Wednesday, June 15, 2016

FURSA ZA KIUCHUMI NI CHANGAMOTO KUBWA KWA WATU WENYE ULEMAVU - DKT POSSI


Na  Mwandishi Maalum, New York
 Mkutano wa Tisa wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu  Wenye Ulemavu ( CRDP), umeanza jana ( Jumanne)  hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  New York, Marekani.
Mada au  ujumbe wa Mkutano huu wa siku tatu   ni “ Utekelezaji wa  Agenda  ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030) Kwa Watu Wote Wenye Ulemavu: Pasipo Kumwacha Yeyote”
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania katika  Mkutano huu, unaongozwa na  Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Dr. Abdallah Possi ( Mb). Wajumbe wengine ni Mhe. Riziki Lulinda ( MB), Mhe. Elly Macha ( Mb) ,Mhe. Stella Ikupa ( Mb) , Bi Josephine Lyengi, Kaimu Kamishna kuhusu watu wenye ulemavu na Bi. Ngusekela  Nyerere , Afisa Mambo ya Nje, Wizara ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Akizugumza  wakati wa majadiliano ya  jumla mara baada ya  hafla ya ufunguzi , Naibu Waziri. Dr. Abdallah Possi  amesema,   changamoto kubwa inayowakabilia watu wenye ulemavu nchini Tanzania,  ni  fursa za kiuchumi.
“Licha ya  mafanikio  kadhaa yakiwamo ya utungaji wa sera,  sheria na  mabadiliko mbalimbali kuhusu  watu wenye ulemavu, bado kuna changamoto nyingi ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi  kwa lengo la kuwapunguzia matatizo watu wenye ulemavu  yakiwamo matatizo ya kutokuwa na fursa sawa  na kuondokana na umaskini”. Akaeleza Naibu  Waziri
Na Kuongeza kwamba, Tanzania kama ilivyo kwa  nchi yingine inakabiliwa pia na vipaumbele vinavyokinzana na ambavyo  ni muhimu lakini    vikiwathiri zaidi watu wenye ulemavu.
Akavitaja baadhi ya  vipaumbele hivyo kuwa  ni pamoja na upatikanaji wa  maji safi na salama,  chakula, huduma za afya, elimu na ukosefu wa ajiria.
Vile vile Naibu Waziri ameleza kuwa  mtazamo  hasi kuhusu watu  watu wenye ulemavu ni changamoto nyingine ambayo inatatiza ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika fursa  mbalimbali za  maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambazo  wangeweza kunufaika nazo  bila ya kujali  hali zao.
Akizungumzia   kuhusu mahitaji ya watu wenye ulemavu nchini Tanzania,  Mhe. Dr. Possi, ameeleza washiriki wa mkutano huu kutoka nchi 164 ambazo zimeridhia mkataba wa watu wenye ulemavu kwamba,  watu wenye ulemavu nchini  Tanzania wanakabiliwa na  tatizo kubwa la kutokuwa  vifaa  saidizi ambavyo  vingewasaidia na kuwawezesha   katika  shughuli zao za kila siku.
Vivile akabainisha  kuwa  mwaka  2015, Tanzania ilikuwa moja ya wadhamini  wakuu wa Azimio kuhusu watu wenye ualibino, azimio ambalo pamoja  na mambo mengine limelenga katika kutafutia ufumbuzi baadhi ya changamoto zimazowakabili  watu wenye ualibino katika  maeneo mbalimbali yakiwamo ya  elimu, afya na  ajira.
“ Bila ya kuwa na  vifaa saidizi  watu wenye  ulemavu wa aina  yoyote ile wanashindwa  kupata fursa anuai ambazo kwayo zingewawezesha kuishi  pasi  utegemezi na hivyo kuchangia katika yao binafsi na maendeleo ya nchi  yao” akasisitiza Naibu Waziri. Na akatumia fursa hiyo ya  kuhimiza upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ili wawe kujitegemea.
Awali  akifungua mkutano  wa tisa  wa Mkataba wa Watu Wenye ulemavu,  Rais wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa,  Bw. Mogens Lykketoft, amesema nchi ambazo  zimeridhia mkataba huo  zinaowajibu wa kuchukua hatua zote muhimu  zikiwamo za  maendeleo jumuishi  kwa watu wenye ulemavu.
“ Kila  nchi mwanachama wa mkataba huu na asiye wamanachama anakazi ya kufanya, lakini katika dunia  ya leo mafanikio hayamo  katika  mikono ya serikali peke yake” akasisitiza Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Na kwa sababu hiyo, ametoa wito kwa serikali zote pamoja na wadau  mbalimbali kufanya kazi kwa pamoja  kwa lengo la kuwawezesha  watu wenye ulemavu  zaidi  ya  bilioni moja.
Pamoja na  hotuba   kutoka kwa  nchi wanachama, mkutano huu ambao ni wa siku tatu  utakuwa na mijadala ya pembezoni  yenye mada tofauti. Mkutano huo pia  unashirikisha Asasi zisizo za kiserikali   zinazojihusisha na  masuala ya watu wenye ulemavu.


No comments: