Tuesday, June 7, 2016

Benki ya Exim ya China yaahidi kushirikiana na Serikali katika sekta ya viwanda

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima akiwa katika mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Exim ya China, Bi. Zhang Shuo alipofika Wizarani kwa mazungumzo. Katika mazungumzo yao Bi. Zhang alieleza nia ya Benki yake kuendelea kushirikiana na Tanzania katika Sekta ya Viwanda. Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani tarehe 07 Juni, 2016.
Sehemu ya ujumbe ulioongozana na Bi. Zhang wakifuatilia mazungumzo. 
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto) pamoja na Maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Mlima na Bi. Zhang (hawapo pichani). Kulia ni Bw. Ali Kondo na Bw. Humphrey Shangarai (katikati). 
Picha ya Pamoja 
=================================================

Benki ya Exim ya China imeahidi kuendelea kuisaidia Serikali ya Awamu ya Tano katika malengo yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili viweze kutoa mchango wa kuzalisha asilimia 40 ya ajira hapa nchini. 

Ahadi hiyo ilitolewa na Bi. Zhang Shuo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo alipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima ofisini kwake leo. 

Katika kikao hicho, Bi. Zhang alieleza kuwa Benki ya Exim ipo tayari kushirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ukiwemo mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati katika kiwango cha Kimataifa cha Standard Gauge. 

Aidha, Bi. Zhang alimfahamisha Dkt. Mlima kuwa Benki yake imeshainidhisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kama vile ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri kisiwani Zanzibar na njia ya kusafirisha umeme kutoka Dar es Salaam – Chalinze hadi Arusha yenye uwezo wa kubeba umeme wa KVA 400. 

Aliendelea kueleza kuwa Benki ya Exim imeanzisha mfuko maalum wa kusaidia maendeleo ya viwanda barani Afrika ambao umetengewa na Serikali ya China Dola za Marekani bilioni 10 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais wa China, Mhe. Xi Jinping aliyoitoa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na China uliofanyika Afrika Kusini Desemba 2015. 

Tanzania itakuwa ni moja ya nchi zitakazonufaika na fedha za mfuko huo ambazo pamoja na mambo mengine, imepanga kuzitumia kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu wezeshi ya barabara, reli, umeme kwenye Eneo la Uwekezaji la Bagamoyo. 

Bi. Zhang alimfahamisha pia Katibu Mkuu kuwa lengo la ziara yake lilikuwa ni kujadili masuala ya kiufundi na wadau mbalimbali ili utekelezaji wa miradi inayokusudiwa uanze haraka iwezekanavyo. Alieleza kuwa amefurahishwa na ziara hiyo kwa kuwa wadau wote alionana nao wameonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania katika kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo. 

Kwa upande wake, Dkt. Mlima aliishukuru Serikali ya China kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuwaletea maendeleo Watanzania. Aliahidi ushirikiano wa Wizara yake na Serikali kwa ujumla kuhakikisha kuwa miradi hiyo inataekelezwa kwa ufanisi bila vikwazo vyovyote. 

Benki ya Exim ya China imeshatoa mikopo kwa Tanzania katika utekelezaji wa miradi mingi na mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na ujenzi wa vinu vya kuzalisha umeme wa Kinyerezi III & IV. 

No comments: