiwa Spika, eneo la tano ni huduma zisizoridhisha za usafiri na usafirishaji kutokana na uchakavu wa miundombinu ya reli, barabara, usafiri wa majini; na udhaifu mkubwa wa shirika la ndege. Eneo la sita ni upungufu katika utoaji haki ikiwa ni pamoja na mlundikano wa kesi mahakamani, wananchi kubambikiwa kesi na polisi, makazi duni na ukosefu wa vitendea kazi kwa askari; eneo la saba ni kodi na tozo za kero kwenye mazao, uhaba wa zana na pembejeo za kilimo, mifugo na uvuvi, uhaba wa masoko ya uhakika, maghala, maafisa ugani na huduma za ugani, na uvuvi haramu; na eneo la nane ni uwezeshaji mdogo kwa makundi maalum hususan wazee, walemavu, wanawake, watoto, vijana, wafanyakazi, wasanii, wanamichezo, wachimbaji wadogo na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

12.     Mheshimiwa Spika, baada ya rejea hiyo, naomba niseme tena kwamba mkazo mkuu wa Bajeti hii ni kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kutatua kero za wananchi. Aidha, Serikali itatekeleza azma ya kuendeleza viwanda ambavyo ndiyo msingi wa uchumi endelevu utakaowezesha Taifa letu kufikia hadhi ya kipato cha kati na hali bora ya maisha ya wananchi walio wengi ifikapo mwaka 2025.

13.       Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 inalenga kuimarisha miundombinu ya msingi kama vile ya maji, umeme na usafirishaji kwa ajili ya kuhakikisha maendeleo ya viwanda nchini na vile vile kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo yanayotumika kama malighafi viwandani. Ili kufanikisha hilo, mkazo mkubwa utawekwa kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na ugawaji wa rasilimali hizo katika maeneo muhimu ya kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda. Jitihada kubwa zitaelekezwa katika kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kuibua vyanzo vipya vya mapato, na kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki - EFDs ili kuongeza makusanyo na vile vile kudhibiti matumizi yasiyokuwa na tija. Hivyo, kauli mbiu ya Bajeti za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka 2016/17 ni “kuongeza uzalishaji viwandani ili kupanua fursa za ajira” (Industrial growth for job creation). Kwa msingi huo, Bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2016/17 imeongezwa kwa kiasi kikubwa na kufikia asilimia 40 ya bajeti yote tofauti na miaka yote ya nyuma ambapo ilikuwa wastani wa asilimia 25. Bajeti hii pia inalenga kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwekeza ili kuvutia ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje katika kuendeleza viwanda na kilimo.

II.      MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2015/16

14.       Mheshimiwa Spika, mpango na bajeti ya Serikali mwaka 2015/16 ililenga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 22.49 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 13.99 zilikuwa ni makadirio ya mapato ya ndani zikijumuisha mapato ya Halmashauri; shilingi trilioni 2.32 ni mikopo nafuu na misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo; shilingi trilioni 4.03 ni mikopo ya kibiashara ya ndani; na shilingi trilioni 2.14 ni mikopo ya kibiashara ya nje. Aidha, kiasi cha shilingi trilioni 16.57 kilipangwa kutumika kwenye matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 5.92 kwenye matumizi ya maendeleo.


Mapato

15.       Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mapato ya ndani yanapatikana, sera za mapato za mwaka 2015/16 zililenga kupunguza misamaha ya kodi isiyokuwa na tija; kuongeza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato; na kuongeza wigo wa mapato. Sera hizo zililenga kukusanya mapato ya kodi ya shilingi trilioni 12.36, mapato yasiyo ya kodi ya shilingi trilioni 1.11 na mapato yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 521.9.

16.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2015 hadi Aprili 2016, jumla ya makusanyo ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) yalikuwa shilingi trilioni 11.48 sawa na asilimia 99 ya makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 11.55 katika kipindi hicho. Mapato ya kodi yalikuwa shilingi trilioni 10.17, sawa na asilimia 100 ya lengo, mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 967.2 sawa na asilimia 105 ya lengo na mapato yaliyokusanywa na Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 344.1, sawa na asilimia 79 ya makadirio kwa kipindi hicho.

17.       Mheshimiwa Spika, mwenendo huo mzuri wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi umetokana na  juhudi za Serikali ya awamu ya tano katika ukusanyaji wa mapato na kupunguza mianya ya ukwepaji wa kodi, tozo na ada mbalimbali. Hata hivyo, mapato ya Halmashauri hayakufikia lengo kutokana na mifumo ya ukusanyaji mapato isiyoridhisha pamoja na kodi ya majengo kutokusanywa kwa kiwango kilichotarajiwa kulingana na fursa zilizopo.

Misaada na Mikopo ya Nje yenye Masharti Nafuu

18.       Mheshimiwa Spika, Serikali ilitarajia kupata shilingi trilioni 2.32 kutokana na  misaada na  mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Hadi Aprili, 2016, misaada na mikopo nafuu iliyopatikana ni shilingi trilioni 1.15, sawa na asilimia 65 ya lengo la kipindi hicho. Kutofikiwa kwa lengo kumetokana na baadhi ya Washirika wa Maendeleo kuweka masharti mapya na kubadilika kwa sera ndani ya nchi zao zinazohusiana na misaada kwa nchi zinazoendelea.

Mikopo yenye masharti ya Kibiashara

19.       Mheshimiwa Spika, mwaka 2015/16, Serikali ilipanga kukopa kiasi cha shilingi trilioni 6.18 ambapo shilingi trilioni 4.03 ni kutoka vyanzo vya ndani  na shilingi trilioni 2.15 kutoka vyanzo vya nje. Fedha hizo zililenga kugharamia miradi ya maendeleo na kulipia dhamana za Serikali za muda mfupi na hatifungani za Serikali zilizoiva. Hadi Aprili, 2016 Serikali ilikopa kutoka vyanzo vya ndani shilingi trilioni 3.94 sawa na asilimia 97.8 ya lengo. Kati ya hizo, shilingi trilioni 2.56 zilikuwa kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali za muda mfupi na hatifungani zilizoiva na shilingi trilioni 1.39 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, kwa upande wa mikopo ya nje, Serikali ilisaini mikataba yenye jumla ya Dola za Kimarekani milioni 674.3 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya usafirishaji, awamu ya pili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam pamoja na mradi wa maji safi na maji taka Arusha. Hata hivyo, hali ya soko la mitaji ulimwenguni ilikuwa mbaya na kusababisha kuongezeka  kwa gharama za mikopo mipya kwa kiwango kikubwa na hivyo kuathiri upatikanaji wa mikopo ya nje.

Matumizi

20.       Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2015/16 pamoja na mambo mengine ililenga kugharamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015; kukamilisha miradi iliyoanza kutekelezwa; na kulinda mafanikio yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya, maji pamoja na maendeleo ya jamii.  Hadi Aprili, 2016 Serikali ilitoa mgao wa matumizi wa shilingi trilioni 16.86 kwenye mafungu mbalimbali sawa na asilimia 89.9 ya lengo la kipindi hicho. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 13.65  zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi  ya kawaida na shilingi trilioni 3.21 kwa ajili ya  matumizi ya maendeleo. Miradi ya maendeleo iliyogharamiwa kwa kutumia fedha za ndani ni pamoja na: usambazaji wa umeme vijijini, ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja, ukarabati wa reli ya kati, ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi I na II, na usambazaji wa maji mijini na vijijini.

Ulipaji wa Madai

21.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kulipa madai mbalimbali yaliyohakikiwa ya makandarasi, wahandisi washauri, watumishi na wazabuni wa huduma na bidhaa  kulingana na upatikaji wa fedha. Hadi Aprili 2016, Serikali imelipa jumla ya shilingi trilioni 1.13, kati ya fedha hizo: shilingi bilioni 689.5 ni kwa ajili ya makandarasi na wahandisi washauri; shilingi bilioni 27.9 kwa ajili ya walimu na malimbikizo ya mishahara ya watumishi; shilingi bilioni 10.0 kwa ajili ya Jeshi la Polisi; shilingi bilioni 211.0 kwa ajili ya mikataba ya kijeshi; na shilingi bilioni 194.0 kwa ajili ya ankara za umeme kwa Wizara, Idara zinazojitegemea na Taasisi za Serikali.
Mafanikio na Changamoto katika Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2015/16

22.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2015/16, Serikali imefanikiwa kutekeleza shughuli muhimu za Bajeti licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.02 kwa mwezi mwaka 2015/16 ikilinganishwa na wastani wa shilingi bilioni 904.0 kwa mwezi mwaka 2014/15; kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia fedha za ndani bila ya kupata msaada kutoka kwa wadau wa maendeleo kama ilivyozoeleka kwa chaguzi zilizopita; na kuanza kwa utekelezaji wa elimu ya msingi bila malipo.

23.     Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni kuongezeka kwa wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 99,069 mwaka 2014/15 hadi 123,798 mwaka 2015/16; kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa ya makandarasi, wazabuni wa huduma na bidhaa na watumishi.

24.     Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, zimejitokeza changamoto kadhaa zikiwemo: ukwepaji wa kodi unaohusisha wafanyabiashara na watumishi wasio waadilifu; uelewa mdogo wa Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani; mwitikio mdogo wa wafanyabiashara katika matumizi ya mashine za kielektroniki yaani EFDs pamoja na wananchi kutodai stakabadhi zitokanazo na mashine hizo katika ununuzi wa bidhaa na huduma; mazingira magumu ya ukusanyaji wa kodi katika sekta isiyo rasmi; uwepo wa wafanyakazi na wanafunzi hewa; na kuwepo kwa mahitaji makubwa yasiyowiana na uwezo wa mapato, yakiwemo mahitaji ya kuboresha miundombinu hususan ya maji, reli, bandari, viwanja vya ndege na barabara.

Usimamizi wa Deni la Taifa

25.     Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana, na Misaada SURA 134.  Katika kuhakikisha kuwa deni la taifa linasimamiwa kikamilifu, Serikali inakamilisha uaandaji wa Sera ya Usimamizi wa Deni la Taifa na kufanya marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 ili iendane na Sera hiyo. Sera hiyo itatoa dira ya muda mrefu katika usimamizi wa deni la Taifa na hivyo kuiwezesha Serikali kuwa na usimamizi madhubuti wa deni la Taifa. Aidha, Sera hiyo itatoa mwongozo wa kukuza na kuongeza ufanisi wa soko la fedha la ndani pamoja na kusaidia utekelezaji wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 kwa ufanisi zaidi.

26.     Mheshimiwa Spika, hadi Machi, 2016 Deni la Taifa lilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 20.94 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani bilioni 19.69 Juni, 2015 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 6.34. Kati ya kiasi hicho, Deni la Serikali lilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 17.93 na Deni la nje la sekta binafsi lilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 3.01. Aidha, Deni la Serikali liliongezeka kwa asilimia 6.01 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani bilioni 16.92 Juni, 2015. Ongezeko hilo lilitokana na mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Baadhi ya miradi iliyoendelea kutekelezwa kutokana na mikopo hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja nchini, mradi wa kimkakati wa kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga, mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kusafishia gesi, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, na mradi wa maji Ruvu chini na Ruvu juu.

27.     Mheshimiwa Spika, pamoja na kuendelea kuongezeka kwa Deni la Taifa, bado ni himilivu. Hii inathibitishwa na Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Taifa (Debt Sustainability Assessment) iliyofanyika Mwezi Septemba, 2015 ambayo ilionesha kuwa deni hilo ni himilivu katika kipindi cha muda wa kati na mrefu. 

Madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Serikali

28.       Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2015/16, Serikali iliahidi kulipa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kutoa hatifungani maalum. Hata hivyo, katika hatua za mwisho za kukamilisha mikataba ya makubaliano kati ya Serikali na mifuko ili kutoa hatifungani maalum, kulijitokeza masuala mbalimbali yakiwemo utofauti katika ukokotoaji wa deni pamoja na michango ya watumishi hewa. Kutokana na tofauti hizo, Serikali kupitia Mkaguzi wa Ndani Mkuu ilianza kufanya uhakiki kwenye mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii. Mkaguzi wa Ndani Mkuu amekamilisha uhakiki kwenye Mfuko wa PSPF na mara zoezi litakapokamilika kwenye mifuko mingine, Serikali itatoa hatifungani maalum kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii. Serikali itafanya pia maboresho katika sekta hii ya hifadhi za jamii ili kuleta ufanisi na tija.

  III.      BAJETI YA MWAKA 2016/17
Shabaha na Misingi ya Bajeti ya Mwaka 2016/17
29.       Mheshimiwa Spika, kufuatia kukamilika kwa zoezi la uchambuzi wa mwenendo wa viashiria vya uchumi jumla na maoteo katika kipindi cha muda wa kati - financial programming, shabaha za uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2016/17 ni kama ifuatavyo:-

(i)           Pato Halisi la Taifa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka 2016 kutoka 7.0 mwaka 2015;
(ii)          Kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei katika wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 na asilimia 8.0 mwaka 2016;
(iii)        Mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri kufikia asilimia 14.8 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16, na kuendelea kuongezeka kufikia asilimia 16.9 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;
(iv)        Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.8 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 kutoka asilimia 12.6 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16;
(v)          Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 23.2 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16 hadi asilimia 27.0 mwaka 2016/17;
(vi)        Nakisi ya bajeti inakadiriwa kuwa asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 kutoka makadirio ya bajeti ya asilimia 4.2 mwaka 2015/16;
(vii)       Nakisi katika urari wa malipo ya kawaida kuwa asilimia 7.9 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16 na kupungua hadi asilimia 7.5 mwaka 2016/17; na
(viii)     Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne Juni 2017.

30.       Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo hayo yatafikiwa kwa kutegemea misingi ya Bajeti ifuatayo:-

(i)           Kuendelea kuwepo kwa amani, usalama, utulivu na utengamano nchini, kikanda na duniani;
(ii)          Utulivu wa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia;
(iii)        Kuwepo kwa hali nzuri ya hewa nchini na katika nchi jirani;
(iv)        Kuendelea kuimarika kwa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii kama vile Pato la Taifa, biashara ya nje, ujazi wa fedha, mapato, matumizi na huduma za jamii;
(v)          Kuimarika kwa sera za fedha na za bajeti zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei na tofauti kati ya riba za amana na za mikopo;
(vi)        Kuendelea  kuimarika na kutengemaa kwa uchumi wa dunia; na
(vii)       Ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi utaongezeka hususan kwenye uwekezaji katika viwanda.

Sera za Mapato kwa mwaka 2016/17

31.       Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano imedhamiria  kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali. Katika mwaka 2016/17, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Katika kufanikisha azma hii, sera za mapato kwa mwaka 2016/17 zimejielekeza kwenye maeneo yafuatayo:

(i)           Kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;
(ii)          Kuendelea kupanua wigo wa walipa kodi ikiwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iweze kuingia katika mfumo wa kodi;
(iii)        Kuimarisha ufuatiliaji wa mapato yanayokusanywa na taasisi na mamlaka mbalimbali za serikali;
(iv)        Kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija; na
(v)          Kuendelea kuimarisha usimamizi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara bandarini, kwenye viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani ili kuhakikisha kodi stahiki zinakusanywa.

Misamaha ya Kodi

32.       Mheshimiwa Spika, Serikali  itaendelea kudhibiti utoaji wa misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini na wawekezaji ili kuhakikisha inakuwa na tija kwa Taifa. Katika kutekeleza hili, Serikali itafanya marekebisho ya sheria husika ili kuondoa matumizi mabaya ya misamaha ya kodi. Marekebisho hayo yatawasilishwa katika muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016. Pamoja na mambo mengine, marekebisho hayo yatalenga kuwataka wanufaikaji kulipa kodi kwa bidhaa watakazoagiza na baadae kuwasilisha maombi ya kurejeshewa kodi hiyo baada ya uhakiki kufanyika.

33.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutangaza na kutoa taarifa za wanufaika wa misamaha ya kodi kila robo ya mwaka ili wadau waweze kufahamu sekta au taasisi iliyonufaika na misamaha hiyo na maeneo ilikoelekezwa. Utaratibu huu utasaidia kudhibiti wafanyabiashara, taasisi na makampuni yanayotumia vibaya misamaha hiyo kwa kujinufaisha wao binafsi na watumishi wa umma wasio waadilifu.

Mapato yasiyo ya Kodi

34.     Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2016/17, usimamizi wa ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi ikiwa ni pamoja na kodi ya majengo utakuwa chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. Uamuzi wa kuipatia TRA  jukumu hili unatokana na uzoefu na mifumo ya ukusanyaji wa mapato waliyonayo nchi nzima lakini pia mafanikio na uzoefu wa nchi nyingine kama Ethiopia na Rwanda. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato. Miongoni mwa makusanyo yanayolengwa ni pamoja na: tozo, faini kama vile za mahakama na usalama barabarani, ada, viingilio kwenye hifadhi za Taifa na viwanja vya michezo pamoja na vibali vya kuvuna maliasili.

35.     Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na utaratibu wa kuziruhusu baadhi ya taasisi za Serikali kutumia mfumo wa kubakiza maduhuli – retention. Utaratibu huu umekuwa ukipunguza mapato kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kuzinufaisha taasisi chache. Hivyo, kuanzia mwaka 2016/17, Serikali itafuta utaratibu huo. Uamuzi huu ni kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 kifungu 58 (a) mpaka (c) ambayo inaelekeza mapato yote ya Serikali yakusanywe na kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Sambamba na matakwa ya Sheria ya Bajeti, tathmini iliyofanyika kuhusu utaratibu wa retention ilibaini kuwa:
(i)           Taasisi zinazohusika na utaratibu wa “retention” zimeacha majukumu yao ya msingi na kuegemea zaidi kwenye shughuli za ukusanyaji mapato. Mifano ni pamoja na Wakala wa Misitu na Kitengo cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi;
(ii)          Baadhi ya taasisi zenye mfumo wa “retention” zinapata fedha nyingi na kuonekana kujinufaisha zaidi wakati Wizara, Idara na Taasisi zingine zinakabiliwa na uhaba wa fedha. Hali hii imesababisha kuongezeka kwa maombi kutoka taasisi nyingine kutaka kujiunga na utaratibu huu;
(iii)        Taasisi zilizo kwenye mfumo wa “retention” bado zinalipwa mishahara asilimia 100 kutoka kwenye mfuko mkuu wa Serikali; na
(iv)        Utaratibu huu wa “retention” umesababisha idara ambazo awali zilikuwa zikichangia Mfuko Mkuu wa Serikali kupitia maduhuli kutochangia na  hivyo kupunguza mapato ya Serikali.
36.       Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu hizo, kuanzia sasa mapato yote yatakusanywa na kuwasilishwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kila fungu litapewa fedha kulingana na bajeti yake. Wizara ya Fedha na Mipango kwa upande wake itahakikisha kwamba fedha kutoka Mfuko Mkuu zinagawiwa kwa Mafungu mbalimbali bila kuchelewa kulingana na mapato yaliyokusanywa.

Sera za Matumizi kwa Mwaka 2016/17

37.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na miongozo mbalimbali. Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo. Katika kutimiza azma hii, Serikali itachukua hatua mbalimbali kama ifuatavyo:
(i)           Kuwianisha matumizi na mapato halisi yatakayopatikana kwa kila mwezi ili kuepuka malimbikizo ya madai. Maafisa Masuuli wanaagizwa kuzingatia maelekezo ikiwemo kuingia miadi baada ya kupokea mgao wa fedha (exchequer) na siyo kabla;
(ii)          Kuhakikisa malipo kwa wazabuni na watoa huduma yanafanyika kwa kuwasilisha Hati za Ununuzi - LPOs zitokanazo na IFMS;
(iii)        Kuwasilisha Bungeni marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kuziba mianya ya upotevu wa fedha katika ununuzi wa umma na kuhakikisha ununuzi unawiana na thamani ya fedha itakayotumika;
(iv)        Kudhibiti matumizi ya taasisi za Serikali yasiyo na tija na kufanya tathmini ya gharama za uendeshaji ili kuchukua hatua stahiki kwa maendeleo ya nchi;
(v)          Kuendelea na zoezi la kuunganisha Halmashauri zote nchini kwenye mfumo wa malipo ya kibenki ili kuongeza udhibiti wa matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha kwamba malipo yanafika kwa wakati;
(vi)        Kuhakikisha kuwa mashirika ya umma yaliyoundwa kwa lengo la kujiendesha kibiashara yanajiendesha kwa faida bila kutegemea ruzuku ya Serikali; na 
(vii)       Kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya matumizi ya fedha za umma hususan katika miradi ya maendeleo.

Maeneo ya Vipaumbele

38.       Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye hotuba yangu ya Hali ya Uchumi, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 una maeneo makuu manne (4) ya vipaumbele:- (i) Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda; (ii) Kufungamanisha Maendeleo ya Uchumi na Rasilimali Watu; (iii) Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji; na  (iv) Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango. Ili kufikia malengo hayo, mikakati itakayotumika ni pamoja na: kuhamasisha wawekezaji na sekta binafsi kuwekeza katika viwanda na maeneo mbalimbali nchini hususan kupitia mfumo wa ubia baina ya serikali na sekta binafsi (PPP); kuondoa vikwazo kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara; na kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango.

Kuongeza Uzalishaji Viwandani

39.       Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, kauli mbiu ya Bajeti ya mwaka 2016/17 ni “kuongeza uzalishaji viwandani ili kupanua fursa za ajira”. Katika kufikia azma hii, Serikali imelenga kutekeleza mikakati mbalimbali itakayochochea uwekezaji katika viwanda. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na: kufanya uthamini wa ardhi na mali na kulipa fidia kwa maeneo maalum ya uwekezaji yaliyotengwa nchini; kugharamia tafiti za viwanda kupitia taasisi za TIRDO, TEMDO, CAMARTEC na COSTECH; kuendeleza miundombinu ya viwanda vidogo kupitia SIDO; kuanzisha kongane za viwanda (industrial clusters); na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia rahisi na nafuu kwa ajili ya viwanda. Katika mwaka 2016/17, Serikali imetenga fedha za maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 50.9 katika fungu 44 na fungu 46 ambazo pamoja na mambo mengine zitagharamia utekelezaji wa maeneo niliyoainisha hapo juu.

40.       Mheshimiwa Spika, kama alivyoelekeza Mhe. Rais wakati wa hotuba ya ufunguzi wa Bunge lako Tukufu, Serikali itahakikisha viwanda vilivyopo vinafanya kazi. Katika mwaka 2016/17, Serikali itakamilisha tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa ili kuweka mikakati ya namna bora ya kuviendeleza. Baadhi ya viwanda hivyo ni viwanda vya nguo, viwanda vya mazao ya mifugo, viwanda vya kusindika mazao yakiwemo mazao ya mpira, korosho, tumbaku, miwa na mpunga. Katika kutekeleza jukumu hilo, fedha za maendeleo zimetengwa katika Mafungu mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza mashamba; na kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, na ya mifugo. Pamoja na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda, Serikali itachukua hatua stahiki dhidi ya wawekezaji waliokiuka masharti ya mikataba ya mauzo ya viwanda walivyobinafsishiwa.

41.       Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya uwekezaji wa viwanda, Serikali imetenga fedha za kuboresha miundombinu ya uwekezaji hususan ya umeme, maji, barabara, bandari na reli. Aidha, Serikali imedhamiria kuondoa urasimu usio wa lazima na kuharakisha utoaji wa maamuzi ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda. Vilevile, zipo hatua mahsusi za kodi zinazopendekezwa katika Bajeti hii ambazo zina lengo la kushawishi na kuhimiza uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda. Serikali pia itaimarisha upatikanaji wa mikopo ya uendelezaji wa viwanda kupitia Benki ya Rasilimali pamoja na taasisi nyingine za fedha.

42.       Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia balozi zetu na Diaspora, itaimarisha diplomasia ya uchumi katika nchi mbalimbali hasa zile zilizoendelea pamoja na nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi, ikiwemo Jamhuri ya Watu wa China, India, Korea Kusini, Afrika Kusini na Brazil ili kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania na hivyo kufanikisha azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda. Vilevile, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini ambayo yatahamasisha kampuni za kigeni zilizoko hapa nchini kuwa mabalozi wetu na kuvutia kampuni nyingine za nje wanakotoka kuja kuwekeza hapa nchini. Hivyo, kama nilivyoeleza awali, jukumu la kuboresha mazingira ya uwekezaji litapewa kipaumbele katika Bajeti ya mwaka 2016/17.

HATUA ZA KUTATUA KERO ZA WANANCHI

43.       Mheshimiwa Spika; bajeti hii itajikita kutatua kero katika maeneo yaliyolalamikiwa na wananchi kama nilivyoeleza hapo awali. Baadhi ya hatua za kibajeti na kiutawala zitakazochukuliwa ni kama ifuatavyo:

Rushwa katika Utoaji wa Huduma

44.       Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na suala la rushwa na ufisadi, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.5 ili kuwezesha uanzishwaji wa mahakama ya mafisadi. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 72.3 katika bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuiwezesha taasisi hii kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Vile vile katika bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali imetenga shilingi bilioni 44.7 kwa ajili ya kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kukagua na kudhibiti matumizi ya fedha za umma.

Hatua za Kuzuia Upotevu wa Mapato

45.       Mheshimiwa Spika, Serikali itadhibiti upotevu wa mapato kwa kuimarisha ufuatiliaji wa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya biashara, bandarini, viwanja vya ndege na mipakani; kuwajengea uwezo watumishi ili waweze kufanya kaguzi za kitaalam hasa katika sekta za madini, maliasili, ardhi, mafuta na gesi asilia; kuhimiza matumizi ya mifumo ya kieletroniki katika kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, pamoja na kupunguza misamaha ya kodi.

46.       Mheshimiwa Spika, Serikali inawapongeza wafanyabiashara walioitikia matakwa ya Sheria Ya Usimamizi wa Kodi ambayo inamtaka kila mfanyabiashara isipokuwa wale ambao wametangazwa rasmi na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato kutotumia mashine za EFD kutoa risiti kila anapouza bidhaa au huduma. Hata hivyo, kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao bado wanakaidi matakwa haya ya kutumia mashine hizo. Napenda kuwasihi wafanyabiashara hao kuanza mara moja kutumia mashine hizo vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya leseni zao za biashara na hawataruhusiwa kufanya biashara hapa nchini kwa kipindi kisichopungua miaka miwili. Aidha, kwa upande wa Serikali, ili kuwa na usimamizi mzuri wa fedha za Serikali na kuhakikisha kwamba zinatumika kama ilivyokusudiwa, kwa mamlaka niliyopewa chini ya Sheria ya Fedha za Umma pamoja na kanuni zake malipo yote lazima yaambatanishwe na ankara za madai au stakabadhi (tax invoice) zilizotolewa na mashine za EFD. Kwa sababu hiyo kuanzia tarehe 1 Julai 2016, ni marufuku kwa Wizara, Taasisi, Wakala za Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya biashara na wazabuni na wafanyabiashara wengine ambao hawatumii mashine za kielektroniki - EFDs. Aidha, malipo yatakayofanywa bila stakabadhi au Ankara zisizokuwa za mashine za EFD ni lazima ziambatanishwe na ushahidi kuwa mfanyabishara husika ametangazwa rasmi na Kamishna wa Mapato kutotumia mashine za EFD.

Hatua za Kudhibiti Matumizi

47.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua za kupunguza na kudhibiti matumizi bila kuathiri ubora wa huduma zinazotolewa na hivyo kuhakikisha uwepo wa ufanisi katika matumizi ya Serikali. Baadhi ya hatua hizo zimeainishwa katika Mwongozo wa kutayarisha Mpango na Bajeti ya mwaka 2016/17 niliouwasilisha hapa Bungeni Februari, 2016. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na:
(i)           Kuhakikisha mikutano yote ikiwa ni pamoja na mikutano ya bodi, mafunzo na semina inatumia kumbi za Serikali na Taasisi za Umma;
(ii)          Kutoa kipaumbele kwa Taasisi za Umma katika kutoa huduma kwa Serikali kama vile bima, usafirishaji wa barua, mizigo na vifurushi, matangazo na usafiri;
(iii)        Kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara;
(iv)        Kudhibiti ulipaji wa mishahara kwa watumishi ili kuepuka malipo yasiyostahili. Aidha, Serikali itaendelea kufanya sensa ya watumishi wote;
(v)          Kudhibiti utoaji wa mikopo ya elimu ya juu ili kuepuka utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wasio stahili;
(vi)        Kuendelea kufanya ununuzi wa magari kwa pamoja na bidhaa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kupata unafuu wa bei;
(vii)       Kuendelea kudhibiti gharama za uendeshaji wa magari ikiwa ni pamoja na matengenezo, mafuta na vilainishi;
(viii)     Kupunguza na kuondoa matumizi yasiyo na tija katika maeneo mbalimbali ikiwemo maadhimisho na sherehe za kitaifa, matamasha, machapisho na safari za ndani na nje ya nchi zisizo na tija;
(ix)        Kuhimiza matumizi ya nakala laini (soft copy) za machapisho mbalimbali hususan yanayozidi kurasa 50 ili kupunguza gharama za uchapishaji na kutunza mazingira; na
(x)          Kudhibiti matumizi ya Taasisi na Mashirika ya Umma yasiyowiana na majukumu yao ya msingi na yasiyo na tija.

Kero katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

48.       Mheshimiwa Spika, azma kuu ya Serikali ni kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa mtazamo wa kibiashara, kukuza viwanda na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na sekta hii. Hata hivyo, bado sekta hii inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo kodi na tozo za mazao zisizo na tija, uhaba wa pembejeo, vifaa duni, masoko, na uhaba wa maafisa ugani.

49.       Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni 1.56 sawa na asilimia 4.9 ya bajeti yote ukiondoa deni la Taifa kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji zikiwemo ununuzi wa pembejeo; kuboresha upatikanaji wa masoko; kuongeza upatikanaji wa zana bora na za kisasa za kilimo, ufugaji na uvuvi; na kuongeza maafisa ugani.

50.       Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kupunguza ama kuondoa kabisa ushuru na kodi mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi zisizo na tija. Nitaeleza hatua mahsusi muda mfupi ujao. Aidha, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania itaendelea kutoa mikopo ya riba nafuu na masharti yanayozingatia hali halisi ya sekta ya kilimo ili kusaidia kuleta mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kijungujiko (subsistence farming) kwenda kilimo cha kibiashara. Katika mwaka 2016/17, Benki ya Kilimo itaendelea kutangaza na kupanua huduma zake kwa wananchi mikoani.

Migogoro ya Ardhi

51.     Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na juhudi za kutatua migogoro katika Sekta ya ardhi ikiwemo migogoro kati ya wakulima na wafugaji, vijiji na hifadhi, wananchi na wawekezaji, uvunjaji wa sheria za ardhi na umiliki wa mashamba pori. Katika kukabiliana na migogoro hiyo, Serikali imetenga shilingi bilioni bilioni 5.0 kwa ajili ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi; shilingi bilioni 13.0 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa umilikishwaji wa ardhi; na shilingi bilioni 8.8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji wa ardhi. Aidha, Serikali imetenga shilingi bilioni 33.4 kwa ajili ya programu ya kuwezesha umilikishaji wa ardhi na uwekaji wa kumbukumbu utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Vilevile, Serikali itaendelea kusajili migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini na kutafuta ufumbuzi kulingana na mazingira ya eneo husika ili kupunguza migogoro baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi.

Huduma zisizoridhisha za Usafiri na Usafirishaji

52.       Mheshimiwa Spika, Serikali  itaendelea kukabiliana na kero zinazotokana na uchakavu wa miundombinu ya reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege. Katika mwaka 2016/17, Serikali imetenga shilingi trilioni 5.47 sawa na asilimia 25.4 ya bajeti yote ukiondoa Deni la Taifa, kwa ajili ya miradi ya ujenzi na uchukuzi. Baadhi ya maeneo yanayohusika ni;
(i)           Ujenzi wa miundombinu ya barabara – kiasi cha shilingi trilioni 2.18 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hasa zenye kufungua fursa za kiuchumi na kukarabati barabara zilizopo
(ii)          Uchukuzi – kiasi cha shilingi trilioni 2.49 kimetengwa kwa ajili ya kuanza kujenga reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge; ununuzi wa ndege mpya tatu za abiria; ununuzi wa meli mpya ziwa Viktoria; ukarabati wa meli katika ziwa Viktoria na ziwa Tanganyika; uboreshaji wa miundombinu ya bandari; na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege. Aidha, Kiasi cha shilingi bilioni 161.4 kimetengwa katika Mfuko wa Reli kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni pamoja na ukarabati wa na Reli.
Umeme
53.       Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni 1.13 sawa na asilimia 5.3 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa ili kugharamia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani. Baadhi ya miradi itakayotekelezwa ni pamoja na: kuongeza kasi ya usambazaji umeme vijijini kupitia REA na kukamilisha miradi ya umeme inayoendelea ikiwemo kuongeza mitambo mingine yenye uwezo wa kufua MW 185 katika mradi wa Kinyerezi – I na Kinyerezi II. Serikali itahakikisha kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linakuwa na uwezo kifedha ili lijiendeshe lenyewe na kuwa na ushindani katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo nafuu ili kupunguza gharama kwa wazalishaji na walaji.

Upatikanaji duni wa huduma za afya, maji na elimu.

54.       Mheshimiwa Spika, kuna changamoto nyingi katika maeneo haya,  ikiwemo kukosekana kwa upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani; na huduma bora za afya. Aidha, kuna changamoto za ubora wa elimu na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa wakati. Bajeti ya mwaka 2016/17 imejielekeza katika kutatua changamoto hizo kama ifuatavyo:
Elimu
55.       Mheshimiwa Spika, sekta ya elimu imetengewa jumla ya shilingi trilioni 4.77 sawa na asilimia 22.1 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa. Fedha hizi zimetengwa kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali za elimu zikiwemo: Elimu Msingi bila malipo; gharama za uendeshaji wa shule ikiwemo chakula, ununuzi wa vitabu, na mitihani; mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu; na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu katika ngazi zote
Afya

56.       Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa huduma bora za afya kwa wananchi, Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni 1.99 sawa na asilimia 9.2 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa kwa ajili ya sekta ya afya. Baadhi ya maeneo yanayohusika ni pamoja na ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi (reagents) ambayo yametengewa shilingi bilioni 180.5; ulipaji wa deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) shilingi bilioni 71.0; na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika ngazi zote.
Maji
57.     Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni 1.02 sawa na asilimia 4.8 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa, kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama nchini. Baadhi ya shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na: ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya maji mijini na vijijini; ulipaji wa madeni ya wakandarasi na utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maji.

Mazingira Wezeshi kwa Sekta Binafsi

58.       Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo juu, katika bajeti ya 2016/17 Serikali imedhamiria kuboresha mazingira ya kufanya biashara, ikiwa ni pamoja na kuwekeza kwenye miundombinu ya reli, barabara, bandari, maji na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika maeneo mbalimbali. Aidha, Serikali itaendelea kupitia kodi, tozo na ada mbalimbali ili kuzipunguza au kuziondoa zile ambazo zinalalamikiwa na wananchi na wawekezaji wa ndani na nje. Miongoni mwa jitihada zitakazochukuliwa na Serikali ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi ni pamoja na kuboresha huduma za upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi, kuimarisha soko la mitaji, kukuza utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi - PPP, na kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa kuboresha miundombinu ya umeme, usafirishaji, maji, usambazaji wa gesi asilia, mfumo wa kodi,  kuweka vivutio mbalimbali, kuondoa urasimu usio wa lazima na kupambana na rushwa.





Uwezeshaji kiuchumi wa Makundi Maalum

(i)   Maendeleo Vijijini

59.       Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kuwezesha wananchi kiuchumi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 ambapo shilingi milioni 50 ziliahidiwa kwa kila kijiji ili kuwawezesha wananchi kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji kupitia Ushirika wa Kuweka na Kukopa (SACCOS) na vikundi vingine vya kiuchumi. Katika kutekeleza ahadi hii, Serikali imetenga shilingi bilioni 59 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu kwa awamu. Mpango huu utaanza kutekelezwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu mara baada ya kukamilisha utaratibu wa matumizi ya fedha hizo ili kuhakikisha kuwa fedha hizi zinatumika ipasavyo.

(ii)  Vijana, Wazee, Wenye Ulemavu, Wanawake na Watoto

60.       Mheshimiwa Spika, Bajeti ya 2016/17 imezingatia mahitaji ya makundi maalum ya vijana, wazee, wenye ulemavu, wanawake na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. Katika mwaka 2016/17 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya makazi ya wazee na mahabusu za watoto; na chakula, dawa na mahitaji mengine ya watoto walio katika mazingira hatarishi. Katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali imetenga asilimia 5.0 ya mapato ya ndani ya kila Halmashauri kwa ajili ya vijana. Aidha, shilingi bilioni 1.0 zimetengwa chini ya Fungu 65 (Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, kifungu cha 2032 mradi namba 4945) kwa ajili ya kuendeleza vijana. Vilevile, shilingi bilioni 5.0 zimetengwa Fungu 65, kifungu cha 2002 mradi namba 6581 kwa ajili ya kuendeleza ujuzi kwa vijana ambao hawana ajira na walio kwenye soko la ajira.

61.       Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya 2016/17, Serikali imetenga asilimia 5.0 ya mapato ya ndani ya kila Halmashauri kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya maendeleo ya wanawake katika Halmashauri husika. Vilevile, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.95 kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi chini ya Fungu 53 (Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kifungu cha 3001 mradi namba 4950). Kuhusu watu wenye ulemavu, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa vifaa vilivyotengenezwa mahsusi kwa ajili yao vinasamehewa kodi ili viweze kupatikana kwa bei nafuu. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha shule maalum za watoto wenye ulemavu na kugharamia mahitaji yao ili kuwajengea mazingira mazuri zaidi ya kujifunzia.

(iii)  Wasanii, Wabunifu na Wanamichezo

62.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Serikali kupitia Fungu 96 imetenga jumla ya shilingi bilioni 3.0 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya sanaa, ubunifu, utamaduni na michezo ikiwa ni pamoja na: kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Ubunifu; kusimamia urasimishaji wa shughuli za   Sanaa; kusimamia na kudhibiti filamu zitakazoingia sokoni bila kufuata taratibu; na kuratibu uendeshaji wa kazi za sanaa nchini.

(iv)Wachimbaji Wadogo wa Madini

63.       Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwezesha wachimbaji wadogo wa madini ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zao na hivyo kuongeza ajira, kukuza kipato cha wachimbaji na wananchi wanaozunguka maeneo ya uchimbaji madini. Katika mwaka 2016/17 Serikali inakusudia kutekeleza yafuatayo: kuwapatia ruzuku; kuwapatia mafunzo; kuwatengea maeneo maalum ya uchimbaji; kuimarisha soko; pamoja na kuziwezesha taasisi zinazohusika na ukaguzi wa usalama wa migodi ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika. Kiasi cha fedha kilichotengwa kwa madhumuni haya katika bajeti ya 2016/17 ni shilingi milioni 900 kwa ajili ya ruzuku ya wachimbaji wadogo.

(v)  Wafanyakazi

64.       Mheshimiwa Spika, ili kuboresha kipato cha wafanyakazi, siku ya Mei Mosi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliagiza kiwango cha kodi ya mapato kwenye mishahara (PAYE) kipunguzwe kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9 ili kupunguza makali ya maisha kwa wafanyakazi. Agizo hilo litaanza kutekelezwa Julai Mosi 2016. Aidha, kuanzia mwaka ujao wa fedha Serikali itaanza kuwasilisha mchango wa mwajiri wa asilimia 0.5 ya mshahara kwenye Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi ili watumishi wa umma wapatapo ajali mahali pa kazi waweze kulipwa na Mfuko. Kadhalika, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kuwezesha watumishi wake kujenga ama kununua nyumba kupitia Bodi ya Mfuko wa Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa Serikali, pamoja na Watumishi Housing Company.
(vi)Vyombo vya Ulinzi na Usalama

65.       Mheshimiwa Spika, Serikali inavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kujipambanua kwa nidhamu ya hali ya juu katika kazi zao. Hata hivyo, Serikali inawaelekeza Maafisa Masuuli wa Mafungu husika kujipambanua vivyo hivyo kwa nidhamu kama hiyo katika matumizi ya fedha na mali za umma. Aidha, katika mwaka 2016/17, utaratibu wa kutoa misamaha ya kodi kwenye maduka ya vyombo vya ulinzi na usalama utasitishwa na nitaeleza utaratibu mpya baadaye. Kadhalika, Serikali itaendelea kujenga nyumba za makazi kwa askari ili kukabiliana na uhaba wa makazi kwa askari nchini.

   IV.      MABORESHO YAMFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO
66.       Mheshimiwa Spika, napenda kuwasilisha sasa mapendekezo ya hatua mpya za kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi, ikiwemo kurekebisha baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada chini ya Sheria mbalimbali na kuboresha taratibu za ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali. Aidha, marekebisho haya yanalenga pamoja na mambo mengine, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya viwanda, kilimo, usafirishaji na kukuza ajira. Marekebisho hayo yanahusu Sheria zifuatazo:-

a.       Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b.      Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
c.       Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
d.      Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82;
e.       Sheria ya Magari (Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Umiliki), SURA 124;
f.        Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, SURA 399 (sambamba na Sheria ya kodi ya Majengo ya Mamlaka ya Miji, SURA 289; Sheria ya Fedha za Umma ya Serikali za Mitaa, SURA 290; Sheria ya Utawala wa Kodi ya mwaka 2015; na Sheria ya Rufani za Kodi, SURA 408);
g.       Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na Majukumu), SURA 370;
h.      Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004;
i.        Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali; na
j.        Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea;

a)   Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148

67.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kama ifuatavyo: -

(i)           Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye maharage ya soya baada ya kubaini kuwa, mazao haya yalisahaulika kuingizwa kwenye orodha chini ya kifungu cha 3 cha jedwali la misamaha linalojumuisha mifugo, mazao ya kilimo ambayo hayajasindikwa na chakula cha binadamu;
(ii)          Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mbogamboga zote na mazao ya mifugo yakiwa hayajasindikwa kama yanavyoonekana  kwenye Ushuru wa Pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sura ya 2 na 3 (mazao ya mifugo yasiyosindikwa), sura ya 7 (matunda na karanga), sura ya 8 (nafaka), sura ya 10 (unga wa nafaka) na sura ya 11 (mbegu za mazao). Hatua hii inakusudia kutoa msamaha wa kodi ya VAT kwenye mazao ya chakula ambayo hayajasindikwa ili kuwezesha upatikanaji wa lishe bora ya msingi kwa gharama nafuu;
(iii)        Kuongeza vitamini na virutubishi kwenye orodha ya vifaa na madawa muhimu yaliyoidhinishwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya kupata msamaha wa kodi. Vitamini na virutubishi hivyo huongezwa kwenye vyakula ili kuboresha lishe kama njia mojawapo ya kuimarisha afya ya jamii;
(iv)        Kuongeza madawa ya kutibu maji yanayotumiwa na binadamu kwenye orodha ya vifaa na madawa muhimu yaliyoidhinishwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya kupata msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani. Madawa haya ni muhimu kwa ajili ya kulinda afya ya msingi kwa kutumia maji salama. Waziri wa Maji na Umwagiliaji atatakiwa kuwasilisha orodha ya madawa hayo kwa Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili ayajumuishe kwenye orodha hiyo;
(v)          Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za utalii hususan kuongoza watalii, kuendesha watalii, utalii wa majini, kuangalia wanyama na ndege wa porini, kutembelea hifadhi na usafirishaji wa watalii ardhini. Hatua hii inachukuliwa kama ilivyokusudiwa wakati wa kutunga Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, ambayo ilianza kutumika rasmi Julai 2015, lakini kwa kutambua mikataba iliyokuwepo wakati huo kati ya watoa huduma za utalii na watalii waliokuwa wanatarajia kuja nchini, ilikubalika kusubiri kukamilika kwa makubaliano hayo kwa mwaka unaomalizika. Huduma hizi pia hutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye nchi nyingine kama vile Kenya, Rwanda na Afrika ya Kusini;
(vi)        Bidhaa zinazotengezwa Tanzania Bara na kuuzwa Zanzibar zitatozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani upande wa Zanzibar, na bidhaa zinazotengezwa Zanzibar na kuuzwa Tanzania Bara zitatozwa kodi hiyo upande wa Tanzania Bara. Lengo la hatua hii ni kuondoa utaratibu uliokuwepo hapo awali wa kufanya marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenda Zanzibar kwa kuwa Sheria ya Kodi hiyo inayotumika sasa haina kifungu kinachoruhusu marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenda Zanzibar kama ilivyokuwa kwenye sheria iliyofutwa. Kwa kuwa kila upande wa Muungano una Sheria yake ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, kodi hii itatozwa sehemu ambako bidhaa au huduma itatumika, yaani “destination principle”. Kwa msingi huo muhimu katika utozaji Kodi ya Ongezeko la Thamani, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itakuwa inakusanya kodi hii kwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara na kupelekwa Zanzibar. Vile vile, Tanzania Bara itakuwa inakusanya kodi hii kwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar na kuletwa Tanzania Bara;
(vii)       Kufanya marekebisho katika orodha ya misamaha ya bidhaa za petroli chini ya kifungu cha 15 cha Jedwali la misamaha la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014 ili kujumuisha pia bidhaa za lami zenye HS Code 27.13, 27.14 na 27.15 ambazo hazikujumuishwa katika Jedwali hilo;
(viii)     Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bima ya vyombo vya usafiri wa anga vinavyotambulika katika HS Code 88.01 na Hs Code 88.02. Hatua hii inapendekezwa kwa kuzingatia kuwa sekta ya usafirishaji wa anga bado ni changa kuweza kuhimili ulipaji wa bima kwa vyombo hivyo vya usafiri. Hivyo kuna umuhimu wa kuhamasisha ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga na hatimaye kukuza utalii. Aidha, hatua hii itasaidia wawekezaji katika sekta ya usafiri wa anga kutumia bima za hapa nchini badala ya nje kwenye mikataba ya ukodishaji; na
(ix)        Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye ada za huduma za kibenki zinazotozwa na benki hizo ili kupanua wigo wa kodi isipokuwa riba kwenye mikopo.

Hatua hizi za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 136,140.3.

68.       Mheshimiwa Spika, sambamba na marekebisho hayo kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani, Serikali itachukua hatua mbalimbali za kiutawala ndani ya Mamlaka ya Mapato ili kuboresha makusanyo ya Kodi hii, ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu kabambe ya ufuatiliaji wa makusanyo na hivyo kupanua wigo wa kodi. Ili kutekeleza azma hii, Serikali itatekeleza yafuatayo:

(i)      kuhakikisha kuwa daftari la usajili wa walipakodi linahuishwa kila wakati ili kuwa na taarifa sahihi za walipa kodi hao;
(ii)    kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wakubwa na wa kati hapa nchini wanapatiwa mashine za kielektroniki na zinatumika kikamilifu;
(iii)   kuendelea kuimarisha ukaguzi wa hesabu za walipakodi ili kuwezesha kodi stahiki kulipwa kwa wakati; na
(iv)   Kuanzisha ofisi mpya za kusimamia mapato kwa ngazi za wilaya katika mikoa ya kikodi kwenye Jiji la Dar es Salaam na vituo vipya vya huduma kwa walipakodi katika maeneo mbalimbali ya majiji na miji mikubwa.

69.       Mheshimiwa Spika, Napendekeza pia kufanya mapitio ya Sheria ya Uwekezaji ili iendane na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.

Hatua za kiutawala kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 268,607.1.

b)   Sheria ya Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty), SURA 147

70.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 kama ifuatavyo: -

(i)         Kufanya marekebisho ya viwango maalum vya kodi (specific duty rates) vya bidhaa zisizo za petrol kwa kiwango cha mfumuko wa bei wa asilimia 5. Marekebisho haya ni kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa inayotaka yafanyike marekebisho ya viwango hivyo vya ushuru kulingana na mfumuko wa bei ili kuendana na thamani halisi ya fedha. Hata hivyo, marekebisho haya hayatafanyika kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa. Mabadiliko ninayopendekeza ni kama ifuatavyo:

a)   Ushuru wa vinywaji baridi, kutoka shilingi 55 kwa lita hadi shilingi 58 kwa lita;

b)   Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini kutoka shilingi 10 kwa lita hadi shilingi 11 kwa lita;
c)    Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini kutoka shilingi 200 kwa lita hadi shilingi 210 kwa lita;
d)   Ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa (unmalted), mfano kibuku, kutoka shilingi 409 kwa lita hadi shilingi 430 Kwa lita; 
e)    Ushuru wa bia nyingine kutoka shilingi 694 kwa lita hadi shilingi 729 kwa lita;
f)     Ushuru wa bia zisizo na kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu kutoka shilingi 508 kwa lita hadi shilingi 534 kwa lita; 
g)    Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka shilingi 192 kwa lita hadi shilingi 202 kwa lita; 
h)   Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka shilingi 2,130 kwa lita hadi shilingi 2,237 kwa lita; 
i)     Ushuru wa vinywaji vikali kutoka shilingi 3,157 kwa lita hadi shilingi 3,315 kwa lita;
j)     Ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa viwandani hautaongezeka;
k)   Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 11,289 hadi shilingi 11,854 kwa kila sigara elfu moja;
l)     Sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 26,689 hadi shilingi 28,024 kwa kila sigara elfu moja; 
m) Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (k) na (l) hapo juu kutoka shilingi 48,285 hadi shilingi 50,700 kwa kila sigara elfu moja;
n)   Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) kutoka shilingi 24,388 hadi shilingi 25,608 kwa kilo;
o)   Ushuru wa “cigar” unabaki kuwa asilimia 30;
p)   Ushuru wa mafuta ya kulainishia mitambo kutoka shilingi 665.50 kwa lita hadi  shilingi 699 kwa lita;
q)   Ushuru wa grisi za kulainishia mitambo kutoka senti 75 kwa kilo hadi senti 79 kwa kilo;  na
r)    Ushuru wa gesi asilia kutoka senti 43 kwa futi za ujazo hadi senti 45 kwa futi za ujazo. 

(ii)          Kuongeza ushuru wa bidhaa (excise duty) unaotozwa kwenye samani zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zinazotambulika katika HS Code 94.01 na HS Code 94.03 kutoka asilimia 15 hadi asilimia 20 kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya samani zinazotengenezwa kwa kutumia mbao zinazozalishwa hapa nchini, kuongeza ajira na kuongeza mapato ya Serikali;
(iii)        Kutokana na ugumu uliojitokeza katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki, Serikali imeamua kupiga marufuku utengenezaji, uuzaji, ununuzi na matumizi ya mifuko ya plastiki yenye kipimo cha unene chini ya microns 50; na
(iv)        Kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma wa simu katika kutuma na kupokea fedha badala ya ushuru huo kutozwa tu kwenye kutuma fedha pekee. Katika utaratibu wa sasa, baadhi ya kampuni zinazotoa huduma zimetumia mwanya kwa kuhamishia sehemu kubwa ya ada hizo kwenye kupokea fedha na hivyo kuwa nje ya wigo wa kodi.
Hatua hizi za ushuru wa bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 63,639.4.

c)  Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;

71.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -
(i)         Kuondoa msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya kiinua mgongo kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano ili kujenga misingi ya usawa na haki katika utozaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa kodi;
(ii)       Kutoza Kodi ya Mapato kwenye mapato yote yatokanayo na hisa kwenye makampuni. Marekebisho hayo yatafanyika kwa kufuta aya ya (d) katika kifungu cha 3 cha Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 cha tafsiri ya maneno “Investment Asset” (rasilimali za uwekezaji) iliyokuwa inatoa msamaha wa kodi kwa wenye hisa chini ya asilimia 25 kwenye makampuni. Hatua hii itaongeza wigo wa kodi kwa ujumla wake na kupunguza misamaha ya kodi;
(iii)     Kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato yanayotokana na ajira kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9. Hatua hii inachukuliwa ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya muda mrefu ya kuwapunguzia mzigo wa kodi wafanyakazi hatua kwa hatua hadi kufikia kiwango cha tarakimu moja. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imekuwa ikipunguza kiwango cha kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 18.5 mwaka 2006/07 hadi kufikia asilimia 9 inayopendekezwa sasa. Kutokana na mabadiliko hayo, viwango vya kodi vya sasa na vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo:



Viwango vya sasa
Ngazi
Mapato kwa Mwezi
Kodi kwa mwezi
1.    
Mapato ya jumla yasiyozidi Shilingi 170,000/=
Asilimia sifuri (0%)
2.    
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 170,000/=lakini hayazidi shilingi 360,000/=
11% ya kiasi kinachozidi Shilingi 170,000/=
3.    
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 360,000/= lakini hayazidi shilingi 540,000/=
Shilingi 20,900/= + 20% ya kiasi kinachozidi Shilingi 360,000/=
4.    
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 540,000/= lakini hayazidi shilingi 720,000/=
Shilingi 56,900/= + 25% ya kiasi kinachozidi Shilingi 540,000/=
5.    
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 720,000/=
Shilingi 101,900/= + 30% ya kiasi kinachozidi Shilingi 720,000/=


Viwango vinavyopendekezwa
Ngazi
Mapato kwa Mwezi
Kodi kwa mwezi
1
Mapato ya jumla yasiyozidi Shilingi 170,000/=
Asilimia sifuri (0%)
2
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 170,000/=lakini hayazidi shilingi 360,000/=
9% ya kiasi kinachozidi shilingi 170,000/=
3
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 360,000/= lakini hayazidi shilingi 540,000/=
Shilingi 17,100+ 20% ya kiasi kinachozidi shilingi 360,000/=
4
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 540,000/= lakini hayazidi shilingi 720,000/=
Shilingi 53,100+ 25% ya kiasi kinachozidi shilingi 540,000/=
5
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 720,000/=

Shilingi 98,100+ 30% ya kiasi kinachozidi shilingi 720,000/=

(iv)        Kutoza kodi ya zuio kwenye malipo yanayofanywa kwenye mifuko ya jamii yanayotokana na mapato ya uwekezaji ili kuweka misingi ya usawa na haki katika utozaji kodi. Hatua hii inalenga kuweka wajibu kwa makampuni wa kutoza kodi ya zuio kwenye malipo yanayofanywa kwenye mifuko ya jamii kutokana na upangishaji, ukopeshaji, n.k; na
(v)          Kumpa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mamlaka ya kukadiria mapato yanayotokana na pango kwa kuweka kiwango cha ukomo wa chini wa thamani kulingana na hali halisi ya soko ili kutoza kodi kwenye mapato hayo (rental income).

Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni  71,586.9.

72.       Mheshimiwa Spika, sambamba na marekebisho hayo kwenye Kodi ya Mapato, hatua mbalimbali za kiutawala ndani ya Mamlaka ya Mapato zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu kabambe ya ufuatiliaji wa makusanyo na kuanzisha ofisi mpya za kusimamia mapato katika maeneo mbalimbali kwenye ngazi za wilaya na vituo vya miji. Hatua hii itajumuisha kusajili walipakodi wapya, na kuhakikisha kunakuwa na ufuatiliaji wa walipakodi waliopo ili walipe kodi stahiki.

Hatua hizi za kiutawala kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 80,108.18.

d)      Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82

73.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kupunguza Tozo ya kuendeleza ufundi stadi (Skills Development Levy) kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 5 hadi asilimia 4.5 ili kuwapatia nafuu ya mzigo wa tozo waajiri na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari pasipo shuruti na hivyo kuongeza mapato ya serikali katika muda wa kati. Hatua hii itapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 28,403.4


e)      Sheria ya Magari (Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Umiliki), SURA 124

74.     Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Magari (Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Umiliki), SURA 124 kama ifuatavyo: -

(i)           Kufanya marekebisho ya viwango vya usajili wa magari na pikipiki kutoka shilingi 150,000 hadi shilingi 250,000 kwa kila gari; na kutoka shilingi 45,000 hadi shilingi 95,000 kwa kila pikipiki; na
(ii)          Kupandisha ada ya usajili wa namba binafsi za magari kutoka shilingi 5,000,000 hadi shilingi 10,000,000 kwa kila baada ya miaka mitatu ili kuhuisha viwango hivyo kulingana na thamani halisi ya fedha.

Hatua hizi kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 26,915.9.

f)          Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, SURA 399; Sheria ya kodi ya Majengo ya Mamlaka ya Miji, SURA 289; Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, SURA 290; Sheria ya Utawala wa Kodi ya mwaka 2015; na Sheria ya Rufani za Kodi, SURA 408

75.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, SURA 399, Sheria ya Kodi ya Majengo ya Mamlaka ya Miji, Sura 289, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290, Sheria ya Utawala wa Kodi ya mwaka 2015 na Sheria ya Rufani za Kodi, Sura 408 ili kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kukusanya kodi ya Majengo ambapo hivi sasa kodi hiyo inakusanywa na Halmashauri. Lengo la marekebisho  haya, pamoja na mambo mengine, ni kama ifuatavyo;
(i)                 Kuiwezesha Mamlaka ya Mapato kukadiria Kodi ya Majengo na kufanya uthamini wa majengo husika;
(ii)          Mamlaka ya Mapato Tanzania kupewa uwezo wa kukusanya Kodi ya Majengo kwa kutumia utaratibu wake wa kawaida kupitia sheria za kodi;
(iii)        Kuweka utaratibu wa namna ya kuhifadhi na kuwasilisha Kodi ya Majengo itakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwenye Halmashauri husika;
(iv)        Kuwezesha taratibu za kutatua migogoro itakayotokana na  ukusanyaji wa Kodi ya Majengo kusimamiwa na Sheria zinazotumika hivi sasa na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kusimamia migogoro ya kodi; na
(v)          Kufanya maboresho katika misamaha ya Kodi ya Majengo ili majengo mengi zaidi yaingizwe katika mfumo wa utozwaji kodi hiyo.

g)      Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na Majukumu), SURA 370

76.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na Majukumu) SURA 370, ili kuzitaka wakala na taasisi zote za usimamizi na udhibiti zilizo chini ya Msajili wa Hazina kuchangia asilimia 15 ya mapato yake ghafi katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Taasisi hizo zitatangazwa kwenye Gazeti la Serikali. Aidha, napendekeza kuiondoa katika orodha hiyo taasisi ya AICC na kuwekwa katika orodha ya taasisi zinazotakiwa kutoa gawio (dividend) kwa Serikali kwa kuwa ni taasisi inayofanya biashara.

h)      Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004

77.       Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya kikao cha maandalizi ya Bajeti (Pre-Budget Consultations of EAC Ministers for Finance) jijini Arusha, Tanzania, kuanzia tarehe 2 hadi 5 Mei, 2016. Katika kikao hicho, walikubaliana kwa pamoja kufanya marekebisho ya viwango vya ushuru wa pamoja wa forodha (EAC Common External Tariff “CET”) na kurekebisha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC-Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa fedha 2016/17 kama ifuatavyo: -

78.     Mheshimiwa Spika, marekebisho ya viwango vya ushuru wa pamoja wa forodha (EAC Common External Tariff “CET”) yaliyokubaliwa yalizingatia kwa sehemu kubwa katika kuendeleza uchumi wa viwanda kwenye ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama ifuatavyo:-

(i)           Tanzania kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye bidhaa ya saruji inayotambuliwa katika HS Code 2523.29.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha na kulinda uzalishaji wa saruji hapa nchini ambao umekuwa ukiongezeka dhidi ya ushindani wa bei ya saruji inayoingizwa nchini kutoka nje;
(ii)          Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 0 hadi asilimia 10 kwenye bidhaa za chuma (flat rolled products of iron or non-alloy steel) zinazotambuliwa kwenye HS Codes: (HS Code 7208.54.00; HS Code 7208.90.00; HS Code 7208.52.00; and, HS Code 7208.53.00). Hatua hii inalenga katika kulinda uzalishaji wa bidhaa hizi hapa nchini. Utafiti uliofanywa na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaonesha kuwa uzalishaji wa bidhaa za chuma umekuwa ukiongezeka na uwezo upo wa kukidhi mahitaji. Hata hivyo kuna ushindani usio wa haki kutoka kwenye bidhaa za vyuma zinazotoka nje ambazo ni za bei ya chini na zisizo na kiwango bora;
(iii)        Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwenye bidhaa za nondo (bars and rods of iron and steel) kwa bidhaa zinazotambulika chini ya HS Codes: (HS Code 7213.10.00; HS Code 7213.20.00; HS Code 7213.99.00; HS Code 7227.10.00; HS Code 7227.20.00; HS Code 7227.90.00; HS Code 7308.20.00; HS Code 7308.40.00; na HS Code 9406.00.90). Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora na za bei ya chini kutoka nje ya nchi;
(iv)        Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye bidhaa za chuma “iron and steel products” zinazotambulika chini ya HS Code 7308.10.00 ambazo ni muhimu katika ujenzi wa madaraja (bridge and bridge sections);
(v)          Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 kwa mwaka mmoja badala ya asilimia 25 kwenye “automotive bolts and nuts” zinazotambulika kwenye HS Code 7318.15.00. Aidha, ushuru huu unapunguzwa kwa kuzingatia kwamba malighafi zinazotumika kutengeneza bidhaa hizi hazizalishwi katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(vi)        Kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa utaratibu wa duty remission kwa wazalishaji wa “bolts and nuts” kwenye malighafi zinazotambulika chini ya HS Code 7228.30.00 na HS Code 7228.50.00 kwa kutoza kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10. Lengo la hatua hii ni kuwawezesha wazalishaji kupata malighafi hizo kwa gharama nafuu kwa kuwa hazizalishwi katika ukanda wa Afrika Mashariki;
(vii)       Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya kiwango cha sasa cha asilimia 10 kwenye nyavu za samaki zinazotambulika chini ya HS Code 5608.11.00. Hatua hii inazingatia kuwa kuna watengenezaji wengi wa nyavu za aina hii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(viii)     Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya kiwango cha sasa cha asilimia 10 kwenye bidhaa za “Oil and Petrol Filters”  zinazotambulika kwenye HS Code 8421.23.00, na “intake air filters” zinazotambulika kwenye HS Code 8421.31.00. Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa hizi zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora na za bei rahisi kutoka nje ya nchi;
(ix)        Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha na kutoza asilimia 0 kwa utaratibu wa duty remission kwenye malighafi za kutengenezea “air filters” za magari kwa wazalishaji wa hapa nchini;
(x)          Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha na kutoza asilimia 0 kwa utaratibu wa duty remission kwenye malighafi (splints) za kutengenezea vibiriti zinazotambulika chini ya HS Code 4421.90.00. Hatua hii imezingatia kwamba hakuna misitu ya kutosha na yenye mbao za kukomaa zinazokidhi mahitaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xi)        Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupunguza msamaha wa Ushuru wa Forodha hatua kwa hatua kwenye Sukari (sugar and sugar confectionery) kutoka kiwango cha sasa ambapo waagizaji wa sukari ya viwandani hulipa asilimia 10. Kutokana na kupunguza msamaha huo, waagizaji watalipa ushuru zaidi hatua kwa hatua. Upunguzaji wa msamaha utakuwa kama ifuatavyo: Mwaka 2016/17 kiwango kitakuwa asilimia 15, 2017/18 kiwango kitakuwa cha asilimia 20, 2018/19 kiwango kitakuwa cha asilimia 25. Hatua hii inachukuliwa kwa kuwa kiwango cha sasa cha asilimia 10 kinadidimiza viwanda vyetu vya ndani na pia ni chachu ya matumizi mabaya ya misamaha husika;
(xii)      Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 za sasa kwa bidhaa zinazotambulika chini ya HS Code 7612 “Aluminium Milk Cans”. Hizi ni bidhaa zilizokamilika tayari kwa kutumika hivyo zinatakiwa kutozwa ushuru wa asilimia 25 unaostahili kwa bidhaa za namna hiyo. Lengo la hatua hii ni kulinda wazalishaji wa ndani wenye uwezo wa kuzalisha bidhaa hizi kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xiii)     Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha na kutoza asilimia 0 malighafi zinazoagizwa na wazalishaji wa Aluminium cans zinazotambulika chini ya HS Codes 7606.12.00 na HS Codes 7606.92.00. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha uzalishaji wa “aluminium cans” katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xiv)     Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwenye ngano (Wheat grain) inayotambuliwa chini ya HS Code 1001.99.10 na HS Code 1001.99.90 kwa mwaka mmoja. Hatua hii imezingatia kwamba nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hazina uwezo wa kuzalisha ngano ya aina hii na kuweza kutosheleza mahitaji. Aidha, itatoa unafuu kwa wazalishaji wa bidhaa na vyakula vinavyotumia ngano na kuimarisha utulivu wa bei ya bidhaa za ngano;
(xv)       Kuongeza kiwango maalumu cha ushuru kwenye mitumba ya nguo na viatu kutoka kiwango cha sasa cha dola za kimarekani 0.2 kwa kilo hadi dola 0.4 kwa kilo. Hatua hii imechukuliwa ili kudhibiti hatua kwa hatua uingizaji nchini wa nguo za mitumba ambazo zimeonekana kuwa siyo salama kwa afya za watu wetu. Aidha, Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kuzuia kabisa uingizaji wa bidhaa hizi baada ya miaka mitatu kuanzia sasa. Hata hivyo Nchi hizi zimekubaliana kuweka mikakati ya kuimarisha na kuhamasisha uzalishaji wa nguo na viatu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kukidhi mahitaji. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji tayari imeandaa mikakati madhubuti ya kuendeleza sekta za ngozi na nguo;
(xvi)     Kuendelea kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma (iron and iron-alloy steel) kwa mwaka mmoja, zinazotambuliwa katika HS Codes:  HS Codes 7210.41.00; HS Codes 7210.49.00; HS Codes 7210.61.00; HS Codes 7210.69.00; HS Codes 7210.70.00; HS Codes 7210.90.00; HS Codes 7212.30.00; and HS Codes 7212.40.00. Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje ya nchi. Utafiti uliofanywa na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki umeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji wa bidhaa za vyuma kupita mahitaji ya soko katika soko la dunia. Hali hiyo imesababisha kushuka sana kwa bei na hivyo kuathiri viwanda vyetu kutokana na ushindani wa bidhaa hizo kutoka nje. Hatua hii ya kuweka viwango maalum vya kodi ni muhimu kulinda viwanda na bidhaa zetu (anti-dumping measure);
(xvii)   Kuendelea kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa mwaka mmoja kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma (Flat-rolled products of bars, rods, sections, angles, shapes, and related products) zinazotambuliwa katika HS Codes: HS Codes 7214.10.00; HS Codes 7214.20.00; HS Codes 7214.30.00; HS Codes 7214.91.00; and HS Codes 7214.99.00. Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje ya nchi;
(xviii)  Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa   mwaka   mmoja   kwa   kila tani moja ya ujazo “metric ton’ kwenye bidhaa za chuma (steel  reinforcement  bars,  angles, sections zinazotambuliwa  chini ya HS Codes: 7216.10.00; HS Codes 7216.21.00; HS Codes 7216.22.00; and HS Codes 7216.50.00.). Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje ya nchi;
(xix)     Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye mafuta ghafi ya kula (crude edible oil) yanayotambulika katika HS Code 1511.10.00 kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha kilimo cha mbegu za mafuta hapa nchini na kukuza viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula. Aidha, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeandaa mkakati maalum wa kuendeleza viwanda vya kuzalisha mafuta yanayotokana na mbegu zinazozalishwa hapa nchini na kutumia fursa soko kubwa lililopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania inayo nafasi ya kuweza kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta;
(xx)      Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwa bidhaa za karatasi zinazotambulika kwenye HS Codes: HS Codes 4804.11.00; HS Codes 4804.19.10; HS Codes 4804.19.90; HS Codes 4804.21.00; HS Codes 4804.29.00; HS Codes 4804.31.00; HS Codes 4804.39.00; HS Codes 4804.41.00; HS Codes 4805.59.00; HS Codes 4805.11.00; HS Codes 4805.12.00; HS Codes 4805.19.00; HS Codes 4805.24.00; HS Codes 4805.25.00; HS Codes 4805.30.00; HS Codes 4805.91.00, na HS Codes 4805.92.00. Hatua hii inachukuliwa ili kulinda viwanda vya hapa nchini vinavyozalisha karatasi za aina hiyo na ajira;
(xxi)     Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za kimarekani 200 – kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa mwaka mmoja kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za nondo zinazotambulika kwenye HS Codes HS Codes 7228.10.00; HS Codes 7228.20.00; HS Codes 7228.30.00; HS Codes 7228.40.00; HS Codes 7228.50.00; HS Codes 7228.60.00; HS Codes 7228.70.00; na HS Codes 7228.80.00. Lengo ni kulinda viwanda vya ndani kutokana na ushindani wa bidhaa kama hizo zinazoagizwa nje; na
(xxii)   Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za kimarekani 200 - kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa mwaka mmoja kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma zinazotambulika kwenye HS Codes 7212.40.00; HS Codes 7215.10.00; HS Codes 7215.50.00; HS Codes 7215.90.00; HS Codes 7216.61.00; HS Codes 7216.69.00; HS Codes 7216.91.00; na HS Codes 7216.99.00.
79.       Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC-Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo: -
(i)           Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki linalotoa msamaha wa ushuru wa forodha ili kuongeza vifaa vya majokofu yanayotumika katika kuhifadhi maiti yanayotambuliwa chini ya HS Code 8418.69.90 kwa matumizi ya hospitali na mamlaka za miji (city councils);
(ii)          Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Chapters 84 and 69) linalotoa msamaha wa ushuru wa forodha ili kuongeza vifaa vinavyotumika kwenye hospitali kuteketeza na kuchoma uchafu (incinerator’s equipments and materials used in hospitals to burn waste);
(iii)        Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuondoa msamaha wa ushuru wa forodha unaotolewa kwenye sare za wafanyakazi wa hospitali.  Msamaha huu unaondolewa kwa kuwa sare hizi zinaweza kuzalishwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(iv)        Kusamehe Ushuru wa Forodha kwa kutumia utaratibu wa “Duty remission” kwa wazalishaji wa hapa nchini wa malighafi zinazotumika kutengeneza betri zinazofahamika kama “deep cycle batteries”. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha uzalishaji wa viwanda vya ndani kwa kuwa deep cycle batteries zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zimesamehewa ushuru kupitia Jedwali la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(v)          Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano (5) la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki linalotoa msamaha wa ushuru wa forodha ili kujumuisha chupa zinazotumika kwa ajili ya kukusanya damu kwenye hospitali (blood collection tubes); na
(vi)        Kusamehe Ushuru wa Forodha kwa kutumia utaratibu wa “Duty remission” kwa malighafi zinazotumika kuzalisha vifaa vya nishati ya umeme wa jua (Solar equipments).

Hatua zote za Ushuru wa Forodha kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato kwa kiasi cha shilingi milioni 42,850.6.

i)        Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali

80.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera na ya kiuandishi katika Sheria mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika muswada wa Sheria ya Fedha 2016.

81.       Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha utekelezaji wa Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015, na kuleta uwajibikaji katika utekelezaji wa Bajeti ya Mfuko wa Mahakama na Mfuko wa Bunge napendekeza kufanya marekebisho yafuatayo:-

(i)   Kurekebisha kifungu cha 29 kifungu kidogo cha 3 cha Sheria ya Utawala wa Bunge, SURA 115 (The National Assembly Administration Act, CAP 115) ili kubainisha kuwa bajeti ya Mfuko wa Bunge itawasilishwa Bungeni na Waziri mwenye dhamana na masuala ya Bunge. Hivi sasa Sheria hii imeweka sharti kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha kuwasilisha Bungeni Bajeti ya Mfuko wa Bunge; na
(ii)  Kurekebisha kifungu cha 59 kifungu kidogo cha 3 cha Sheria ya Utawala wa Mahakama, SURA 237 (The Judiciary Administraion Act, CAP 237) ili Bajeti ya Mfuko wa Mahakama iwasilishwe Bungeni na Waziri mwenye dhamana na masuala ya mahakama. Kifungu hiki kwa sasa kimeweka sharti kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha kuwasilisha Bungeni Bajeti ya Mfuko wa Mahakama.

j)        Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea

82.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi. Aidha, napendekeza kufuta baadhi ya ada na tozo ambazo zimeonekana kuwa kero kwa wananchi na kikwazo katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini. Tozo na ada ninazopendekeza kuzifuta ni kama ifuatavyo:

           (i)      Mamlaka ya Chakula na Dawa (Tanzania Foods and Drugs Authority – TFDA):

a)         Kibali cha kusafirisha chakula nje ya nchi kwa shilingi 50,000;
b)        Kushikilia dawa za binadamu na mifugo zinazotengenezwa na viwanda vya ndani kwa shilingi 100,000;
c)         Kudurufu cheti cha dawa za binadamu na mifugo zinazotengenezwa na viwanda vya ndani kwa Dola za Kimarekani 50;
d)        Kudurufu cheti cha dawa za binadamu na mifugo zinazotengenezwa na viwanda vya nje ya nchi kwa Dola za Kimarekani 100;
e)         Tathimini ya matangazo ya bidhaa zinazotengenezwa nchini kwa Dola za Kimarekani 50;
f)          Matangazo yanayofanyiwa tathimini fupi kwa bidhaa zinazotengenezwa nchini kwa Dola za Kimarekani 25;
g)         Kudurufu cheti cha usafi wa chakula, dawa na vifaa tiba vinavyotengenezwa nje ya nchi kwa Dola za Kimarekani 100;
h)        Kudurufu cheti cha vifaa tiba vinavyotengenezwa ndani ya nchi kwa Dola za Kimarekani 30;
i)          Kudurufu cheti cha dawa zinazotengenezwa nchini kwa Dola za Kimarekani 50;
j)          Kushikilia vitendanishi vinavyotengenezwa nje ya nchi katika rejesta kwa Dola za Kimarekani 150;
k)        Kushikilia vipodozi vinavyotengenezwa ndani ya nchi katika regesta kwa shilingi 30,000;
l)          Ukaguzi wa kiwanda cha dawa cha ndani ya nchi kabla ya kusajiliwa kwa Dola za Kimarekani 250;
m)       Wawakilishi wa makampuni ya dawa ya nje ya nchi kwa Dola za Kimarekani 1,000;
n)        Malighafi za vipodozi zinazoingizwa nchini kwa shilingi 50,000,000;
o)         Malighafi za dawa zinazoingizwa nchini kwa shilingi 100,000,000;
p)        Kibali cha hospitali kununua dawa zenye madhara ya kulevya kutoka bohari kwa Dawa ya shilingi 10,000;
q)         Ada ya uingizaji nchini wa dawa zenye madhara ya kulevya ya shilingi 50,000;
r)         Cheti cha kusafirisha bidhaa nje ya nchi kwa shilingi 50,000;
s)         Cheti cha utambuzi wa dawa inayosafirishwa nje ya nchi kwa  50,000;
t)          Ukaguzi wa kiwanda kidogo kipya cha kusindika chakula kwa shilingi 100,000;
u)        Cheti cha kuteketeza bidhaa;
v)         Cheti cha Afya kwa ajili ya kusafirisha bidhaa nje ya nchi  kwa shilingi 50,000; na
w)        Kibali cha kufanya maonyesho ya biashara ya bidhaa inayodhibitiwa kwa shilingi 200,000.

         (ii)      Bodi ya Pamba:

a)   Mchango wa mwenge kwa kila kiwanda cha kuchambua pamba wa shilingi 450,000; na

b)   Ada ya vikao vya Halmashauri za wilaya wanapojadili maombi mbalimbali ya wafanyabiashara wa pamba ya shilingi 250,000.

       (iii)      Bodi ya Chai: Kodi ya moto na uokoaji.

        (iv)      Bodi ya Kahawa: Ada ya leseni ya kusindika kahawa ya Dola za Kimarekani 250.

          (v)      Bodi ya Korosho:

a)   Ushuru wa chama kikuu cha ushirika wa shilingi 20 kwa kilo;
b)   Ushuru wa kusafirisha korosho wa shilingi 50 kwa kilo;
c)    Gharama za mtunza ghala kwa shilingi 10 kwa kilo;
d)   Kikosi kazi kwa ajili ya ufatiliaji wa masuala mbalimbali kwa kuchangia shilingi 10 kwa kilo; na
e)    Makato ya unyaufu.

83.       Mheshimiwa Spika, napenda nilifahamishe Bunge lako Tukufu pamoja na wananchi kwamba, hatua ninazopendekeza za kufuta tozo na ada nilizozifanya ni za awali tu wakati Serikali inaendelea kufanya uchambuzi na tathmini ya kina kuhusu tozo na ada zinazotozwa na mashirika, taasisi na wakala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Serikali za Mitaa. Hatua hizi ni endelevu katika kuhakikisha kuwa tunaboresha mazingira ya kufanya biashara ili nchi yetu iweze kuwa na nafasi nzuri ya kiushindani katika biashara na kuvutia uwekezaji. Aidha, lengo la hatua hizi ni pamoja na kuondoa kero kwa wananchi na kuwapa unafuu katika uendeshaji wa shughuli za kiuchumi.

84.     Mheshimiwa Spika, napendekeza pia kurekebisha baadhi ya viwango vya ada na tozo mbalimbali kama zitakavyoainishwa kwenye Sheria ya Fedha 2016 na nyingine kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali (GNs) na Mawaziri wenye dhamana na ada na tozo hizo.

k)   Kodi na Tozo Kwenye Bidhaa za Mafuta ya Petroli

85.       Mheshimiwa Spika, kwa muda sasa bei ya mafuta (petroli, dizeli na ya taa) imekuwa ikishuka katika soko la dunia, hali ambayo imesaidia kuleta unafuu wa gharama katika shughuli za kiuchumi hususan kwa wananchi masikini maana bei za mafuta haya zinagusa kila mtu. Hivyo, Serikali imeamua kuwa Ushuru wa Barabara, Ushuru wa Petroli na Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya petroli utabaki kama ilivyo sasa. Hivyo, Mfuko wa barabara na Mamlaka ya Usambazaji Umeme Vijijini watumie fedha hizi vizuri.

l)     Misamaha ya Kodi kwa Majeshi ya Ulinzi na Usalama

86.       Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi (Ushuru wa Bidhaa, Kodi ya Ongezeko la Thamani na Ushuru wa Forodha) kwa majeshi ya Ulinzi na Usalama kupitia kwenye migahawa na maduka maalum ambayo yanauza bidhaa mbalimbali kwa mahitaji ya askari. Katika kufanya hivyo, kumekuwa na changamoto ya kuwepo kwa matumizi mabaya ya misamaha hiyo. Aidha, kutokana na hali hiyo ya upotevu wa mapato, Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeondokana na utaratibu huu isipokuwa Rwanda na Tanzania ambazo zinatoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.


87.     Mheshimiwa Spika, katika kikao cha Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti kwa mwaka 2015/16, Serikali ya Tanzania ilitakiwa kuangalia njia mbadala ya kutoa unafuu wa gharama kwa majeshi yake badala ya utaratibu wa kutoa misamaha. Ili kuendelea kutoa huduma kwa majeshi hayo pasipo kupoteza mapato ya Serikali, napendekeza kuwapatia posho majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama ili kuwawezesha kununua mahitaji yao wenyewe. Dhamira ya hatua hii ni kusitisha msamaha wa kodi kwa majeshi ili kuondoa uvujaji mkubwa wa mapato na wakati huo huo, kuendelea kuwapatia askari wetu mahitaji yao muhimu kwa utaratibu mzuri zaidi. Aidha, lengo la hatua hii ni kuhakikisha kuwa motisha unaotolewa unawanufaisha walengwa, yaani askari, badala ya wajanja wachache kuendelea kunufaika na misamaha hiyo.

Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi

88.     Mheshimiwa Spika, Hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2016, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.

  V.        SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2016/17

89.       Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi jumla pamoja na misingi na sera za bajeti kwa mwaka 2016/17, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 29.54 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Bajeti ya mwaka 2016/17 inatarajiwa kuwa na ongezeko la jumla ya shilingi trilioni 7.04 sawa na asilimia 31.1 ikilinganishwa na Bajeti ya mwaka 2015/16 ya shilingi trilioni 22.49.

90.       Mheshimiwa Spika, Serikali inalenga kukusanya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri ya jumla ya shilingi trilioni 18.46 sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, mapato ya kodi ni shilingi trilioni 15.11 sawa na asilimia 13.8 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni shilingi trilioni 2.69 na shilingi bilioni 665.4 kwa mtiririko huo. Makisio ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yameongezeka kwa kuwa kuna viashiria vingi vinavyoonesha kwamba TRA kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi zinazokusanya maduhuli wana uwezo wa kukusanya kiasi hiki cha mapato. Hivyo, Serikali itasimamia kwa karibu na kuziba mianya yote ya uvujaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuhakikisha kuwa malengo ya ukusanyaji yanafikiwa.

91.     Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kutupatia misaada na mikopo ya jumla ya shilingi trilioni 3.60 ambayo ni asilimia 12 ya bajeti yote. Kati ya kiasi hicho,  shilingi trilioni 2.75 ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo; shilingi bilioni 372.1 ni misaada na mikopo kwa mifuko ya pamoja ya kisekta; na shilingi bilioni 483 ni misaada na mikopo ya kibajeti (GBS).

92.     Mheshimiwa Spika, ili kuziba nakisi ya bajeti, katika mwaka 2016/17 Serikali inatarajia kukopa jumla ya shilingi trilioni 7.48 kutoka katika vyanzo vya ndani na nje. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 5.37 zinategemewa kukopwa katika soko la ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva pamoja na mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kulipia malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa. Aidha, ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu na kuhakikisha inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo kikamilifu, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 2.10 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.
93.     Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya jitihada kubwa za kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kugharamia, pamoja na mambo mengine, miradi ya maendeleo. Utekelezaji wa miradi hiyo pia hutegemea mikopo ya nje ya kibiashara ambayo upatikanaji wake hutegemea hali ya soko la fedha duniani. Katika mwaka 2016/17, kuna miradi mikubwa hususan ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge na uimarishaji wa bandari ambayo matayarisho yake yanahitaji muda na umakini mkubwa hasa uhakika wa upatikanaji wa fedha. Hivyo, utekelezaji wa miradi hii unatarajiwa kuanza katika nusu ya pili ya mwaka wa fedha 2016/17 baada ya kutathmini hali ya upatikanaji wa fedha zaidi na kukamilisha maandalizi ya msingi ikiwa ni pamoja na kumpata mkandarasi na kuingia mkataba. Matarajio ya Serikali ni kuwa mkandarasi atakabidhiwa eneo (site) ndani ya miezi tisa (9) ya kwanza ya 2016/17.

94.     Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, katika mwaka 2016/17 Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 29.54 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 17.72 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi trilioni 11.82 sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ambapo kiasi cha shilingi trilioni 8.70 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 3.12 ni fedha za nje.

95.       Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, sura ya bajeti kwa mwaka 2016/17 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali, ukurasa wa 92 wa kitabu cha hotuba hii. 














 Mfumo wa Bajeti  wa Mwaka 2016/17


VI.        HITIMISHO
96.       Mheshimiwa Spika, wananchi wetu wengi wamechoka na adha ya umaskini: Watanzania wanataka kipato cha kuweza kukidhi mahitaji yao ya msingi. Wananchi wanataka huduma bora zaidi hususan upatikanaji wa maji, elimu, afya, umeme na makazi; akina mama wamechoka kutembea na ndoo za maji kichwani; watoto wetu shuleni wamechoka kukaa chini na kugombania matundu machache ya vyoo; vijana wanataka ajira; kilio cha mauaji ya kikatili ya albino ni fedheha kwa nchi yetu; wananchi bado wananyimwa haki zao kutokana na kukithiri kwa rushwa; Watanzania wanataka nchi yenye neema; Watanzania wanataka Serikali inayofanya kazi kwa ufanisi; Watanzania wanataka mazingira safi na endelevu; Watanzania wanataka miundombinu na usafiri wa kisasa na salama; Watanzania wanataka miji na makazi yaliyopimwa na yaliyopangwa vizuri; na pia Watanzania wanapenda amani, utulivu, utangamano na furaha. Hata hivyo, napenda nisisitize kuwa Tanzania mpya ambayo wote tunaitamani iko mikononi mwetu!!


97.     Mheshimiwa Spika, katika kuhitimisha hotuba yangu napenda kuwaambia Watanzania wenzangu siri ya maendeleo. Siri ya kuifikia Tanzania mpya tunayoitamani! Kwanza, maendeleo hayaji hivi hivi! Maendeleo yanataka dhamira na utashi, juhudi na maarifa; maendeleo yanataka vitendo, siyo maneno! Maendeleo yanataka pawepo dira ya kutuongoza tunakotaka kwenda. Ili kufanikiwa, lazima kuyafahamu vizuri mazingira tulipo na njia ya kupita, hususan fursa na hatari zilizo mbele yetu. Maendeleo yanataka mwelekeo (focus), vipaumbele, malengo na viashiria vya hatua iliyofikiwa; maendeleo yanahitaji nidhamu ya hali ya juu hususan katika matumizi ya rasilimali (watu, fedha, muda, vitendea kazi na mali). Maendeleo yanataka usimamizi makini wa utekelezaji. Hivyo, maendeleo yanataka hatua kali za kumwajibisha yeyote anayekwamisha na kuhujumu juhudi zetu kwa kutotimiza wajibu, uzembe, rushwa, ubadhirifu n.k. Maendeleo yanahitaji kujinyima au kujitoa (sacrifice) na kwa maana hiyo yafaa Watanzania tujitafakari juu ya kujengeka kwa utamaduni wa kuchangishana michango mingi ya sherehe za anasa na badala yake tujielekeze kusaidiana katika masuala ya maendeleo kama ada za shule, gharama za matibabu n.k. Aidha, maendeleo yanahitaji muendelezo wa hatua stahiki badala ya kurukia mambo mapya kabla ya kukamilisha yaliyoanza kutekelezwa (consistency of action); Maendeleo yanapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii (hard work). Hivyo, maendeleo hayatakuja kwa kucheza pool table na kunywa viroba muda wote; maendeleo yanapatikana kwa kuthubutu (boldness) na kujiamini (self confidence) na hatimaye kuamua kujitegemea.

98.       Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niseme juu ya utegemezi kwa misaada kutoka kwa wahisani. Tangu Uhuru wafadhili wameendelea kutupatia misaada ambayo imetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu. Hata hivyo, pamoja na kuwa lengo la misaada ni kujazia uwezo wa taifa kutekeleza miradi ya maendeleo au kukabiliana na maafa, ni vizuri watanzania wenzangu tukaelewa kuwa kwa upande mwingine misaada inaweza kuwa sumu ya maendeleo! Misaada inaweza kuwa uchochoro wa sera na miradi mibovu, inapoteza kujiamini na masharti yanayoambatana na misaada yanapunguza uhuru wa kujiamulia mambo. Misaada pia inaweza kuchochea rushwa na kuzorotesha jitihada za ndani hususan za ukusanyaji mapato. Mwanazuoni anayeitwa Sebastian Edwards katika kitabu chake – Toxic Aid: Economic Collapse and Recovery in Tanzania (2014) amefichua ukweli huo kwa maneno yafuatayo, nanukuu:-

“After analysing in great depth Tanzania’s history during its first two decades as an independent nation, it is clear to me that the official aid community had a major responsibility in one of the most colossal collapses of a poor country in the history of the modern world.  When one adds and subtracts everything – the misguided policies, the blunders, the growing corruption, and the socially worthwhile projects- the balance is hugely negative.   The inescapable conclusion of that exercise is that during 1961-81 aid was worse than ineffective; it was toxic”!  Mwisho wa kunukuu.
Hivyo, ni muhimu sana kama taifa tutambue jambo hili na tufanye kila linalowezekana kupunguza utegemezi kwa misaada ya wahisani kwa kulinda utulivu wa uchumi, kujenga uwezo wetu wenyewe hususan kukuza sekta ya viwanda ili kupanua wigo wa kukusanya zaidi mapato ya ndani na kwa ufanisi zaidi. Ni muhimu sana tuweke msukumo zaidi wa kukuza na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje pamoja na kuimarisha biashara katika mahusiano yetu na nchi rafiki.
99.          Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho na muhimu sana ni kuwa maendeleo endelevu yanapatikana haraka katika mazingira ya amani na usalama. Hivyo ni lazima tunu ya amani katika nchi yetu ilindwe kwa nguvu zote.

100.      Mheshimiwa Spika, Rai yangu kwa watanzania: Mungu ametujalia rasilimali nyingi; Mama zetu walizaa na wanaendelea kuzaa watoto wenye akili timamu, wabunifu na wenye uwezo wa kutatua changamoto kuu na vikwazo kwa maendeleo ya Tanzania mpya. Hivyo, tukiongozwa na uzalendo, uchungu wa nchi hii na uthubutu wa Rais wetu Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli, lazima sasa tudhamirie kuigeuza Tanzania kuwa nguvu kuu ya kiuchumi katika kanda hii ya Afrika (economic power house) katika kipindi cha miaka kumi ijayo. Tukiwa na nia moja, inawezekana, na hakika Mungu yuko upande wetu.

101.      Mheshimiwa Spika, ningependa pia kuchukua nafasi hii kuwakumbusha viongozi wenzangu na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa matumizi ya muda ambao ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya Taifa letu. Watanzania wengi tunatumia muda vibaya kwa mambo yasiyokuwa na tija na hatuzingatii muda katika kutimiza majukumu yetu. Kwa upande wa watumishi wa umma, kumekuwa na mazoea ya kutumia muda mrefu kwenye vikao na mikutano na kuacha majukumu ya msingi ya kuwahudumia wananchi. Vilevile, wananchi hasa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa wamekuwa wakitumia muda mwingi wa kazi kufanya mambo yasiyokuwa na manufaa kwao binafsi na Taifa kwa ujumla, hususan; unywaji wa pombe, kucheza pool, uzururaji, kamari, sinema za mitaani, kukaa vijiweni na kupoteza muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii. Hivyo, natoa rai kwa watanzania wote kuthamini matumizi mazuri ya muda kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuchochea maendeleo yetu binafsi na Taifa kwa ujumla.

102.      Mheshimiwa Spika,  Ninapoelekea kumalizia hotuba hii, napenda kusisitiza mambo yafuatayo ambayo yanalenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa matumizi ili kuweza kutekeleza bajeti kama ilivyopangwa:

Kwanza, Serikali itaongeza msukumo katika matumizi ya mashine za EFD ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anatoa risiti za mashine za EFD na wanachi wanadai risiti pale wanapofanya manunuzi ya bidhaa au huduma. Katika kutimiza azma hii Wizara yangu itaunda Kikosi Maalum cha kufuatilia utekelezaji wa agizo hili katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ili kuhakikisha wale wote wataokiuka utaratibu huu wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria. Ninapenda kutoa rai kwa viongozi wote, hususan Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge, Madiwani na Viongozi wa Dini kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi wetu kwa kuhakikisha kuwa tunadai risiti za EFD pale tunaponunua bidhaa au huduma. Aidha, viongozi wote mnaombwa kuhamasisha wananchi kudai risiti za EFD. Kila asiyetoa risiti na asiyedai risiti ajue anatenda kosa na anasaliti jitihada zetu za kuijenga Tanzania mpya. 
Pili, vituo vyote vya kuuzia mafuta ya petroli vinaagizwa kukamilisha ufungaji wa mashine za EFD kwenye pampu za kuuzia mafuta hayo ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2016 ili kuhakisha kuwa Serikali inakusanya kodi stahiki. Serikali itafanya ukaguzi kwenye vituo vyote vya mauzo ya mafuta hapa nchini na kuchuka hatua za kisheria kwa wale watakaokaidi agizo hili.
Tatu, katika kudhibiti misamaha ya kodi inayotolewa kwa wafanyabiashara, watumishi wa umma, mashirika ya dini na taasisi zisizo za kiserikali, kuanzia mwaka ujao wa fedha watalazimika kulipa kodi kwanza kwa bidhaa watakazoagiza. Kodi hiyo itarejeshwa kwa wanufaikaji baada ya ukaguzi kufanyika na kujiridhisha kuwa bidhaa hizo zimetumika kwa malengo yaliyokusudiwa.  Aidha, Serikali itawataka wanufaika kuwasilisha maombi yao Wizara ya Fedha na Mipango kabla ya kuagiza bidhaa husika ili kupata kibali cha uagizwaji wa bidhaa hizo.
Nne, Maafisa Maasuuli wote wanaagizwa kutumia vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato unaofanywa na Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Mashirika na Taasisi za Umma ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato. Aidha, kodi na tozo hizo zitakazokusanywa zipelekwe benki ndani ya masaa 24.
Tano, kuanzia mwaka ujao wa fedha utaratibu wa kubakiza sehemu ya makusanyo, yaani mfumo wa retention umefutwa. Taasisi zote zilizokuwa zikitumia mfumo huo zitalazimika kuwasilisha mapato yote kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Utoaji wa fedha kutoka Hazina kwenda kwenye taasisi hizo utazingatia utaratibu wa kawaida kulingana na bajeti iliyoidhinishwa.
Sita, Maafisa Masuuli wanaelekezwa kuzingatia agizo la Serikali la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika maeneo yaliyoainishwa ikiwa ni pamoja na: safari za nje ya nchi, mafunzo nje ya nchi, posho za vikao, warsha na makongamano, sherehe na maadhimisho ya kitaifa, ununuzi wa samani, ununuzi na uendeshaji wa magari, n.k. ili kupata fedha zaidi na kuzielekeza kwenye miradi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi.
Saba, Waajiri wanatakiwa kuwasilisha kodi ya mapato ya wafanyakazi – PAYE pamoja na michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati. Aidha, kwa wale wenye malimbikizo ya PAYE na michango, wanaagizwa kuwasilisha malipo hayo kabla ya tarehe 31 Desemba, 2016 vinginevyo hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao. Maafisa Masuuli, Wakuu wa Taasisi, Mashirika na Kampuni Binafsi wanaagizwa kusimamia utekelezaji wa agizo hili.
Nane, Maafisa Masuuli wanaelekezwa kutumia mfumo wa nakala laini (soft copy) katika kusambaza nyaraka mbalimbali za Serikali zinazozidi kurasa 50 isipokuwa kwa mafungu yanayotakiwa kusambaza nakala ngumu (hard copy) kutokana na matakwa ya kikanuni/kisheria. Hatua hii inalenga kupunguza matumizi makubwa ya gharama za kuchapisha na kudurufu nyaraka hizo na kulinda mazingira.
Tisa, katika mwaka wa fedha 2016/17 madai yote yanayohusu huduma za umeme, maji na simu yatalipwa moja kwa moja (centrally) na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kutumia bajeti za mafungu husika. Aidha, Maafisa Masuuli wanaagizwa kulipa kwa wakati ankara za huduma za umeme, maji na simu ili kuepuka malimbikizo ya madai mapya.
Kumi, Maafisa Masuuli wanaagizwa kufanya ununuzi kwa kutumia Hati za Ununuzi - LPOs zitokanazo na mfumo wa IFMS. Aidha, wazabuni na watoa huduma wanaelekezwa kuhakikisha wanapatiwa  Hati za Ununuzi - LPOs zitokanazo na mfumo wa IFMS. Hivyo, kuanzia mwaka 2016/17 Hati za ununuzi zitakazotolewa nje ya utaratibu huu hazitatambuliwa kama hati halali za ununuzi.

103.      Mheshimiwa Spika, mafanikio ya utekelezaji wa bajeti niliyowasilisha yatategemea ushirikiano wa kila mmoja wetu ili kufikia malengo yanayokusudiwa. Kama nilivyoeleza hapo awali, bajeti ya mwaka 2016/17 itategemea zaidi mapato ya ndani katika utekelezaji wake, hivyo kila taasisi ya Serikali inahimizwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kufikia lengo la mapato linalokusudiwa na hatimaye kutoa huduma bora kwa wananchi wetu. Ninaomba sote tushirikiane kwa pamoja na kila mmoja awajibike katika nafasi yake ili tuijenge Tanzania ya viwanda.

104.      Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, niwashukuru kwa dhati wananchi wa Tanzania, hususan wakulima, wafugaji na wavuvi, wafanyabiashara, watumishi wa umma na walioko sekta binafsi, na Diaspora ambao wanafanya kazi kwa bidii kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.  Ninyi ndiyo nguzo/muhimili wa Taifa linalojitegemea. Serikali inawathamini sana. Ninawashukuru pia vijana, Taifa la kesho. Wale waliopo shuleni na vyuoni someni kwa bidii mpate maarifa na ujuzi wa kuijenga nchi yenu. Na wale wengine tumieni nguvu zenu na ubunifu wenu katika kilimo cha mazao ya thamani kubwa, ufugaji, na huduma ikiwa ni pamoja na tasnia za ubunifu, muziki, filamu, komedi, mitindo ambako bado kuna fursa tele za kujipatia kipato halali ili kukidhi mahitaji ya maisha.

105.      Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa naomba kuwatambua na kuwashukuru Washirika wetu wa Maendeleo wanaotarajia kuchangia Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17 kama ifuatavyo: nchi za Canada, Jamhuri ya watu wa China, Denmark, Finland, Hispania, India, Ireland, Italia, Japani, Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, na Uswisi, pia taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwemo Arab Bank for Economic Development in Africa (BADEA), Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Global Fund, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Organisation of the Petroleum Exporting Countries (OPEC Fund), Saudi Fund, Kuwait Fund, na Umoja wa Ulaya. Aidha, napenda kutambua uhusiano mzuri tulionao na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) chini ya Mpango wa Ushauri wa Kisera unaojulikana kama Policy Support Instrument (PSI). Rai yangu kwa marafiki zetu ni kuwa: Endeleeni kutuunga mkono hususan katika jitihada zetu za kujenga uchumi wa viwanda kwa kuwavutia wawekezaji kutoka katika nchi zenu na kututafutia fursa za masoko ya bidhaa zetu. Mtimize ahadi zenu kwa wakati nasi tunawaahidi kutumia michango yenu kwa ufanisi na uwazi.

HAPA KAZI TU!          MUNGU IBARIKI TANZANIA!

106.       Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.


No comments: