Friday, May 20, 2016

KATIBU MKUU MAMBO YA NDANI YA NCHI ATUNUKU VYEO KWA MAAFISA 327 WA JESHI LA MAGEREZA, CHUO CHA MAGEREZA KIWIRA, MKOANI MBEYA.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Rwegasira akiwa katika Jukwaa akipokea Salaam ya heshima kutoka kwa Gwaride Maalum lililoandaliwa na Wahitimu wa Mafunzo ya Uongozi Daraja la Pili katika sherehe za kufunga Mafunzo hayo ya Maofisa wa Jeshi la Magereza, Chuo cha Magereza Kiwira kilichopo, Rungwe Mbeya(kushoto) ni Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Rwegasira akikagua moja ya Gadi ya Wanaume inayoundwa Gwaride rasmi la sherehe hizo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Rwegasira akimvisha cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Magereza mmoja wa Wanafunzi Wahitimu kwa niaba ya Wahitimu wote wa Mafunzo ya Uongozi Daraja la Pili. Mwanafunzi huyo amefanya vizuri katika Mafunzo hayo.
Onesho Maalum la kujihami kutoka kwa Askari wa Jeshi la Magereza katika namna ya kupambana na adui yeyote wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao. 

Na Lucas Mboje, Rungwe.
JUMLA ya Askari 327 wa Jeshi la Magereza, kati yao wanaume 257 na wanawake 81 wametunukiwa cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Magereza baada ya kuhitimu mafunzo ya Uongozi daraja la Pili kozi namba 1 katika Chuo cha Magereza Kiwira, Wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya.

Cheo hicho wametunukiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira katika Sherehe za ufungaji wa mafunzo hayo zilizofanyika katika Viwanja vya Chuo hicho leo Mei 20, 2016.

Akizungumza katika sherehe hizo Meja Jenerali Rwegasira amesema Askari na Maafisa wa Jeshi la Magereza nchini wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Haki za Binadamu na Utawala Bora kila wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kazi.

Jenerali Rwegasira amesema Maafisa hao wahitimu wakazingatie elimu waliyopewa wakati wa mafunzo ili wakawe mfano kipindi cha utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja na kuhamasisha na kuwaongoza wenzao ambao hawakupatiwa elimu kama yao.

Aidha, amewaasa kutowatesa Wafungwa walioko magerezani bali kuwahudumia kwa kuzingatia kanuni na taratibu za uendeshaji wa magereza kwani Wafungwa ni Binadamu kama watu wengine ispokuwa tu wameikosea jamii.

"Tuzingatie falsafa ya kwamba mfungwa yupo gerezani kwa ajili ya kutumikia adhabu na si kwa kuongezewa adhani. Kwa kufanya hivyo, Serikali yetu itakuwa inazingatia Utawala wa Sheria na hivyo kuwa Taifa linalozingatia na kuheshimu Haki za Binadamu na Utawala Bora". Alisisitiza Jenerali Rwegasira.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja amesema kuwa changamoto nyingi ambazo kwa kiasi fulani zimeathili utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo ni pamoja na ufinyu wa bajeti, makazi duni ya maafisa na askari, uhaba wa vitendea kazi na uchakavu wa vyombo vya usafiri.

Kamishna Jenerali Minja ameongeza kuwa tayari Jeshi hilo limechukua hatua mbalimbali za kufanya maboresho kwa lengo la kufanya Jeshi la Magereza kuwa la kisasa katika kutekeleza majukumu yake kisayansi na kwa ufanisi unaotarajiwa.

Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(kushoto) akifurahia jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi(katikati). Kulia ni Mkuu wa Chuo cha Magereza Kiwira, SACP. Stanford Ntirundura.
Askari Wanafunzi ambao wanaendelea na Mafunzo yao ya Awali wakifuatilia sherehe hizo za kufunga Mafunzo ya Uongozi Daraja la Pili.
Maafisa Wandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza wakiteta jambo mara baada ya kufungwa rasmi kwa Mafunzo ya Uongozi Daraja la Pili(kulia) ni ACP. Solomon Urio(katikati) ni ACP. Lazaro nyanga(kushoto) ni ACP. Ismail Mlawa.

(Picha zote na Lucas Mboje).

No comments: