Wednesday, May 11, 2016

SERIKALI KUSHINDANISHA WAWEKEZAJI SEKTA YA NISHATI


Na Veronica Simba

Serikali imesema ushindani kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta ya nishati, ndiyo njia bora zaidi itakayowezesha kuwapata wawekezaji wenye vigezo vinavyotakiwa.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyasema hayo jana, Mei 10, alipokutana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KOYO kutoka Japan, Norio Shoji na Ujumbe wake, ambayo imeonesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji na usafirishaji wa umeme nchini, kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo gesi asilia na jua.

“Kampuni nyingi zimeonesha nia ya kuwekeza kwenye sekta ya nishati. Serikali inao uhitaji mkubwa wa wawekezaji walio makini, hivyo tunahitaji kuwapata wawekezaji wenye vigezo kwa kutumia ushindani unaozingatia uwazi,” alisisitiza Profesa Muhongo.

Aliongeza kuwa, ili kuwarahisishia wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya nishati nchini, Wizara inaandaa taarifa maalum itakayobainisha maeneo yanayohitaji uwekezaji pamoja na vipaumbele vyake.

Alisema, taarifa hiyo itakuwa tayari na kutolewa mwishoni mwa mwezi huu (Mei 31, 2016) na kwamba itasambazwa kwa wadau wote wa ndani na nje ya nchi kupitia njia mbalimbali za mawasiliano, ikiwamo tovuti ya wizara.

Profesa Muhongo alieleza kuwa, taarifa hiyo pamoja na mambo mengine, itawapa fursa wawekezaji wenye nia, kuchagua aina ya uwekezaji wanaohitaji kufanya na katika maeneo ambayo wanadhani watakuwa na uwezo wa kumudu ushindani kutoka kwa wawekezaji wenzao kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Akifafanua zaidi, Profesa Muhongo alisema kuwa, zoezi la kuwashindanisha wawekezaji walioonesha nia, litakuwa ni endelevu na litakuwa likifanyika kila baada ya muda fulani, ambao utabainishwa katika taarifa husika inayotarajiwa kutolewa.

Akitoa mfano, alisema kuwa, siyo lazima kumpata mwekezaji katika zoezi la ushindanishaji, hivyo ni muhimu zoezi liwe endelevu ili kuweza kutoa fursa kwa wawekezaji wengi zaidi kushiriki na hivyo kumpata mwekezaji mwenye vigezo vyote ambavyo Serikali inavihitaji.

“Endapo tutaendesha zoezi la ushindanishaji wawekezaji na wote walioshindanishwa wasipotimiza vigezo vinavyotakiwa, hatulazimiki kumchukua yeyote tu. Tutakachofanya ni kutokumchukua yeyote kati yao na hivyo kuendelea na zoezi hilo baada ya muda tutakaoubainisha, hadi pale tutakapowapata wawekezaji wenye vigezo tunavyovitaka.”

Profesa Muhongo alibainisha kuwa, mchanganyiko wa nishati ambao Serikali imekusudia kuutumia kama vyanzo vya kuzalisha umeme nchini kwa sasa ni pamoja na gesi asilia, maji, upepo, jua, makaa ya mawe, mvuke (maji moto) na tungamotaka.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kushoto), akiagana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KOYO kutoka Japan, Norio Shoji (Kulia) pamoja na Ujumbe wake, baada ya kikao baina yao. Kushoto kwa Waziri ni baadhi ya Viongozi na Maofisa wa Wizara na Taasisi zake walioshiriki kikao hicho kilichofanyika Mei 10, mwaka huu Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam. KOYO imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya nishati nchini.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dkt Mhandisi Juliana Pallangyo (Kulia), akisalimiana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KOYO kutoka Japan, Norio Shoji, baada ya kikao baina ya Waziri wa Nishati wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Kampuni husika, kilichofanyika Mei 10 mwaka huu Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam. Kampuni ya KOYO imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya nishati nchini.
 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Katikati), akiwa katika kikao na Ujumbe kutoka Kampuni ya KOYO ya Japan (Kushoto). Kulia ni baadhi ya Viongozi na Maofisa wa Wizara na Taasisi zake walioshiriki kikao hicho kilichofanyika Mei 10 mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam. Kampuni hiyo imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya nishati nchini.




No comments: